Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 7/8 kur. 16-19
  • Matera—Jiji la Makao ya Kipekee ya Pangoni

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Matera—Jiji la Makao ya Kipekee ya Pangoni
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mazingira Yasiyo ya Kawaida
  • Mfumo Wenye Kuvutiawa Kukusanya Maji
  • Nyumba Mwambani
  • Kuzorota na Urudisho
  • Ngazi Inayoelekea Angani
    Amkeni!—2000
  • Maji Yanayobubujika Ili Kutokeza Uzima wa Milele
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • Je, Wajua?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2011
  • Kapadokia—Mahali Ambapo Watu Waliishi Katika Nyumba Zilizochongwa na Upepo na Maji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 7/8 kur. 16-19

Matera—Jiji la Makao ya Kipekee ya Pangoni

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA ITALIA

MIAKA 50 hivi iliyopita, watu fulani walifikiri kwamba makao hayo yasiyo ya kawaida yalikuwa yamekuwa namna fulani ya “moto” wa Dante, ikifanya wenye mamlaka watoe amri ya watu kuondoka mahali hapo. Nusu yake ikiwa imekaliwa tena, makao hayo sasa hata yametiwa ndani ya Urithi wa Ulimwenguni wa Kitamaduni na Kiasili, yakilindwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni (UNESCO).

Tunazungumzia nini? Na kwa nini yametokeza maitikio tofauti hivyo kadiri wakati ulivyopita? Jibu kwa swali la kwanza ni sahili: Sassi (kihalisi, “Miamba” katika Kiitalia) ya Matera, iliyo kusini mwa Italia, juu tu ya kisigino cha “buti” ya Italia. Lakini ili kujibu la pili, twahitaji kufahamu Sassi ni nini na kujua historia yake kidogo. Kwa nini usiandamane nasi tunapozuru Sassi na upate kujua jambo fulani kuzihusu?

“Miongoni mwa mandhari za Italia ambazo hutokeza mshangao mkubwa zaidi,” kulingana na mwandikaji Guido Piovene, zile Sassi hukaribia kufanyiza jiji lililo na “uvutio wa ajabu sana.” Ili kupata mwono wa mandhari yote, twaenda mahali pafaapo kutazama palipofanyika kiasili panapoelekeana na bonde jembamba lenye kina. Kwenye upande ule mwingine wa bonde hili, mbele yetu, ndipo lilipo jiji la Matera. Katika nuru nyangavu ya wakati wa kiangazi, twaona nyumba zilizojishikamanisha mwambani; zaonekana kama kwamba zilijengwa moja juu ya nyingine. Barabara nyembamba kati yake ziendapo hadi chini ya bonde hilo jembamba, hizo hufanyiza fundo lililofungamana likifanana kwa njia fulani na ngazi za uwanja duara mkubwa wa maonyesho. Mashimo mengi tunayoona kwenye nyuso za mwamba ni, au yamekuwa, makao. Kwa ufupi, hizi ndizo Sassi—nyumba za pango zilizofanyizwa kutoka mwambani!

Mazingira Yasiyo ya Kawaida

Ili kufika kwenye Sassi—jiji kuu la kale la Matera—ni lazima tupitie jiji la kisasa, likiwa na msongamano wake wa magari na kelele. Kuingia jiji la kale ni kama kupitia badiliko la wakati; twatokezea katika mazingira yasiyo ya kawaida ambapo vurugu ya wakati huu yabadilika hatua kwa hatua kuwa mandhari za wakati uliopita.

Usitarajie kuona wakazi wa pangoni wakitoka. Leo, huwezi kuona tena mapango ya awali ya kale, kwa kuwa majengo ya kijuu-juu ya magange, ikiwa si majengo kamili, yamejengwa mbele ya makao hayo katika mitindo ya vipindi tofauti-tofauti: enzi za kati, enzi za karne ya 17 za kupita kiasi, na ya kisasa. Tuzidipo kwenda, mandhari yaonekana ikibadilika mbele ya macho yetu wenyewe.

Kulingana na waakiolojia, maelfu machache ya miaka iliyopita vikundi vya wahamahamaji, yaelekea wachungaji, walikaa katika eneo hili. Mapango mengi ya kiasili yaliyotapakaa katika eneo hilo yaliandaa kimbilio mbali na hali za hewa na wanyama-wawindaji. Muda si muda, mapango mengi yakakaliwa. Matokeo ya waakiolojia yanaonyesha kwamba eneo hilo limekaliwa kwa kuendelea tangu wakati huo.

Hata hivyo, Sassi zenyewe, zilikaliwa hatua kwa hatua. Katika nyakati za Ugiriki na Roma, kulikuwa na vijiji vidogo kwenye kilele cha juu zaidi cha mwinuko wa mwamba, mahali ambapo kwa wakati huu ni kitovu cha jiji la kale. Katika nyakati hizo za kale, aandika Raffaele Giura Longo, Sassi zilikuwa “mabonde mawili ya pori, majaruba mawili yaliyoenea mbavuni mwa kilima cha jiji la kale juu na kuelekeana na mwinamo mkuu kuingia kwenye bonde jembamba; hazikukaliwa lakini . . . zilifunikwa na mimea mingi sana.” Tangu nyakati za mapema za Enzi za Kati, kwa ulimaji wa utaratibu wa magange na utengenezaji wa barabara, mabaraza ya jiji, na nyumba kutumia miamba iliyochimbuliwa, Sassi zikaanza kupata mwonekano wazo wa kiasili.

Kulikuwa na uhitaji wa nyumba na mahali pa kuweka wanyama na kuendelea na utendaji uliohusiana na ufugaji wa wanyama, kama vile utokezaji wa jibini. Hata hivyo, utendaji mkuu ulikuwa kilimo. Mashamba ya mboga yalianzishwa kwenye matungazi mapana yaliyochimbuliwa ubavuni mwa bonde lenye kina kirefu linaloelekeana na Sassi. Ishara za matungazi hayo zaweza kuonekana bado. Sehemu kubwa ya maisha ya kijamii ilikuwa hasa katika ujirani, nyua zilizozingirwa na makao kadhaa.

Mfumo Wenye Kuvutiawa Kukusanya Maji

Yaweza pia kusemwa kwamba historia ya Sassi ni ile ya pigano la mwanadamu lililo sawia dhidi ya, na kutegemea mwamba na maji. Ingawa hayakuwa mengi kupita kiasi, katika msimu wa mvua maji ya mvua yalimomonyoa mashamba ya kilimo ya matungazi—ambayo yalifanyizwa kwa kazi ngumu nyingi sana—yalipokuwa yakitiririka mbavuni mwa bonde hilo. Hivyo wakazi wa Sassi waliona uhitaji wa kutengenezea maji ya mvua mifereji na kuyakusanya.

Lakini yangekusanywa jinsi gani na wapi? Kwenye matungazi, matangimaji yalichimbwa na kufanywa yasivuje. Mfumo wa mifereji na michirizi ulipitisha maji yoyote yaliyopatikana kuelekea matangimaji haya, ambayo mwanzoni yalitumiwa kuhusiana na kilimo badala ya matumizi mengine yoyote. Kulingana na msanifuujenzi Pietro Laureano, idadi ya matangimaji, ikiwa “kubwa sana kupita mapango yaliyokaliwa au yale yaliyohitajiwa kwa maji ya kunywa,” hutoa ushahidi kwamba “matangimaji ya Sassi yalikuwa hapo awali mfumo wenye kuvutia wa kukusanya maji kwa ajili ya unyunyizaji.”

Mfumo huo pia uliandaa maji ya kunywa ya kutosha, na kadiri idadi ilivyoongezeka, jambo hilo likawa la maana hata zaidi. Kwa sababu hii, mpango wenye akili ukaanzishwa. Matangimaji yaliunganishwa moja na jingine, kwenye kiwango kimoja na pia kwenye matungazi katika viwango tofauti. “Kama mfumo wa kiwanda kikubwa cha utoneshaji, yaliruhusu utakasaji wenye kuendelea wa maji hayo kadiri yalivyopita kutoka tangimaji moja hadi jingine.” Kisha maji hayo yalichotwa kutoka kimoja cha visima vingi vilivyotapakaa kwenye Sassi. Matundu ya baadhi ya visima hivi yaweza kuonwa hata leo. Ilikuwa nadra kupata maji mengi sana katika eneo kame.

Nyumba Mwambani

Tuteremkapo kwenye ngazi na kufuata mzingo wa barabara nyembamba, twatambua kwamba ujirani huu wa kale umepangwa kwa njia ya orofa zenye kushuka, hivi kwamba mara nyingi twajipata tukitembea juu ya paa za nyumba ambazo hufunguka kwenye matungazi yaliyo chini. Katika mahali fulani, kuna orofa kumi za makao, moja juu ya nyingine. Hapa, mwanadamu anaishi karibu sana na mwamba. Mapema kama karne ya 13, hati rasmi ziliita ujirani huu “Sassi.”

Twasimama nje ya mojawapo ya makao hayo. Sehemu ya nje yenye kupangwa kwa uangalifu sana na ya kisasa kwa kulinganisha haipasi kutupumbaza, kwa kuwa hapa kiingilio cha majuzi katika gange kimeongezwa kwenye kile cha awali. Haya ni makao ya kiasili ya Sassi. Baada ya kupita mlango, twateremka mfululizo wa ngazi kuingia katika chumba kikubwa ambapo utendaji mwingi wa kinyumbani wa familia ulitendeka. Twateremka ngazi zaidi kuingia katika chumba cha pili, na mbele yacho kuna kingine tena. Vyumba fulani vilikuwa matangimaji ya kale ambayo yalifanywa iwezekane kuishi ndani yake—tundu lililo juu, ambapo maji yalikuwa yakiingilia, lilifunikwa, na kiingilio cha chumba hicho kikajengwa kwa kuchimba ubavu wa tungazi. Vyumba vya ndani zaidi wakati mmoja vilitumiwa kuweka wanyama wa kubeba mizigo tu, huku familia ikiishi katika vyumba vilivyokuwa karibu na kiingilio. Nuru na hewa viliandaliwa na tundu kubwa juu ya mlango. Ni wazi kwamba wakazi wa leo wa Sassi hawaweki tena wanyama wa kubeba mizigo ndani ya nyumba zao!

Makao mengi yako chini ya kiwango cha barabara. Kwa nini? Kwa sababu kiingilio na nyumba fulani za pango zenyewe zilichimbuliwa kwa mwinamo wa kadiri fulani ili kutumia miale ya jua. Wakati wa kipupwe, wakati ambapo jua hufikia hatua yake ya chini zaidi kwenye upeo wa macho, miale yake yaweza kuingia ndani ya nyumba, ikimulika na kuipasha joto; wakati wa kiangazi miale ya jua ilifika kwenye kiingilio tu, na ndani palibaki pakiwa na ubaridi na unyevu. Kwenye ukuta wa nyuma wa pango tunalozuru, twaona kishubaka kilichochongwa kikiwa na “rafu” kadhaa. Ni saa ya kivuli, iliyoundwa ili kuonyesha msogeo wa jua wakati wote mwakani. Turudipo nje, twapata hisia isiyo ya kawaida. Ubaridi wa pango hilo tayari ulikuwa umetufanya tusahau joto la kiangazi lililokuwa nje!

Kuzorota na Urudisho

Mbali na mazingira yasiyo ya kawaida, Sassi zimepatwa na mabadiliko kadhaa. Ingawa kwa karne nyingi zimebaki zikiwa na upatano na kwa kiasi fulani kiini cha jijini chenye matokeo mazuri, katika karne ya 18 jambo fulani lilibadilika. Majengo na barabara mpya zilizuia mfumo wenye matokeo wa usimamizi wa maji, zikitokeza matatizo katika uondoshaji wa kawaida wa taka. Tokeo ni kwamba maradhi yaliongezeka. Na zaidi, mabadiliko katika uchumi wa eneo hilo yalitokeza umaskini wenye kuongezeka miongoni mwa familia za wakulima wa Sassi, ambazo zilikuwa zikizidi kusongamana.

Kuzorota kwenye kuendelea kwa eneo hili maridadi kulionekana kuwa kusikoepukika. Kwa hiyo, kwa wazo la kutatua tatizo kabisa katika miaka ya mapema ya 1950, uamuzi rasmi ulifanywa wa kuondoa watu kwenye Sassi. Kwa zaidi ya wakazi wa Matera 15,000 walioishi hapa, hilo lilimaanisha hali yenye kuhuzunisha, hasa ukifikiria mahusiano ya kijamii, kwa kuwa vifungo vya ukaribu vya urafiki vilivyokuwa vimefanyizwa katika ujirani huo vilivunjwa.

Hata hivyo, wengi wanaamini kwamba mji huu wa kimandhari wa ajabu haupasi kupotezwa. Hivyo, kwa sababu ya kazi nzuri ya urudisho, Sassi polepole zaanza kurudishwa katika hali ya awali na kukaliwa tena. Leo, watalii wengi hupenda kujionea mazingira yenye kuenea yale mabaraza ya mji wa kale na barabara zenye kufungamana za Sassi. Ikiwa utapata kuja katika sehemu hii ya ulimwengu, kwa nini usipitie kuzuru jiji hili la karne nyingi ambalo lilifanyizwa kutoka mwambani?

[Picha katika ukurasa wa 17]

1. Mwono wa mandhari yote wa Sassi ya Matera; 2. “ujirani,” ukiwa na kisima mbele kushoto; 3.  ndani ya mojawapo ya makao ya kawaida; 4. kishubaka kilichotumika kama saa ya kivuli; 5. mtaro ambao wakati mmoja ulitumiwa kupeleka maji kwenye matangimaji

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki