“Mnara Unaoimba” wa Australia
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA
SANAA, tekinolojia, na sayansi mara nyingi zimeungana katika muziki kutokeza ala za muziki za aina mbalimbali zenye ubora wa kutokeza sana. Ingawa zeze za Antonius Stradivarius na filimbi za Theobald Böhm huenda zimejulikana sana, kwa ujumla carillon yenye fahari haijulikani.
Lakini carillon ni nini, nayo hupigwaje? Kuzuru mojawapo carillon zilizo kuu kutatuelimisha na labda kuimarisha uthamini wetu kwa muziki wao wa kipekee.
Ala ya Muziki Iliyo Kubwa Sana
Hiyo Carillon ni mojawapo ala za muziki zilizo kubwa zaidi nayo ni ya kale. Hiyo huwekwa katika mnara wa kengele na hivyo basi kwa kufaa imeitwa “mnara unaoimba.” Ile carillon na mnara wa kengele ulio Canberra, jiji kuu la Australia, ilikuwa zawadi ya yubile kutoka kwa serikali ya Uingereza katika 1963 ili kusherehekea miaka 50 tangu kuanzishwa na kupewa jina kwa jiji hilo. Hiyo carillon iko katika Kisiwa cha Aspen katikati ya Ziwa Burley Griffin lenye kuvutia.
Mnara huu wa kengele wenye kimo cha meta 50 umefanyizwa kwa nguzo tatu zenye umbo la pembetatu, kila moja ya nguzo hizo ikiwa imeshikanishwa kwa upande moja wa pembetatu kuu yenye pande sawa. Juu sana na zikiwa zimening’inia kati ya hizo nguzo tatu kuna vyumba vya orofa vyenye kubeba hiyo carillon yenyewe.
Lifti katika mnara huo yatupeleka hadi orofa ya kwanza, ambako twakuta kibodi mbili zinazofanana na zile za organ. Kibodi ya kwanza ni ya carillonneur, kama ambavyo mpiga carillon huitwa, ya kufanyia mazoezi muziki wake. Nyundo za kibodi hii hupiga tu vipande vya kutoa sauti.
Karibu tu nyuma ya kibodi ya kufanyia mazoezi kuna kibodi yenyewe ya carillon. Lakini hiyo si kibodi ya kawaida, kwa sababu hii ina vidoto vikubwa vya mti oki vyenye kipenyo cha sentimeta mbili. Safu ya juu ya vidoto yawakilisha vidoto vijulikanavyo vyenye rangi nyeusi vya piano au organ. Vidoto hivyo vimechomoza kwa karibu sentimeta tisa, huku safu ya chini (ikiwakilisha vidoto vyeupe vya piano) vikichomoza kwa karibu sentimeta 17. Tofauti na mpiga-piano au mpiga organ, mpiga carillon hatumii vidole vyake bali yeye hupiga akiwa amefumba viganja. Hiyo ndiyo sababu kuna mapengo makubwa kati ya vidoto—ili mpigaji aweze kuepuka kugusa vidoto vingine anapopiga muziki.
Ufundi wa Hali ya Juu Kikweli
Toka juu ya kibodi kuu, waya zimepanda kwenye orofa ya juu, na kila kidoto cha octave nne na nusu kimeunganishwa kwa waya ya feleji yenye mkazo wa kipekee. Ili tujue waya hizo zote zaelekea wapi, twapanda lifti hadi orofa ifuatayo. Hapo kengele mbili kubwa sana, kila moja ikiwa na uzito wa tani sita, zaning’inia kwa njia ya kutisha. Kisha, tuangaliapo juu kati ya kengele hizo, twaona kengele nyinginezo 51 zikining’inia juu yazo zikipanda kwa mfuatano wa zile kubwa hadi ndogo zaidi, hiyo ndogo zaidi ikiwa na kilo saba tu.
Kengele zote zimewekwa mahali pafaapo ili kuzuia hitilafu yoyote ya sauti, ambayo mara kwa mara husababishwa na sauti za juu zaidi za baadhi ya kengele. Kila kengele, ikiwa na nyundo ya chuma iliyo laini ndani yayo, hutendanishwa na waya ya feleji iliyounganishwa kwa kila kidoto katika kibodi iliyo chini. Mkazano hurekebishwa ifae kabisa hali ya kila mpiga carillon na vilevile ifae halihewa ya wakati huo.
Mambo Fulani ya Kupendeza
Kengele za carillon za Canberra zilikalibiwa katika kiwanda cha kusubia cha John Taylor and Company cha Uingereza nazo ni vielelezo vizuri vya sanaa ya kale vya karne ya 20. Muziki wa kengele hizo waweza kusikiwa kuvuka maji ya ziwa na kufika bustani zilizo karibu.
Hii si carillon kubwa zaidi ulimwenguni, lakini ikiwa na kengele 53 imo miongoni mwa zile kubwa zaidi, kwa sababu carillon nyingi zina kengele kati ya 23 na 48. Lakini carillon kubwa zaidi iko New York City. Hiyo ina kengele 74. Hiyo pia ina kengele kubwa zaidi iliyolinganywa sauti ulimwenguni. Kengele hii ina uzito wa tani zaidi ya 18 nayo hutoa sauti ya chini ya C, kwa kulinganishwa na carillon ya Canberra yenye sauti ya chini nyembamba ya F.
Sasa tufurahie wonyesho wa muziki unaofanywa na yule mpiga carillon. Je, tuketi katika bustani chini? Hapa hatutaweza tu kusikiliza muziki murua kabisa wa “mnara unaoimba” bali kwa wakati uo huo tutafurahia maajabu ya uumbaji unaotuzingira. Utulivu wa jioni na kimo chenye kuvutia cha hizo kengele zaungana kutokeza muziki uonekanao kuwa mtamu na wa kipekee sana, ukijaza mioyo yetu shukrani kwa zawadi ya kimungu ya muziki.
[Picha katika ukurasa wa 25]
Kengele katika mnara