Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 5/8 kur. 5-12
  • Je, Msingi wa Mageuzi Wakosekana?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je, Msingi wa Mageuzi Wakosekana?
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mfumo-Tegemeano—Je, Ni Kizuizi cha Mageuzi?
  • Mfumo-Tegemeano wa Kuganda kwa Damu
  • “Ukimya Sana Wenye Kutisha”
  • Matatizo ya Kuanza kwa Uhai
  • Kwa Nini Watu Wengi Zaidi Wanaamini Mageuzi?
  • Je, Kweli Kuna Aina Yoyote ya Uhai Inayoweza Kuitwa Duni?
    Maswali Matano Muhimu Kuhusu Chanzo cha Uhai
  • Maswali Mawili Muhimu
    Amkeni!—2015
  • Uhai Ulianzaje?
    Habari Zaidi
  • Kumhoji Mtaalamu wa Biokemia
    Amkeni!—2006
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 5/8 kur. 5-12

Je, Msingi wa Mageuzi Wakosekana?

NI NINI kiini cha nadharia ya Darwin ya mageuzi? “Ikifafanuliwa kabisa, kibiolojia, . . . mageuzi yamaanisha njia ambayo uhai ulianza kutokana na kitu kisicho na uhai na kuendelea kujikuza kwa njia za asili pekee.” Mageuzi ya Darwin yadai kwamba “uhai wote, au angalau sehemu zao zote zenye kupendeza, zilitokana na uteuzi asilia ambao ulitokeza kiholela viumbe tofauti-tofauti.”—Darwin’s Black Box—The Biochemical Challenge to Evolution,a cha Michael Behe, profesa-mshiriki wa biokemia katika Chuo Kikuu cha Lehigh, Pennsylvania, Marekani.

Mfumo-Tegemeano—Je, Ni Kizuizi cha Mageuzi?

Darwin alipositawisha nadharia yake, wanasayansi hawakujua jinsi chembe-hai ilivyo tata sana. Biokemia ya kisasa, ambayo ni kuchunguza uhai katika kiwango cha molekuli, imefunua baadhi ya utata huo. Pia imezusha maswali mazito na shaka juu ya nadharia ya Darwin.

Sehemu za chembe zimefanyizwa kwa molekuli. Chembe ndizo vitu vyenye kujenga viumbe hai vyote. Profesa Behe ni mfuasi wa Katoliki ya Kiroma naye anaamini katika mageuzi katika kueleza maendeleo ya baadaye ya wanyama. Hata hivyo, yeye anazusha shaka nzito kama kweli mageuzi yaweza kueleza jinsi chembe ilivyopata kuwapo. Yeye asema juu ya mashine za molekuli ambazo “hutoa mizigo kutoka mahali fulani hadi fulani katika chembe hiyo kupitia ‘barabara kuu’ zilizofanyizwa kwa molekuli nyinginezo . . . Chembe husafiri kwa kutumia mashine, hujinakili kwa kutumia mashine, humeng’enya chakula kwa kutumia mashine. Kwa ufupi, mashine za hali ya juu sana za molekuli huongoza kila utendaji wa chembe. Kwa hiyo kila kijambo kidogo cha uhai kimefanyizwa kwa njia bora zaidi, na mashine ya uhai ni tata sana.”

Sasa, utendaji huu wote unatukia katika nafasi inayotoshanaje? Chembe ya kawaida ina upana wa milimeta 0.03 pekee! Katika nafasi hiyo ndogo sana, kuna utendaji tata ambao ni muhimu kwa uhai. (Ona picha, ukurasa wa 8-9.) Si ajabu kwamba imesemwa: “Jambo kuu ni kwamba chembe—ambayo ni msingi wenyewe wa uhai—ni tata sana.”

Behe abisha kwamba chembe inaweza kutenda ikiwa tu ina sehemu zayo zote. Kwa hiyo, haiwezi kutenda inapobadilika polepole na hatua kwa hatua kupitia mageuzi. Yeye atumia mfano wa mtego wa panya. Chombo hiki sahili chaweza tu kufanya kazi ikiwa sehemu zacho zote zimewekwa. Kila sehemu ikiwa peke yayo—kikanyagio, spring’i, kishikilio, kipigio, kishikio—si mtego wa panya nao hauwezi kufanya kazi. Sehemu zote zinahitajika wakati uleule na lazima zote ziwekwe mahali pazo ndipo zifanyize mtego wa panya ufanyao kazi. Hali kadhalika, chembe yaweza tu kufanya kazi wakati sehemu zayo zote zipo. Yeye atumia mfano huo kueleza kile anachokiita “mfumo-tegemeano.”b

Jambo hilo hutokeza tatizo kubwa kwa hatua za mageuzi, ambazo huhusisha kutokea kitaratibu kwa sehemu fulani-fulani zenye mafaa. Darwin alijua kwamba nadharia yake ya mageuzi ya kitaratibu kupitia uteuzi asilia ilikabili tatizo kubwa aliposema: “Ikiwa inaweza kuthibitishwa kwamba kuna kiungo chochote tata, ambacho hakiwezekani kufanyizwa kwa marekebisho madogo-madogo ya mfululizo, nadharia yangu ingeambulia patupu.”—Origin of Species.

Chembe ya mfumo-tegemeano ni kizuizi kikuu kwa kuitikadi nadharia ya Darwin. Kwanza, mageuzi hayawezi kueleza jinsi vitu visivyo na uhai vilivyopata kuwa hai. Kisha, kuna tatizo la chembe ya kwanza iliyo tata, ambayo ni lazima ingetokea kwa ghafula ikiwa na kila sehemu. Yaani, chembe (au, mtego wa panya) ni lazima ijitokeze yenyewe, ikiwa na kila sehemu na kufanya kazi!

Mfumo-Tegemeano wa Kuganda kwa Damu

Kielelezo kingine cha mfumo-tegemeano ni utendaji ambao sisi huchukua kivivi-hivi—kuganda kwa damu. Kwa kawaida, maji yoyote yale yatavuja mahali ambapo pana tundu nayo yataendelea kuvuja mpaka kiwekeo hicho kiwe kitupu. Lakini, sisi tunapotoboa au kukata ngozi yetu, mvujo huo huzibwa haraka kwa mgando wa damu. Na kama madaktari wajuavyo, “kuganda kwa damu ni mfumo tata sana na wenye mambo mengi ambao una sehemu nyingi za protini zinazotegemeana.” Hizo huchochea kile kiitwacho mfululizo wa kuganda. Hatua hiyo tata ya kupona “hutegemea sana wakati na mwendo ambao utendanaji tofauti-tofauti hutukia.” La, sivyo, mtu aweza kuganda damu yote na kuwa ngumu, au kwa upande mwingine, anaweza kuvuja damu hadi afe. Wakati na mwendo ni muhimu sana.

Uchunguzi wa kibiokemia umeonyesha kwamba kuganda kwa damu hutia ndani mambo mengi sana, ambayo hata moja haliwezi kukosa ili damu igande. Behe auliza: “Mara damu ianzapo kuganda, ni nini kinachoifanya isiendelee kuganda hadi damu yote . . . iwe ngumu?” Yeye aeleza kwamba “mfanyizo, vizuizi, uimarisho, na kuondolewa kwa mgando wa damu” ni sehemu zinazotegemeana za mfumo wa kibiolojia. Sehemu yoyote ikishindwa, basi mfumo wote utashindwa kufanya kazi.

Russell Doolittle, ambaye ni mwanamageuzi na profesa wa biokemia katika Chuo Kikuu cha California, auliza: “Mfumo huu tata na wenye usawaziko ulifanyizwaje kupitia mageuzi? . . . Yaani, ikiwa kila protini ilitegemea kutendeshwa na nyingine, basi mfumo huo wa mgando wa damu ungeanzaje kuwapo? Ama sehemu yoyote ile ingetumikaje bila sehemu nyinginezo zote?” Akitumia hoja za kimageuzi, Doolittle ajaribu kueleza chanzo cha mfumo huo. Hata hivyo, Profesa Behe ataja kwamba “bahati kubwa sana inahitajika kuweka jeni zifaazo katika sehemu zifaazo.” Aonyesha kwamba maelezo ya Doolittle na lugha yake rahisi yaficha magumu mengi sana.

Kwa hiyo, mojawapo mambo makuu yenye kupinga mageuzi ni kizuizi kikubwa sana cha mfumo-tendeano. Behe asema: “Nakazia kwamba uteuzi wa asili, ambalo ndilo jambo kuu la nadharia ya Darwin, unafaulu tu ikiwa kuna kitu cha kuteua—kitu ambacho kina manufaa sasa hivi, wala si kwa wakati ujao.”

“Ukimya Sana Wenye Kutisha”

Profesa Behe asema kwamba baadhi ya wanasayansi wamechunguza “violezo vya hisabati za mageuzi au njia mpya za hisabati za kulinganisha na kusoma mfululizo wa DNA.” Hata hivyo, yeye afikia mkataa huu: “Hisabati hizo hudhani kwamba mageuzi halisi ni ya kitaratibu na kiholela; haziyathibitishi (nazo haziwezi) kuyathibitisha.” (Italiki za fungu la mwisho ni zetu.) Mapema alikuwa amesema: “Ukitafuta fasihi za kisayansi juu ya mageuzi, na ukikazia akili kutafuta maswali ya jinsi mashine za molekuli—ambazo ndizo msingi wa uhai—zilivyositawi, utapata ukimya sana wenye kutisha. Utata wa msingi wa uhai umezuia jaribio la sayansi kuufafanua; mashine za molekuli zimeweka kizuizi ambacho bado hakijavunjwa na mweneo wa nadharia ya Darwin.”

Hilo lazusha mfululizo wa maswali kwa wanasayansi wanyoofu kufikiria: “Kitovu cha utendanaji wa usanidimwanga kilianzaje? Usafiri wa ndani ya molekuli ulianzaje? Ile biosynthesis ya kolesteroli ilianzaje? Ile retinal ilianzaje kuhusika na uwezo wa kuona? Njia za ishara za phosphoprotein zilianzaje?”c Behe aongezea: “Uhakika wa kwamba hakuna hata moja ya matatizo hayo yanayojadiliwa, acha kusuluhishwa, ni dhihirisho kubwa kwamba nadharia ya Darwin haiwezi kueleza chanzo cha mifumo mingi ya kibiokemia.”

Ikiwa nadharia ya Darwin haiwezi kufafanua msingi wa chembe za molekuli, basi itawezaje kufafanua vizuri kuwapo kwa mamilioni ya spishi yanayoishi katika dunia hii? Kwani, mageuzi hata hayawezi kutokeza aina mpya za familia kwa kuziba mapengo yaliyo kati ya familia moja na nyingine.—Mwanzo 1:11, 21, 24.

Matatizo ya Kuanza kwa Uhai

Hata nadharia ya Darwin ya mageuzi iwe yenye kukubalika machoni pa wanasayansi kama nini, hatimaye ni lazima wakabili swali hili, Hata tukisema kwamba aina nyingi za vitu vyenye uhai vilikuja kupitia uteuzi asilia, uhai wenyewe ulianzaje? Yaani, tatizo si kusalimika kwa viumbe bora, bali kuwasili kwa kiumbe bora na cha kwanza! Hata hivyo, kama ionyeshwavyo na maneno ya Darwin juu ya mageuzi ya macho, yeye hakuhangaikia tatizo la jinsi uhai ulivyoanza. Yeye aliandika: “Jinsi neva ipatavyo kuwa nyetivu kwa nuru ni jambo lisilotuhangaisha sawa na tusivyohangaika na jinsi uhai ulivyoanza.”

Mwandikaji wa mambo ya sayansi wa Ufaransa Philippe Chambon aliandika: “Darwin mwenyewe alijiuliza jinsi asili ilivyoteua vitu vilivyotokea kabla ya vitu hivyo kuanza kuwa vyenye utendaji kabisa. Orodha ya mambo yasiyoweza kufafanuliwa na mageuzi haina kikomo. Na wanabiolojia wa leo ni lazima wakubaliane kwa unyenyekevu na Profesa Jean Génermont wa Chuo Kikuu cha South Paris katika Orsay, kwamba ‘nadharia bandia ya mageuzi haiwezi kufafanua kwa utayari chanzo cha viungo tata vya mwili.’”

Kwa kufikiria jinsi mageuzi hayawezi kabisa kutokeza viumbe tata mbalimbali, je, wewe huona ugumu wa kukubali kwamba kila kitu kilikuja kupitia mageuzi kwa njia ifaayo kwa nasibu tu? Je, unajiuliza ni vipi viumbe vyovyote vingesalimika katika vita vya kusalimika kwa viumbe bora wakati ambapo bado macho yavyo yalikuwa yanapitia mageuzi? Au wakati ambapo inasemekana eti vilikuwa vinafanyiza vidole hafifu kwenye mwili ulio nusu binadamu? Je, unajiuliza jinsi chembe zilivyosalimika zikiwa katika hali ya nusu-nusu na za kutofaa?

Robert Naeye, mwandikaji wa gazeti Astronomy aliye pia mwanamageuzi, aliandika kwamba uhai duniani umetokana na “mfululizo mrefu wa matukio yasiyowezekana [ambayo] yalitukia kwa njia sawa tu na kutufanya tuwepo, kana kwamba tumeshinda bahati-nasibu ya mamilioni ya dola mara milioni moja mfululizo.” Kuwaza kwa njia hiyo labda kwaweza kutumiwa katika kila kiumbe-hai kilichopo leo. Haiwezekani kabisa. Na bado tunatazamiwa kuamini kwamba kwa nasibu mageuzi pia yalitokeza wa kiume na wa kike kwa wakati uleule ili spishi mpya iendelezwe. Na kufanya jambo hilo hata lisiwezekane zaidi, ni lazima pia tuamini kwamba wa kiume na wa kike hawakupitia mageuzi wakati uleule tu bali pia mahali palepale! Kama hawangekuja pamoja basi kuzaana hakungekuwapo!

Kwa hakika, ni ujinga mkubwa sana kuamini kwamba uhai uliopo katika mamilioni ya viumbe kamili ulitokana na mamilioni ya kamari zilizofanikiwa.

Kwa Nini Watu Wengi Zaidi Wanaamini Mageuzi?

Kwa nini mageuzi yanapendwa sana na kukubaliwa na watu wengi sana kuwa ndiyo maelezo ya pekee ya jinsi uhai ulivyoanza duniani? Sababu moja ni kwamba hayo ndiyo maoni ya kawaida yanayofundishwa shuleni na katika vyuo vikuu, na ni ole wako ukijaribu kuyatilia shaka. Behe aeleza: “Wanafunzi wengi hujifunza kutokana na vitabu vyao vya mafunzo jinsi ya kuona ulimwengu kupitia mageuzi. Lakini, wao hawajifunzi jinsi mageuzi ya Darwin yangetokeza mifumo yoyote tata ya kibiokemia ambayo vitabu hivyo hufafanua.” Yeye aongezea: “Ili kuelewa mafanikio ya nadharia ya Darwin kuwa maoni ya kawaida na kushindwa kwayo kuwa sayansi kwenye kiwango cha molekuli, ni lazima tuchunguze vitabu vya mafundisho ambavyo vinatumiwa kufundisha wale wanaotaka kuwa wanasayansi.”

“Kama wanasayansi wote ulimwenguni wangeulizwa, wengi zaidi wangesema wao waamini nadharia ya Darwin kuwa kweli. Lakini, wanasayansi, kama ilivyo na kila mtu, hutegemeza maoni yao kwenye maoni ya watu wengine. . . . Pia, kwa ubaya, mara nyingi uchambuzi hutupiliwa mbali na jamii ya kisayansi kwa kuogopa kwamba itawapa nguvu creationists. Ni jambo la kushangaza kwamba kwa sababu ya kulinda sayansi, uchambuzi halali wa kisayansi dhidi ya uteuzi asilia umepuuzwa.”d

Kuna jambo gani lifaalo na lenye kutegemeka badala ya nadharia ya Darwin ya mageuzi? Makala yetu ya mwisho katika mfululizo huu itazungumzia suala hilo.

[Maelezo ya Chini]

a Ambacho kimerejezewa kuanzia hapa na kuendelea kuwa (Darwin’s Black Box)

b “Mfumo-tegemeano” hufafanua “mfumo mmoja wenye sehemu kadhaa zinazofaana na kupatana ambazo huchangia utendaji sahili, na sehemu yoyote ikiondolewa mfumo huo hushindwa kabisa kufanya kazi.”

c Usanidimwanga ni utendaji ambamo chembe za mmea, kwa kutumia nuru na chanikiwiti, hufanyiza wanga kutokana na kaboni dioksidi na maji. Huo huitwa na wengine kuwa utendanaji muhimu zaidi unaotukia katika hali ya asili. Ile Biosynthesis ni utendaji ambamo chembe-hai zinatengeneza misombo tata ya kemia. Ile retinal inahusika na mfumo tata wa macho. Njia za kupeleka ishara za phosphoprotein ni sehemu muhimu za utendaji wa chembe.

d Creationism hutia ndani itikadi ya kwamba dunia iliumbwa kwa siku sita halisi au, katika hali fulani, kwamba dunia ilifanyizwa kwa miaka 10,000 hivi pekee iliyopita. Ingawa Mashahidi wa Yehova wanaamini uumbaji, wao si creationists. Wao waamini kwamba masimulizi ya kitabu cha Mwanzo cha Biblia yaruhusu dunia iwe na mamilioni ya miaka.

[Blabu katika ukurasa wa 6]

“Ikiwa inaweza kuthibitishwa kwamba kuna kiungo chochote tata, ambacho hakiwezekani kufanyizwa kwa marekebisho madogo-madogo ya mfululizo, nadharia yangu ingeambulia patupu.”

[Blurbs katika ukurasa wa 10]

Ndani ya chembe, mna “Ulimwengu wa tekinolojia ya hali ya juu sana na yenye utata wa ajabu.”—Evolution: A Theory in Crisis

Maagizo yaliko katika DNA ya chembe, ”kama yangeandikwa, yangejaza vitabu 1,000 vyenye kurasa 600 kila kimoja.”—National Geographic

[Blabu katika ukurasa wa 11]

“Hisabati hizo hudhani kwamba mageuzi halisi ni ya kitaratibu na kiholela; haziyathibitishi (nazo haziwezi) kuyathibitisha.”

[Blabu katika ukurasa wa 12]

“Ni jambo la kushangaza kwamba kwa sababu ya kulinda sayansi, uchambuzi halali wa kisayansi dhidi ya uteuzi asilia umepuuzwa.”

[Sanduku katika ukurasa wa 8]

Molekuli na Chembe

Biokemia—“uchunguzi wa msingi halisi wa uhai: molekuli ambazo hufanyiza chembe na tishu, ambazo huchochea utendanaji wa kemikali wa umeng’enyaji, usanidimwanga, kinga, na nyinginezo nyingi.”—Darwin’s Black Box.

Molekuli—“sehemu ndogo zaidi ambayo elementi au msombo waweza kugawanywa bila kubadili hali zayo za kemikali na sura; kikundi cha atomu zinazofanana au zilizo tofauti ambazo zimeshikanishwa pamoja na kani za kemikali.”—The American Heritage Dictionary of the English Language.

Chembe—kifanyizo cha msingi cha viumbe hai. “Kila chembe ni kitu ambacho kimejipanga kwa hali ya juu sana na ambacho kinasababisha muundo wa kiumbe na utendanaji wacho.” Ni chembe ngapi ambazo hufanyiza mtu mzima? Trilioni 100 (100,000,000,000,000)! Tuna karibu chembe 155,000 kwa kila sentimeta moja ya mraba kwenye ngozi, na ubongo wa binadamu una kati ya nyuroni bilioni 10 hadi bilioni 100. “Chembe ndiyo jambo kuu la uhai kwa sababu ni katika chembe ambamo maji, chumvi, molekuli kubwa-kubwa, na tando zinatokeza uhai.”—Biology.

[Sanduku katika ukurasa wa 9]

‘Utata Usio na Kifani’ wa Chembe

“Ili kufahamu uhalisi wa uhai kama ambavyo umeonyeshwa na biolojia ya molekuli, ni lazima tupanue chembe mara milioni 1,000 mpaka chembe iwe na kipenyo cha kilometa 20 na kufanana na ndege kubwa sana iwezayo kufunika jiji kubwa kama London au New York. Kile ambacho tungeona sasa kingekuwa kitu ambacho ni tata kisicho na kifani na chenye ubuni unaopatana. Nje kwenye chembe tungeona mamilioni ya matundu, yaliyo kama madirisha ya ndege kubwa sana, yakijifunga na kujifungua ili kupitisha vifaa vinavyoingia na kutoka. Kama tungaliingia mojawapo matundu hayo tungalijikuta katika ulimwengu wa tekinolojia ya hali ya juu sana na yenye utata wa ajabu. Tungeona vijia vingi sana vilivyopangwa kwa utaratibu sana na mahandaki yanayotoka nje yanayoingia katika kila sehemu ya chembe, mengine yakielekea kwenye kitovu cha kumbukumbu katika kiini na mengine yakienda kwenye viwanda na sehemu za utendanishaji wa vitu. Kiini chenyewe kingekuwa chumba kikubwa sana cha mviringo chenye kipenyo cha zaidi ya kilometa moja, kikifanana na kuba laini ambamo ndani yacho tungeona kilometa nyingi sana za minyororo ya molekuli za DNA zikiwa zimewekwa kinadhifu kwa utaratibu mzuri. Vitu vingi tofauti-tofauti na mali-ghafi zingepitishwa katika mahandaki mengi kwa utaratibu sana zikienda na kutoka kwenye viwanda kadhaa vilivyo katika sehemu za nje za chembe.

“Tungeshangaa kwa jinsi miendo ya vitu vingi vinavyodhibitiwa katika mahandaki mengi sana yasiyoonekana, yote yakifanya kazi katika muungano mkamilifu. Tungeona kotekote kutuzunguka, katika kila mahali tutazamapo, kila aina ya mashine zinazofanana na roboti. Tungeona kwamba sehemu sahili zaidi inayofanya kazi ya chembe, zile molekuli za protini, ni mashine zilizo tata ajabu za molekuli, kila moja ikiwa na atomu 3,000 zikiwa zimejipanga katika muundo wa kuonekana kwa pande tatu. Tungeshangaa hata zaidi tutazamapo utendaji ambao hatuujui wenye kusudi fulani wa mashine hizo za kiajabu za molekuli, hasa tutambuapo kwamba, japo ujuzi wetu mwingi wa fizikia na kemia, kubuni mashine moja kama hiyo ya molekuli—yaani protini moja tu inayofanya kazi—kungetushinda kabisa kwa wakati huu na hata labda hakutaweza kufanywa mpaka angalau mwanzo wa karne ifuatayo. Na bado uhai wa chembe wategemea maelfu ya utendaji mwingi wenye kupatana, kwa hakika hata makumi ya maelfu, na labda mamia ya maelfu ya aina mbalimbali za molekuli za protini.”—Evolution: A Theory in Crisis.

[Sanduku katika ukurasa wa 10]

Mambo ya Hakika na Hekaya

“Kwa mtu ambaye anaona yuko huru kutafuta visababishi vyenye hekima, uamuzi wa mara moja ni kwamba mifumo mingi ya kibiokemia ilibuniwa. Haikubuniwa na sheria za asili, wala na nasibu na uhitaji; bali, ilipangwa. . . . Uhai duniani kwenye kiwango cha chini kabisa, katika sehemu zao muhimu kabisa, ni tokeo la utendaji wenye akili.”—Darwin’s Black Box.

“Hakuna shaka kwamba baada ya karne moja ya jitihada zenye bidii wanabiolojia wameshindwa kutetea [nadharia ya Darwin ya mageuzi] katika jambo lolote kubwa. Jambo la hakika ni kwamba asili haijatokeza mfululizo wa viumbe vinavyohusiana kwa ukaribu ambao nadharia ya Darwin yadai, wala ustahili wa nasibu kuwa chanzo cha uhai haujathibitishwa.”—Evolution: A Theory in Crisis.

“Uvutano wa nadharia ya mageuzi kwenye nyanja zilizo tofauti sana na biolojia ni mojawapo mifano bora zaidi katika historia ya jinsi wazo la kudhaniwa tu ambalo halina uthibitisho mzuri wa kisayansi linavyoweza kubadili kufikiri kwa jumuiya nzima na kudhibiti mtazamo wa kizazi fulani cha watu.”—Evolution: A Theory in Crisis.

“Sayansi yoyote iliyopita . . . ambayo haitii ndani uwezekano wa ubuni au uumbaji kutokana na uthibitisho haitafuti kweli, nayo ni mtumishi (au mtumwa) wa fundisho la kifalsafa lenye matatizo, yaani, naturalism.”—Origins Research.

“Ni hekaya . . . kwamba Charles Darwin alisuluhisha tatizo la chanzo cha utata wa kibiolojia. Ni hekaya kwamba tunafahamu au hata kufahamu vizuri chanzo cha uhai, au kwamba maelezo yafaayo yarejezea tu vile viitwavyo eti visababishi vya asili. Kwa hakika, hekaya hizo na nyinginezo za naturalism za kifalsafa zinapendwa kwa kadiri fulani. Huwezi kuzishutumu sana miongoni mwa wangwana. Lakini hupaswi vilevile kuzikubali bila kuzichambua.”—Origins Research. “Faraghani wanasayansi wengi hukiri kwamba sayansi haifafanui chanzo cha uhai. . . . Darwin hakupata kuwazia utata mkubwa sana uliopo hata katika hali za chini kabisa za uhai.”—Darwin’s Black Box.

“Mageuzi ya molekuli hayategemei mamlaka ya kisayansi. . . . Kuna madai kwamba mageuzi kama hayo yalitukia, lakini hakuna hata moja linaloungwa mkono na majaribio au hesabu. Kwa kuwa hakuna mtu ambaye amepata kuona mageuzi ya molekuli, na kwa kuwa hakuna uthibitisho wa kuunga mkono ujuzi huo, yaweza kusemwa kwa hakika kwamba . . . sisitizo la nadharia ya Darwin ya mageuzi ya molekuli ni majivuno tu.”—Darwin’s Black Box.

[Sanduku katika ukurasa wa 12]

Mageuzi—“Mchezo wa Nasibu”

Nadharia ya mageuzi hakika ni ndoto ya mcheza-kamari. Kwa nini? Kwa sababu kulingana na mwanamageuzi huyo, hiyo hushinda hata kama haiwezi kamwe kushinda.

Robert Naeye aandika: “Kwa sababu mageuzi hasa ni mchezo wa nasibu, tukio lolote lionekanalo kuwa dogo sana lingetukia kwa njia tofauti kidogo, jambo ambalo lingekomesha mwendo wa mageuzi kabla ya kugeuka kwa wanadamu.” Lakini la, tunatakiwa tuamini kwamba kila kamari ilishinda, mara mamilioni. Naeye akiri: “Mfululizo wa matatizo hudhihirisha kwamba ni vigumu zaidi kwa uhai wenye akili kutokea kuliko vile wanasayansi walivyodhani pindi moja. Labda kuna vizuizi vingi ambavyo wanasayansi hawajapata kuona bado.”

[Mchoro katika ukurasa wa 8, 9]

Mchoro Sahili wa Chembe

Ribosomu

Vitu ambamo protini hufanyiziwa

Sitoplazimu

Eneo lililopo kati ya kiini na kiwambo-chembe

Wavu tendani

Tando ambazo huhifadhi au kusafirisha protini zilizotengenezwa na ribosomu zilizoshikanishwa kwazo

Kiini

Hicho ndicho kitovu chenye kuongoza utendaji wote wa chembe

Kijiini

Mahali ambapo ribosomu hufanyizwa

Kromosomu

Hizo zina DNA za chembe, ambazo ndizo vipangaji vya mambo ya urithi

Vakuoli

Huweka akiba ya maji, chumvi, protini, na kabohidrati

Lisosomu

Huweka akiba ya vimeng’enya vya umeng’enyaji

Golgi

Vifuko vya utando ambavyo hupakia na kusambaza protini zilizotengenezwa na chembe

Kiwambo-chembe

Utando unaodhibiti kinachoingia na kutoka kwenye chembe

Sentrioli

Ni muhimu katika utengenezaji wa chembe

Mitokondria

Mahali panapotengenezewa ATP, ile molekuli ambayo huipa chembe nishati

[Picha katika ukurasa wa 7]

Sehemu zilizo tofauti-tofauti si mtego wa panya—ni lazima mtego wa panya uwe na kila sehemu ili ufanye kazi.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki