Kisiwa cha Cocos—Hadithi Zake za Hazina Zilizozikwa
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Kosta Rika
KUNA kisiwa karibu kilometa 480 hivi kusini-magharibi mwa pwani ya Kosta Rika kijulikanacho kwa hadithi zake za hazina zilizozikwa. Wengine wanaamini kwamba Robert Louis Stevenson alitegemeza kitabu chake kijulikanacho sana Kisiwa Chenye Hazina kwenye hadithi za hazina za maharamia zilizozikwa huko.
Wasanifu wa ramani na mabaharia wamekiita kisiwa hicho kwa majina tofauti-tofauti tangu kivumbuliwe katika karne ya 16. Kati ya wenyeji wanaozungumza Kihispania, leo kisiwa hicho chajulikana kuwa Isla del Coco (Kisiwa cha Nazi).
Kati ya Kosta Rika na Visiwa vya Galápagos, kuna ardhi ya chini ya bahari ijulikanayo kuwa Mwinuko wa Cocos. Utendaji wa kivolkeno katika mwinuko huo ulitokeza kisiwa chake pekee. Ardhi hii ndogo yenye mawemawe ndiyo kisiwa pekee katika Bahari ya Pasifiki ya kitropiki ya mashariki ambayo hupokea mvua ya kutosha kutegemeza msitu wa kitropiki. Kila mwaka kisiwa hiki hupata karibu milimeta 7,000 za mvua!
Yule mshairi Mwingereza wa karne ya 18 Coleridge alieleza hali mbaya ya baharia wa zamani ambaye alikuwa na “maji, maji, kila mahali, bila hata tone moja la kunywa.” Hata hivyo, katika karne za 17 na 18, maji matamu ya Kisiwa cha Cocos yalitumika kama chemchemi baharini kwa mabaharia walioweza kukipata kisiwa hicho.
Hekaya ya Hazina Iliyofichwa
Katika enzi ambayo uwasiliano wa kimataifa na biashara ulitegemea usafiri wa baharini, unyang’anyi kwa kutumia silaha kwenye bahari kuu au uharamia, ulitisha jamii. Maharamia walikuwa tisho kwa mmoja na mwenzake pia.
Baada ya mji mdogo wa pwani au meli kutekwa nyara na maharamia, mali iliyoibwa iligawanywa kati ya wafanyakazi wa meli. Hivyo, kila haramia alikumbwa na tatizo la jinsi atakavyolinda salama mali zake zilizopatikana kwa njia isiyo halali zisiibiwe na wenzake. Njia waliyopendelea ilikuwa kuificha hazina katika sehemu ya siri wakiwa na tumaini la kuitoa baadaye. Ramani iliyoonyesha hazina ilipo, ikiwa na maandishi ya siri yaliyoeleweka tu na mwenye kuyaandika, ikawa ufunguo wa kupata hazina iliyofichwa.
Hekaya moja kuhusu Kisiwa cha Cocos yaeleza kuwa uvamizi uliofanikiwa wa meli na miji iliyo kwenye Pwani ya Pasifiki ya Amerika ya Kati ulifanya kikundi kimoja cha maharamia kiwe na dhahabu na vito vingi kupita kiasi. Kwa sababu kisiwa hicho kilikuwa na maji matamu mengi na nyama nyingi (nguruwe waliletwa huko mwishoni mwa karne ya 18), nahodha wa meli alichagua kutumia Kisiwa cha Cocos kama kitovu cha utendaji wao.
Kulingana na simulizi jingine la hadithi hiyo, ugawanyaji wa mali iliyoibiwa ulichukua muda wa siku nzima. Dhahabu ilipimwa kwa vyungu. Kwa sababu ya hofu ya kupoteza mali zao kwa wenzao wenye pupa, maharamia wote walipendelea kuzika hazina mahali fulani katika kisiwa. Wakitumia kamba ili kupanda majabali yaliyoizunguka pwani ya kisiwa hicho, kila haramia alipotelea kwenye msitu wa kitropiki. Huku maharamia fulani wakitumaini kumbukumbu lao, wengine walirudi na ramani ambazo ni wao tu wangezielewa, ambazo zingewarudisha kwenye hazina zao. Hata hivyo, jitihada yote hii yenye kuchosha ilikuwa ya bure. Hekaya hiyo yaendelea kusema kwamba baada yao kuweka akiba bidhaa zao, maharamia hao waling’oa nanga katika majahazi yao makubwa ili kutafuta mapato makubwa zaidi. Walipofika kwenye bandari iliyofuata, nahodha, akihofia uasi, aling’oa nanga baada ya kuwapeleka walioshukiwa kuwa waasi kwenye nchi kavu. Tumaini lake kuwa wangetambuliwa kuwa maharamia na kunyongwa karibu lingetimizwa. Kile alichoshindwa kutazamia ni uwezo wa washiriki wake wawili wenye vyeo vya juu zaidi wa kufanya mipango na wenye mamlaka waliotaka kumkamata huyo nahodha. Jeshi la Wanamaji la Uingereza lilipeleka meli kulifuata sana jahazi hilo kubwa, tokeo likiwa kukamatwa na kuuawa kwa kapteni na wafanyakazi wake.
