Vijana Huuliza . . .
Namna Gani Kuonea Fahari Jamii Yako?
“Sikuzote mmoja wa wanashule wenzangu huzungumza juu ya jamii na rangi ya watu wengine,” atweta Tanya mwenye umri wa miaka 17. “Katika mengi ya maongezi yake, yeye hudai kuwa yu bora kuwapita.”
NI JAMBO la asili tu mtu kuonea fahari familia yake, utamaduni, lugha, au mahali alipotoka. “Mimi ni Mvietnam,” asema msichana mdogo mwenye umri wa miaka 15 anayeitwa Phung, “na ninaonea fahari utamaduni wangu.”
Ingawa hivyo, mara nyingi, kuonea fahari jamii wakati wote huambatana kwa ukaribu na ubaguzi wa jamii. Hivyo, fahari hiyo yaweza kuwa uovu ambao kwa hila huharibu uhusiano, hata inapokuwa imefichwa kwa hila na uungwana wa bandia. Yesu Kristo alisema: “Kutoka katika wingi wa moyo kinywa husema.” (Mathayo 12:34) Na hisia zenye kina kirefu za kujiona kuwa bora—au za madharau—mara nyingi hujitokeza, zikisababisha madhara na maumivu.
Nyakati nyingine hata kuonea fahari jamii hutokeza jeuri. Katika miaka ya majuzi kumekuwa kichochezi cha vita, ghasia, na “utakasaji wa kikabila.” Hata hivyo, huhitaji kuwa shahidi wa umwagikaji wa damu ili kukabili upande mbaya wa fahari ya jamii. Kwa kielelezo, je, unaona uthibitisho wake shuleni, kazini, au katika ujirani wako? “Kwa wazi, ndiyo,” aeleza kijana Mkristo anayeitwa Melissa. “Baadhi ya wanashule wenzangu huwafanyia mizaha watoto wanaoongea kwa matamshi ya kigeni, na husema wao ni bora kuwashinda.” Vivyo hivyo Tanya aripoti: “Shuleni nimewasikia watoto wakiwaambia wengine waziwazi: ‘Mimi ni bora kuliko wewe.’” Katika uchunguzi mmoja wa Marekani, karibu nusu ya waliohojiwa walisema kwamba walikuwa wamejionea kibinafsi aina fulani ya ubaguzi wa kijamii katika mwaka uliopita. “Uvutano wa kijamii shuleni mwetu umeenea sana,” asema kijana anayeitwa Natasha.
Sasa dhania unaishi katika nchi au eneo ambalo limekuwa na mmiminiko wa wahamaji, wakigeuza kwa kutazamisha hali ya shule yako, ujirani, au kutaniko la Kikristo. Je, unahisi kukosa starehe kidogo juu ya hili? Basi labda fahari ya jamii ni jambo ambalo linaongoza kufikiri kwako kuliko ulivyong’amua.
Fahari Inayofaa Dhidi ya Isiyofaa
Je, hili lamaanisha kwamba kwa asili fahari ni kitu kisichofaa? Si lazima iwe hivyo. Biblia huonyesha kwamba fahari ya aina inayofaa ina mahali pake. Wakati mtume Paulo alipoandikia Wakristo katika Thesalonike, alisema: “Sisi wenyewe twawaonea nyinyi fahari miongoni mwa makutaniko ya Mungu.” (2 Wathesalonike 1:4) Vivyo hivyo, kujistahi kwa angalau kiasi fulani ni jambo linalofaa na la kawaida. (Waroma 12:3) Kwa hiyo si kosa hasa kwa mtu kuonea fahari kwa kiasi fulani jamii yake, familia, lugha, rangi, au mahali alipotoka. Bila shaka Mungu hangetaka tuaibikie mambo kama hayo. Wakati mtume Paulo alipodhaniwa kuwa mhalifu Mmisri, yeye hakusita kusema: “Mimi, kwa kweli, ni Myahudi wa Tarso katika Kilikia, raia wa jiji ambalo si lenye kukosa umashuhuri.”—Matendo 21:39.
Hata hivyo, fahari ya jamii huwa mbaya inapositawisha hisia yenye kupita kiasi ya kujitukuza au wakati inaposababisha mtu awadharau wengine. Biblia husema: “Kumcha BWANA ni kuchukia uovu; kiburi na majivuno, na njia mbovu, na kinywa cha ukaidi pia nakichukia.” (Mithali 8:13) Na Mithali 16:18 hutaarifu: “Kiburi hutangulia uangamivu; na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko.” Kwa hiyo mtu kujisifu kuwa ni wa jamii iliyo bora zaidi ni jambo lenye kumchukiza Mungu.—Linganisha Yakobo 4:16.
Machimbuko ya Fahari ya Jamii
Ni nini husababisha watu wawe na fahari ya kupita kiasi juu ya jamii yao? Kitabu Black, White, Other, cha Lise Funderburg, chasema: “Kwa watu wengi, mawazo yao ya kwanza (na ambayo hudumu kwa muda mrefu zaidi) kuhusu jamii hutokana na wazazi na familia.” Kwa kusikitisha, mara nyingi pia mawazo yenye kupitishwa na wazazi fulani hayana usawaziko au yamepotoka. Huenda vijana fulani wakaambiwa waziwazi kwamba watu wa jamii yao ni bora zaidi na kwamba watu wa jamii nyingine ni tofauti au ni wa hali ya chini. Ingawa hivyo, mara nyingi, vijana huona tu wazazi wao hawajishughulishi hata kidogo na watu wa jamii nyingine. Hili pia laweza kuwa na uvutano mkubwa juu ya kufikiri kwao. Uchunguzi hufunua kwamba ingawa matineja na wazazi huenda wakakosa kuwa na maoni sawa juu ya mambo kama vile mavazi au muziki, vijana walio wengi hushiriki maoni ya wazazi wao juu ya jamii.
Mitazamo isiyosawazika kuhusu jamii yaweza pia kusitawi kutokana na uonezi na kutendwa vibaya. (Mhubiri 7:7) Kwa kielelezo, waelimishaji wameona kwamba watoto wa vinavyosemekana kuwa vikundi vidogo mara nyingi hukosa kujistahi. Katika kujaribu kurekebisha jambo hili, waelimishaji fulani wametokeza somo la shule linalofunza watoto historia ya jamii yao. Kwa kupendeza, wahakiki hubisha kuwa kukazia huku fahari ya jamii hutokeza tu ubaguzi wa kijamii.
Jambo linalompata mtu binafsi laweza pia kuchangia kusitawi kwa mitazamo isiyofaa ya kijamii. Tukio lisilopendeza kati yako na mtu wa jamii tofauti huenda likaongoza mtu kufikia mkataa wa kwamba washiriki wote wa jamii hiyo ni wenye kuchukiza au wenye kushikilia sana imani zao. Hivyohivyo hisia hasi zaweza kuamshwa wakati vyombo vya habari vinapokazia mahitilafiano ya kijamii, ukatili wa polisi, na maandamano ya kuteta au vinapoonyesha sifa mbaya za vikundi vya kikabila.
Ngano ya Ubora wa Kijamii
Vipi dai la wengine kwamba jamii yao ina haki ya kujihisi kuwa bora kuliko nyingine? Kwanza, wazo la kwamba watu kwa kweli wanaweza kugawanywa katika jamii hususa tofauti-tofauti linatilika shaka. Makala moja katika Newsweek iliripoti: “Kwa wanasayansi ambao wamefanya utafiti juu ya suala la jamii, jamii ni dhana iliyo ngumu sana kuelewa na ambayo si rahisi kufasili.” Kweli, kunaweza kuwa na “tofauti zenye kuonekana katika rangi ya ngozi, umbile-asili la nywele na umbo la macho au pua ya mtu.” Hata hivyo, Newsweek lilisema kwamba “tofauti hizi ni za kijuujuu tu—na hata wakijaribu namna gani, kwa msingi wanasayansi wameshindwa kuonyesha tofauti zozote kubwa ambazo hutofautisha kikundi fulani cha kijamii kutoka kwa kingine. . . . Kwa msingi, kwa wanasayansi wengi wanaofanya kazi katika nyanja hizi, jamii ni ‘dhana ya rangi tu’—mchanganyiko [uliofisidiwa] wa ubaguzi, ushirikina na ngano.”
Hata ikiwa tofauti za kisayansi kati ya jamii zingeweza kuonyeshwa, wazo la jamii “iliyotakata” ni ubuni. Kichapo The New Encyclopædia Britannica husema: “Hakuna jamii zilizotakata; vikundi vyote vya kijamii vilivyoko sasa vimechanganyikana kabisa.” Hata hali iweje, Biblia hufundisha kwamba Mungu “alifanya kutoka kwa mtu mmoja kila taifa la watu.” (Matendo 17:26) Bila kujali rangi ya ngozi, umbile-asili la nywele, au sura ya uso, kwa kweli kuna jamii moja—jamii ya kibinadamu. Wanadamu wote wana uhusiano kupitia baba yetu wa zamani Adamu.
Wayahudi wa kale walijua vema chanzo kimoja cha jamii zote. Na bado, hata baada ya kuwa Wakristo, wengine walishikilia itikadi ya kwamba walikuwa bora kuliko wasio Wayahudi—kutia ndani waamini wenzao wasio Wayahudi! Mtume Paulo alipinga kabisa dhana ya ubora wa jamii kwa kutaarifu, kama ilivyorekodiwa kwenye Waroma 3:9: “Wayahudi na vilevile Wagiriki wako chini ya dhambi.” Kwa hiyo hakuna kikundi cha kijamii kiwezacho kujisifu kuwa na msimamo wa pekee pamoja na Mungu. Kwa kweli, ni kupitia imani tu katika Yesu Kristo kwamba watu mmoja-mmoja wanaweza kuwa na uhusiano pamoja na Mungu. (Yohana 17:3) Na ni mapenzi ya Mungu kwamba “watu wa namna zote waokolewe na kuja kwenye ujuzi sahihi wa kweli.”—1 Timotheo 2:4.
Kutambua kwamba jamii zote ni sawa machoni pa Mungu kwaweza kuwa na matokeo yenye kutazamisha juu ya namna unavyojiona mwenyewe na unavyowaona wengine. Kunaweza kukusukuma kuwatendea wengine kwa adhama na staha, kuthamini na kuvutiwa na tofauti zao. Kwa kielelezo, Melissa mchanga, aliyetajwa mapema, hajiungi na wanashule wenzake katika kuwachekelea vijana wanaoongea kwa matamshi ya kigeni. Anasema: “Mimi huwaona wale wanaozungumza lugha mbili kuwa wenye akili. Ijapokuwa ningependa kuongea lugha nyingine, ninaweza kuongea moja tu.”
Kumbuka, pia, kwamba ingawa watu wa jamii na utamaduni wako bila shaka wana mengi ya kuonea fahari, ndivyo na watu wa jamii nyinginezo. Na ingawa huenda likafaa kuonea fahari kwa kiasi fulani utamaduni wako na yale yaliyotimizwa na wazazi wa kale waliokufa, inaridhisha zaidi kuonea fahari yale ambayo umetimiza binafsi kupitia jitihada na kufanya kazi kwa bidii! (Mhubiri 2:24) Kwa kweli, kuna jambo moja la kutimiza ambalo Biblia hukuhimiza uonee fahari. Kama inavyotaarifiwa kwenye Yeremia 9:24, Mungu mwenyewe husema: “Bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni BWANA.” Je, waweza kujisifia hilo?
[Picha katika ukurasa wa 26]
Kujua maoni ya Mungu juu ya jamii hutusaidia kufurahia ushirika wa watu wa jamii nyingine