Wangeweza Kufanyaje Hivyo?
WATU waliiteteaje biashara ya watumwa? Wanahistoria watoa uangalifu kwa ule uhakika wa kwamba kufikia karne ya 18, watu wachache walishutumu umaadili wa utumwa. Kile kitabu The Rise and Fall of Black Slavery chaonelea hivi: “Wakati ule Columbus alipofika bila kutazamia kwenye West Indies, wala makasisi wala maandishi ambayo kanisa lilikuwa limekubali hayakupatia masetla wa wakati ujao wonyesho wa kwamba utumizi wao wa kazi ya kutumikisha ungeweza kufikiriwa kuwa usio wa maadili, ingawa wanakanisa mmoja-mmoja walikuwa wameonyesha mashaka. . . . Hakukuwa na dalili kwamba uanzilishi wa utumwa, ukiwa umefungamana kama ulivyokuwa na jamii ya Ulaya, ulikuwa unapaswa kupingwa.”
Baada ya biashara ya kuvuka Atlantiki kufikia kilele, makasisi wengi walitumia usababu wa kidini ili kuunga mkono utumwa. Kile kitabu American Slavery chataarifu hivi: “Wahudumu Waprotestanti [katika Amerika] walichangia fungu kubwa katika kukinga utumwa . . . Yawezekana usababu wa kidini ulioenea na wenye matokeo sana ulikuwa oni sahili la kwamba utumwa ulikuwa sehemu ya mpango wa Mungu ili kuwatolea watu wa cheo cha chini baraka za Ukristo.”
Lakini kutendewa mara nyingi kwa ujeuri na kwa unyama kulikofanyiwa watumwa kulitaka utetezi zaidi kuliko ule ujifanyaji wa kutoa “baraka za Ukristo.” Hivyo mabwana wa kikoloni pamoja na waandishi na wanafalsafa katika Ulaya walijiambia kwamba weusi hawakuwa sawa na weupe. Edward Long, mwenye shamba kubwa ambaye alikuwa aandike History of Jamaica, alionelea hivi: “Tunapofikiria kuhusu asili ya watu hawa, na kutofanana na jamii ile nyingine ya kibinadamu, je, haitulazimu kukata kauli kwamba wao ni wa spishi tofauti?” Matokeo ya kufikiri kama huko yalielezwa na liwali wa Martinique hivi: “Nimefikia hatua ya kuamini kikamili kwamba mmoja lazima awatendee Weusi kama vile mmoja anavyowatendea hayawani.”
Hatimaye upendezi wa kibinafsi wa uchumi na mahangaiko ya ubinadamu yalichangia kumaliza biashara ya watumwa ya kuvuka Atlantiki. Tangu mwanzoni watu wa Afrika walikinza kutumikishwa, na kufikia mwishoni-mwishoni mwa karne ya 18, uasi ulikuwa jambo la kawaida. Wamiliki watumwa wenye hofu walijipata katika hali ya matata zaidi. Wao pia walikuja kutilia shaka kama, badala ya kuwa na watumwa wa kudumu, huenda ikawa rahisi kidogo kulipia utumishi wa watumwa ulipohitajika.
Wakati huohuo, maoni ya kimaadili, kidini, na ubinadamu dhidi ya utumwa yalipata utegemezo uliozidi kuongezeka katika Ulaya na Amerika. Harakati za kutangua utumwa zikawa na nguvu. Licha ya utanguaji kisheria wa biashara ya watumwa katika nchi nyingi kutoka mwaka wa 1807 na kuendelea, athari za utumwa zilibaki.
Mfululizo wa televisheni, The Africans: A Triple Heritage, kwa njia yenye kugusa moyo ulitoa hisia za wana na mabinti wa Afrika: “Kabla ya kuanza kwa biashara ya watumwa tuliishi katika . . . Afrika. Na kisha watu tusiowajua wakaja na kuchukua baadhi yetu. Leo, tumetapakaa kotekote hivi kwamba jua halichwi kamwe kwa wazao wa Afrika.” Kuwapo kwa mamilioni ya watu wa Afrika kwenye Amerika Kaskazini na Kusini, Karibea, na Ulaya ni matokeo yaliyo wazi ya biashara ya utumwa.
Watu bado hujadili suala la ni nani wa kulaumiwa kwa ajili ya biashara ya watumwa ya kuvuka Atlantiki. Basil Davidson, mtaalamu katika historia ya Afrika, aandika hivi katika kitabu chake The African Slave Trade: “Afrika na Ulaya kwa kuunganishwa zilihusika.”
“Ufalme Wako Uje”
Kuna jambo fulani la kujifunza—jambo ambalo lahusisha utawala wa binadamu. Mwanamume mwenye hekima aliandika hivi: “Nilifikiria matendo yote ya unyanyasaji yaliyofanyika chini ya jua,—na Alaa! machozi ya wanyanyaswao, na hawana mfariji, na kwa upande wa wanyanyasaji wao kuna uwezo.”—Mhubiri 4:1, Rotherham.
Kwa kusikitisha, maneno hayo, yaliyoandikwa muda mrefu kabla ya kuanza kwa biashara ya Kiafrika ya watumwa, yaendelea kuwa kweli leo. Wanyanyaswao na wanyanyasaji bado wangali nasi, na katika baadhi ya mabara ndivyo na watumwa na mabwana zao. Wakristo wajua kwamba karibuni, kupitia serikali ya Ufalme wa Mungu, Yehova “atamwokoa mhitaji aliapo, na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi.” (Zaburi 72:12) Kwa sababu hiyo na nyingine, wao huendelea kusali kwa Mungu hivi: “Ufalme wako uje.”—Mathayo 6:9.