Katika karne iliyopita, hekaya hii imechochea matumaini ya watafuta-hazina. Lakini, kama ionyeshwavyo na simulizi lifuatalo, wanaotazamia kuwa watafuta-hazina watakuwa waangalifu kabla ya kuanza safari ya uvumbuzi katika Kisiwa cha Cocos. Makala iliyochapishwa katika The New York Times la Agosti 14, 1892, ilifafanua utafutaji wa Nahodha August Gisler kugundua hazina ya dhahabu, fedha, na vito, vyenye thamani ya dola 60,000,000. Utafutaji wa hazina wa Gisler ulihusisha kujitenga na watu na kuvumilia hali mbaya zaidi za kisiwa hiki cha msitu kilichokuwa chenye upweke. Alitumia angalau dola 50,000 za pesa zake binafsi na zaidi ya miaka 19 akitafuta hazina. Katika 1908, Gisler aliondoka Kisiwa cha Cocos, akiwa amefilisika na kuvunjika moyo bila hazina yoyote ya kuonyesha juhudi zake zote.
Jambo la kwamba Gisler hakufua dafu katika kutafuta hazina katika kisiwa hicho halikumvunja moyo kila mmoja. Kumekuwa na safari za uvumbuzi zilizopangwa zaidi ya 500 kwenye kisiwa hicho. Kulingana na habari inayopatikana, hakuna yeyote aliyepata utajiri uliotajwa kwenye hekaya hiyo.
Hazina ya Asili Katika Kisiwa cha Cocos
Hivi karibuni, aina tofauti ya mtafutaji wa hazina amevutiwa katika Kisiwa cha Cocos. Watalii wanaopendezwa na ekolojia na wanaviumbe na wanasayansi wengine wamevutiwa na mimea na wanyama wa kisiwa hicho na hazina yenye thamani ya viumbe vya majini katika maji yanayokizunguka.
Kisiwa hicho kimefunikwa kwa mimea ya kitropiki yenye kusitawi sana. Spishi zipatazo 450 za wadudu na athropodi zimetambulishwa, hata ingawa yakadiriwa kuwa kuna spishi zaidi ya 800 kwenye kisiwa hicho. Kuna mito 28, ambayo hupinda kuizunguka mandhari yenye mawemawe na kumwaga maji yake kwenye majabali yakifanyiza maporomoko mazuri sana ya maji.
Mmoja wa zile spishi 97 za ndege wa kisiwa hicho ni membe mweupe. Ana tabia yenye kufurahisha ya kuzunguka-zunguka hewani juu ya vichwa vya watu, akionekana kuwa asiyewaogopa wenye kuzuru kisiwa hicho. Mwelekeo huu wenye kupendeza sana umempatia ndege huyu lakabu ya Kihispania espíritu santo, au roho takatifu, ikirejezea kwenye simulizi la Kibiblia la ubatizo wa Yesu.—Ona Mathayo 3:16.
Chini kwenye kina cha maji yanayokizunguka Kisiwa cha Cocos kuna ulimwengu uliojaa hazina za kiasili. Kati ya watalii wanaopendezwa na ekolojia wanaokitembelea kisiwa hiki ni wapiga mbizi, ambao hustaajabia wingi wa papa-nyundo. Papa-nyundo na papacheupe hupatikana katika maji haya na wameshuhudiwa wakisafiri katika vikundi vya kati ya papa 40 na 50. Wapiga mbizi wanavutiwa pia na usafi wa maji. Wao hustaajabishwa na wonyesho wa rangi wa samaki wa kitropiki wanaokula kwenye mwani na planktoni.
Nchi ya Kosta Rika imethamini sana tangu zamani hazina zake za kibiolojia. Kwa sasa, asilimia 18 ya ardhi inalindwa kama mbuga ya taifa na mfumo wa hifadhi. Katika mwaka wa 1978, Kisiwa cha Cocos kilitangazwa kuwa sehemu ya huo mfumo wa mbuga, ambao kwa sasa una sehemu 56 zilizo chini ya ulinzi katika nchi hiyo. Katika 1991 sehemu iliyo chini ya ulinzi iliongezwa kufikia kilometa 24 kukizunguka kisiwa. Kushika doria na kulinda mazingira ya majini kutokana na uvuvi wa kibiashara kwatokeza mwito wa ushindani. Wanamazingira wahofia kuwa uvuvi usiozuiliwa waweza kuharibu mifumikolojia katika ulimwengu wa chini ya maji unaokizunguka kisiwa hicho.
Kufikia wakati huu, Kisiwa cha Cocos chaendelea kujulikana kwa habari zake za maharamia jasiri na hazina yake iliyozikwa. Bado huwapendeza na kuwavutia watafuta-hazina kutoka kote ulimwenguni. Hata hivyo utajiri mkubwa zaidi wa kisiwa hicho uko katika mali ya asili yake.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Picha zilizo kwenye ukurasa wa 25-26: Kwa hisani ya José Pastora, Okeanos
[Picha katika ukurasa wa 26]
Papacheupe (1) na papa-nyundo (2, 3) husafiri katika maji yanayozunguka Kisiwa cha Cocos katika vikundi vya kati ya papa 40 na 50