Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 8/8 kur. 25-27
  • Hobi Yangu Ni Astronomia

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Hobi Yangu Ni Astronomia
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Nyota au Sayari?
  • Msaada Wapatikana
  • Mwezi na Sayari
  • Nyota
  • Maneno ya Kuonya
  • Nyota na Mwanadamu—Je! Kuna Uhusiano?
    Amkeni!—1994
  • Mfumo Wetu wa Pekee wa Jua—Jinsi Ulivyotokea
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Kuchora Ramani za Mbingu Wakati Huo na Sasa
    Amkeni!—2000
  • “Utukufu” wa Nyota
    Amkeni!—2012
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 8/8 kur. 25-27

Hobi Yangu Ni Astronomia

NAISHI kwenye Kisiwa cha Kaskazini cha New Zealand, katika Pasifiki ya Kusini. Tangu nilipokuwa kijana mwenye miaka 15, nimekuwa nikipendezwa na astronomia. Ni hobi tulivu ambayo yaweza kuwa sahili au tata kulingana na utakavyo. Uwe na hakika kwamba huhitaji kuwa na digrii katika fizikia au kuwa stadi wa hisabati ili ufurahie astronomia.

Hobi nyingi huhitaji vifaa. Kwa hiyo, utahitaji nini? Macho yako hasa. Unapokwenda nje kwa mara ya kwanza kutoka vyumba vyenye nuru vya nyumba yako, itachukua dakika kumi hivi kwa macho yako kujirekebisha kwenye nuru iliyopungua. Ikiwa wewe ni mkazi wa jijini, huenda ukaona vile taa za barabarani na za nyumba zinavyosumbua. Waweza kufanya nini kuhusu hilo? Kwa matokeo mazuri, simama mahali palipokingwa na vyanzo hivi vya nuru.

Utafurahia hali nzuri za kutazama katika usiku wenye giza, usio na mawingu pasipo mwezi. Mwezi hutolea angahewa nuru isiyong’aa sana, ikisababisha nyota zisizo na nuru nyingi kutoonekana. Waweza kuona nyota ngapi kwa macho yako matupu? Kwa kawaida kati ya 2,000 na 4,000. Ni vigumu zaidi kuona nyota zilizo karibu zaidi na upeo macho kwa sababu unatazama kupitia angahewa zito zaidi, jambo ambalo hutokeza kufifia na kupindwa zaidi kwa nuru. Hushangaza watu fulani kwamba ni idadi ndogo sana kwa kulinganishwa ya nyota iwezayo kuonwa kwa macho matupu, kwa kuwa yaonekana kuna mamilioni ya nyota tunapotazama angani mara ya kwanza.

Nyota au Sayari?

Kuona sehemu nyangavu zaidi ya nuru huzusha swali, Je, ni nyota au ni sayari? Nyota ni vyanzo vya nuru, injini kuu za kinyuklia zinazotokeza viishara vya sumakuumeme angani. Ziko mbali sana na dunia, ya karibu zaidi—kando na jua—ikiwa umbali wa miaka-nuru 4.3. Nuru husafiri kwa kilometa 299,000 hivi kwa sekunde. Kwa kuwa nuru kutoka katika nyota husafiri mbali sana ili kutufikia, hiyo huwa hafifu. Kisha ni lazima ipitie unene wa angahewa la dunia, ambao hupinda-pinda miale ya nuru. “Metameta, nyota ndogo, jinsi nishangaavyo kile ulicho,” wasema wimbo wa nasari, ukiongeza uhai katika mbingu zenye ukimya. Ikimetameta, hiyo ni nyota.

Hata hivyo, sayari, huakisi tu nuru kutoka kwa jua, kama tu vile mwezi ufanyavyo. Hizo ziko karibu zaidi nasi, zikiwa washiriki wa familia ya jua, mfumo wa jua. Kwa hiyo sayari ziwezazo kuonwa kwa macho matupu huakisi nuru ambayo ni thabiti na isiyometameta.

Msaada Wapatikana

Ikiwa mngependa kuchungua-chungua zaidi, acheni niwaambie juu ya misaada ambayo hufanya hobi yangu ifurahishe zaidi. Wa kwanza ni atlasi ya nyota. Nakala niliyo nayo sasa ni Norton’s Star Atlas, Toleo Lililorekebishwa. Ina ramani bora za mbingu, na habari ambayo humjulisha mtu asiyefahamu sana msamiati wa astronomia.

Msaada wangu wa pili ni planisphere, ambayo ni diski mbili za plastiki, moja juu ya nyingine, ambazo zimeshikanishwa katikati na kuba. Diski ya juu, ikiwa na dirisha, yaweza kuzungushwa-zungushwa kando ya ile ya chini ikiwa na chati ya nyota ambayo imechapwa juu yayo, nayo yaweza kuwekwa wakati na tarehe ihitajiwayo. Sasa uko tayari kupambanua ni nyota zipi ziwezazo kuonwa kutoka mahali pako pa kutazama kwa saa na wakati wa mwaka na kwa latitudo yako. Katika New Zealand Philips’ Planisphere yaweza kununuliwa kwa urahisi au kuagizwa kutoka maduka mengi ya kuuza vitabu. Unaponunua planisphere, utahitaji kujua latitudo ya mji wa kwenu, kaskazini au kusini ya ikweta.

Je, ununue darubiniupeo? Ikiwa utafuatia hobi hii, nafikiri utafanya hivyo hatimaye. Kuna aina tatu—pindaji, akisi, na pindaji-akisi. Zuru maktaba ya umma ya kwenu kwa ajili ya vitabu vya astronomia na darubiniupeo. Ni rahisi mno kujitengenezea darubiniupeo akisi. Nunua kitabu kisicho ghali kinachozungumzia jinsi ya kutengeneza darubiniupeo ya kiastronomia. Utaupata ukiwa mradi wenye kupendeza sana.

Darubini huandaa mwono ulioenea wa anga. Waweza kuona vichala vyenye kuvutia vya nyota vikining’inia kama vito katika anga jeusi la kimahameli. Waweza kuona vijistari vya mawingu vinavyothibitika kuwa nebula, mawingu ya vumbi na gesi, vilivyoko umbali wa miaka-nuru mingi katika anga. Ukanda wenye kumeta wa Njia ya Kimaziwa waweza kuonekana kutoka mahali popote Duniani. Pia, darubini ni nzuri zaidi kwa kuona kila mahali angani unapotafuta au kutazama nyotamkia, vizururaji, ambavyo pindi kwa pindi huja bila kutazamiwa katika anga lililo karibu nasi. Magazeti ya habari ya kwenu yanaweza kuwa na makala ya kila juma yawezayo kukusaidia kutazama anga la usiku.

Je, una kompyuta ya kibinafsi? Kuna programu fulani juu ya astronomia ambazo mwenye kuanza hobi aweza kuzifurahia, kuongezea zilizo tata zaidi. Mimi hutumia kompyuta yangu kuhifadhi aina zote za habari zinazohusu hobi yangu. Pia kuna magazeti yapendwayo sana juu ya astronomia. Mara kwa mara, Amkeni! huchapa makala juu ya habari hiyo.

Mwezi na Sayari

Bila shaka, hakuna ugumu katika kujua mahali ulipo mwezi. Unapoweza kuonekana, huo hutawala anga la usiku. Mwezi mpevu ni wenye kuvutia kwelikweli kwa kuwa ielekeayo kusafiri kutoka mashariki hadi magharibi usiku upitapo ukielekea kucha. Kutazama kwa ukaribu zaidi, nyota zikiwa kiongozi, hufunua kwamba mwezi husafiri hasa upande uleule tunaosafiri, kutoka magharibi hadi mashariki. Tazama hili kwa kipindi cha muda wa saa moja au mbili au siku mbili zenye kufuatana, ukitazama kikao cha nyota zisizosonga zikilinganishwa na mwezi. Kwa sababu dunia inazunguka kwenye mhimili wayo mbio zaidi kuliko jinsi mwezi unavyozunguka, sisi huacha mwezi nyuma.

Tatizo laweza kumkabili mwastronomia wakati mwezi ni mpevu—nuru nyingi mno. Sikuzote nimefurahia sana kuutazama mwezi wakati ambapo umetokea kwa siku 4 hadi 7 au 22 hadi 24, kwa kuwa vivuli vya milima na kingo za kreta zao ni ndefu zaidi na zenye ncha kali zaidi. Kwa kuwa mwezi ndilo gimba pekee la kimbingu lililo karibu zaidi ambalo sisi huweza kuona mandhari zao zenye kudumu kwa macho matupu, uso wao hutokea kwa namna tofauti kutegemea kama uko kaskazini au kusini ya ikweta.

Ndivyo ilivyo pia kuhusu makundinyota, au vigezo vya nyota vilevile, hivyo ikifanya kuwa vyema zaidi kwako kutumia ramani zilizochapwa kwa ajili ya kizio chako. Au sivyo, zote zitakuwa juu-chini na sehemu za nyuma kuwa mbele—zikitatanisha, hasa kwa mtu anayeanza. Ni lazima itajwe kwamba darubiniupeo ya kiastronomia hutokeza kitu kinachoonwa kikiwa juu-chini. Lakini ziko wapi sayari? Kwanza, kuna vitu viwili tupaswavyo kujua: Ekliptiki na zodiaki ni nini?

Ekliptiki ni kijia cha wazi cha jua kwenye safari yalo ya kila mwaka, nyota zikiwa nyuma. Ekliptiki hupenyeza ikweta ya kimbingu kwa digrii 23.5 hivi. Zodiaki, ambayo humaanisha “mzingo wa wanyama,” ni ukanda wa nyota wa kuwaziwa unaofuata ekliptiki digrii zipatazo 8 pande zote mbili. Jua, mwezi, na sayari ziwezazo kuonwa kwa macho matupu sikuzote zimo katika mipaka ya zodiaki. Kujua kwamba unatazama sayari kunathibitishwa na kutazama kwa siku zenye kufuatana, kwa sababu sayari haikai mahali pamoja tofauti na nyota zisizosonga.

Lakini ni sayari gani ninayotazama? Zebaki na Zuhura sikuzote zitakuwa magharibi katika anga la jioni na mashariki wakati wa asubuhi, kamwe haziwi juu ya kichwa. Zuhura hushindwa na Mwezi tu. Yaelekea waijua kuwa nyota ya asubuhi au nyota ya jioni. Sayari zinazozunguka Jua ng’ambo ya dunia husafiri kutoka mashariki hadi magharibi. Mihiri, Sumbula, Sarateni, na Zohali zaweza kuonekana pia kwa macho matupu. Mwanzoni kutakuwa na uhitaji wa kuulizia habari kutoka chanzo fulani cha habari kuhusu kikao chazo, kwa kuwa hizo hujificha miongoni mwa nyota.

Nyota

Sikuzote utapata nyota zikiwa sehemu zenye kuvutia za nuru. Kujifahamisha makundinyota kwaweza kuwa mwanzo wa uhusiano mpya pamoja na kazi hii yenye kutia hofu ya Muumba.

Tunapendezwa kimahususi na nyota fulani. Moja ni Siriasi; ndiyo nyota nyangavu zaidi kupita zote. Pia ni nyota maradufu, ikiwa nyota mbili katika obiti kuzunguka kitovu kimoja. Nyota ya pili kwa wangavu ni Kanopa. Vyombo vya anga vimetumia nyota hii ili kupata kikao chavyo katika anga na kugeuza antena zao kuelekea dunia ili kurahisisha mawasiliano.

Maneno ya Kuonya

(1) Astronomia yapasa kuwa hobi, si tamaa isiyotulizika. Kanuni bora zaidi ni, “Muumba kabla ya kiumbe.” (2) Usitazame jua kamwe, wakati wowote ule, au kutafutatafuta angani popote karibu nalo kwa darubiniupeo au darubini; adhabu yaweza kuwa upofu. (3) Usiamini kila kitu unachosoma. Vitabu vya zamani vyaweza kukupotosha, kama ilivyo na nadharia nyingi zisizothibitishwa. (4) Usiwe na haraka kutumia fedha zako kwa vifaa, kwa kuwa huenda ukapoteza upendezi.

Hobi yangu ni jasirio lisilokwisha la ugunduzi na mshangao. Hata kwa kuishi milele katika ulimwengu mpya wa Mungu hatutajifunza mafumbo yote ya ulimwengu wote mzima. (Mhubiri 3:11; 8:17) Lakini wakati huo itavutia milele kujifunza zaidi na zaidi kuuhusu.—Imechangwa.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki