Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 9/22 kur. 26-27
  • Furoshiki Yenye Matumizi Mengi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Furoshiki Yenye Matumizi Mengi
  • Amkeni!—1994
  • Habari Zinazolingana
  • Usikose Kumjali Mwenzi Wako!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Tai za Zamani na za Sasa
    Amkeni!—2000
  • Ni Nani Aliyezibuni Zote Hizi?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Kente Nguo ya Wafalme
    Amkeni!—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 9/22 kur. 26-27

Furoshiki Yenye Matumizi Mengi

NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA JAPANI

Furoshiki ni kitambaa cha Kijapani cha kufungia vitu—kitambaa cha kufungia vitu kilicho na utofauti. Huonekana maridadi. Ni maridadi kwa mguso. Nacho hufungika maridadi. Kuchagua na kufunga furoshiki kumekuwa usanii, upokezwao kutoka kizazi hadi kizazi kwa zaidi ya miaka elfu moja.

SI KITAMBAA chochote tu kifaacho. Rangi, mtengenezo, na aina ya kitambaa ni lazima yote yafikiriwe. Pindi inayohusika huamua pia ni furoshiki ipi itakayotumiwa. Kwa kielelezo, zawadi yaweza kutolewa ikiwa imefungwa katika furoshiki ya hariri yenye chapa za michoro ya kimapokeo, kama vile maua ya cheri au plamu. Nyakati fulani huenda mpaji hata akasisitiza kwamba mwenye kupokea akubali kitambaa kilichofunguliwa kiwe ni sehemu ya zawadi yenyewe.

Bila shaka, vitambaa vya kufungia vitu hupatikana vikiwa vya ukubwa mbalimbali na hufaa kwa makusudi mbalimbali. Matikiti ya mviringo yaweza kufungwa ndani yavyo, au hata chupa ndefu za divai ya mchele. Furoshiki fulani ni kubwa sana hivi kwamba magodoro matatu au manne yaliyokunjwa yaweza kufungwa ndani yavyo. Vitambaa hivi vizuia-vumbi kwa kawaida huwa vya pamba na husisimua sana watoto wadogo wapendao kuvivaa kwa michezo ya kuonyesha mavazi. Kwa upande mwingine, vijana fulani hutumia vitambaa vidogo sana. Kwa kweli, ukitupa jicho katika visanduku vya watoto vya kuchukulia chakula cha mchana utaona kwamba vitambaa vya kujipangusia mwili na vya mfukoni hutumiwa pia kama furoshiki za kadiri ndogo. Watoto wafunguapo furoshiki hizi za kadiri ndogo ili wale vyakula vyao vya mchana, vitambaa safi hivyo hutumika kuwa vipangusa-mdomo vya mezani. Ingawa hivyo, furoshiki zilizo nyingi zakaribia ukubwa wa skafu ya kichwani ya mraba.

Njia ya kawaida ya kutumia furoshiki katika Japani ni kuweka kitu kitakiwacho kufungwa kikiwa kimekunjwa ncha ya chini ya kushoto hadi ya juu kulia, katikati. Ikiwa kifurushi kinachofungwa ni cha umbo la mstatili, kitambaa kilichozidi sehemu za kando hufungwa vizuri kuzunguka kifurushi, kwanza upande mmoja kisha ule mwingine ili kila upande ukunjwe kuelekea mahali tofauti. Hii huacha kona mbili za kitambaa zikitokeza kwenye miisho. Ndipo sasa ifikapo sehemu iliyo ngumu. Kona mbili hizi hupitishwa vizuri juu ya kile kifurushi na kufungwa fundo mara mbili. Kwa kufaa, hili litakuwa fundo dogo ambalo hatimaye litafanana na kipepeo mdogo maridadi. Hata hivyo, kulingana na ukubwa wa kifurushi, “mabawa” ya kipepeo huyo huenda yakafanana zaidi na masikio regerege ya sungura. Lakini usikate tamaa! Baada ya sekunde chache yaweza kukunjwa vizuri kama upinde.

Ili kifurushi kiwe cha mraba, kona zinazoelekeana za furoshiki hufungwa juu ya kifurushi, fundo moja likiwa juu ya jingine ili fundo moja tu lionekane. Wajapani huweza kukivuta kitambaa chote kikiwa kimekazika hodari kisha kukikusanya juu kwa njia ya kuvutia. Umbo hilo lililojichora vizuri ni maridadi. Ingawa kifurushi hicho chaweza kubebwa kwa kushikwa kwenye fundo, iwapo ni cha zawadi, kwa kawaida hutegemezwa kwa chini ili kuhifadhi umbo hilo.

Neno furoshiki humaanisha kwa uhalisi “shuka ya bafuni,” jina lililopata kuwa maarufu katika karne ya 17. Kwa kushikwa na hofu ya moto, wakati huo watu walijaribu kuepuka kuwasha mioto ya kuchemsha maji ya kuoga. Basi hawakuwa na la kufanya ila kwenda kwenye bafu za umma. Humo walitandaza kitambaa chao cha mraba, wakavua nguo, na kukitumia kufunga mavazi yao ndani yacho walipokuwa wakioga. Uogaji wa umma ni kama umefifia kabisa, lakini jina furoshiki, “shuka ya bafuni,” limedumu.

Katika muhula ambapo mapokeo yanatoweka kasi, furoshiki inaendelea kuwapo. Familia zilizo nyingi zaripoti kuwa zina furoshiki karibu nane, na madai yao huelekea kuthibitishwa na vitambaa vingi vionekanavyo vikiwa vimefunga mizigo katika sehemu za kubebea vitu katika magari-moshi ya kasi sana ya Japani. Abiria wakiwa na mavazi ya Magharibi, huchanganya vizuri makale na mapya, mapokeo na mamboleo.

Mauzo yalishuka kwa kitambo maduka yalipoanza kuwapa wanunuzi wao mifuko ya plastiki na mifuko mikubwa ya karatasi. Hata hivyo, mambo yamebadilika. Vibandiko vyenye majina ya wabuni-mitindo na mabuni ya ki-siku-hizi vimefanya furoshiki ivutie sana wanawake wapenda-mitindo wa Japani. Furoshiki huchukuana vizuri na vazi la kimono kwa jinsi ambayo mkoba wa ngozi hauwezi kuchukuana nalo. Kwa hiyo vazi la kimono litumiwapo kwa pindi za pekee, nayo furoshiki hutumiwa kwa vifurushi vikubwa.

Kwa kweli, vitambaa vya kufungia vitu vyastahili sifa nyingi. Furoshiki zilizotengenezwa kwa fumwale za kiasili hazidhuru mazingira. Zaweza kutumiwa tena na tena. Hizo ni ndogo. Ni nyepesi. Ni rahisi kuzibeba. Hizo huwa mifuko ya umbo au ukubwa wowote papohapo. Furoshiki zikiwa mikononi mwa watalii wa kigeni wasiojua ni nini, hizo huwa kama skafu maridadi na vitambaa vya kuwekwa mezani tu. Na hivi majuzi Wajapani wameanza kuiga wageni na wameanza kutumia furoshiki kwa njia hiyohiyo, na pia kama viwekeleo vya mezani, kwilti (shuka nzito) za kutandika zenye viraka maridadi, aproni, mapambo yaliyoning’inizwa ukutani, na kama kitu kinginecho wafikiriacho. Kwa kweli, watu wanaanza kugundua jinsi furoshiki iwezavyo kutumiwa kwa njia nyingi.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki