Upasuaji Bila Kisu Kidogo cha Kupasulia
MWANZONI, hata ingawa Christine aliumwa na kichwa vikali sana, halikufikiriwa kuwa jambo la kushtua kwa hofu; kwa vyovyote kiliacha kuuma siku ileile. Lakini Christine akapata mavune ya shingo. Halafu kuumwa na kichwa kukarudi, akawa kanganya—dalili zisizo za kawaida kwa yeyote, hata kwa mtoto wa miaka minane.
Hospitalini eksirei ya kompyuta (CT) scan ilionyesha kwamba Christine alikuwa na arteriovenous malformation (AVM) katika ubongo wake—hali ambayo ateri huwa zimetatanika pamoja na mishipa ya damu.a Bila matibabu, huenda Christine hatimaye angepatwa na mshtuko wa akili wenye kuua.
Kufikia miaka ya majuzi AVM kama hizo zilikuwa zikitibiwa tu kwa kupasua ndani ya ubongo. Katika utaratibu huu, daktari-mpasuaji huvuta nyuma ngozi ya kichwa na nywele na hukata fuvu la kichwa. Kisha lazima aepuke vizuizi kupitia mzingile wa neva na tishu za ubongo ili afikie jeraha. Mapitio ya mafunzo ya utibabu yafunua kwamba katika mwaka wa 1995, kulikuwa na ugumu katika karibu asilimia 12 ya upasuaji wa AVM.
Wazazi wa Christine walipendelea Kisu cha Gamma badala ya kisu cha upasuaji. Jina lenyewe Kisu cha Gamma ladanganya kwa kiasi fulani, kwani Kisu cha Gamma si kisu halisi. Badala ya hivyo, ni mbinu inayotoa mihimili 201 iliyolengwa vizuri ya mnururisho kupitia fuvu la kichwa lisilopasuliwa. Kila mwali wa mwanga ukiwa pekee ni dhaifu sana kuweza kuharibu tishu unayopenyeza. Lakini mihimili yote 201 hulengwa kwa makini ili kupitisha na kutoa kipimo kikubwa cha mnururisho kwenye eneo halisi lenye jeraha.
Kisu cha Gamma kimethibitika kuwa chenye kupunguza gharama kwa kulinganisha matokeo, na kuna visa vichache vya maambukizo ya baada ya upasuaji kuliko ilivyo na upasuaji wa ubongo wa kawaida. Lakini utaratibu huu hutekelezwaje?
Zile Hatua Nne za Upasuaji wa Eksirei
Upasuaji wa eksirei kwa kutumia Kisu cha Gamma hufanywa katika hatua nne za msingi. Kwanza kichwa cha mgonjwa huwekwa katika fremu nyepesi ambayo itamshikilia mgonjwa ili asisonge wakati wa matibabu. Pili, “ramani” ya ubongo wa mgonjwa hutokezwa, kwa kutumia ama CT scan, magnetic resonance imaging (MRI), ama angiogram. Kisha, mifano ya ubongo huhamishwa hadi kwa mfumo wa matibabu wa mtambo wa kompyuta, ambao hutenganisha shabaha na kuhakikisha ni namba gani zinazotumika kuonyesha shabaha ilipo.
Hatimaye, ni wakati wa duru ya matibabu, ambapo kichwa cha mgonjwa huwekwa katika kofia ya chuma iliyo na mianya 201 ambayo miale ya gamma hutolewa. Muda wa matibabu? Dakika 15 hadi 45 tu, wakati ambao mgonjwa anatulizwa kidogo kwa dawa na hahisi maumivu.
Matibabu yanapoisha, mgonjwa hubaki hospitalini ili kuchunguzwa na kwa kawaida huruhusiwa kwenda nyumbani kufikia asubuhi inayofuata. Ilikuwa hivyo kwa Christine aliyetajwa mwanzoni. Alitibiwa Alhamisi, akaruhusiwa kurudi nyumbani Ijumaa, kurudi shuleni Jumatatu iliyofuata.
Ni Nini Hutendeka kwa Ile AVM?
Upasuaji wa eksirei hauharibu kihalisi ile arteriovenous malformation. Badala ya hivyo, hiyo husababisha chembe zilizo kandokando ya mishipa kuongezeka, hivyo zikiziba kabisa mtiririko wa damu kwenye eneo lililo na tatizo. Likiwa tokeo, labda kwa mwaka mmoja au miwili, mishipa iliyo na kasoro haipati tena gawio la damu. Kisha ile arteriovenous malformation hunywea na hatimaye huyeyushwa na mwili.
Kisu cha Gamma kimetumiwa pia kwa kutibu vivimbe vidogo vyenye kuleta dhara ambavyo vinaonekana vizuri vilevile na baadhi ya vivimbe vilivyoenea kwenye ubongo kutokana na kansa katika sehemu nyingine za mwili. Kwa kuongezea, tiba hii imeonyesha matokeo yenye kutazamisha kwa kutibu trigeminal neuralgia (hali yenye uchungu inayoathiri neva ya uso), kifafa, ugonjwa wa kutetemeka, na visa fulani vya uchungu usioisha haraka.
Bila shaka, kuna vivimbe fulani vya ubongo na hali ambazo Kisu cha Gamma hushindwa kutibu. Ikiwa maendeleo katika upasuaji wa eksirei yatatokeza matibabu yenye matokeo zaidi bado twangojea kuona. Kwa wakati huu, upasuaji wa eksirei kwa kutumia Kisu cha Gamma hutoa tumaini kwa wagonjwa wengi wenye vivimbe.
[Maelezo ya Chini]
a CT scan, ni picha ya eksirei ionyeshayo sehemu za ndani za mwili.
[Sanduku katika ukurasa wa 21]
Maendeleo ya Upasuaji wa Eksirei
Kisu cha Gamma kilitokezwa karibu miaka 50 iliyopita na mpasuaji wa ubongo Lars Leksell na mwanabiolojia-fizikia Börje Larsson. Leksell aligundua kwamba kipimo kimoja cha mnururisho kingeweza kuharibu jeraha lililojijenga katika ubongo bila kupasua—kwa sababu hiyo, bila kuvuja damu au hatari ya kupata ambukizo.
Leksell aliuita utendaji wake mpya upasuaji wa eksirei wa stereotactic. Hatimaye, madaktari walikuwa na namna ya kutibu sehemu za ubongo ambazo hapo mwanzoni hawangezifikia, bila kutumia kisu cha upasuaji ili kupitia kwa kupindapinda bila ustadi, mzingile wa neva na tishu za ubongo zenye kutaka uangalifu mkubwa. Hata hivyo, utumizi wa hatua hii mpya ulihitaji kungoja kwa miaka mingi maendeleo ya mbinu za kisasa za kupiga picha kama vile CT scan na MRI, ambazo zaweza kuwaonyesha wapasuaji mahali hususa pa kulenga mnururisho. Mtambo wa kwanza wa Kisu cha Gamma ulianzishwa katika Stockholm katika mwaka wa 1968.
[Picha katika ukurasa wa 20]
Zile Hatua Nne za Upasuaji wa Eksirei kwa Kutumia Kisu cha Gamma
1. Kuweka fremu
2. Kutokeza mifano ya ubongo
3. Mifano iliyowekwa katika kompyuta husaidia katika kupanga matibabu
4. Duru ya matibabu
[Hisani]
Mifano kwa hisani ya Elekta Instruments, Inc., watengenezaji wa Kisu cha Gamma®