Hatari!—Nina Sumu
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Australia
WAHAMIAJI na wageni wanaozuru Australia mara nyingi huambiwa kwamba nyoka na buibui wenye sumu wako karibu kila mahali katika nchi hiyo kubwa. Lakini, kati ya spishi zijulikanazo za buibui, ni karibu spishi 1,700 pekee zinazopatikana hapa. Ni chache tu ambazo kwa kweli zinapaswa kuwa na kibandiko kisemacho “Hatari! Nina Sumu,” lakini spishi nyingi zaidi hazina sumu.
Kwa habari ya nyoka, spishi zipatazo 2,500 zinaishi pamoja nasi Duniani. Kati ya hizo ni spishi 140 zinazopatikana Australia, na karibu 20 pekee ndizo zina sumu. Je, kweli kuna uwezekano wa kukutana na viumbe hao wenye sumu?
Je, Wanapatikana Majijini?
Sanasana wengi wa nyoka na buibui wenye sumu hupatikana mashambani. Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa majiji ya mwambao wanahitaji kutahadhari ifaavyo, hasa kwa habari ya buibui. Kwa kielelezo, kama jina lake lidokezavyo, buibui aitwaye funnel-web wa Sydney anapatikana Sydney, ambalo ni jiji kubwa zaidi la Australia. Ana meno marefu meusi ambayo yamechomoza nje naye aweza kuogofya sana.
Buibui funnel-web wa kiume hutambulishwa kwa mwiba mkali kwenye mguu wake wa pili, naye ndiye hatari—sumu yake ikiwa yenye nguvu mara tano kuliko ya kike. Jina rasmi la Kilatini la buibui huyu ni Atrax robustus. Kitabu The Funnelweb kilisema hivi katika 1980: “Wakati wa miaka sabini ambayo imepita watu wapatao kumi na tisa wamejulikana kuwa walikufa kwa kuumwa na buibui Funnelweb.” Katika 1980 dawa ya kwanza yenye kufanikiwa dhidi ya sumu ya buibui funnel-web ilitengenezwa.
Buibui mwingine wa kujihadhari naye ni yule mgongo-mwekundu, aliyepewa jina hilo kwa sababu ya mlia mwekundu wa kimachungwa kwenye tumbo lake jeusi lenye kung’aa. Nyakati nyingine mlia huo ni wa rangi nyekundu-nyeupe au hata kijivu hafifu. Mgongo-mwekundu wa kike ndiye hatari. Dawa ya sumu yake iwezayo kuua ilipatikana 1956. Mgongo-mwekundu hupatikana kotekote Australia naye ni wa jamii ya black widow ajulikanaye sana.
Jihadhari! Nyoka!
Nyoka wamepatikana kwenye nyua na vichaka vya nyumba zilizo katika viunga vya miji, hasa wakati wa usiku. Nyoka kadhaa ni hatari—kama vile nyoka tiger, death adder (kifutu-kifo), na taipan. Nyoka tiger ana urefu wa karibu meta 1.5. Anaweza kutambuliwa kwa milia myeusi mgongoni mwake. Akikasirika, yeye aweza kutoa sauti kubwa nyembamba ya kukohoa-kohoa.
Nyoka death adder hutofautiana kwa rangi, lakini ana nyongeza ya rangi nyeupe na kimanjano kwenye mkia wake, ambao yeye huupinda-pinda ili kuvutia windo. Yeye hupatikana katika maeneo ya mchanga, ambako yeye hulala kwa umbo la nusu-duara. Nyoka death adder ana urefu wa karibu futi mbili tu na ni mnene.
Kwa upande mwingine, taipan aweza kufikia urefu wa meta tatu! Yeye ni mwenye rangi ya kikahawia na pua yenye rangi hafifu. Ana vifuko vikubwa vya sumu, na wengine wana meno yanayokaribia sentimeta moja kwa urefu. Farasi mmoja alikufa dakika tano baada ya kuumwa na taipan!
Namna Gani Nikiumwa?
Dawa ya sumu za buibui na nyoka zinapatikana, na vituo vya habari za sumu viko tayari kusaidia mchana na usiku kotekote Australia. Njia za kutibu maumo ya nyoka zimeboreka. Wazo la kwamba jeraha lapaswa kukatwa mara moja kisha sumu inyonywe na kutemwa linaonwa na wengi kuwa si la kikale tu bali ni lenye kudhuru. Shauri la wenye mamlaka ya kitiba sasa ni kumweka mgonjwa akiwa ametulia na kufunga mpira au bendeji katikati ya mahali palipoumwa na moyo. Kisha, bendeji ifungwe kwa nguvu mahali palipoumwa na mguu ugangwe. Baada ya hilo huyo mgonjwa apaswa kumwona daktari au apelekwe hospitali haraka iwezekanavyo.
Buibui funnel-web na mgongo-mwekundu hawapatikani kwa urahisi ndani ya nyumba. Mgongo-mwekundu hukaa katika pembe za vibanda au katika eneo lolote kimya na tulivu, kama vile gari la zamani, rundo la takataka, au choo cha nje. Tahadhari wasije wakabebwa kimakosa na kupelekwa nyumbani.
Hatari Ni Kubwa Kadiri Gani?
Waaustralia wengi hawajapata kuona mgongo-mwekundu au death adder na hawajui mtu yeyote ambaye ameumwa na hao. Ukweli ni kwamba hakuna hatari ya kuumwa na buibui au nyoka mwenye sumu ikiwa mtu ametahadhari ifaavyo. Viumbe wengi wenye sumu hujaribu kukuondokea nao waweza kuwa wakali wakati tu wamekasirika au wakiwa wamefungiwa njia.
Hata hivyo, ni jambo la hekima kutahadhari. Mwanasayansi Mwaustralia ambaye ni mtaalamu wa viumbe wenye sumu “hutunza bustani akiwa amevaa glavu, huvua samaki akiwa amevaa mabuti na kusafiri akitahadhari.” Kwa nini yeye huvaa mabuti? Labda kwa sababu ya aina za pweza na yavuyavu, pamoja na stonefish wenye sumu.
Afadhali tuwaeleze kuwahusu wakati mwingine.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Buibui mgongo-mwekundu wa kike
[Hisani]
Juu: Kwa hisani ya Australian International Public Relations
[Picha katika ukurasa wa 24]
“Death adder” wa kaskazini
[Hisani]
Kwa hisani ya Ross Bennett, Canberra, Australia
[Picha katika ukurasa wa 25]
Buibui “funnel-web”
[Hisani]
Kwa hisani ya Australian International Public Relations
[Picha katika ukurasa wa 25]
“Taipan”
[Hisani]
Kwa hisani ya J. C. Wombey, Canberra, Australia