Kuzaliwa kwa Nyota Katika “Kiota” cha Tai
● NYOTA huzaliwaje? Kwa nini nyinginezo ni kubwa na nyangavu zaidi kuliko nyingine? Katika njia yenye kutazamisha seti ya picha zilizopigwa na Darubini-Upeo ya Anga ya Hubble huenda zikafunua utaratibu wa kufanyizwa kwa nyota. Utendaji huu wa kipekee unatokea ndani ya Eagle Nebula, wingu la gesi na vumbi katika galaksi yetu ya Njia ya Kimaziwa.
Kwa watazamaji-nyota walio duniani, Eagle Nebula ina sura ya ndege kama vile tai akiwa amenyoosha mabawa yake na kucha zilizotokezwa. Mwastronomia Jeff Hester na wenzake kwenye Chuo Kikuu cha Serikali cha Arizona walipendezwa kupiga picha eneo la kucha, ambazo zikiwa moja-moja hufanyiza safu kama nguzo ambazo hufanana na mikonga ya tembo. Hapo, mnururisho wa urujuanimno umekuwa ukibadili molekuli za hidrojeni kuwa ioni—yaani, kuziondolea elektroni zazo.
Ramani yenye sehemu nyingi ya picha za Hubble hufunua makumi ya vitu vinavyofanana na vidole vikitokeza mwishoni mwa nguzo hizo. Kwenye ncha za vidole hivyo, gesi yenye kutoneshwa hufanyiza matufe ambayo katika hayo nyota na, kulingana na waastronomia fulani, labda hata sayari huenda zinafanyizwa. Hata hivyo, ukuzi wa vitu hivi unazuiwa na mmwagiko mwingi wa gesi kutoka nyota ndogo mia moja hivi ambazo zilifanyizwa kutoka nebula hiyo mapema. Nyota iliyo nyangavu zaidi kati ya hizi yaweza kuwa nyangavu mara 100,000 kuliko jua letu, au yenye joto zaidi ya mara nane kuliko jua letu. Mnururisho wazo yaonekana tayari umezorotesha sehemu zisizo nene sana za nebula. Utaratibu huu uitwao photoevaporation, waweza kuzuia ufanyizaji wa nyota kwa kuondoa vitu ambavyo kama sivyo vingemezwa na nyota hizo zenye kukua. Katika picha gesi hizi zenye kuvukizika huonekana kama mvuke wenye kupaa kutoka safu za gesi na vumbi.
Ili moja ya matufe haya yenye gesi lianze kung’aa, ni lazima liwe kubwa mno kuweza kutokeza utendanaji wa kinyukilia. Wanasayansi wanakadiria kwamba ukubwa walo ni lazima uwe asilimia 8 ya jua. Kwa kuongezea, ni lazima vumbi la kutosha lililo kandokando hapo liondolewe ili nuru iweze kuponyoka. Hata hivyo, ikiwa tufe hilo haliwi kubwa vya kutosha kuweza kung’aa, laweza kuwa tu tufe la gesi nyeusi liitwalo mbilikimo-kikahawia. Hivi majuzi, waastronomia waligundua mbilikimo-kikahawia wa kwanza awezaye kutambuliwa.
Kufanana kwa mawingu ya vumbi katika Eagle Nebula na mawingu makubwa ya radi yaonekanayo wakati wa dhoruba kwaweza kukupumbaza ufikirie kwamba mawingu hayo ya vumbi si makubwa sana. Kwa uhakika, kila nguzo ya vumbi ni ndefu sana hivi kwamba mmweko wa nuru utokao mwisho mmoja ni lazima usafiri kwa karibu mwaka mmoja ili kufika mwisho ule mwingine. Pia, kila tufe “duni” katika picha linakaribia kutoshana na mfumo wetu wa jua. Isitoshe, Eagle Nebula iko mbali sana hivi kwamba nuru kutoka kwayo ilichukua miaka 7,000 hivi kutufikia—ikisafiri kwa mwendo wa kilometa 299,792 kwa sekunde. Hii yamaanisha kwamba twaona Eagle Nebula kama ilivyokuwa kabla ya mwanadamu kuumbwa.
Waastronomia huonelea kwamba yaonekana kufanyizwa huko kwa nyota hutukia katika nebula nyinginezo pia, kama vile Orion Nebula. Hata hivyo, mwono kamili kutoka kwa vielelezo hivi vingine huzuia utazamaji wa wazi wa utaratibu huo. Nyota pia zaweza kufa kwa kuungua tu, kwa kulipuka kwa nguvu mno katika mlipuko wa nyota kubwa, au kwa kumomonyoka chini ya kani ya uvutano na kuwa shimo jeusi. Muumba wa ulimwengu wote mzima, Yehova Mungu, huweka hesabu ya nyota hizo, kwa kuwa anajua idadi yazo na majina yazo. (Isaya 40:26) “Kiota” cha tai cha nyota huenda kikaonyesha baadhi ya njia ambazo kwazo Mungu amekuwa ‘akiiumba nuru’ na kutokeza nyota ambazo hutofautiana katika utukufu.—Isaya 45:7; 1 Wakorintho 15:41.—Imechangwa.
[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 15]
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 14]
J. Hester na P. Scowen, (AZ State Univ.), NASA