Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 8/8 kur. 16-20
  • Zile Katakombu Zilikuwa Nini?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Zile Katakombu Zilikuwa Nini?
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Historia ya Katakombu
  • Kuzuru Katakombu
  • Mchanganyiko wa Mawazo
  • Vijia vya Chini ya Ardhi vya Odessa
    Amkeni!—2010
  • Chini ya Ardhi ya Paris
    Amkeni!—1999
  • Mambo Yenye Kupendeza Jijini Roma
    Amkeni!—2001
  • Sanamu
    Amkeni!—2014
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 8/8 kur. 16-20

Zile Katakombu Zilikuwa Nini?

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA ITALIA

Katika vipitio vyenye giza-giza, zilizofichika katika sehemu za ndani za Roma ya kale, ni katakombu. Hizo ni nini hasa? Kwa nini zilijengwa?

KWA msingi, katakombu ni mahandaki yaliyochimbuliwa mwambani ili kutumiwa kuwa makaburi. Inafikiriwa kwamba neno “katakombu,” la maana isiyo hakika (yawezekana, “kwenye mashimo”), lilikuwa jina la mahali lililofafanua kaburi hususa kwenye Barabara Kuu ya Apio karibu na Roma. Hatimaye, lilitumika kwa makaburi yote ya kuchimbwa. Hata ingawa kuna katakombu nyingi katika sehemu nyingi za eneo la Mediterania, zile zilizoko Roma ndizo zinazojulikana vyema zaidi na pia ndizo kubwa kuliko zote—urefu wazo kwa ujumla wakadiriwa kuwa mamia kadhaa ya kilometa. Katakombu nyingi kufikia 60 zimepatikana, zote zikiwa kilometa chache nje ya hilo jiji la kihistoria kandokando ya barabara kuu zilizojengwa na maliwali ambazo ziliunganisha Roma na mikoa yalo.

Yaelekea kwamba katika karne ya kwanza, Wakristo Waroma hawakuwa na makaburi yao wenyewe bali walizika wafu wao kandokando ya wapagani. Kufikia katikati ya karne ya pili, wakati waliodai kuwa Wakristo tayari walikuwa wameanza kuathiriwa na mawazo ya kipagani, waumini wenye mali walitoa mahali kwa ajili ya makaburi ya “Wakristo.” Ili kutatua tatizo la nafasi bila kwenda mbali sana kutoka jijini, kuchimba kulianza.

Historia ya Katakombu

Uchimbuzi wa kwanza yaelekea ulifanywa kando ya ubavuni mwa milima au katika machimbo yaliyoachwa. “Halafu,” aeleza Ludwig Hertling na Engelbert Kirschbaum katika kitabu chao juu ya katakombu, “kazi zilianza kwenye ujia uliokuwa na kimo sawa na cha mtu. Mahandaki ya kando yalichimbwa kwenda kulia na kushoto, ambayo baadaye yangeunganishwa mwisho kabisa kwa kipitio kingine kilicho sambamba na cha kwanza. Hivyo mfumo sahili wenye miingiliano na ulioendelea kuwa mkubwa na tata zaidi uliundwa.”

Maendeleo makubwa zaidi ya yote yalikuwa wakati wa karne za tatu na nne; kufikia wakati huu, lililotokea kwa eti dini ya Kikristo lilikuwa limetiwa dosari kabisa na mafundisho na mazoea ya kipagani. Kukiwa na kule kulikoitwa eti kuongolewa kwa Konstantino katika 313 W.K., katakombu zilikuja kuwa mali ya Kanisa la Roma, na nyingine hatimaye zikawa kubwa mno. Kwa ujumla, katakombu za Kiroma zingeweza kuwa na mamia ya maelfu ya maziara, kama si mamilioni.

Wakati wa kipindi hiki makaburi yalipambwa na kupanuliwa, na vigazi vipya vya kupandia vikajengwa ili kurahisisha mfikio kwa maziara kwa ajili ya wageni wenye kuongezeka kwa wingi. Umashuhuri wa yaliyoonwa kuwa maziara ya mapapa na wafia-imani ulikuwa umeenea kwa kiwango kikubwa (hasa katika magharibi mwa Ulaya) hivi kwamba hizo katakombu zikaja kuwa vitu vya kuzuriwa na watu wengi. Kufikia kuanguka kwa Roma na yale mashambulizi ya watu wa kigeni mwanzoni mwa karne ya tano, eneo lote likawa hatari mno, na utumizi wa katakombu kuwa makaburi ukakoma.

Wakati wa karne ya nane, hayo maziara yalipata uharibifu mkubwa kwa kuwa yalichukuliwa nyara na kuporwa si tu na majeshi yaliyokuwa yakishambulia bali pia, kulingana na Hertling na Kirschbaum, na “wapatanishi wa Kiroma waliojishusha” ambao walitoa viwango vikubwa vya kumbukumbu takatifu kwa “wakuu wa nyumba za watawa Wajerumani na Wafranki walioendelea kuwa wenye pupa ya vikumbusho vya mambo ya kale ya watakatifu” ili kuongeza umashuhuri wa makanisa na makao ya watawa yao. Akiwa ameshindwa kurudisha au kukinga katakombu, Papa Paul I alibeba mingi ya mifupa iliyobaki kwa usalama ndani ya kuta za jiji, ambapo basilika kubwa zilijengwa juu ya kile kilichoaminiwa kuwa masalio ya “wafia-imani watakatifu.” Katakombu zenyewe ziliachwa na kusahauliwa.

Miongozo ya kale iliyoandikwa katika katakombu ya karne ya tano hadi ya tisa, ambayo ilitayarishwa ili kuongoza wageni kwenye maziara mashuhuri, iliandaa vidokezi vyenye thamani kwa wasomi ambao, katika karne ya 17 na halafu ya 19, walianza kutafuta, kutambulisha, na kuchunguza makaburi yaliyofichwa na magofu na mimea. Tangu wakati huo, utafiti mwingi na urudisho umefanywa, na leo yawezekana kutembelea sehemu kadhaa mahali huku kwenye kuchochea kumbukumbu.

Kuzuru Katakombu

Tuko kwenye Barabara Kuu ya Apio, barabara iliyopitiwa na mtume Paulo alipopelekwa Roma akiwa mfungwa. (Matendo 28:13-16) Hata ingawa tuko kilometa tatu tu nje ya kuta za jiji la kale, tayari tuko katika eneo wazi la mashambani, tukiwa tumezingirwa na miti yenye fahari ya msonobari na saiprasi inayokua miongoni mwa majumba ya ukumbusho na magofu ya barabara hii kuu iliyokuwa wakati mmoja yenye shughuli nyingi.

Baada ya kununua tiketi zetu za kiingilio, twateremka vigazi vyenye mwinamo hadi kina cha meta 12 hivi. Mwongozi aelezea kwamba katakombu hii imepangwa kwenye tabaka tano tofauti, ikifikia kina cha meta 30, ambapo chini yayo maji yalipatikana. Kwa hakika, Roma imezungukwa na masazo yaliyoenea ya tuff, mwamba laini na upenyekao wa kivolkeno, ulio rahisi kuuchimbua lakini wakati uleule wenye nguvu na mgumu.

Tunatembea kwenye ujia mwembamba, wenye upana wa meta moja na kimo cha meta 2.5. Zile kuta za hudhurungi nzito zimeparuzika-paruzika na ni zenye unyevu na kwa wazi bado zina ishara zilizoachwa na sururu za wafanyakazi waliochimba mahandaki haya yaliyosongamana. Hayo maziara katika pande zote mbili yalifunguliwa na kuporwa kitambo, lakini baadhi yayo bado yana vijipande vya mifupa. Tunaposonga katika giza, twatambua tumezungukwa na maelfu ya maziara.

Njia isiyo ghali na ya kutumika zaidi kuliko zote ya kuzika wafu ilikuwa kuchimba mashubaka ya kimstatili mbavuni mwa kuta, moja juu ya jingine. Mashubaka haya kwa kawaida yaliwekwa mwili mmoja lakini nyakati fulani miili miwili au mitatu. Yalifungwa kwa matofali, mabamba ya jiwe ya marumaru, au vigae vya udongo mwekundu, na kufunikwa na chokaa. Mengi hayana tarehe. Yanaweza kutambuliwa na vitu vidogo vilivyowekwa nje—sarafu au kombe za baharini zilizobandikwa katika chokaa isiyokauka au, kama vile katika Katakombu ya Prisila, mdoli mdogo uliotengenezwa kwa mfupa, yaelekea ulioachwa na wazazi waliohuzunika wakiombolezea upotezo wa mapema mno wa binti yao. Maziara mengi ni madogo mno, yakitoshea tu watoto waliozaliwa karibuni.

“Twaweza kujuaje umri wa katakombu?” twauliza. “Hakuna kukisia kuhusu hilo,” mwongozi wetu ajibu. “Mwaona alama hii?” Twainama kuchunguza ishara iliyobandikwa kwenye kigae kikubwa cha udongo mwekundu iliyotumiwa kufunika moja ya mashubaka. “Kibandiko hiki cha tofali kilibandikwa wakati kigae hiki kilipotengenezwa. Viwanda, vingi vyavyo vikiwa mali ya maliki, vilibandika habari kwenye matofali na vigae vilivyotokeza vikionyesha chimbo ambapo udongo ulitolewa, jina la karakana, mnyapara, makonsuli (mahakimu wakuu) wa mwaka huo, na kadhalika. Hili ni jambo lenye mafaa mno katika kujua tarehe hususa ya maziara. Katakombu za kale kuliko zote zilitiwa tarehe katikati mwa karne ya pili W.K., na za karibuni zaidi mwaka wa 400 W.K. hivi.”

Mchanganyiko wa Mawazo

Baadhi ya waliotumia maeneo haya walikuwa na ujuzi fulani wa Maandiko Matakatifu, kwa kuwa maziara kadhaa yamepambwa kwa mandhari za Biblia. Hata hivyo, hakuna ishara ya ibada ya Mariamu au ya vichwa vingine vilivyokuwa vya kawaida sana katika sanaa “takatifu” ya baadaye kama vile ile iitwayo eti usulubisho.

Pia twaona maumbo ambayo hayana uhusiano na Biblia. “Ni kweli,” akiri mwongozi. “Mandhari nyingi katika katakombu hizi na nyingine zilitolewa kutoka sanaa za kipagani. Waweza kupata kijimungu cha Kigiriki na Kiroma na shujaa Orfia; Kyupidi na Saike, ambao wanawakilisha hali ya nafsi katika uhai huu na ule unaofuata; mavuno ya mizabibu, mfano wa Kidayonisia unaojulikana sana wa kipindi cha furaha cha baada ya uhai. Uliochukuliwa hasa kutoka sanaa ya kisanamu, kulingana na msomi mmoja Myesuiti, Antonio Ferrua, ni unafsishaji wa vitu visivyo na uhai: ile misimu minne ikiwakilishwa na kyupidi; mandhari nyinginezo tata zikionyesha misimu minne ya mwaka, Kiangazi kikiwakilishwa na suke la mahindi na maua; na kadhalika.”

Vichwa vyenye kurudiwa-rudiwa ni: tausi, mfano wa hali ya kutoweza kufa, kwa kuwa mnofu wake ulifikiriwa kuwa safi; foeniksi wa kingano, pia akifananisha hali ya kutoweza kufa, kwa kuwa alisemekana kufa katika miale ya moto na kufufuka tena katika majivu; nafsi za wafu, zikizungukwa na ndege, maua, na matunda, zikifurahia mlo katika uhai wa baada ya kufa. Mchanganyiko halisi wa mawazo ya kipagani na Kibiblia!

Baadhi ya maandishi ni wonyesho wenye kugusa wa imani, ukielekea kuonyesha itikadi ya kwamba wafu wamelala, wakingojea ufufuo: “Aquilina alala kwa amani.” (Yohana 11:11, 14) Kinyume cha mafundisho ya Kimaaandiko, maandishi mengine yanaonyesha wazo la kwamba wafu wanaweza kusaidia au kuwasiliana na wanaoishi: “Kumbuka mume wako na watoto”; “Tuombee”; “Nawaombea”; “Niko katika amani.”

Lakini kwa nini kuna mchanganyiko huu wa wazo la Kimaandiko na la kipagani? Mwanahistoria J. Stevenson asema hivi: “Ukristo wa Wakristo fulani uliingiwa na mawazo yaliyotoka kwa upagani.” Kwa wazi, Wakristo “waaminifu” katika Roma hawakuwa wakitenda tena kwa upatano na ujuzi waliopokezwa na wanafunzi wa kweli wa Yesu.—Warumi 15:14.

Tuendeleapo na ziara yetu, uvutano uliowekwa na kujitoa kwa wafu kusiko kwa Kimaandiko unakuwa wazi zaidi. Wengi walitamani kuzikwa karibu na maziara ya mtu aliyefikiriwa kuwa mfia-imani, kukiwa na wazo kwamba kutokana na cheo chake katika raha ya kimbingu, huyo mfia-imani angeweza kuingilia, akisaidia mnyonge kupata thawabu ileile.

Wengi wanawaza kwamba katakombu zilikuwa chini tu ya jiji, lakini sivyo ilivyo. Zote ziko kilometa chache nje ya jiji. Kwa hakika katiba ya Roma, ilikataza kuzika mtu jijini. Sheria ya Twelve Tables, iliyoanzishwa katika karne ya tano K.W.K., ilitaarifu hivi: Hominem mortuum in urbe ne sepelito neve urito (Wafu hawawezi kuzikwa au kuchomwa katika jiji).

Mwongozi aonelea hivi: “Makaburi haya yalijulikana sana kwa serikali, yalijulikana sana hivi kwamba wakati wa mnyanyaso wa Maliki Valerian, wakati ambapo Wakristo walizuiwa kuingia ndani ya katakombu, Papa Sixtus 2 aliuawa alipopatikana hapa (258 W.K.).”

Tukibeta tena katika sehemu hiyo yenye vipitio vingi, twaona nuru nyangavu-nyangavu ya mchana ikimulika sehemu ya mwisho ya ujia, na twatambua kwamba ziara yetu imefikia mwisho. Twamuaga mwongozi wetu, tukimshukuru kwa habari yenye kupendeza, na tunapopanda kigazi kingine chenye mwinamo ili kurudi juu, tunachochewa kukumbuka yale tuliyoona.

Je, haya yaweza kuwa masalio ya Ukristo wa kweli? Kwa hakika sivyo. Maandiko yalitabiri kwamba muda mfupi baada ya kifo cha mitume, kutiwa dosari kwa mafundisho yaliyofundishwa na Yesu na wanafunzi wake kungezuka. (2 Wathesalonike 2:3, 7) Kwa kweli, uthibitisho ambao tumeona, wa ibada ya wafu na ya wafia-imani na wazo la nafsi isiyoweza kufa, ni ushahidi wenye nguvu, si wa imani iliyo na msingi katika mafundisho ya Yesu, bali badala yake ushahidi wa athari zenye nguvu za kipagani zilizokuwa tayari miongoni mwa Wakristo Waroma waasi-imani katika karne ya pili hadi ya nne ya Wakati wa Kawaida wetu.

[Blabu katika ukurasa wa 18]

Yaliyofikiriwa kuwa maziara ya mapapa yalikuja kuwa vitu vya kuzuriwa na watu wengi

[Blabu katika ukurasa wa 19]

Katakombu moja ina tabaka tano tofauti- tofauti, ikifikia kina cha meta 30

[Blabu katika ukurasa wa 20]

Katakombu zaonyesha athari ya uasi-imani uliotabiriwa kutoka kwa kweli ya Biblia

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kulia: Ndege fulani walitumiwa kama mifano ya hali ya kutoweza kufa

[Hisani]

Archivio PCAS

Mbali kulia: Plani ya vipitio vingi vya baadhi ya katakombu za Kiroma

Chini kulia: Kibandiko cha bibi-arusi, chenye mafaa kwa ajili ya kutia tarehe maziara

[Hisani]

Soprintendenza Archeologica di Roma

Chini: Kaburi la mapapa

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki