Fumbo la Kuruka kwa Wadudu Lafumbuliwa
WANASAYANSI wamestaajabu kwa muda mrefu jinsi ambavyo wadudu, wakiwa na miili mizito na mabawa dhaifu, huweza kubaki hewani. Viumbe hawa wadogo huelekea kupuuza kanuni za kawaida za elimu mwendo. Sasa watafiti katika Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza, wamevumbua jinsi ambavyo wadudu hufanya tendo hili lielekealo kuwa gumu sana.
Ili kujifunza kuhusu mruko wa mdudu, wanasayansi hao walifunga uzi wa pamba kumzunguka nondo aitwaye hawkmoth aliyewekwa kwenye njia ya upepo. Waliingiza kwa pampu moshi usio na sumu na wakaona jinsi moshi ulivyosonga nondo huyo alipopigapiga mabawa yake. Halafu, wakajenga kigezo chenye ukubwa wa mara 10 zaidi ambacho kilisogeza mabawa yake mara 100 polepole zaidi na wakatazama kwa matokeo yaliyoonekana wazi sasa. Walipata kuwa wakati mabawa ya nondo yalipoanza kupiga kuelekea chini, kizingia, au kizingia cha hewa, kinafanyizwa chini ya bawa. Kanieneo kidogo juu ya bawa hutokeza mwinuko, ikimvuta mdudu kuelekea juu. Kizingia kikiisha, nondo angepoteza mwinuko na kuporomoka chini. Badala ya hivyo, mzunguko wa hewa husonga kandokando ya bawa la mbele kuelekea kwenye ncha ya bawa, na hivyo mwinuko unaofanyizwa na kupiga mabawa kuelekea chini, unaolingana na mara moja na nusu ya uzito wa nondo, humwezesha mdudu huyo kupeperuka kwa urahisi.
Wahandisi wa vyombo vya angani tayari walijua kwamba ndege iitwayo delta-wing (yaitwa hivyo kwa sababu yafanana na herufi ya Kigiriki Δ) hutokeza vizingia kwenye ncha za mabawa, vitokezavyo mwinuko. Lakini sasa kwa vile wanajua jinsi ambavyo vizingia hutokeza mwinuko kwa wadudu wanaopigapiga mabawa yao, wanataka kuchunguza jinsi ya kutumia kwa kujifaidi ajabu hiyo katika kubuni propela na helikopta.