Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 2/22 kur. 4-9
  • Kisasi cha Vijiumbe-Maradhi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kisasi cha Vijiumbe-Maradhi
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ushindi Ulionekana Kuwa Hakika
  • Maradhi ya Kale Yarudi
  • Maradhi Mapya Yenye Kuangamiza
  • Kwa Nini Maradhi Mapya Yanazuka?
  • Mapungukio ya Sayansi ya Kitiba
  • Hali ya Mambo Leo
  • Magonjwa ya Kuambukiza Katika Karne ya 20
    Amkeni!—1997
  • Jinsi Viini Sugu Vinavyoibuka Tena
    Amkeni!—2003
  • Matokeo ya Jitihada za Kupambana na Magonjwa
    Amkeni!—2004
  • Ulimwengu Usio na Magonjwa
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 2/22 kur. 4-9

Kisasi cha Vijiumbe-Maradhi

KARNE ya 20 imeona maendeleo ya ajabu katika sayansi ya kitiba. Kwa maelfu ya miaka, binadamu wameelekea kutokuwa na uwezo kabisa dhidi ya pigo la vijiumbe-maradhi vyenye kufisha. Lakini mambo yalianza kubadilika katikati mwa miaka ya 1930 wakati ambapo wanasayansi walivumbua sulfanilamidi, kitu cha kwanza ambacho kingeshinda bakteria bila ya kumwumiza vibaya mtu aliyeambukizwa.a

Katika miaka iliyofuata, wanasayansi walitokeza dawa mpya zenye nguvu ya kupigana na maradhi yenye kuambukiza—klorokwini kushambulia malaria na viuavijasumu kushinda mchochota wa pafu, homa isababishayo vipele vyekundu ngozini na kifua kikuu. Kufikia 1965 zaidi ya bidhaa tofauti-tofauti 25,000 za viuavijasumu zilikuwa zimetokezwa. Wanasayansi wengi walifikia mkataa kwamba maradhi yasababishwayo na bakteria hayakuwa tena ya hangaiko kubwa au ya upendezi wa utafiti. Kwa vyovyote, ya nini kuchunguza maradhi ambayo hivi karibuni hayatakuwapo tena?

Katika nchi zilizositawi za ulimwengu, chanjo mpya zilipunguza kwa kutazamisha kiwango cha surua, matubwitubwi, na surua ya Kijerumani. Kampeni kubwa ya chanjo, iliyoanzishwa katika 1955, ilikuwa na mafanikio sana hivi kwamba visa vya hayo maradhi katika Ulaya Magharibi na Amerika Kaskazini vilipungua kutoka 76,000 mwaka huo hadi chini ya 1,000 mwaka 1967. Ndui, maradhi makubwa yenye kuua, yalimalizwa ulimwenguni pote.

Karne hii imeona pia kuvumbuliwa kwa hadubini ya elektroni, kifaa kilicho na nguvu mno hivi kwamba huwezesha wanasayansi kuona virusi ambavyo ni vidogo mno mara milioni moja kuliko ukucha wa kidole cha mtu. Hadubini hizo, pamoja na maendeleo mengine ya kitekinolojia, yamefanya iwezekane kufahamu na kupigana na maradhi yenye kuambukiza zaidi ya wakati mwengineo wote.

Ushindi Ulionekana Kuwa Hakika

Likiwa tokeo la ugunduzi huu, jamii ya kitiba ilijawa na uhakika. Vijiumbe-maradhi vya maradhi yenye kuambukiza vilikuwa vikishindwa na dawa za kisasa. Kwa hakika ushindi wa sayansi juu ya vijiumbe-maradhi ungekuwa wa haraka, wenye kukata maneno, kamili! Ikiwa tiba kwa maradhi hususa haikupatikana wakati huo, ingepatikana karibuni.

Mapema kama 1948, katibu wa serikali wa Marekani George C. Marshall alijivuna kwamba kuyashinda maradhi yenye kuambukiza kulikuwa dhahiri. Miaka mitatu baadaye, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilidai kwamba malaria ya Asia ingekuwa maradhi “yasiyo na umaana mkubwa tena.” Kufikia katikati mwa 1960, itikadi kwamba enzi ya tauni na maradhi yenye kuambukiza ilikuwa imepita ilienea sana hivi kwamba mkuu wa afya wa Marekani William H. Stewart aliwaambia maofisa wa afya kwamba wakati ulikuwa umetimia wa kutohangaikia tena maradhi ya kuambukiza.

Maradhi ya Kale Yarudi

Hata hivyo, wakati wa kutohangaikia maradhi ya kuambukiza haukuwa umetimia hata kidogo. Vijiumbe-maradhi havikutoweka kutoka sayari kwa sababu tu sayansi ilikuwa imevumbua dawa na chanjo. Mbali na kushindwa, vijiumbe-maradhi vyenye kuua vijulikanavyo sana vilirudi kwa kisasi! Kwa kuongezea, vijiumbe-maradhi vingine vyenye kufisha vilizuka—vijiumbe-maradhi ambavyo mbeleni havikujulikana na madaktari. Hivyo, vijiumbe-maradhi vyote vya zamani na vipya vinaenea haraka sana, vikitisha, kutesa, au kuua mamilioni yasiyohesabika ya watu ulimwenguni pote.

Maradhi yenye kuua ambayo wakati mmoja yalifikiriwa kuwa chini ya udhibiti yamezuka tena, yakiwa yenye kufisha zaidi ya wakati mwingineo wote na magumu zaidi kutibu kwa dawa. Kielelezo kimoja ni kifua kikuu (TB). WHO lilitaarifu majuzi hivi: “Tangu 1944, dawa za TB zimetumiwa sana katika Japani, Amerika Kaskazini na Ulaya ili kupunguza kwa kutazamisha visa vya TB na kifo. Hata hivyo, jitihada za kudhibiti TB katika nchi ambazo hazijasitawi sana zimepuuzwa, . . . ikiwezesha hayo maradhi yarudi kwa nchi tajiri kwa aina hatari zaidi, zenye kukinza madawa mengi.” Leo TB, kwa kawaida ikisabasishwa na bakteria zipatikanazo hewani ambazo hukaa mapafuni, huua watu milioni tatu hivi kila mwaka—zaidi ya 7,000 kila siku. Kufikia mwaka 2005, kiwango cha kifo kinaweza kuongezeka hadi milioni nne kila mwaka.

Wauaji wengine wa kale pia wanaongezeka. Kipindupindu sasa kimeenea sana katika sehemu nyingi za Afrika, Asia, na Amerika ya Latini; hicho hupata na kuua idadi zenye kuongezeka za watu. Aina mpya kabisa imejitokeza katika Asia.

Kipingapopo, kinachoenezwa na mbu Aëdes aegypti, kinaongezeka kwa haraka pia; hicho sasa hutisha watu bilioni 2.5 katika zaidi ya nchi 100 ulimwenguni pote. Tangu miaka ya 1950, aina mpya zaidi yenye kufisha ya maradhi yenye kusababisha mvujo wa damu imezuka na kuenea kotekote katika nchi za Kitropiki. Inakadiriwa kwamba hayo huua karibu watu 20,000 kila mwaka. Sawa na maradhi mengi yenye kuenezwa na virusi, hakuna chanjo za kulinda dhidi ya hayo maradhi na hakuna dawa ya kuyatibu.

Malaria, ambayo sayansi wakati mmoja ilitumaini kumaliza, sasa huua watu milioni mbili hivi kila mwaka. Vyote vimelea vya malaria pamoja na mbu ambao huvibeba vimeendelea kuwa vigumu zaidi kuua.

Maradhi Mapya Yenye Kuangamiza

Labda maradhi yajulikanayo sana kati ya maradhi ambayo yamezuka hivi majuzi kutaabisha jamii ya kibinadamu ni UKIMWI. Maradhi haya yasiyoweza kutibiwa yanasababishwa na kirusi ambacho hakikujulikana miaka 12 hivi iliyopita. Lakini, kufikia mwishoni mwa 1994 idadi ya watu ambao waliambukizwa na hivyo virusi ilikuwa kati ya milioni 13 na 15.

Maradhi mengine ambayo mbeleni hayakutambuliwa yatia ndani virusi-hanta vya mapafu. Yakienezwa na panya wa shambani, yalitokea kusini-magharibi mwa Marekani na kuthibitika kuwa hatari mno katika nusu ya visa vilivyoripotiwa. Aina mbili za homa ya kutokwa damu—zote mpya, zote zenye kuua—zimetokea katika Amerika Kusini. Maradhi mengine yenye kuogofya yamezuka pia—virusi vyenye majina ya kigeni, yasiyo ya kawaida—Lassa, Bonde la Ufa, Oropouche, Rocio, Q. Guanarito, VEE, ndui ya nyani, Chikungunya, Mokola, Duvenhage, LeDantec, kirusi cha Msitu wa Kyasanur, kirusi cha Msitu wa Semliki, Crimean-Congo, O’nyongnyong, Sindbis, Marburg, Ebola.

Kwa Nini Maradhi Mapya Yanazuka?

Kukiwa na ujuzi na mali yote ambayo sayansi ya kitiba ya kisasa inayo, kwa nini vijiumbe-maradhi vyenye kuua vinathibitika kuwa vigumu sana kuvishinda? Sababu moja ni mwendo ulioongezeka wa jamii ya leo. Usafiri wa kisasa waweza kufanya ugonjwa ulioenea mahali fulani uenee duniani pote. Usafiri wa ndege hufanya kuhama kwa maradhi yenye kufisha kuwe rahisi, yakiwa ndani ya mtu aliyeambukizwa, kutoka sehemu moja ya ulimwengu hadi sehemu nyingineyo yote ya ulimwengu kwa muda wa saa chache tu.

Sababu ya pili ambayo huchochea kuenea kwa vijiumbe-maradhi, ni ukuzi wenye kuongezeka wa idadi ya watu ulimwenguni—hasa majijini. Bila shaka, takataka hutokezwa katika majiji. Takataka huwa na viwekeo vya plastiki na magurudumu yaliyojaa maji ya mvua. Katika nchi za Kitropiki, hilo hutokeza kuzaana kwa mbu ambao huwa vichukuzi vya maradhi yenye kuua kama vile, malaria, homa-njano, na kipingapopo. Kwa kuongezea, kama tu vile msitu wenye miti mingi uwezavyo kuchochea moto, ndivyo idadi zilizosongamana ziandaavyo hali zinazofaa kwa ueneaji wa haraka wa kifua kikuu, mafua makali, na maradhi mengine yapitishwayo hewani.

Sababu ya tatu ya kurudi kwa vijiumbe-maradhi ni mabadiliko katika mwenendo wa binadamu. Vijiumbe-maradhi ambavyo hupitishwa kingono vimeongezeka na kuenea likiwa tokeo la kiwango kisicho na kifani cha mahusiano ya ngono ya wenzi kadhaa, ambayo yamekuwa ndiyo kitabia cha sehemu ya mwisho ya karne ya 20. Kielelezo kimoja ni kuenea kwa UKIMWI.b

Sababu ya nne inayofanya vijiumbe-maradhi vyenye kuua vithibitike kuwa vigumu sana kushindwa ni kwamba mwanadamu ameingilia misitu mikubwa na misitu ya kitropiki. Mtungaji Richard Preston ataarifu hivi katika kitabu chake The Hot Zone: “Kuzuka kwa UKIMWI, Ebola, na virusi vingi vya misitu ya kitropiki kwaonekana kuwa tokeo la kiasili la kuharibu mazingira ya kitropiki. Virusi vinavyozuka vinatoka katika sehemu za dunia zilizoharibiwa kimazingira. Vingi vyavyo hutoka katika kingo zilizoharibiwa za misitu ya kitropiki . . . Misitu ya kitropiki ni hifadhi kubwa sana za uhai kwenye sayari, zikiwa na aina nyingi zaidi za mimea na wanyama ulimwenguni. Misitu ya kitropiki pia ni hifadhi kubwa zaidi za virusi ulimwenguni, kwa kuwa viumbe-hai vyote huwa na virusi.”

Hivyo binadamu wamekuwa karibu sana na wadudu na wanyama wenye halijoto isiyotegemea mazingira ambao ndani yao virusi hukaa, kuzaana, na kufa bila kuleta madhara. Lakini kirusi “kirukapo” kutoka kwa mnyama hadi kwa binadamu, hicho kirusi chaweza kuwa chenye kufisha.

Mapungukio ya Sayansi ya Kitiba

Sababu nyinginezo zinazofanya maradhi yenye kuambukiza yarudi na kuongezeka zahusiana na sayansi ya kitiba yenyewe. Bakteria nyingi sasa zashinda viuavijasumu ambavyo viliziua mbeleni. Kwa kushangaza, viuavijasumu vyenyewe vimesaidia kutokeza hali hii. Kwa kielelezo, ikiwa kiuavijasumu huua asilimia 99 ya bakteria zenye kudhuru ndani ya mtu aliyeambukizwa, asilimia moja iliyosalimika ambayo ilikinza kiuavijasumu yaweza sasa kukua na kuzaana kama aina yenye nguvu ya magugu katika shamba lililolimwa hivi majuzi.

