Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 11/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kizazi Kilichokata Tumaini
  • Mvurugo wa Kituo cha Angani
  • Nyani Wataka-Vita
  • Wavutaji Katika Asia
  • Seminari Yalegeza Sera juu ya Ngono
  • Vitafuno na Kuoza kwa Jino
  • Itikadi ya Wanasayansi Katika Mungu
  • Virusi Vinavyosafiri Ulimwenguni
  • Ule Mto Ganges Unaotoweka
  • Uharamia Waenea Upesi
  • Jinsi Unavyoweza Kutunza Meno Yako
    Amkeni!—2005
  • Kwa Nini Umwone Daktari wa Meno?
    Amkeni!—2007
  • Kuyalinda Meno Dhaifu
    Amkeni!—2000
  • Historia ya Maumivu ya Meno
    Amkeni!—2007
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 11/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Kizazi Kilichokata Tumaini

Uchunguzi mbalimbali unaolinganisha mitazamo ya vijana wa leo wenye umri wa miaka 15 hadi 24 na vijana wa vizazi viwili vilivyopita, umefunua kwamba kuna ongezeko katika matumizi mabaya ya madawa, viwango vya uhalifu, na kujiua, laripoti The Australian. Richard Eckersley, mchanganuzi stadi aliye pia mwandikaji wa sayansi, alijumlisha hisia za vijana wengi leo, akisema: “Vijana huamini kwamba maisha yanapaswa kuwa yenye kusisimua na kufurahisha, kwamba wanahitaji kujitegemea, kwamba wapaswa kuchagua mtindo-maisha wowote watakao, kwamba serikali haziwezi kusuluhisha matatizo ya jamii, na kwamba wao [vijana] hawana uwezo wowote wa kubadilisha hali za kijamii.” Msichana mmoja mwenye umri wa miaka 15, anayeitwa Shanu, alisema: “Idadi ya watu inaongezeka na tunahitaji kushindania kazi chache za kuajiriwa, makao haba, na uhaba wa kila kitu.”

Mvurugo wa Kituo cha Angani

Baada ya miaka 11, wale wanaotumia kituo cha angani cha Urusi kiitwacho Mir wanajifunza kukabiliana na tatizo lililo la kawaida kwa wakazi wa dunia—jambo la kufanya na takataka zilizoongezeka. Katika anga isiyokuwa na uzito, vifaa vya lazima kama vile mavazi ya angani, nyaya za kompyuta, vifurushi vya chakula, vyombo, na spea ni lazima zifungwe kwenye sakafu, darini, na kwenye kuta. Lakini vitu vikiwa vimerundamana kwa karibu sentimeta 30 katika sehemu zote, kuta za Mir zaelekea kumaliza nafasi. Kituo cha Anga cha Kimataifa kilicho kipya kitakapopelekwa angani, kitu kimoja ambacho wanaanga wataweza kuwa nacho ni kifaa kilichojengwa ndani cha takataka. Hilo bila shaka lingethaminiwa sana, kwa kuwa mpaka sasa, baada ya chakula, wakazi wa Mir wamekuwa wakiponda mikebe na kuiweka mikebe iliyo tupu ndani ya masanduku ya chakula, na kuzifunga kwenye kuta.

Nyani Wataka-Vita

Madereva katika mojawapo ya barabara kuu zilizo na shughuli zaidi za Afrika Kusini walikutana na hatari isiyo ya kawaida mapema mwaka huu—mawe mengi yanayovurumishwa na kundi la nyani. Kulingana na International Herald Tribune, nyani hao waliwavamia watumiaji wa barabara ipitayo kati ya milima iunganishayo Cape Town na Johannesburg. Ingawa hakukuwa na ripoti kuhusu majeruhi au aksidenti za magari, polisi wa barabarani, walipigana na nyani kwa mawe katika jitihada ya kuwaondoa wanyama hao kutoka kwenye barabara kuu. Hakukuwa na washindi dhahiri kabisa walioripotiwa katika vita hii ya kurushiana mawe kati ya polisi na nyani.

Wavutaji Katika Asia

Inakadiriwa kuwa katika Vietnam karibu asilimia 73 ya wanaume wote huvuta sigareti. Hiki ndicho “kiwango cha juu zaidi cha wavutaji wa sigareti miongoni mwa wanaume katika dunia,” waripoti utafiti uliochapishwa katika The Journal of the American Medical Association. Kwa kulinganisha, yaonekana kuwa zaidi ya asilimia 4 tu ya wanawake wa Vietnam huvuta sigareti. Nchi nyinginezo za Asia zinazopakana na Bahari ya Pasifiki zinafuata kiolezo hichohicho. Kwa mfano, katika Indonesia asilimia 53 ya wanaume na asilimia 4 ya wanawake huvuta sigareti; huku katika China, asilimia 61 ya wanaume na asilimia 7 ya wanawake huvuta sigareti.

Seminari Yalegeza Sera juu ya Ngono

Seminari ya Kanisa la Episkopali katika Virginia “imelegeza sera yake ya miaka 25 inayozuia wanafunzi na wahadhiri kutofanya ngono bila ya ndoa na mwenendo wa ugoni-jinsia-moja,” laripoti gazeti The Christian Century. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter J. Lee, alisema: “Ni lazima tukiri kwamba wanaseminari wengi wako katika miaka yao ya 30 au 40. Hakuna wanawake wa kusimamia wala hakuna ukaguzi unaofanywa usiku kuona kama watu fulani hawapo.” Kwa miaka 11 iliyopita ujiandikishaji katika seminari hiyo umepungua kwa asilimia 33. Kwa kuongezea, kwa miaka 25 iliyopita, wastani wa umri wa wanafunzi wanaojiunga na seminari umeongezeka kutoka umri wa miaka 27 hadi umri wa miaka 40. “Kile ninachojaribu kufanya nikiwa mwenyekiti wa kamati ni kuzuia mwingine wa miaka 28 asinyimwe nafasi ya kujiandikisha kwa sababu tuligundua alikuwa anafanya ngono na mchumba wake,” akasema Lee.

Vitafuno na Kuoza kwa Jino

Imejulikana kwa muda mrefu kwamba kupunguza kula vyakula vyenye sukari kwaweza kusaidia kupunguza kuoza kwa jino. Hata hivyo, lililo la maana zaidi ni kuangalia wakati na mara ngapi unapokula vitafuno, laripoti mwongozo wa familia kuhusu meno, How to Keep Your Family Smiling. Peremende au kabohidrati zilizosafishwa zinapokutana na utando wa meno yako, asidi hufanyizwa. Asidi hii, nayo hushambulia jino lako kwa karibu dakika 20, yasema hiyo broshua. Katika wakati huu, vijishimo vyaweza kuanza. Zaidi ya hilo, “hili laweza kutokea kila wakati ulapo vitafuno vyenye sukari au wanga.” Kwa hiyo ikiwa unataka kula vitafuno, “ni afadhali kula kitu kizima mara moja,” na hivyo kuhatarisha meno yako kwa asidi mara moja tu. Ama sivyo, kurudia-rudia kula hicho kitafuno kwa muda mrefu wa wakati hutokeza shambulio refu la asidi. Ili kuzuia kuoza kwa jino, madaktari wa meno wanapendekeza, upige meno yako mswaki kwa angalau mara mbili kwa siku. Pia, usisahau kusafisha katikati ya meno kila siku kwa kutumia nyuzi za kusafishia meno.

Itikadi ya Wanasayansi Katika Mungu

Katika mwaka wa 1916, mwanasaikolojia Mmarekani James Leuba, aliuliza wanasayansi 1,000 walioteuliwa kivivi-hivi ikiwa waliamini katika Mungu. Jibu lao? Miongoni mwa wanasayansi waliojibu, asilimia 42 waliitikadi katika Mungu, laripoti The New York Times. Leuba alibashiri kuwa itikadi katika Mungu ingedidimia wakati elimu ingesambaa. Sasa, baada ya miaka 80 baadaye, Edward Larson, wa Chuo Kikuu cha Georgia, amerudia kufanya uchunguzi maarufu wa Leuba. Akitumia maswali yaleyale na njia zilezile, Larson aliuliza wanabiolojia, wanafizikia, na wanahisabati ikiwa waliamini katika Mungu anayewasiliana na wanadamu. Matokeo yaonyesha kwamba karibu idadi sawa ya wanasayansi leo, wapatao asilimia 40, huitikadi katika Mungu. Kulingana na Dakt. Larson, “Leuba hakufahamu vizuri ama uwezo wa binadamu wa kusababu ama uwezo wa sayansi wa kutimiza mahitaji yote ya binadamu.”

Virusi Vinavyosafiri Ulimwenguni

Matangi ya maji machafu ya ndege huwa na kemikali ambazo hukusudiwa kuua virusi, lakini virusi vingine huokoka hata vinapowekewa kemikali hiyo, laripoti gazeti New Scientist. Mark Sobsey, mwanasayansi wa mazingira kwenye Chuo Kikuu cha North Carolina, alipata kwamba karibu nusu ya maji machafu aliyoyafanyia majaribio kutoka kwa ndege zinazosafiri kimataifa zinazotua Marekani yalikuwa na virusi hai. Katika Marekani takataka zinazotoka kwenye ndege kwa kawaida hushughulikiwa katika vituo vya umma vya maji machafu na baadaye hutupwa kwenye mazingira. Kwa hiyo kuna hatari ya kwamba baadhi ya virusi hivi vyaweza kusambaza magonjwa kama vile mchochota-ini aina ya A na E, uvimbe wa utando wa ubongo, na ugonjwa wa kupooza. Sobsey aongezea: “Unamna-namna wa magonjwa ambayo yanaweza kusambazwa na mashirika ya ndege ulimwenguni watia wasiwasi sana.”

Ule Mto Ganges Unaotoweka

Ule mto Ganges, uitwao Ganga katika India, hufikiriwa kuwa mtakatifu na mamia ya mamilioni ya Wahindu. Mto Ganges pia ni tegemezo kuu la kilimo kandokando katika njia yake yote. Lakini sasa maji yake yanadidimia kwa kasi, yakiacha maeneo mapana ya ardhi kavu kati ya huo mto na zile zilizokuwa kingo zake, laripoti India Today. Maji yake ambayo yamepungua kwa haraka yaonekana kama ni matokeo ya mvua zisizotosha na vilevile matumizi yaliyoongezeka ya maji ya mto kwenye sehemu za juu kwa ajili ya umwagiliaji. Mbali na kutisha kilimo katika eneo hili, mchangatope unaotokana na ukosefu wa maji waweza kusababisha bandari ya Calcutta isiweze kutumika, yasema ripoti hiyo.

Uharamia Waenea Upesi

Ripoti za mashambulizi ya maharamia zinaongezeka, lasema International Maritime Bureau—kutoka visa 90 katika mwaka wa 1994 hadi 226 miaka miwili tu baadaye. Ukuzi huu unawatia wasiwasi maofisa wanamaji wa biashara na watalii. Hata hivyo, tarakimu halisi yaweza kuwa mara mbili juu zaidi kwa kuwa, “wenye meli wengi hawajishughulishi kuripoti visa vinavyotokea kwa sababu uchunguzi ambao hufuatilia waweza kukawia na hivyo kusababisha gharama kubwa sana,” lasema The Sunday Telegraph la London. Maeneo ambayo karibuni yamekuwa yenye hatari hasa ni ile Bahari ya Mediterania karibu na Albania na Libya na Bahari ya China Kusini. Mwakilishi wa Uingereza wa Wanamaji wa biashara alisihi Uingereza iwe katika mstari wa mbele kwenye kikosi maalumu cha jeshi la kimataifa la UM la kupigana na maharamia. Lakini msemaji wa wenye meli alisema kwamba “haamini kama kikosi maalumu cha jeshi la UM kinaweza kufanya jambo lolote kuhusu tatizo hili kwa sababu mashambulizi mengi hutokea ndani ya mipaka ya mataifa,” gazeti hilo likaripoti.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki