Waliyaita Vitumbuizo
UWANJA huo wa duara ulijawa na msisimko. Makumi ya maelfu yalikuwa yamekusanyika kwa ajili ya mojawapo tamasha zenye kusisimua zaidi za Roma ya kale. Bendera, waridi, na mazulia ya ukutani yenye rangi yaliremba uwanja kwa furaha. Chemchemi zilirusha maji yaliyotiwa manukato, yakibadili hewa kidogo kwa harufu zenye kupendeza. Matajiri walijipamba kwa mavazi yao ya kifahari kupita yote. Kelele za umati ziliingiliwa pindi kwa pindi na mianguo ya vicheko, lakini furaha hiyo ilikuwa kinyume cha mambo yenye kuogofya yaliyokuwa karibu kutukia.
Muda si muda mlio wa tarumbeta wenye kuashiria hali mbaya uliita wapiganaji wawili waje kwenye pigano. Umati ulikuwa katika hali ya kichaa washindanaji hao walipoanza kukatana-katana kwa ukatili usio na huruma. Kugongana kwa panga hakukuweza kusikika kwa sababu ya kelele za kushangilia zenye kutia uziwi za watazamaji. Ghafula, kwa mbinu yenye wepesi, mshindani mmoja alimwangusha mpinzani wake. Matokeo ya baadaye ya mpiganaji aliyeangushwa yalikuwa mikononi mwa watazamaji. Ikiwa wangepunga vitambaa vyao vya mkononi, angeishi. Kwa ishara moja tu ya vidole gumba vyao, kusanyiko hilo—wanawake na wasichana wakiwa ndani—liliamuru pigo la kifo. Kwa dakika chache tu mwili usio na uhai uliburutwa kutoka kwenye sakafu ya uwanja, mchanga uliolowa damu ulilimwa kwa sepetu, mchanga mwingine ulitapakazwa, na umati ulijiandaa kwa machinjo yaliyobaki.
Kwa watu wengi walioishi katika Roma ya kale, hayo yalionwa kuwa kitumbuizo. “Hata wafundishaji kamili wa maadili hawakupinga ufurahiaji huu wa umwagikaji wa damu,” chasema kitabu Rome: The First Thousand Years. Na mchezo wa upiganaji hadi kifo ulikuwa aina moja tu ya vitumbuizo vilivyozorota ambavyo Roma iliandaa. Mapigano halisi ya kimanowari yalifanywa ili watazamaji wenye tamaa ya kumwagwa kwa damu wafurahie. Hata ufishaji wa hadharani ulifanywa, ambapo mhalifu aliyehukumiwa kifo angefungwa kwenye mti wa mateso na kunyafuliwa na mahayawani-mwitu walioshindishwa njaa.
Kwa wale ambao hawakupendelea umwagikaji wa damu, Roma iliandaa mchanganyiko wa michezo ya jukwaani. Kwenye maigizo hayo—michezo mifupi kuhusu maisha ya kila siku—“uzinzi na mahusiano ya kimapenzi ndiyo yalikuwa vichwa vikuu,” akaandika Ludwig Friedländer katika Roman Life and Manners Under the Early Empire. “Lugha iliyotumiwa ilijaa usemi wenye matusi, na vichekesho vilikuwa vya utovu wa adabu, kukiwa na wingi wa kukunja uso, ishara za mwili zenye matusi, na zaidi ya yote, dansi za kustaajabisha za mwambatano wa filimbi.” Kulingana na The New Encyclopædia Britannica, “kuna uthibitisho kwamba vitendo vya uzinzi vilifanywa kihalisi kwenye jukwaa la maigizo wakati wa Milki ya Roma.” Kwa sababu nzuri Friedländer aliyaita maigizo hayo “kwa wazi aina ya mwigizo wa kushangaza ulio mbaya sana kuliko yote katika ukosefu wa adili na uchafu,” na akaongeza: “Maonyesho yaliyokuwa machafu zaidi ndiyo yaliyoshangiliwa zaidi.”a
Namna gani leo? Je, upendezi wa mwanadamu katika vitumbuizo umebadilika? Fikiria uthibitisho, kama unavyozungumziwa kwenye makala ifuatayo.
[Maelezo ya Chini]
a Nyakati fulani, ufishaji ulikuwa ukifanywa jukwaani ili kufanya maonyesho ya kidrama yawe halisi. Kitabu The Civilization of Rome chaonelea hivi: “Lilikuwa jambo la kawaida kwa mhalifu aliyehukumiwa kifo kuchukua mahali pa mwigizaji wakati wa msiba.”
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck