Bonde Kuu la Ufa
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Kenya
HILO ni handaki kubwa sana, bonde lililo kwenye uso wa dunia ambalo ni kubwa mno hivi kwamba linaweza kuonekana kutoka kwenye mwezi! Likinyooka kutoka Bonde la Yordani upande wa kaskazini mwa Israeli na kuteremka kote kufikia Msumbiji—kilometa nyingi ajabu zipatazo 6,400—hilo limeteremka sana katika marefu ya kontinenti ya Afrika.
Mwaka wa 1893, mwanajiolojia wa Scotland J. W. Gregory alichunguza kindani ajabu hii ya asili. Gregory alifahamu kwamba handaki hili kubwa halikufanyizwa kwa mmomonyoko wa maji wala wa upepo bali ulifanyizwa “kwa miamba iliyozama kwa wingi sana, huku ardhi ya kandokando ikibaki vilevile.” (Linganisha Zaburi 104:8.) Yeye aliuita mpasuko huo mkubwa kwenye uso wa dunia Bonde Kuu la Ufa.
Wanasayansi leo bado hawaelewi kabisa nguvu za chini ya ardhi ambazo zilifanyiza bonde hili maelfu ya miaka iliyopita. Hata hivyo, mtu hawezi kujizuia kuvutiwa sana na vitu vingi tofauti-tofauti vinavyopatikana ndani yake. Sehemu ya Bonde Kuu la Ufa iliyo katika Afrika, inayoanzia Ethiopia, ina mojawapo ya sehemu zenye kutisha zaidi duniani kote, lile liitwalo Bonde la Danakil (pia huitwa Eneo la Afar). Bonde hilo kubwa sana la chumvi limepakana na Bahari Nyekundu nalo ni jangwa linaloenea kwa kilometa 150,000 za mraba. Hapo ardhi imeshuka hadi meta 120 chini ya usawa wa bahari. Halijoto zaweza kupanda kufikia digrii 54 Selsiasi. Tokea hapo bonde hilo huinuka hadi milima yenye baridi ya Ethiopia—yenye urefu wa meta 1,800 juu ya usawa wa bahari, vilele vya milima vikifikia urefu wa meta 4,300. Misitu minene ya mvua hufunika miinuko ya milima hiyo yenye rutuba, ikinywesha maji mito mingi, kama vile Naili Buluu. Likisafiri kuelekea kusini katika tawi lake la mashariki, bonde hilo huendelea kuinuka na kushuka kwa njia ya kutazamisha sana.
Vyenye kutapakaa kotekote katika Bonde la Ufa ni vilele vya milima ya volkeno vyenye maumbo tofauti-tofauti na ukubwa mbalimbali na vilevile mabonde madogo-madogo ambayo hutokana nalo. Katika bonde la magharibi, miendo ya volkeno imefanyiza safu za milima ya Ruwenzori na Virunga ambazo zimevuka mipaka ya Rwanda, Zaire, na Uganda. Vilele fulani vingali vinaonyesha ishara za utendaji wa moto kutoka ardhini na, pindi kwa pindi, hutoa moshi na lava zilizo nyekundu sana. Karibu na bonde la mashariki, vilele vya volkeno za zamani kama vile Kilimanjaro na Mlima Kenya ni virefu sana hivi kwamba vimefunikwa kwa theluji japo joto kali sana la ikweta. Chemchemi za moto ambazo hutoa mvuke na maji yaliyochemka sana hupatikana kotekote katika marefu ya Bonde la Ufa, jambo linalothibitisha kwamba bado kuna msukosuko chini sana ya uso wa dunia.
Kusini zaidi, katika Tanzania, uwanda mkubwa sana wa mbuga wapakana na bonde hilo. Uwanda huo unaitwa siringet katika lugha ya Kimasai, neno limaanishalo “tambarare pana.” Ukijulikana zaidi kwa jina Mbuga ya Serengeti, nyasi zake nyingi hudumisha makundi makubwa sana ya wanyama wa pori. Hapa ndipo uhamaji mkuu wa nyumbu hutukia—tukio la kustaajabisha kwa kweli!
Maziwa ya Bonde la Ufa
Kandokando ya sehemu ya mashariki ya Bonde la Ufa katika Afrika kuna mfululizo wa maziwa ambayo yana magadi kidogo. Kemikali hizo zimetoka kwenye sehemu za volkeno au zimeingia katika maziwa kupitia utendaji wa volkeno chini ya ardhi. Baadhi ya maziwa, kama vile Ziwa Turkana kaskazini mwa Kenya, yana alkali kidogo sana. Likiwa limezingirwa na maelfu ya kilometa za mraba ya vichaka vya jangwa vilivyotawanyika-tawanyika, nyakati nyingine Ziwa Turkana hugeuka rangi na kuwa kijani-kibichi kilicho maridadi sana nalo ndilo makao ya idadi kubwa zaidi ya mamba ulimwenguni pote. Maziwa kama Ziwa Magadi la Kenya na Ziwa Natron katika Tanzania yamejaa sana chumvi hivi kwamba hayo hufanyiza utando mgumu wa magadi meupe yaliyokauka. Kisababishi ni nini? Ukosefu wa mito ya kuondoa maji ambayo kwa kawaida yangeondoa chumvi hizo. Maji mengi hutoweka kupitia uvukizaji, yakiacha ukolezo mwingi wa madini. Ni wanyama wachache wawezao kuokoka katika na hata kandokando ya maji hayo machungu ya maziwa ya Bonde la Ufa. Hata hivyo, tofauti kubwa ni wale heroe wenye kupendeza wenye rangi ya pinki ambao huhama kutoka ziwa moja la magadi hadi jingine, wakila miani midogo sana ambayo husitawi sana katika maji hayo ya magadi. Hapo heroe hukusanyika kwa mamilioni, wakifanyiza rangi ya pinki tupu.
Mkazi mwingine anayesitawi katika maji hayo ambayo kwa kawaida hufisha ni samaki mdogo mno aitwaye tilapia grahami. Samaki huyu akinzaye alkali hupatikana mara nyingi karibu na chemchemi za mvuke zilizo chini ya maji, ambapo maji ni moto sana hivi kwamba yanachoma mkono. Lakini samaki hao wadogo huishi hapo, wakila miani ya ziwa.
Ni maziwa machache tu ya bonde la mashariki ambayo yana maji matamu. Ziwa Naivasha, nchini Kenya, ni mojawapo. Ziwa hilo liko meta 1,870 juu ya usawa wa bahari, na maji yake safi ni makao ya samaki wa aina mbalimbali pamoja na makundi ya viboko wenye kuota jua. Kandokando ya ziwa hilo kuna mafunjo mengi ya kijani-kibichi na mimea mingi ya majini, ambayo ni makao ya zaidi ya spishi 400 tofauti-tofauti za ndege maridadi. Likiwa na mandhari ya mikakaya ya rangi ya kimanjano na safu za milima zenye kuzingira, kwa kweli Ziwa Naivasha ni maridadi sana.
Katika mfumo wa bonde la ufa mna ziwa ambalo ni la pili kwa ukubwa ulimwenguni kati ya maziwa yenye maji matamu, yaani Ziwa Viktoria. Maji yake yameenea Kenya, Uganda, na Tanzania, nalo ni mojawapo ya vyanzo vya Mto Naili. Kusini zaidi, maji ya Ziwa Tanganyika hufikia kina cha meta 1,440. Hili ndilo ziwa la pili lenye kina zaidi ulimwenguni.
Wanyama wa Aina Mbalimbali
Bonde la Ufa la Afrika Mashariki hutegemeza wanyama wa pori wa aina mbalimbali. Nyati, twiga, vifaru, na tembo ni baadhi ya wanyama wakubwa ambao huzurura katika pori za bonde hili, lenye mapana sana. Katika sehemu kavu zisizo na maji, pundamilia, choroa, na mbuni waweza kuonekana. Swala wenye madaha hurukaruka hewani wapigapo mbio kuvuka mbuga. Baadhi ya paka wenye madoa kama chui na duma huwinda katika mbuga, na mngurumo wa simba mwenye fahari mara nyingi waweza kusikika wakati wa usiku. Juu sana katika safu ya mlima wa Virunga, gorila walio nadra sana kuonekana hukaa. Chini sana katika sakafu ya bonde, makundi ya nyani hutembea polepole yakivuka bara lenye mawemawe yakitafuta wadudu, mbegu, na nge. Wakipaa juu sana, tai na tai-mizoga wenye nguvu sana ambao wana mabawa mapana sana hupelekwa na mikondo ya hewa ya joto. Dura, kisigajiru, hondohondo, na kasuku walio maridadi huishi katika michongoma ya nyanda za chini. Mijusi wenye maumbo, ukubwa, na rangi mbalimbali hukimbia haraka-haraka, kana kwamba miguu yao inachomwa kwa moto.
Wahamahamaji wa Bonde la Ufa
Bonde la Ufa la Afrika Mashariki ni makao ya makabila mengi ya sehemu kavu ambao ni wachungaji na vilevile wahamahamaji. Wao ni watu wa maisha magumu sana ambao hutembea kwa hatua ndefu ambazo ni kawaida wa wahamahamaji wa Afrika. Katika maeneo ambamo mvua ni haba, mara nyingi vijiji vizima huhama ili kutafuta malisho mapya kwa mifugo yao. Bila pasipoti wala viza, wao huvuka kwa huru mipaka isiyo na alama ya nchi tofauti-tofauti nao huonekana kama hawajali maendeleo na njia nyinginezo za maisha. Katika maeneo hayo ya upweke, maisha ni ya polepole. Saa hupimwa kwa macheo na machweo ya jua. Mali za mtu hupimwa kulingana na ngamia, mbuzi, ng’ombe, au kondoo ambao anao au kulingana na idadi ya watoto katika boma lake.
Nyumba hutengenezwa kwa usahili lakini kwa werevu. Matawi ya miti hukunjwa na kufungwa pamoja ili kufanyiza kibanda kinachofanana na kuba. Kisha sehemu ya nje inafunikwa kwa nyasi zilizofumwa, ngozi za wanyama, au udongo uliochanganywa na samadi ya ng’ombe. Nyumba hizo mara nyingi huwa na moto wa kupikia, sehemu ndogo ya wanyama wa kufugwa, na kitanda ambacho huenda hata kikawa ngozi tu ya mnyama. Moto utokao kwenye meko hujaza nyumba kwa moshi, ukifanya kusiwe na nzi wala mbu ndani. Mara nyingi kijiji au kikundi cha familia hujenga vibanda vyao vidogo vyenye umbo la kuba kwa mviringo vikiwa vimezingirwa na kingo za michongoma zisizoweza kupenyeka, ili kulinda mifugo yao dhidi ya wanyama wa pori wakati wa usiku.
Kotekote katika Bonde Kuu la Ufa kuna vikundi vya watu tofauti-tofauti vyenye sura, lugha, na desturi tofauti-tofauti, kwa kulingana na makabila yao na mahali wanapotoka. Itikadi za kidini pia hutofautiana sana. Wengine wamesilimu; wengine wamekuwa Wakristo kwa jina tu. Wengi ni washirikina nao huelekea kuona kila kitu ambacho hawawezi kuelewa kuwa kimesababishwa na nguvu zisizo za asili. Katika miaka ya karibuni mengi ya maeneo ya upweke yamefunguka kwa sababu ya uvutano wa kigeni kupitia mashirika yanayoandaa elimu na utunzaji wa afya.
Haishangazi kwamba Mashahidi wa Yehova pia wanajitahidi kuwatembelea wahamahamaji hao wanaoishi maisha magumu. Mashahidi wanatumaini kuwajulisha ahadi ya Biblia ya wakati ambapo hakuna mtu atajaribu kupata riziki katika eneo kame. Biblia yasema: “Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi.” (Isaya 35:1) Kwa wakati huu, Bonde Kuu la Ufa ladumu likiwa kumbukumbu kwa uumbaji mbalimbali wa Mfanyi wa vitu vyote, Yehova Mungu.
[Ramani katika ukurasa wa 14]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
ISRAELI
MISRI
SAUDI ARABIA
Bahari Nyekundu
YEMENI
Ghuba ya Aden
ERITREA
SUDAN
UGANDA
RWANDA
BURUNDI
ZAIRE
ZAMBIA
MALAWI
JIBUTI
ETHIOPIA
SOMALIA
KENYA
TANZANIA
MSUMBIJI
[Hisani]
Mountain High Maps® Copyright © 1995 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Kwenye Mbuga ya Serengeti, tukio la kustaajabisha kwa kweli hutukia—uhamaji mkuu wa nyumbu
[Hisani]
Chini: © Index Stock Photography and John Dominis, 1989
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Heroe hukusanyika kwa mamilioni, wakifanyiza rangi ya pinki tupu
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Mashahidi wa Yehova hushiriki ujumbe wa Biblia na watu wa Bonde la Ufa