Wali au Mchele—Wapenda Upi Zaidi?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA INDIA
‘JE, WEWE hula wali au mchele?’ Hilo ni swali ambalo wewe ukiwa mgeni katika nyumba ya Kihindi huenda ukaulizwa. Katika India karibu asilimia 60 ya wali uliwao huchemshwa kidogo tu. Lakini huenda ukashangaa kujua kwamba katika mataifa ya Magharibi, karibu kila mtu hula kile ambacho Wahindi hukiita mchele (mbichi)!
Yote haya huenda yasisikike ya ajabu utambuapo kwamba tunazungumzia, si njia ya kupika wali wa kuliwa, bali njia ambayo Wahindi hutumia katika kutayarisha mpunga unapovunwa. Kwa hiyo, ni nini hufanywa katika upuraji huo, na kwa nini? Tazamo la karibu zaidi la mchele na kutayarishwa kwao ukiwa nafaka ya kuliwa litaandaa majibu yenye kunurisha.
Chakula Kikuu cha Mamilioni
Mapato ya kiakiolojia na rekodi za kale zaonyesha kwamba mpunga ulilimwa katika India na China kule nyuma sana kufikia mileani ya tatu K.W.K. Wakaaji wa kale wa India waliuita dhanya, au “kiruzuku jamii ya binadamu.” Bado ni jina lifaalo kwa sababu watu wengi zaidi huishi kwa kutegemea mchele kuliko zao jinginelo liliwalo. Walio wengi wa watu hawa huishi katika Asia, ambako, kulingana na chanzo kimoja, watu zaidi ya milioni 600 hujipatia nusu ya kalori zao za kila siku kutokana na wali pekee na zaidi ya asilimia 90 ya mpunga wa ulimwengu hulimwa na kuliwa wali.
Ile delta ya tropiki yenye umajimaji ya Ganges ni mojapo maeneo ya ulimwengu yenye kulimwa mpunga mwingi zaidi. Mvua nyingi na halijoto zenye ujoto, na pia wafanya-kazi wengi, hufanya mahali hapa pafae kabisa kwa kulima mpunga. Acheni tuukubali mwaliko wa rafiki zetu wakaa-kijijini katika mkoa huu tujionee wenyewe kuvunwa na kutayarishwa kwa mpunga.
Kuvuna Mashamba ya Mpunga
Basi letu latupeleka Jaidercote katika Bengal Magharibi, nasi twaendelea na safari yetu kwa riksho ya magurudumu matatu hadi eneo la ndani-ndani. Muda si muda twaona utendaji wa sulubu mashambani. Huku hakuna cha mashine za kupura na kuvuna! Bali, akina baba, wana, wajomba na ami, na ndugu wana shughuli katika yale mashamba ya mpunga, wakikata kwa umairi konzi-konzi za vishina kwa safari moja wakitumia miundu midogo. Mmoja wa wavunaji, kwa kuhisi kamera yetu, amaliza haraka kufunga tita lake kwa ukanda wa jani kavu na kushika juu-juu akiwa amejipanga hodari kupigwa picha. Twacheka jinsi wanakijiji hawa wamekuwa wapenzi wa kupigwa picha.
Yale matita yaachwa yakauke katika jua kwa siku moja au mbili. Kisha washirika wachanga zaidi wa familia waweza kusaidia, wakisafirisha nyumbani vibunda vidogo-vidogo vya matita makavu yanayochakacha yakiwa yamesawazishwa kwa umaridadi juu ya vichwa vyao.
Mwishowe, twawasili kijijini. “U hali gani, Dada?” twamsalimu mwenyeji wetu, tukitumia mtajo wa staha. Tabasamu yake yatuhakikishia kwamba mambo yote ni sawasawa, nasi twamwona mke wake akichapusha mwendo akatayarishe chai.
Tunapokunywa chai yetu ya asubuhi, twauliza mavuno ya mwaka yamekuwaje. “Si mabaya sana,” yule mwanamume ajibu kwa kuzuia hisia kama kawaida ya wakulima, lakini ndipo aomboleza kwamba kwa kutumia mbegu zenye mavuno mengi katika miaka ya majuzi zaidi, rasilimali za ardhi zinakamuliwa mno. Mwanzoni zilitokeza yale yaliyoonekana kuwa mazao ya muujiza, lakini sasa mambo ni mengine kabisa. Zile mbolea za kemikali zihitajiwazo kwa mbegu za mavuno mengi ni ghali, naye haziwezi.
Kupura na Kuchemsha Nusu
Tumalizapo kumbwe yetu, twahimiza familia hiyo iendelee na kazi yao ya kuvuna, tuliyokuja kuitazama. Katika nyumba hii kupura kumekwisha kufanywa. Chini kidogo tu kwenye kijia, kwenye nyumba ya jirani mmoja, wanawake wana shughuli. Wagongesha tita moja-moja juu ya kikwezo cha mianzi na kuziacha punje zianguke kupitia mianya iliyopo. Majani makavu yanayobakia yakusanywa kuwa rundo.
Mchele, uitwao pia mpunga uliotwangwa, umefunikwa na ganda lisilo laini, ambalo halipendezi kamwe kwa kuliwa. Kwa wale wapendeleao kula mchele mbichi-mbichi, hatua zaidi tu ifuatayo ni kuambua lile ganda, na labda kukwatua na kueupisha punje ikiwa zao hilo ni kwa ajili ya soko la kigeni lenye wateuzi wenye madaha.
Hata hivyo, zao lipatikanalo hapa si la kusafirishwa nje bali ni la kuliwa na familia zenyewe za wakulima. Wao huiweka nafaka katika tikri, au ghala yenye ukubwa wa kifamilia iliyoezekwa kwa nyasi. Kwa jumla watu wa delta ya Ganges hula wali, lakini sisi twatania mwenyeji wetu, tukidokeza kwamba mwaka huu apaswa kutayarisha mlo wa mchele.
“Sivyo kamwe,” ajibu. “Katika janibu hizi sisi tumezoea wali na hatupendi mchele kwa kadiri hiyohiyo.”
Tumesikia kwamba wali hutayarishwa kwa utaratibu wa kuroweka na kuchemsha kidogo tu, lakini hatuna hakika hili hufanywaje. La kufurahisha ni kwamba rafiki yetu ajitolea kuonyesha utaratibu ambao familia yake hutumia. Hakuna uhitaji wa vifaa maalumu kwa sababu ni kiasi kidogo tu hutayarishwa kwa safari moja ili kutimiza mahitaji ya familia kwa juma moja au mawili. Wao wajaza hanri kubwa, au nyungu ya kupikia, huku zile punje zilizofunikwa kwa maganda zikiwa zimewekwa ndani ya tikri kisha waongezea lita moja ya maji. Kisha kitu hicho chapashwa moto katika ile miali mianana ya jiko liwashwalo kwa majani makavu, liitwalo oonoon, mpaka maji yawe yamevukizwa. Halafu vilivyomo vyaachwa usiku kucha ndani ya hodhi yenye maji safi, na baada ya kuchujwa, vyarudishwa katika hanri ili vitoe mvuke mpaka vikauke tena. Mwishowe, zile punje zatandazwa chini ziwe ngumu katika jua, pindi kwa pindi zikigeuzwa kwa mguu.
Hii ilionekana kama kazi nyingi ya ziada kwetu, lakini kuna faida fulani katika utaratibu huu mbali na kutimiza upendezi wa familia. Kuchemsha kidogo tu huruhusu vitamini na vilishaji fulani katika punje ya mchele zifyonzwe kwa kina kirefu ndani ya kilisha-tete, au ile sehemu ya kuliwa, ya mpunga uliotwangwa. Halafu vitu hivi havichujuliwi sana wakati wa ule uoshaji na upikaji ufuatao. Tokeo ni mlo wenye lishe zaidi. Thamani hiyo ya ziada iliyo chakulani yaweza kumaanisha tofauti halisi kati ya uhai na kifo kwa wale waishio hasa kwa kutegemea kula wali.
Manufaa nyingine ithaminiwayo kwa utayari na wakulima wenyewe ni kwamba punje zilizochemshwa kidogo tu huhifadhiwa kwa urahisi zaidi na ganda ni rahisi zaidi kuambuliwa. Jambo hilo, pamoja na ugumu ulioongezeka, husaidia kupunguza hali ya kuvunjika-vunjika.
Kuionja Punje
“Sasa ni wasaa wa kupata chai na kumbwe zaidi,” asema mwenyeji wetu. Twatembea kurudi kwenye nyumba yake ambako Dida (Nyanya) anatayarisha moori. Mchele mvimbe huu uliotayarishwa sasa tu wapendwa sana na wote, hasa na watoto. Dida amechuchumaa karibu na oonoon, akikaanga vikombe vichache vya mchele usio na maganda uliochemshwa kidogo tu alioutia unyevu na kuuchanganya na chumvi kidogo. Sasa punje hizo zimekauka na kuachana hivi kwamba yeye anyunyiza chache-chache kuziingiza katika kikaangio cha chuma chenye mchanga moto. Aendeleapo kuupasha moto mchanga huo, ule mchele wavimba kuwa na ukubwa ulio mara kadhaa za ule wa kawaida. Kisha ule moori uliokwisha kutayarishwa waenguliwa juu ya ule mchanga kwa kitita cha vitawi kabla haujapata fursa ya kuungua. Pia vitawi hivyo vyatumika kuadhibu vikono vyenye hamu ya kujichovya ndani ya kile kikapu cha moori wenye moto.
Sisi twafurahia moori wetu pamoja na nazi iliyokatwa sasa hivi, lakini twafanya uangalifu tusile mwingi mno, kwa kuwa twakumbuka kwamba saa za chakula cha mchana haziko mbali sana.
Utaratibu wa mwisho kuuona ni uambuaji maganda. Mpaka hivi majuzi tu jambo hili lilifanywa kwa mchi na kinu kiitwacho dhenki, lakini sasa, viondoa-maganda viendeshwavyo na mashine hufanya kazi ya haraka zaidi, hata katika sehemu za ndani sana nchini. Badiliko hili laombolezwa na baadhi ya wakale, kwa kuwa mchele uambuliwao na dhenki huiacha ngozi nyekundu ya ndani (ngozi-nje) ya punje ikiwa imegandamana palepale, ikileta ladha safi na vilishaji zaidi kwenye chakula kile. Hata hivyo, mashine hiyo hubandua kila kitu—ganda, makapi, na kadiri kubwa ya viinitete—ikiacha kilisha-tete kile cheupe tu chenye wanga ambacho watu wengi hukitaka sana leo.
Sasa wale mabibi wana hamu nyingi wakitaka tuile karamu ambayo wamekuwa wakitayarisha. Wameupika wali uliochemshwa kidogo tu kwa kufanya utokote, na sasa wajazwa marundo-marundo yenye mvuke moto juu ya sahani ambazo ni majani ya ndizi. Kisha yaja mapishi ya dengu, mboga za kienyeji, na samaki wa vidimbwi ili tuwale pamoja na wali ule. Sisi sote twakubaliana kwamba hii ni mojapo sehemu zenye kufurahika zaidi za ziara yetu.
Ndiyo, mpunga ni uandalizi wa kupendeza, uwe waliwa ukiwa wali au mchele, nao ni moja la manyasi mabichi ambayo Mungu alichipusha yawe “maboga kwa matumizi ya mwanadamu.”—Zaburi 104:14.
[Sanduku katika ukurasa wa 26]
Jhal Moori
Katika sehemu nyingi za India, kumbwe ya mchele mvimbe huuzwa barabarani na wanavibanda waliovalia urangi wa kupendeza. Jhal moori huo wenye ladha nzuri na wenye kujenga waweza kutayarishwa kwa urahisi nao ni badiliko zuri la kupumzisha vile vyakula vya kumbwe zilizotangulia kutiwa katika pakiti.
Kwa kuanza na kikombe kimoja cha mchele mkavu, mvimbe, usioongezewa utamu, ongeza nyunyizo la vitu vinavyofuata, kulingana na upendezi wako: nyanya zilizokatwa kuwa ndogo sana, vitunguu, tango, pilipili hoho za kijani (za hiari), karanga chache, adesi (za hiari), chaat masala (mchanganyo wa vikolezo vya ungaunga, vipatikanavyo katika maduka ya Kihindi) au kidokoo (kifinyo) cha chumvi na pilipili, nusu-kijiko-chai ya mafuta haradali au mafuta mengine ya mboga. Sukasuka vichanganyio pamoja kwa nguvu, na ule mara hiyo.
Kwa kuwa mapendezi hutofautiana, mwanakibanda auzaye moori huruhusu mlaji achague kutoka kwenye unamna-namna wake mwingi wa mboga katekate na vikolezo ni kitu gani na kiasi gani chapasa kuongezwa. Wewe waweza pia kupakua kumbwe hiyo kwa mtindo wa fondue, ukiruhusu wageni wako wajichanganyie moori wao wenyewe.
[Picha katika ukurasa wa 24]
(1) Kupura mashina ya mpunga (2) Kupepeta (3) Dida akitayarisha “moori” (4) Kikapu ‘cha Moori’ kikiwa na vichanganyio mbalimbali