Ile Shule ya Kiafrika Ilifunza Nini?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA GHANA
ETI shule ya Kiafrika? Baadhi ya watu wa Magharibi huenda wakashangaa kujua kwamba mpango kama huo kwa kweli ulikuwako katika nyakati za kale. Kwa kusikitisha, ile sinema yenye kuonyesha Mwafrika akiwa mtu wa jamii duni akiwa amebeba fumo bado yabaki akilini mwa watu. Wengi hawawezi kuwazia jinsi Mwafrika wa kale angeweza kwa njia yoyote kuwa aliyeelimika.
Ni kweli kwamba Waafrika waliolelewa katika jamii za kitamaduni hawakupata mazoezi ya kusoma vitabu na kujifunza rasmi. Hata hivyo, muda mrefu kabla ya mfumo rasmi wa elimu wa Kiulaya kuletwa katika bara hili, jamii nyingi za Kiafrika zilikuwa na mifumo ya kielimu yenye matokeo ambayo ilisaidia watoto kuwa tayari kutenda na kusitawi katika tamaduni zao. Kwa kielelezo, ebu fikiria elimu ya Waakani, watu wa Ghana wasemao Kitwi.
Elimu ya Nyumbani
Miongoni mwa Waakani, nyumbani kulitumika kama darasa la msingi. Elimu ya mtoto ilianza alipokuwa akijifunza usemi kutoka kwa wazazi wake. Wakati uleule, pia alipokea masomo yake ya kwanza ya adabu. Kwa kielelezo, wakati mgeni alikuwa akisalimu mtoto, huyo mtoto angefunzwa itikio lifaalo na la upole. Baadaye, wakati mtoto alitumwa kupeleka ujumbe, angeambiwa njia ya upole ambayo angepeleka ujumbe wowote uliowasilishwa.
Falsafa ya kielimu ya Waakani ilikuwa sawa na ile iliyoonyeshwa katika Biblia kwenye Mithali 22:6: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.” Wazazi, hasa baba, walipendezwa na kulea watoto. Ikasema methali fulani ya Waakani: “Mtoto asipofanana na mama, afanana na baba yake.”
Kadiri mtoto alivyokua, ndivyo na kina cha elimu yake. Masomo kuhusu maisha yaliwasilishwa, si kupitia vitabu, bali kupitia hadithi za kuwazia, hadithi kama zile kuhusu buibui wa kisakale aliyeitwa Kwaku Ananse. Watoto walivipenda visakale hivi wee! Mapema katika upepo mwanana wa jioni, ama usiku wenye mbalamwezi na baridi, wao wangekaa kuzunguka moto na kwa moyo kufurahia hadithi hizi za ushindi na ushinde.
Hadithi moja maarufu ilisimulia kwamba Ananse alisafiri kwa mapana na marefu duniani ili kuweka hekima yote ya ulimwengu katika nyungu fulani. Utume wake ukionekana kukamilika, aliamua kuangika hiyo nyungu juu sana kwenye mti fulani, hivi kwamba hakuna yeyote angeweza kuifikilia hekima hii. Alianza mpando mgumu juu ya huo mti, nyungu yenye kusheheni hekima ikiwa imefungwa kwa uzi na kuning’inia tumboni mwake. Alipokuwa aking’ang’ana, kifungua mimba wake, Ntikuma, alitokea na kumwita Ananse: “Aha, baba, Baba! Ni nani aliyepanda mti nyungu ikiwa kwenye tumbo? Kwa nini usiiweke mgongoni ili upate nafasi ya kuparamia vizuri?” Ananse alimtazama mwanaye na kupaaza: “Wathubutuje kunifundisha?”
Lakini sasa ilikuwa wazi kwamba hekima fulani bado haikuwa ndani ya nyungu yake! Kwa kughadhabishwa na ung’amuzi huu, Ananse aliivunja hiyo nyungu, ikapasuka na kutawanya-tawanya hekima yote. Wale waliokuwa wa kwanza kufika pale wakawa wale wenye hekima kupita wote. Funzo: Hakuna aliye na uwezo wa kufanya hekima kuwa mali yake. Waakani basi wangeweza kusema hivi: “Mtu mmoja hafanyizi baraza.”—Linganisha Mithali 15:22; 24:6.
Stadi za Maishani
Elimu ya Waakani pia ilitia ndani mazoezi katika stadi za maishani. Wavulana wengi walifuata kazi-maisha za baba zao—kwa kawaida ukulima. Lakini kulikuwa na stadi nyinginezo za kujifunza, kama vile uwindaji, ugemaji, na ufundi kama vile kufuma vikapu. Kwa ufundi uliohitaji ustadi mwingi, kama vile kuchonga mti ama kufuma, wavulana walizoezwa na wale wenye umahiri wa kazi. Na wasichana je? Mazoezi yao hasa yalikazia stadi za nyumbani kama vile kuzidua mafuta ya mimea, kutengeneza sabuni na ufinyanzi, kusokota pamba, na mambo mengine yafananayo na hayo.
Sayansi haikupuuzwa katika “taaluma” ya shule ya kitamaduni. Ujuzi kuhusu miti-shamba yenye kutibu, kuitayarisha na utumiaji, ulipitishwa na baba hadi kwa mwana ama na mzazi-mkuu hadi kwa mjukuu. Mtoto pia alijifunza kuhesabu nambari, kwa kutumia vidole vyake pamoja na gololi, mawe, na alama kwenye vijiti. Michezo kama vile oware na kucheza dama iliboresha stadi za kuhesabu.
Kwa kuhudhuria vipindi vya mahakama ya hadharani, kijana Mwakani pia angepata ufahamu wenye kina kuhusu mifumo ya kisiasa na kimahakama. Maziko pamoja na vipindi vya msherehekeo zilikuwa fursa za kufyonza nyimbo za maziko, ushairi, historia, muziki, upigaji-ngoma, na uchezaji-dansi wa mahali hapo.
Daraka kwa Jumuiya
Miongoni mwa Waakani, mtoto hakutengwa na watu. Mapema maishani alifahamishwa daraka lake kwa jumuiya. Alijifunza masomo yake ya kwanza kuhusiana na hili alipojiunga na marika wake kucheza. Katika maisha ya baadaye angeshiriki katika utendaji wa kishirika kama vile kazi ya kijumuiya. Alipotenda kwa kukosa adabu, nidhamu ingetolewa, si tu na wazazi wake lakini na mshiriki yeyote wa jumuiya mwenye umri mkubwa. Kwa hakika, ilichukuliwa kuwa daraka la kimaadili la mtu mzima kutoa nidhamu kwa mtoto yeyote aliyekuwa na adabu mbaya.
Nidhamu kama hiyo ilipokewa vizuri kwa sababu watoto walifunzwa kuwaheshimu watu wazima. Kwa hakika, Waakani walizoea kusema hivi: “Mwanamke mzee si nyanya wa mtu mmoja tu.” Kwa hivyo staha na kutumikia walio wazee-wazee ulikuwa wajibu. Na mtoto yeyote ambaye bila sababu ifaayo, akikataa kutumikia mtu mzima angeripotiwa kwa wazazi wake.
Elimu ya Kidini
Waakani walikuwa wa kidini sana, wakiwa na mtazamo wa kicho kuelekea asili na ulimwengu wote mzima usiojulikana kwao. Kweli, wao walikuwa wenye kuabudu miungu mingi, wakiamini katika miungu mingi. Hata hivyo, Waakani waliamini katika kuwako kwa mmoja Aliye Mkuu. (Warumi 1:20) Neno la Waakani la “Mungu,” mungu yeyote, ni onyame. Hata hivyo, kwa Waakani neno hilo lilionekana kutotosha kumfafanua Muumba. Hivyo, walimwita Onyankopɔn, kumaanisha “Mungu Mmoja Aliye Mkuu.”
Miungu wadogo waliabudiwa kwa kuitikadi kwamba ulikuwa mpango wa Mungu Mmoja Aliye Mkuu. Akilini mwao waliifananisha na jinsi chifu mkuu alivyotumikiwa kupitia kwa chifu wadogo wa kitarafa. Hali iwavyo, kila mtoto wa Kiakani alifunzwa dini hii.
Elimu ya Kitamaduni Leo
Katika miaka ya majuzi mamilioni ya Waafrika wamehamia majiji makubwa ambapo maagizo rasmi ya darasani yamechukua mahali pa njia za kitamaduni za kuelimisha. Hata hivyo, shule ya kitamaduni ya Kiafrika yaendelea kusitawi katika baadhi ya jumuiya, hasa katika maeneo ya mashambani. Ala, baadhi ya Waafrika pia wamepata manufaa za aina zote mbili za elimu ya kitamaduni na kirasmi!
Kwa kielelezo, ebu fikiria mhudumu Mkristo katika Ghana anayeitwa Alfred. Licha ya kufunzwa elimu rasmi, yeye ana staha kwa hali nyingi za maisha ya kitamaduni. Asema Alfred: “Wengi wa watu wa kabila langu ambao hawajui kusoma, wajapokuwa na mazoezi yao ya kitamaduni tu, ni walimu wazuri sana kuhusu hali mbalimbali za uhalisi wa maisha. Kufanya kazi pamoja na Wakristo wenzangu miongoni mwao kumenifunza njia nyingi zenye matokeo za kutoa ujumbe wangu kwa njia sahili, yenye kueleweka na kila mtu. Hivyo naweza kuwafikia watu wa malezi ya kitamaduni pamoja na wale wenye elimu rasmi. Mara nyingi, mimi huchukua methali fulani ama kielezi kitumiwacho na wenyeji hawa, hukisanifisha, na kukiingiza katika mihadhara yangu ya Biblia. Mara nyingi hili hutokeza mshangilio wenye idili kutoka kwa wasikilizaji! Hata hivyo, kwa kweli sifa yapasa iwaendee wanaume na wanawake hawa waliozoezwa kitamaduni.”
Kwa wazi basi, shule ya Kiafrika ina sehemu nyingi zenye kupendeza na yastahiki staha, si kudharauliwa. Huenda haikutokeza maajabu ya kitekinolojia, lakini ilitokeza muundo wa familia wenye nguvu, hisia ya kufanya mambo kijumuiya, watu wenye akili chonjo, hali yenye kupendeza ya ucheshi, na roho ya ukarimu na ukaribishaji. Basi si ajabu, wengi wa Waafrika waishio jijini hujitahidi kudumisha uwasiliano na watu wa ukoo waishio mashambani kwa kuwazuru pindi kwa pindi. Pindi kama hizo huwa hazikosi duru zenye kuchekesha. Wakaa jijini mara nyingi hujikwaa kuhusu desturi za kitamaduni. Kwa kielelezo, mara nyingi hawajui kwamba wanaposalimia kikundi cha watu kwa mkono, njia ‘ifaayo’ ni kusalimu kutoka kulia hadi kushoto. Bado, ziara kama hizo zaweza kuburudisha vikundi vyote.
Hata hivyo, ni lazima ikubaliwe kwamba ingawa shule ya kitamaduni ya Kiafrika ilifunza kicho na ujitoaji, haikutoa ujuzi wenye kutoa uhai kuhusu Yehova na Mwanaye, Yesu Kristo. (Yohana 17:3) Mashahidi wa Yehova wana pendeleo la kufanya kazi miongoni mwa Waakani na makabila mengine ya Kiafrika ili kuandaa ujuzi huu muhimu. Wao wamefunza maelfu ya Waafrika wanaokosa elimu rasmi ya kusoma na kuandika ili kwamba waweze kujisomea Neno la Mungu wao wenyewe. Kwa wale “wenye uhitaji wa kiroho,” hii ndiyo elimu iliyo muhimu sana mtu angeweza kupata.—Mathayo 5:3, New World Translation.
[Picha katika ukurasa wa 25]
Miongoni mwa Waakani, mtoto alifunzwa kung’amua daraka lake kwa jumuiya
[Picha katika ukurasa wa 26]
Majumba ya Ufalme ya Mashahidi wa Yehova huandaa madarasa ya kujifunza kusoma na kuandika