Wagonjwa huchochea hilo tatizo wanapokosa kumaliza kiasi cha viuavijasumu walichoandikiwa na daktari wao. Huenda wagonjwa wakaacha kumeza tembe mara tu wanapoanza kuhisi vyema zaidi. Ingawa huenda vijiumbe-maradhi dhaifu zaidi viliuawa, vyenye nguvu zaidi husalimika na kuzaana kimya-kimya. Mnamo majuma machache, hayo maradhi yanatokea tena, lakini wakati huu ni vigumu zaidi, au haiwezekani, kuyatibu kwa dawa. Aina hizi za vijiumbe-maradhi zenye kukinza dawa zinaposhambulia watu wengine, tatizo zito zaidi la afya ya umma hutokea.

Wastadi kwenye shirika la WHO walitaarifu hivi majuzi: “Ukinzaji [dhidi ya viuavijasumu na vitu vinginevyo vya kuua vijiumbe-maradhi] umeenea sana katika nchi nyingi na ukinzaji wa dawa nyingi huacha madaktari wakielekea kutoweza kabisa kutibu kwa mafanikio idadi inayoongezeka ya maradhi. Katika hospitali pekee, maambukizo yakadiriwayo kuwa milioni moja hutukia kila siku ulimwenguni pote, na mengi yayo ni yenye kukinza dawa.”

Utiaji-damu mishipani, ambao unatumiwa kwa kuendelea tangu vita ya ulimwengu ya pili, umesaidia pia kueneza maradhi yenye kuambukiza. Licha ya jitihada za sayansi za kuhakikisha damu haina vijiumbe-maradhi vyenye kufisha, utiaji-damu mishipani umechangia kwa njia kubwa sana kuenezwa kwa mchochota wa ini, cytomegalovirus, bakteria yenye kukinza viuavijasumu, malaria, homa-njano, maradhi ya Chagas, UKIMWI, na maradhi mengine yenye kuogofya.

Hali ya Mambo Leo

Ingawa sayansi ya kitiba imepata ujuzi mwingi sana katika karne hii, kunabaki mafumbo mengi. C. J. Peters huchunguza vijiumbe-maradhi hatari kwenye Vitovu vya Kudhibiti Maradhi, maabara kuu zaidi ya umma ya Marekani. Katika mahojiano ya Mei 1995, yeye alisema hivi kuhusu Ebola: “Hatujui kwa nini ni yenye kumdhuru mwanadamu sana hivyo, na hatujui inachofanya [au] mahali ilipo, wakati haisababishi magonjwa haya yaliyoenea sana. Hatuwezi kuipata. Hakuna familia nyingineyo ya kirusi . . . ambayo hatuna ufahamu kuihusu kama hii.”

Hata wakati ambapo kuna ujuzi wa kitiba wenye matokeo, dawa, na chanjo za kupigana na maradhi, kuzitumia kwa wale wanaozihitaji hutaka fedha. Mamilioni huishi katika umaskini. World Health Report 1995 ya WHO yataarifu hivi: “Umaskini ndio sababu kuu inayofanya watoto wasichanjwe, maji safi na usafi usiandaliwe, na dawa zenye kutibu na matibabu mengineyo yasipatikane . . . Kila mwaka katika ulimwengu unaositawi watoto milioni 12.2 walio chini ya umri wa miaka 5 hufa, wengi wao kutokana na visababishi ambavyo vingaliweza kuzuiwa kwa kiasi kidogo mno cha fedha. Wanakufa sanasana kwa sababu watu hawajali hali yao, na zaidi ya yote wanakufa kwa sababu wao ni maskini.”

Kufikia 1995, maradhi yenye kuambukiza na vimelea vilikuwa wauaji wakubwa zaidi ulimwenguni, vikimaliza uhai wa watu milioni 16.4 kila mwaka. Kwa kuhuzunisha, mamilioni ya watu yasiyohesabika huishi katika hali ambazo zinafaa kwa kuzuka na kuenea kwa vijiumbe-maradhi vyenye kufisha. Fikiria hali yenye kuomboleza leo. Zaidi ya watu bilioni moja huishi katika umaskini wa kupita kiasi. Nusu ya idadi ya watu ulimwenguni hukosa kupata kwa ukawaida matibabu ya kitiba na dawa za muhimu. Kwenye barabara za majiji makubwa yaliyochafuliwa mamilioni ya watoto walioachwa huzurura, wengi wao wakijidunga dawa za kulevya na kupiga ukahaba. Mamilioni ya wakimbizi wanadhoofika katika kambi zisizo safi kati ya kipindupindu, kuhara damu, na maradhi mengineyo.

Katika vita kati ya mwanadamu na vijiumbe-maradhi, hali zimeendelea kupendelea vijiumbe-maradhi.

[Maelezo ya Chini]

a Sulfanilamidi ni msombo wa kifuwele ambao kutoka kwao dawa za salfa hufanyizwa katika maabara. Dawa za salfa zaweza kuzuia kukua kwa bakteria, zikiruhusu mifumo ya kinga ya mwili iue bakteria.

b Vielelezo vingine vya maradhi yenye kupitishwa kingono: Ulimwenguni pote kuna watu wapatao 236 milioni walioambukizwa trichomoniasis na watu 162 milioni hivi wenye maambukizo ya chlamydial. Kila mwaka kuna visa vipya vipatavyo 32 milioni vya chunjua ya viungo vya uzazi, 78 milioni vya kisonono, 21 milioni vya herpes ya viungo vya uzazi, 19 milioni vya kaswende, na milioni 9 vya chancroid.

[Blabu katika ukurasa wa 6]

“Katika hospitali pekee, maambukizo yakadiriwayo kuwa milioni moja hutukia kila siku ulimwenguni pote, na mengi yayo ni yenye kukinza dawa.” Shirika la Afya Ulimwenguni

[Sanduku katika ukurasa wa7]

Vijiumbe-Maradhi Vinapokinza

Kijiumbe-maradhi kidogo kinachoitwa bakteria “kina uzani wa gramu chache mno kama 0.00000000001. Nyangumi-Samawi ana uzani wa gramu 100,000,000 hivi. Hata hivyo, bakteria yaweza kumwua nyangumi.”—Bernard Dixon, 1994.

Miongoni mwa bakteria zinazohofiwa kuliko zote zipatikanazo hospitalini ni aina zenye kukinza dawa za Staphylococcus aureus. Aina hizi hupata wagonjwa na watu waliodhoofika, zikisababisha maambukizo mabaya mno ya damu, mchochota wa pafu, na mshtuko mbaya mno. Kulingana na jumla moja, staphylococcus huua watu 60,000 hivi katika Marekani kila mwaka—wengi kuliko wale ambao hufa katika aksidenti za magari. Kwa kipindi cha miaka kadhaa, aina hizi za bakteria zimekuwa zenye kukinza viuavijasumu hivi kwamba kufikia 1988 kulikuwa na kiuavijasumu kimoja tu kilichokuwa na matokeo dhidi yazo, ile dawa vancomycin. Hata hivyo, mara ripoti za aina zenye kukinza vancomycin zikaanza kuzuka kutoka kotekote ulimwenguni.

Lakini, hata wakati viuavijasumu vifanyapo kazi vipaswayo kufanya, matatizo mengine yaweza kutokea. Katikati mwa 1993, Joan Ray alienda hospitali katika Marekani kwa ajili ya upasuaji wa kawaida. Alitarajia kurudi nyumbani baada ya siku chache tu. Badala ya hivyo, alilazimika kubaki hospitalini kwa siku 322, sababu hasa ikiwa maambukizo aliyopata baada ya upasuaji. Madaktari walipigana na hayo maambukizo kwa kiasi kingi cha viuavijasumu, kutia ndani vancomycin, lakini vijiumbe-maradhi vilikinza. Joan asema hivi: “Singeweza kutumia mikono yangu. Singeweza kutumia miguu yangu. . . . Singeweza hata kuchukua kitabu kukisoma.”

Madaktari waling’ang’ana kupata kujua kwa nini Joan bado alikuwa mgonjwa baada ya miezi mingi ya matibabu ya viuavijasumu. Matokeo ya maabara yalionyesha kwamba zaidi ya ambukizo la staphylococcus, Joan alikuwa na aina nyingine ya bakteria katika mfumo wake—enterococcus yenye kukinza vancomycin. Kama jina hilo lidokezavyo, bakteria hii haikudhuriwa na vancomycin; ilielekea pia kuwa na kinga dhidi ya kila kiuavijasumu kinginecho chote.

Kisha madaktari wakajua jambo ambalo liliwashangaza mno. Hiyo bakteria haikukinza tu dawa ambazo zingeiua lakini, kinyume cha walivyotarajia, hasa ilitumia vancomycin ili kusalimika! Daktari wa Joan, mtaalamu wa maradhi yenye kuambukiza, alisema: “[Hizo bakteria] zahitaji vancomycin hiyo ili kuzaana, zikiikosa hazitaongezeka. Kwa hiyo, katika maana fulani, zinatumia vancomycin kama chakula.”

Madaktari walipoacha kumpa Joan vancomycin, hizo bakteria zilikufa, na Joan akapata nafuu.

[Picha katika ukurasa wa 8]

Vijiumbe-maradhi husitawi wagonjwa wanapotumia viuavijasumu isivyofaa

[Picha katika ukurasa wa 9]

Utiaji-damu mishipani hueneza vijiumbe-maradhi vyenye kufisha

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki