Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 6/8 kur. 17-19
  • Sababu ya Mwili Wako Kuhitaji Usingizi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sababu ya Mwili Wako Kuhitaji Usingizi
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Fungu la Usingizi
  • Usingizi wa Kiasi Gani?
  • Hatari Zitokanazo na Ukosefu wa Usingizi
  • Kupata Usingizi Mzuri wa Usiku
  • Nifanye Nini Ili Nipate Usingizi wa Kutosha?
    Vijana Huuliza
  • Usingizi Ni Starehe Tu au Ni Muhimu?
    Amkeni!—2003
  • Kupata Usingizi Unaohitaji
    Amkeni!—2004
  • Usingizi—Kwa Nini Ni Muhimu Sana?
    Amkeni!—2011
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 6/8 kur. 17-19

Sababu ya Mwili Wako Kuhitaji Usingizi

“JAMANI ni nini ningetoa ili nipate usingizi mzuri usiku!” Lalamiko hilo ni la kawaida siku hizi. Watu wengi daima hujisulubu, nayo mikazo ya kila siku na ukakamao wa maisha ya kisasa husababisha madhara kwa wengi.

Wanatiba, maofisa wa polisi, wazima-moto, madereva wa malori, wafanyakazi wa kupokezana zamu, mama wenye watoto wachanga, na wengine wengi wako miongoni mwa wale wenye uelekeo wa kupokonywa usingizi ambao miili yao huhitaji. Mamilioni ya watu wanaokata tamaa kutokana na kukosa usingizi wanataka sana kujua jinsi ya kupata usingizi mnono wenye kuburudisha.

Fungu la Usingizi

Usingizi, ama angalau kipindi cha pumziko, waonekana kuwako kila mahali miongoni mwa viumbe vilivyo hai. Ikiwa umepata kufuga wanyama kama vile paka, mbwa, ama ndege, bila shaka umeona kwamba paka na mbwa kwa ukawaida hujikunyata na kulala na kwamba ndege huwa kimya na kulala giza liingiapo. Karibu wanyama wote, ndege, na wadudu wana uhitaji wa usingizi, ama angalau vipindi vya utendaji uliopungua. Kwa wanadamu, usingizi ni uhitaji usioepukika.

Watu wengine hufikiri usingizi kuwa tu kipindi cha pumziko. Lakini ni zaidi ya hilo. “Kwa kweli usingizi ni utaratibu fulani tata wa utanukano wa misuli na kulegea, mpigo na mpando wa damu ukipanda na kushuka nayo akili ikitokeza filamu nyingi za kujitengenezea yenyewe,” lasema Toronto Star. “Wakati mtu anapolala,” yataarifu The World Book Encyclopedia, “utendaji wote hupungua na misuli hulegea. Mpigo wa moyo na kiasi cha kupumua hupungua.”

Ijapokuwa wanasayansi, madaktari, na watafiti wamechunguza usingizi kwa miongo mingi, mafumbo ya kimsingi kuhusu fungu lawo muhimu hubaki bila kufumbuliwa. Wachunguzi hawa hata hawajavumbua usingizi hasa ni nini ama kwa nini sisi hulala. Asema hivi Dakt. Eliot Phillipson wa maabara ya utafiti wa usingizi katika Queen Elizabeth Hospital ya Toronto: “Hatujui matukio ya kibiolojia yanayotukia katika usingizi ambayo huturudisha upya.”

Wakati wa usingizi, mabadiliko hutukia katika mwili yaathiriyo mfumo wetu wa kinga. Sehemu mbalimbali za mwili hulegea na kupata pumziko, zikirudisha upya uchakavu na uchovu kutokana na utendaji wa siku. Kazi ya usafishaji wa ujumla ifanywayo kupitia mkondo wa damu huendelea kwa ustadi, na usawaziko wa kikemikali hurudishwa upya. Hivyo usingizi waweza kulinganishwa na kikundi cha wafanyakazi cha usiku ambacho huja ili kurekebisha na kusafisha kwa ajili ya siku ifuatayo.

Mojapo ya kazi muhimu za usingizi ni kuruhusu mfumo wa hisi kupata nguvu upya kutokana na kutumika kwawo wakati wa mchana. Kama vile The World Book Encyclopedia isemavyo, “usingizi hurudisha upya nishati mwilini, hasa katika ubongo na mfumo wa hisi.”

Usingizi wa Kiasi Gani?

Watu wazima wengi huhitaji muda wa saa saba ama nane za usingizi kila usiku. Wengine huhitaji saa chache zaidi, wengine hata nyingi zaidi. Kuna wengine ambao husema kwamba wao huhitaji saa nne ama tano tu, ingawa wengine wao huenda wapate lepe kidogo wakati wa mchana. Vitoto huhitaji usingizi zaidi kuliko watu wazima.

Hasa watu wazeekapo, waweza kupata kwamba wao huamka-amka mara kadhaa wakati wa usiku. Wengine huenda wakahisi kwamba jambo hili ni dalili ya mwanzo wa matatizo mazito ya usingizi. Hata hivyo, ingawa watu wakubwa zaidi huenda wasiwe na ubora wa usingizi waliokuwa nao walipokuwa wachanga zaidi, majaribio yameonyesha kwamba kuamka-amka wakati wa usiku si jambo linalohitaji kufadhaisha. Kwa kawaida, kipindi cha kuamka-amka huwa kifupi, labda dakika kadhaa tu, kabla hawajalala tena.

Ijapokuwa, hata umri wako uwe upi, mmoja hapaswi kutarajia kuwa na usingizi mnono usiku mzima. Usingizi hutukia katika mizunguko fulani ya usingizi mnono ikibadilishana na usingizi mwepesi. Wakati wa usiku, mtu huenda akawa na baadhi ya mibadilikano hii.

Hatari Zitokanazo na Ukosefu wa Usingizi

“Watafiti wanaendelea kuhangaika zaidi na zaidi kuhusu idadi ya watu ambao kwa kiasi kikubwa hupata usingizi kidogo sana. Kukosa usingizi kwa kipindi kirefu, wao waonya, kwaweza kuwa na athari zenye kudhuru kwetu sisi na kwa watu wanaotuzunguka,” likaripoti The Toronto Star.

“Watu waliokosa usingizi hupungua nishati na hupapwa haraka. Baada ya siku mbili bila usingizi, mtu hupata kwamba kuwa makini kwa muda mrefu kunakuwa tatizo. . . . Makosa mengi hufanywa, hasa katika kazi za kawaida, na umakinifu hupotea nyakati nyingine. . . . Watu wasiopata usingizi kwa zaidi ya siku tatu wanakuwa na tatizo kubwa la kufikiri, kuona, na kusikia kabisa. Wengine wanakuwa na vipindi vya kuona chechele, ambapo wao huona vitu ambavyo kwa hakika havijakuwako,” yasimulia The World Book Encyclopedia.

Majaribio yamepata kwamba baada ya siku nne za kukosa usingizi, mwenye kujaribiwa angeweza kufanya kazi chache tu zilizo za kawaida. Kazi zinazohitaji umakinifu ama hata uchonjo mdogo sana wa kiakili zinakuwa zisizowezekana. Kupoteza umakinifu na uchonjo wa kiakili haukuwa mbaya hivyo. Baada ya siku nne na nusu, kulikuwa na dalili za upunguani, na mwono wa mtu wa vitu vinavyomzunguka ulikuwa usio wa kawaida kamwe.

Ukosefu wa usingizi waweza kusababisha matatizo makubwa. Watu wengi wenye usingizi wamepata kulala wakiwa wangali wanaendesha gari na kuhusika katika aksidenti zenye kufisha. Kukosa kulala kwaweza pia kuongoza kwenye matatizo ya familia na ndoa, kwani ukosefu wenye kuendelea wa usingizi humfanya mmoja kuwa mwenye kuchokozeka zaidi na mgumu kupatana naye. Kupata usingizi mzuri wa usiku ni muhimu sana kuliko wengine wawezavyo kudhani.

Kupata Usingizi Mzuri wa Usiku

Mtaalamu wa usingizi Dakt. Jeffrey J. Lipsitz wa Kitovu cha Matatizo ya Usingizi cha Metropolitan Toronto adokeza yafuatayo ili kupata usingizi mzuri wa usiku. Lala katika mazingira salama, kimya, yenye giza na kwenye kitanda chenye kupumzisha. Usipate lepe ya wakati wa jioni, hata ikiwa hukulala vizuri usiku uliotangulia; jaribu kubaki ukiwa macho hadi wakati wako wa kawaida wa kwenda kitandani. Epuka kafeni kabla ya wakati wa kulala. Usitumie kitanda unaposoma ama kutazama televisheni. Epuka mazoezi ya kujikakamua mno na milo mizito kabla tu ya kwenda kulala. Dumisha utaratibu wa saa za kulala, kwa sababu hili litasaidia mwili kupata ukawaida wa kulala na kuamka.

Jizoeze kuwa na ukawaida wa kupoa na kutulia kabla ya kwenda kitandani. Epuka mambo ambayo huenda yakakusisimua na kisha ukose kulala. Kwa mfano, epuka filamu, programu za televisheni, ama usomaji wenye kusisimua. Kuwa na mazungumzo yenye kuchochea kabla tu ya kwenda kulala kwaweza pia kukufanya usilale.

Kwa wengine, kuoga kwa maji yenye ujoto (si yenye moto sana) ama kusoma habari yenye kustarehesha kwasaidia. Ndivyo na vitu vyenye kuhamasisha usingizi husaidia, kama vile maziwa yenye ujoto, maziwasiagi, divai kidogo, ama chai ya miti-shamba ya hops, mint, ama chamomile—lakini isiwe chai yenye kafeni.

Hata hivyo, kwa ujumla imeafikiwa, kwamba kupoa na kutulia peke yake kabla ya kwenda kitandani huenda kusitoshe. Maisha yaliyosawazishwa kwa mazoezi ya kawaida na ambayo hayana mahangaiko na kukata tamaa yasababishwayo na uchoyo, wivu, uhasama, na tamaa ya umashuhuri huchangia kuweza kupata usingizi mzuri wa usiku. Na ndivyo yalivyo maisha yasiyo na ulaji na ulevi na maisha yasiyo na kukosa furaha kunakosababishwa na ukosefu wa maadili.

Kuridhisha tamaa yetu ya kiroho kwaweza kuchangia fungu fulani muhimu katika kupata usingizi mnono, wenye kupumzisha. Itatusaidia kufahamu ulimwengu tata tunamoishi na kufuatia njia ya maisha iliyosawazika na yenye kuridhisha. Mtumishi mwenye hekima wa Mungu atutia moyo kusitawisha ufahamu wa kina na kushikilia hekima ya Yehova, kwani hili litaongoza kwenye “maisha yenye kupendeza na furaha.” Kisha aongezea hivi: “Hutakuwa na hofu uendapo kulala, nawe utakuwa na usingizi mnono usiku mzima.”—Mithali 3:21-24, Today’s English Version.

[Blabu katika ukurasa wa 18]

Watu wazima wengi huhitaji usingizi wa muda wa saa saba ama nane kila siku

[Picha katika ukurasa wa 18]

Ukosefu wa usingizi kwa kipindi kirefu kwaweza kuwa na athari zenye kudhuru

[Picha katika ukurasa wa 18]

Watu wengi wanakuwa na matatizo makubwa kupata usingizi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki