Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 3/8 kur. 24-26
  • Desturi ya Kale ya Waamerika Wahindi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Desturi ya Kale ya Waamerika Wahindi
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuzuru Eneo Lililotengwa la Waamerika Wahindi
  • Kukusanya Vichanganyiko
  • Hiyo Taratibu
  • Taratibu ya Kipekee ya Kutia Moto
  • Amkeni! Liliokoa Uhai wa Mtoto Aliye Tumboni
    Amkeni!—2010
  • Biblia Inabadili Maisha
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2011
  • Shangilia Katika Tumaini
    Amkeni!—2006
Amkeni!—1996
g96 3/8 kur. 24-26

Desturi ya Kale ya Waamerika Wahindi

HAIDHURU unaenda wapi ulimwenguni, utapata kwamba kila mahali pana aina zapo za sanaa za kidesturi. Picha zilizochorwa, visanamu, vitu vilivyochongwa vya mbao, vyombo vya udongo, au vitu vinginevyo vyaweza kwa kawaida kupatikana katika maduka ya zawadi na ya vitu vya thamani. Je, umepata kununua vyovyote vya vitu hivi ili kupamba nyumba yako? Ikiwa ndivyo, kwa nini usiangalie uone mahali ambapo kitu hicho kilitengenezwa hasa. Usishangae ukipata kwamba kilitengenezwa katika nchi nyingine.

Kwa karne nyingi mafundi wamechonga herufi za majina yao chini ya vyombo vyao ili kuonyesha ni nani waliovitengeneza. Hata hivyo, leo yaelekea sana utapata kibandiko au muhuri unaoonyesha kwamba kitu hicho, kimefanyizwa kwa mashine, si kwa mikono. Vifanano hivyo vya kutengenezwa na mashine vinaenea sana, na inakuwa vigumu kupata vitu vya sanaa vilivyotengenezwa kidesturi. Hata hivyo, je, vitu vya kidesturi vilivyotengenezwa mahali fulani vyaweza kupatikana?

Kuzuru Eneo Lililotengwa la Waamerika Wahindi

Tuligundua kwamba kweli vyaweza kupatikana tulipozuru rafiki ambao ni Waamerika Wahindi ambao bado wanatengeneza vitu vyao vya sanaa ya kidesturi. Wao ni wa kabila la Kihindi la Santa Clara Pueblo, wanaojulikana hasa kwa vyombo vyao vya udongo vilivyong’arishwa vyeusi—baadhi ya vyombo vya udongo vyenye kuvutia zaidi ulimwenguni. Vyombo vyao vya kidesturi ni tofauti sana na vitu vilivyotengenezwa kwa mashine vipatikanavyo katika maduka mengi katika kusini-magharibi mwa Marekani.

Rafiki zetu, Joe na Anita, wamekuwa wakitengeneza vyombo vya udongo kwa njia ya kidesturi kwa muda wa miaka mingi. Anita alianza kutengeneza vyombo vya udongo pamoja na mama yake alipokuwa na umri wa miaka sita. Kimoja cha vyombo vya Anita kiko katika Smithsonian Institution katika Washington, D.C., katika wonyesho walo wa Sanaa za Waamerika Wahindi.

Tulifika makao ya Joe na Anita walipokuwa tu wakijitayarisha kuanza fungu jipya la vyombo vya udongo. Kwa hiyo sasa tungeweza kujionea jinsi vinavyotengenezwa. Tumepata kutengeneza vyombo vya udongo sisi wenyewe wakati uliopita. Lakini tulivitengeneza kwa njia ya kisasa kwa kalibu, mchanganyo wa udongo, na tanuri. Kile tulikuwa tujionee kilikuwa njia ya kale, iliyopitishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Hakuna tekinolojia ya kisasa katika taratibu hiyo. Kila kitu kinatengenezwa bila kutumia sehemu zilizo tayari.

Kukusanya Vichanganyiko

Kwanza, ilibidi Joe na Anita wakusanye vichanganyiko. Tulienda kwa gari lao la kubebea mizigo hadi kwenye upande wa mlima ambapo wao hupata udongo. Kwa kuwa upande huo wa mlima uko kwenye eneo lililotengwa, udongo huu unapatikana tu kwa washiriki 2,400 hivi wa kabila la Santa Clara Pueblo. Wengi wao hutengeneza vyombo vyao vya udongo kwa njia ya kidesturi tangu nyuma kufikia miaka ya 1500. Tulipofika mlimani, Joe alichukua sururu yake na kuelekea kwenye mwanya ulio na udongo.

Mwanya huo huenea kwa ulalo kwenye sehemu ya chini ya mlima. Ilimlazimu Joe kulala kiupande ili kuchimba kwenye mwanya, akitoa vipande vikubwa vya udongo vyenye ukubwa wa matofali hivi. Hili laweza kuwa hatari, kwa kuwa kadiri unavyochimba ndani, ndivyo kuzidivyo kuwa na hatari ya kuporomoka kwa mwamba. Baada ya Joe kumaliza kutoa kati ya kilogramu 60-70 za kile alichotaja kuwa udongo bora sana, tulikuwa tayari kuondoka. Lakini sikuweza kujizuia kuuliza kwa nini hawakuchukua mamia kadhaa ya kilogramu za udongo kwa wakati mmoja na kuwasaidia kuepuka kurudi safari kadhaa. Anita alituambia: “Hiyo si njia ya Kihindi ya kufanya mambo.” Wao huchukua tu kutoka ardhi kile watatumia kwa wakati huo. Udongo mwingi ungepotezwa ikiwa ungeachwa bila kutumiwa na kuwa mgumu.

Kisha, tulikwenda kwenye sehemu nyingine ya mlima kuchukua mchanga mweupe. Hili lilikuwa rahisi zaidi—ilimaanisha kuchota ndoo moja au mbili zilizojaa. Kisha tukarudi nyumbani kwao.

Hiyo Taratibu

Kwanza udongo unalowekwa majini kwa siku kadhaa. Kisha unachekechwa mara tatu au nne. Mchanga pia unachekechwa mara kadhaa. Baada ya hilo, Joe atachanganya sehemu hizo mbili pamoja kwa upatano ufaao. Kupima sehemu moja ya udongo na sehemu moja ya mchanga hakufanywi. Jambo la maana ni uzoefu. Lazima kuwe na kiwango fulani cha mchanga katika udongo ili kusaidia chombo cha udongo kudumisha umbo lacho kinapotiwa moto. Kukiwa na mchanga mwingi au mchache chungu kitapasuka au kuvunjika vipande-vipande. Anita alituambia kwamba alipoanza mara ya kwanza kufinyanga vyombo vya udongo peke yake, angepeleka udongo kwa mama yake ili mama yake auguse na kumjulisha ikiwa kulikuwa na mchanga wa kutosha. Baada ya muda mfupi akajifunza kujua mwenyewe.

Akitumia miguu mitupu, Joe aliukanda udongo pamoja na mchanga hadi alipohisi ulikuwa sawa. Sasa walikuwa tayari kufinyanga vyombo vya udongo. Kalibu hazikutumiwa. Kila kipande ni cha kipekee na hufanyizwa umbo kwa mkono. Anita hutumia saa nyingi kufanyiza umbo chombo kimoja kabla ya kukiweka kando ili kikauke. Kinapokauka nusu na kuwa kigumu kidogo kufikia kiwango cha ugumu wa ngozi, kinaweza kuchongwa kwa mkono vigezo na mistari. Halafu kinaachwa kikauke kabisa, jambo ambalo linaweza kuchukua hadi juma moja, ikitegemea unyevu. Sasa kiko tayari kwa ajili ya kupigwa msasa. Hili hulainisha udongo na kuutayarisha kwa ajili ya ung’arishaji.

Ung’arishaji unafanywa kwa mkono kwa kutumia jiwe laini la chini ya mto. Lazima ufanywe sawasawa. Kung’arisha sana au kidogo, kwaweza kufanya kipande kising’are baada ya kutiwa moto. Hakipakwi rangi yoyote. Taratibu ya ung’arishaji ndiyo hutoa mng’aro wenye kupendeza.

Taratibu ya Kipekee ya Kutia Moto

Sasa kwa hatua ya mwisho: kutia moto vyombo hivyo vya udongo. Ili kufanya hili, wanawasha moto katika uga wao. Tanuri hazitumiwi hapa! Jiko la kuokea linafanyizwa kwa kurundika vipande vya kuni vikiwa wima na kuweka kuni zaidi juu ya vipande vilivyo wima, vikifanyizwa kama jiko la kuokea kukiwa na sehemu ya mwisho iliyo wazi kwa ajili ya kuingiza vyombo vya udongo. Kisha kuni zawashwa moto. Kwa uzoefu wanajua wakati ambapo moto uko katika halijoto ifaayo kuweza kuingiza vyombo vya udongo.

Vyombo vya udongo vinapotiwa moto, rangi yavyo ya kiasili itakuwa nyekundu. Kisha, kwa wakati barabara, Joe achukua hatua isiyo ya kawaida. Yeye arundika samadi ya farasi motoni! Hii ndiyo hufanya vyombo vya udongo viwe vyeusi. Oksijeni katika jiko la kuokea inapopunguzwa, oksidi nyekundu ya chuma katika huo udongo hubadilika kuwa oksidi nyeusi ya chuma. Bila shaka kwa harufu unaweza sikuzote kujua kuna mtu anayetia moto vyombo vya udongo vyeusi katika eneo hilo!

Bidhaa iliyomalizika ni kitu cha kuonea fahari, na watu wengi ulimwenguni pote hufurahia urembo wayo. Mwanzoni, vyombo hivyo vya udongo vilitumiwa kwa makusudi halisi, kama vile kwa kuhifadhi vichanganyiko mbalimbali vya nyumbani. Katika sehemu fulani za ulimwengu, bado vinatumiwa kwa namna hiyo. Lakini chombo hiki cha udongo ambacho tumenunua kitatumiwa kurembesha nyumba yetu na kutangaza kwa fahari kwamba tumezuru Santa Clara Pueblo, ambapo desturi za kale za Waamerika Wahindi bado zinashikiliwa.—Imechangwa.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Vipande vya udongo vyenye ukubwa wa tofali vinachimbuliwa

Udongo unafanyizwa umbo kwa mkono

Vyombo vya udongo vinatiwa moto katika jiko la kidesturi la kuokea

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki