Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 3/22 kur. 6-9
  • Mkazo Mzuri, Mkazo Mbaya

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mkazo Mzuri, Mkazo Mbaya
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Aina Tatu za Mikazo
  • Kuwa Mnyetivu kwa Mkazo
  • Jinsi ya Kudhibiti Mfadhaiko
    Amkeni!—2010
  • Jinsi Mfadhaiko Unavyotuathiri
    Amkeni!—2010
  • Visababishi na Madhara ya Mfadhaiko
    Amkeni!—2005
  • Mfadhaiko Hatari Kubwa kwa Afya
    Amkeni!—2010
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 3/22 kur. 6-9

Mkazo Mzuri, Mkazo Mbaya

“Kwa kuwa mkazo ni itikio la mwili lisilo hususa kwa mahitaji yoyote, kila mtu ana mkazo wa kadiri fulani nyakati zote.”—Dakt. Hans Selye.

ILI mcheza zeze aweze kutokeza muziki, ni lazima kamba kwenye chombo chake ziwe na mkazo—lakini kwa kadiri fulani tu. Kamba zikiwa na mkazo mno, zitakatika. Lakini kamba zikiwa legelege mno, hazitatokeza sauti kamwe. Mkazo ufaao upo mahali fulani katikati ya sehemu hizo mbili.

Ndivyo ilivyo na mkazo. Mkazo mwingi mno unaweza kudhuru, kama ambavyo tayari tumeona. Lakini namna gani kama hatuna mkazo kamwe? Ingawa tazamio hilo laweza kuonekana kuwa zuri, kwa kweli unahitaji mkazo—angalau kwa kadiri fulani. Kwa kielelezo, ebu wazia kwamba unapovuka barabara, kwa ghafula unaona gari likikuelekea kwa kasi. Ni mkazo unaokuwezesha kuepuka kujeruhiwa—haraka!

Lakini mkazo hausaidii katika hali za dharura pekee. Pia unahitaji mkazo ili utimize kazi zako za kila siku. Kila mtu ana mkazo wa kadiri fulani nyakati zote. ‘Njia ya pekee ya kuepuka mkazo ni kufa,’ asema Dakt. Hans Selye. Yeye aongezea kwamba ule usemi “ana mkazo” haumaanishi chochote kama ambavyo usemi “ana joto” usivyomaanisha chochote. “Tumaanishalo hasa na semi kama hizo,” asema Selye, “ni mkazo au joto la mwili la kupita kiasi.” Katika muktadha huu tafrija pia inahusisha mkazo, na ndivyo ilivyo na usingizi, kwa kuwa ni lazima moyo wako uendelee kupiga na mapafu yako yaendelee kufanya kazi.

Aina Tatu za Mikazo

Kama vile kulivyo na viwango mbalimbali vya mkazo, pia kuna aina mbalimbali za mkazo.

Mkazo mkali hutokana na mikazo ya maisha ya kila siku. Mara nyingi, hiyo huhusisha hali zisizopendeza ambazo zinahitaji kutatuliwa. Kwa kuwa hizo ni hali ambazo hutukia tu bila kutarajiwa na pia ni za muda tu, kwa kawaida mkazo huo waweza kudhibitiwa. Bila shaka, kuna wengine ambao hupata tatizo moja baada ya jingine—kwa kweli, utu wao huonekana kama umejaa mvurugo. Hata kiwango hiki cha mkazo mkali chaweza kudhibitiwa. Lakini, mwenye mkazo aweza kukinza hali za kubadili maisha yake, mpaka anapotambua matokeo ambayo mtindo-maisha wake wenye fujofujo humletea yeye na wale walio karibu naye.

Ingawa mkazo mkali ni wa muda tu, mkazo wa kudumu ni wa muda mrefu. Mwenye mkazo haoni njia ya kuondoa hali inayomletea mkazo, uwe ni ole wa umaskini au huzuni ya kufanya kazi inayodharauliwa—au kukosa kazi. Mkazo wa kudumu pia waweza kutokana na matatizo ya familia ambayo yanadumu. Kumtunza mtu wa ukoo asiyejiweza kwaweza kutokeza mkazo vilevile. Hata uwe unasababishwa na nini, mkazo wa kudumu hudhoofisha mtu siku baada ya siku, juma baada ya juma, mwezi baada ya mwezi. “Jambo baya zaidi kuhusu mkazo wa kudumu ni kwamba watu huuzoea,” chasema kitabu kimoja juu ya habari hiyo. “Watu hutambua mara moja mkazo mkali kwa sababu ni jambo jipya linalowapata; wao hupuuza mkazo wa kudumu kwa sababu ni jambo la zamani, ambalo wamelizoea, na, nyakati nyingi, hauwasumbui.”

Mkazo unaotokana na mfadhaiko ni athari ya msiba mkubwa, kama vile kubakwa, aksidenti, au msiba wa kiasili. Mashujaa wengi wa vita na waokokaji wa kambi za mateso hupatwa na mkazo wa aina hii. Dalili za mkazo unaotokana na mfadhaiko zaweza kutia ndani kumbukumbu zilizo dhahiri kabisa juu ya kisa kilichotokeza mfadhaiko huo, hata baada ya miaka mingi, pamoja na kuzidi kuwa mnyetivu kwa matukio madogo-madogo. Nyakati nyingine mwenye mkazo hupatikana kuwa anaugua hali iitwayo tatizo la mkazo unaotokana na mfadhaiko wa kisa kibaya kilichotokea (PTSD).—Ona sanduku juu.

Kuwa Mnyetivu kwa Mkazo

Wengine husema kwamba jinsi tunavyoitikia mkazo kwa wakati huu hutegemea sana kadiri ya mkazo na aina ya mkazo ambao tumepata kuwa nao katika wakati uliopita. Wao husema kwamba visa vibaya vyenye kuleta mfadhaiko vyaweza hasa kubadili “njia” ya kemikali ya itikio katika ubongo, ikimfanya mtu awe mnyetivu zaidi kwa mkazo katika wakati ujao. Kwa kielelezo, katika uchunguzi uliofanyiwa mashujaa 556 wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, Dakt. Lawrence Brass alipata kwamba wale ambao walikuwa wafungwa wa vita walikuwa na uwezekano wa mara nane wa kupatwa na mshiko wa moyo kuliko wale ambao hawakupata kuwa wafungwa wa vita—hata baada ya miaka 50 ya kisa cha kwanza cha mfadhaiko. “Ule mkazo anaopata mtu kwa kuwa mfungwa wa vita ulikuwa mkali sana hivi kwamba ulibadili jinsi watu hawa walivyoitikia mkazo katika wakati ujao—uliwafanya wawe wanyetivu kwa mkazo.”

Matukio yenye kuleta mkazo yaliyoonwa katika umri wa utoto hayapasi kupuuzwa, wataalamu wasema, kwa kuwa hayo yaweza kuwa na athari kubwa sana. “Watoto wengi wenye mfadhaiko hawapelekwi kutibiwa,” asema Dakt. Jean King. “Wao hupitia tatizo hilo, na kuendeleza maisha zao, na hatimaye kuja kutuona miaka mingi baadaye, wakiugua mshuko wa moyo au maradhi ya moyo.” Kwa kielelezo, fikiria, mfadhaiko wa kupoteza mzazi. “Mkazo wa kadiri hiyo unaotukia ukiwa ungali mchanga waweza kubadili njia ya itikio la ubongo,” asema Dakt. King, “ukifanya ubongo usiwe na uwezo sana wa kudhibiti mkazo wa kawaida, ambao hutukia kila siku.”

Bila shaka, jinsi mtu anavyoitikia mkazo inaweza kutegemea mambo mengine vilevile, kutia ndani hali yake ya kimwili na misaada mingi awezayo kupata ya kumsaidia kukabiliana na matukio yenye kuleta mkazo. Lakini, hata uwe umesababishwa na nini, mkazo unaweza kudhibitiwa. Kwa kweli, hilo si jambo rahisi. Dakt. Rachel Yehuda aonelea: “Kumwambia mtu ambaye amekuwa mnyetivu kwa mkazo kwamba atulie tu ni kama kumwambia mtu mwenye tatizo la kukosa usingizi alale tu usingizi.” Hata hivyo, kuna mengi ambayo mtu aweza kufanya ili kupunguza mkazo, kama vile makala ifuatayo itakavyoonyesha.

[Sanduku katika ukurasa wa 7]

Mkazo Unaotokana na Kazi—“Tukio la Tufeni Pote”

Ripoti ya Umoja wa Mataifa yasema: “Mkazo umekuwa mojawapo ya masuala mazito zaidi ya kiafya katika karne ya 20.” Kuwapo kwa mkazo kazini ni dhahiri sana.

• Idadi ya madai yanayohusiana na mkazo yaliyofanywa na wafanyakazi wa serikali nchini Australia imeongezeka kwa asilimia 90 katika kipindi cha miaka mitatu tu.

• Uchunguzi uliofanywa nchini Ufaransa ulifunua kwamba asilimia 64 ya wauguzi na asilimia 61 ya walimu husema kwamba wao wamekasirika kuhusu mazingira yenye kusababisha mkazo ambamo wao hufanyia kazi.

• Magonjwa yanayohusiana na mkazo hugharimu Marekani karibu dola bilioni 200 kila mwaka. Inafikiriwa kwamba asilimia zipatazo 75 hadi 85 kati ya aksidenti zote za kiviwanda zimehusiana na mkazo.

• Katika nchi baada ya nchi, wanawake walipatikana kuwa wanaugua kutokana na mkazo kuliko wanaume, yaelekea kwa sababu wao hufanya kazi nyingi zaidi nyumbani na kazini.

Kwa hakika, mkazo wa kazi ni “tukio la tufeni pote,” kama inavyotajwa na ripoti moja ya UM.

[Sanduku katika ukurasa wa 8]

PTSD—Itikio la Kawaida kwa Tukio Lisilo la Kawaida

‘Miezi mitatu baada ya gari letu kupata aksidenti, bado nilishindwa kuacha kulia, au kulala usiku. Hata kuondoka nyumbani kuliniogofya sana.’—Louise.

LOUISE augua kutokana na mkazo unaotokana na mfadhaiko wa kisa kibaya kilichotokea (PTSD), ambao ni ugonjwa wenye kudhoofisha unaojulikana kwa kumbukumbu zenye kujirudia-rudia au ndoto za tukio lenye kutokeza mfadhaiko. Mtu mwenye PTSD pia aweza kuwa mwenye kushtuka kupita kiasi. Kwa kielelezo, mtaalamu wa mambo ya akili Michael Davis asema juu ya shujaa mmoja wa Vietnam ambaye katika siku yake ya kufunga ndoa aliruka vichakani aliposikia sauti ya gari likitoa mlipuko. “Kulikuwa na ishara zote katika mazingira hayo ambazo zingalimwonyesha kwamba hali ni shwari,” asema Davis. “Ilikuwa ni miaka 25 baada ya vita; alikuwa Marekani, wala si Vietnam; . . . alikuwa amevaa koti jeupe, bali si mavazi ya vita. Lakini kichocheo cha kwanza kilipotokea, alitoroka kujificha.”

Mfadhaiko unaotokana na mambo ya vitani ni mmojawapo tu wa visababishi vya PTSD. Kulingana na The Harvard Mental Health Letter, tatizo hilo laweza kutokana na “tukio lolote au matukio fulani ambayo yanahusu kifo au tisho la kifo, au majeraha mabaya au tisho la kujeruhiwa kimwili. Inaweza kuwa msiba wa asili, aksidenti, au tendo la kibinadamu: gharika, moto, tetemeko la dunia, aksidenti ya gari, kulipuliwa kwa bomu, kufyatuliwa kwa risasi, mateso, kutekwa, kushambuliwa, kubakwa, au kumtenda mtoto vibaya.” Kushuhudia tu tukio baya au kulijua—labda kupitia ushuhuda wenye kutokeza sana au picha—kwaweza kutokeza dalili za PTSD, hasa ikiwa watu wenye kuhusika ni washiriki wa familia au marafiki wa karibu.

Bila shaka, watu huitikia mfadhaiko kwa njia tofauti-tofauti. “Watu wengi zaidi ambao hupitia mambo yenye kusababisha mfadhaiko hata hawasitawishi dalili mbaya za matatizo ya akili, na hata kama kuna dalili, hizo si lazima zifanane na zile za PTSD,” yaeleza The Harvard Mental Health Letter. Vipi kuhusu wale ambao mkazo wao hutokeza PTSD? Baada ya muda, wengine huweza kudhibiti hisia zinazohusiana na mfadhaiko na kupata kitulizo. Wengine huendelea kung’ang’ana na kumbukumbu za tukio lenye kuleta mfadhaiko miaka mingi baada ya tukio hilo kutukia.

Kwa vyovyote vile, wale wanaougua PTSD—na wale wanaotaka kuwasaidia—wapaswa kukumbuka kwamba kupata nafuu kwahitaji subira. Biblia huwahimiza sana Wakristo ‘waseme kwa kuliwaza nafsi zilizoshuka moyo’ na ‘wawe wenye ustahimilivu kuelekea wote.’ (1 Wathesalonike 5:14) Kwa Louise, aliyetajwa mwanzoni, miezi mitano ilipita kabla ya yeye kuweza tena kuendesha gari. “Japo maendeleo ambayo nimefanya,” yeye alisema miaka minne baada ya hiyo aksidenti, “siwezi kufurahia kuendesha gari kama zamani. Ni jambo ambalo ni lazima nifanye, kwa hiyo nalifanya. Lakini nimefanya maendeleo sana tangu wakati ule ambapo sikujiweza baada ya hiyo aksidenti.”

[Picha katika ukurasa wa 9]

Wafanyakazi wengi wa ofisini wana mkazo sana

[Picha katika ukurasa wa 9]

Si mkazo wote ulio mbaya kwako

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki