Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 4/22 kur. 20-24
  • Kupigania Kwetu Haki ya Kuhubiri

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kupigania Kwetu Haki ya Kuhubiri
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Msimamo Wangu kwa Ajili ya Kweli ya Biblia
  • Kukamatwa na Kutendwa Vibaya
  • Kesi
  • Mgawo Mpya wa Kuhubiri
  • Kukamatwa Tena na Kutiwa Gerezani
  • Mahakama Kuu Kuliko Zote Yaamua
  • Pigano Linaloendelea
  • “Kutetea na Kuthibitisha Kisheria Habari Njema”
    Mashahidi wa Yehova—Wapiga-Mbiu wa Ufalme wa Mungu
  • Wahubiri wa Ufalme Wanapeleka Kesi Mahakamani
    Ufalme wa Mungu Unatawala!
  • “Vitu vya Kuchukiwa na Mataifa Yote”
    Mashahidi wa Yehova—Wapiga-Mbiu wa Ufalme wa Mungu
  • Kulinda Kisheria Habari Njema
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 4/22 kur. 20-24

Kupigania Kwetu Haki ya Kuhubiri

Kama ilivyosimuliwa na Grace Marsh

Miaka michache iliyopita, Profesa Newton, ambaye wakati huo alishirikiana na Chuo cha Huntingdon katika Montgomery, Alabama, alinihoji kuhusu mambo yaliyofanyika zaidi ya miaka 50 iliyopita. Katika mwaka wa 1946 kesi ya mahakama iliyohusu utendaji wangu nikiwa mhudumu wa Mashahidi wa Yehova iliamuliwa na Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani. Upendezi wa Profesa Newton katika yale yaliyofanyika uliniletea kumbukumbu nyingi. Acha nianze na utoto wangu.

NILIZALIWA katika mwaka wa 1906, katika Randolph, Alabama, Marekani, nikiwa Mwanafunzi wa Biblia, kama Mashahidi wa Yehova walivyojulikana wakati huo, wa kizazi cha nne. Baba ya babu yangu Lewis Waldrop na babu yangu Sim Waldrop walibatizwa kuwa Wanafunzi wa Biblia katika mwisho-mwisho wa miaka ya 1800.

Mwana wa Sim Waldrop, Joseph, alikuwa baba yangu. Joseph alimvutia msichana aliyeitwa Belle kwa kumpa kijitabu kilichofunua fundisho la dini la moto wa helo. Belle alipendezwa sana na yale aliyosoma hivi kwamba alishiriki kijitabu hicho na baba yake, ambaye pia alipendezwa sana nacho. Baadaye Joseph alimwoa Belle, wakapata watoto sita. Mimi nilikuwa wa pili.

Kila usiku, Baba alikuwa akikusanya familia pamoja kuzunguka meko na alikuwa akisoma kwa sauti kutoka katika Biblia na gazeti la Mnara wa Mlinzi. Tulipomaliza kusoma, sote tulikuwa tukipiga magoti Baba alipokuwa akitoa sala yenye kuhisiwa moyoni. Kila juma, tulisafiri kilometa kadhaa katika kigari chenye kukokotwa na farasi hadi nyumbani mwa Babu yangu Sim kwa ajili ya mkutano pamoja na Wanafunzi wa Biblia wenzetu.

Shuleni wanadarasa wenzetu walitudhihaki, wakituita Waruseli. Hilo halikuwa tukano kama walivyolikusudia kuwa, kwani nilikuwa namstahi sana Charles Taze Russell, msimamizi wa kwanza wa Watch Tower Bible and Tract Society. Nilisisimuka jinsi gani kumwona kwenye kusanyiko katika Birmingham, Alabama, katika mwaka wa 1914! Ningali naweza kukumbuka akiwa amesimama jukwaani akiieleza ule wonyesho wa picha uitwao “Photo-Drama of Creation.”

Katika mwaka wa 1920 familia yetu ilihamia Robertsdale, mji mdogo mashariki mwa Mobile, Alabama. Miaka mitano baadaye niliolewa na Herbert Marsh. Herbert nami tulihamia Chicago, Illinois, na mwana wetu Joseph Harold, akazaliwa huko muda mfupi baadaye. Kwa kusikitisha, niligeukia mbali kutoka kwa dini ya utotoni, lakini ilikuwa ingali moyoni mwangu.

Msimamo Wangu kwa Ajili ya Kweli ya Biblia

Siku moja katika mwaka wa 1930, kwa ghafula nilitambua umuhimu wa kweli wakati nilipomwona bwana-kabaila akimwangusha kwa nguvu Mwanafunzi wa Biblia chini ngazini. Nilikasirika na kuzungumza na bwana-kabaila wetu kuhusu tabia yake. Aliniarifu kuwa ikiwa ningemkaribisha mwanamume huyo katika nyumba yetu, mume wangu nami hatungeendelea kuishi hapo. Kama ilivyotarajiwa, nilimkaribisha Mwanafunzi huyo wa Biblia kwa ajili ya kikombe cha chai.

Mume wangu nami tulihudhuria mkutano wa Wanafunzi wa Biblia Jumapili iliyofuata na tulifurahi kukutana na Joseph F. Rutherford, ambaye alikuwa amekuwa msimamizi wa Watch Tower Society baada ya kifo cha Russell. Wakati huo Rutherford alikuwa akitembelea Chicago. Matukio haya yalinisukuma niwe mtendaji tena katika huduma ya Kikristo. Muda mfupi baada ya hapo, tulihamia tena Robertsdale, Alabama.

Kwenye mkusanyiko mmoja katika Columbus, Ohio, katika mwaka wa 1937, niliamua kuwa painia, kama wahudumu wa wakati wote wa Mashahidi wa Yehova waitwavyo. Baada ya muda, mume wangu Herbert alibatizwa, na baada ya muda mfupi akaanza kutumikia akiwa mwangalizi-msimamizi katika Kutaniko la Robertsdale. Mwana wetu Harold, mara nyingi alikuwa mwandamani wangu katika huduma ya nyumba hadi nyumba.

Katika mwaka wa 1941, nilipokea mwaliko wa kutumikia nikiwa painia wa pekee katika Brookhaven, Mississippi. Violet Babin, dada Mkristo kutoka New Orleans, alikuwa mwenzi wangu. Tulikubali kichocheo hicho na tukachukua gari letu la kukokotwa pamoja na watoto wetu kuweka msingi katika Brookhaven. Waume wetu walikuwa wajiunge nasi baadaye.

Mwanzoni, tulikuwa na mafanikio katika utumishi wetu, Harold na binti ya Violet walikuwa wakifanya vizuri shuleni. Hata hivyo, baada ya Pearl Harbor kupigwa kwa bomu na Wajapani katika Desemba mwaka wa 1941 na Marekani kutangaza vita, mwitikio kuelekea kazi yetu ulibadilika kwa ghafula. Kulikuwa na roho ya uzalendo wa kupita kiasi na hofu ya njama. Kwa sababu ya kutokuwamo kwetu katika siasa, watu walitushuku, hata wakitushtaki kuwa wapelelezi wa Ujerumani.

Harold alifukuzwa shuleni kwa sababu ya kukataa kushiriki katika sherehe ya kusimamisha bendera. Mwalimu wake aliniambia kuwa Harold alikuwa mwerevu na mwenye tabia nzuri, lakini mkuu wa shule alihisi kuwa alikuwa kielelezo kibaya kwa sababu hakuisalimu bendera. Msimamizi wa shule alikasirishwa sana na uamuzi ambao mkuu wa shule na halmashauri ya shule walifanya katika jambo hili hivi kwamba alijiuzulu akajitolea kumlipia karo Harold katika shule ya kibinafsi!

Kila siku tulitishwa na vikundi vya wafanya-ghasia wenye jeuri. Katika tukio moja polisi walitusukuma kutoka katika mlango wa nyumba ya mama mmoja, wakavunja vinanda vyetu vya gramafoni kwenye mti, wakavunja rekodi zetu za mihadhara ya Biblia, wakararua Biblia zetu na fasihi vipande-vipande, na mwishowe kuchoma moto kila kitu walichokuwa wametwaa kutoka kwetu. Walituambia tuondoke mjini kabla hakujawa na giza au sivyo tungefukuzwa na kikundi cha wafanya-ghasia. Tuliandika barua upesi na kuzipeleka wenyewe kwa wakuu wa mji, tukiomba ulinzi. Lakini wakakataa kutupatia ulinzi wowote. Hata nilipiga simu kwa Idara ya Upelelezi ya FBI katika Jackson, Mississippi, na kuomba msaada. Wao pia walitushauri tuondoke mjini.

Usiku huo karibu wanaume mia moja wenye hasira walilizunguka gari letu la kukokotwa. Tulikuwa wanawake wawili peke yetu na watoto wetu. Tulifunga milango, tukazima taa, na kusali kwa Yehova kwa bidii. Mwishowe, umati ulitawanyika bila kutuumiza.

Baada ya kuona matukio haya, Herbert aliamua kujiunga nasi huko Brookhaven mara moja. Tulimrudisha Harold kwa wazakuu wake huko Robertsdale, ambapo mkuu wa shule wa huko alituhakikishia kuwa atapata elimu. Tuliporudi Brookhaven, gari la kukokotwa lilikuwa limeharibiwa na idhini ya kutukamata ilikuwa imepigiliwa msumari kwenye moja ya kuta za ndani. Licha ya kupingwa huku, tulisimama imara na kuendelea katika huduma yetu.

Kukamatwa na Kutendwa Vibaya

Katika Februari ya mwaka wa 1942, Herbert nami tulikamatwa tulipokuwa tukiongoza funzo la Biblia katika nyumba moja ndogo ya wastani. Mwanamume mwenye nyumba alikasirika sana kwa sababu ya jinsi tulivyotendwa hivi kwamba alichukua bunduki yake akatisha kumpiga risasi huyo polisi! Tulishtakiwa kwa kuingia bila ruhusa tukapatwa na hatia katika kesi iliyofanywa siku iliyofuata.

Tuliwekwa katika seli ndogo chafu, na yenye baridi kwa muda wa siku 11. Mhudumu Mbaptisti wa hapo alitutembelea tulipokuwa huko, akituhakikishia kuwa ikiwa tutakubali kuondoka mjini, angetumia mamlaka yake ili tuachwe huru. Tulifikiri hili lilikuwa kejeli, kwani mamlaka yake ndiyo iliyokuwa imetuingiza pale.

Pembe moja ya seli yetu ilikuwa imetumika kama choo hapo awali. Mahali hapo palijawa tele na kunguni. Chakula kiliandaliwa katika mikebe michafu, ambayo haikusafishwa. Likiwa tokeo la hali hizo, nilipatwa na nimonia. Daktari aliletwa kuniona, tukaachiliwa. Usiku huo kikundi cha wafanya-ghasia kilikuja kwenye gari letu la kukokotwa, kwa hiyo tulienda nyumbani Robertsdale kungojea kesi yetu.

Kesi

Wabaptisti kutoka sehemu zote za jimbo walikuja Brookhaven kwa ajili ya kesi yetu, ili kutegemeza mhudumu Mbaptisti ambaye alihusika katika kukamatwa kwetu. Hili lilinisukuma kumwandikia barua ndugu-mkwe wangu Oscar Skooglund, mhudumu madhubuti wa kanisa la Baptisti. Ilikuwa barua yenye hamaki ambayo haikuandikwa kwa busara sana. Hata hivyo, jinsi nilivyotendwa na kile nilichoandika lazima kilimwathiri Oscar kwa njia yenye mafaa, kwa sababu baada ya muda mfupi, akawa Shahidi wa Yehova mwenye bidii.

Mawakili wetu, G. C. Clark na Victor Blackwell, Mashahidi wa Yehova wenzetu, walikuwa wamesadiki kuwa hatungefanyiwa kesi ya haki huko Brookhaven. Kwa hiyo wakaamua kupinga kila kitu ili kesi itupiliwe mbali kwa sababu ya kupinga kulikoendelea. Kila wakati mwendesha-mashtaka aliposema jambo, mmoja wa mawakili wetu alilipinga. Walipinga angalau mara 50. Mwishowe, hakimu alitupilia mbali mashtaka yote.

Mgawo Mpya wa Kuhubiri

Baada ya kupumzika na kurudia afya yangu, nilirudia upainia pamoja na mwana wangu Harold. Katika mwaka wa 1943 tulipewa mgawo karibu na nyumbani, Whistler na Chickasaw, jumuiya ndogo karibu na Mobile, Alabama. Nilifikiri kuwa maeneo haya mapya yangekuwa yasiyo na hatari zaidi, kwani Mahakama Kuu Kuliko Zote ya Marekani ilikuwa imekata kesi kadhaa za Mashahidi wa Yehova kwa kuwapendelea na mwelekeo wa umma kuelekea kazi yetu ulikuwa umeanza kuboreka.

Upesi tulikuwa na kikundi cha wanafunzi wa Biblia katika Whistler, na tulihitaji mahali petu wenyewe pa kukutania. Mtu yeyote ambaye angeweza kutumia nyundo alifanya kazi katika Jumba la Ufalme letu dogo, na watu 16 walihudhuria mkutano wetu wa kwanza. Hata hivyo, Chickasaw, hali ilikuwa tofauti kwa sababu ulikuwa mji wa kampuni, uliomilikiwa na Shirika la Kutengenezea Meli la Gulf. Na bado, ulionekana kama mji mwingine wowote mdogo, ukiwa na kituo cha biashara, posta, na maduka ya kununua vitu.

Siku moja katika mwezi wa Desemba ya 1943, Aileen Stephens, painia mwenzi pamoja nami tulikuwa tukitoa magazeti yetu ya Biblia ya karibuni zaidi kwa wapita-njia katika Chickasaw wakati Naibu wa Chatham alipotuambia kuwa hatukuwa na haki yoyote ya kuhubiri, kwa vile tulikuwa katika mali ya kibinafsi. Tulieleza kwamba hatukuwa wachuuzi na tulikuwa tumelindwa na Mabadiliko ya Kwanza ya Katiba ya Marekani.

Kukamatwa Tena na Kutiwa Gerezani

Juma lililofuata Aileen nami tulikutana na E. B. Peebles, makamu wa msimamizi wa shirika la Kutengenezea Meli la Gulf tukaeleza umuhimu wa utendaji wetu wa kidini. Alituonya kwamba utendaji wa Mashahidi wa Yehova haungekubaliwa katika Chickasaw. Tulieleza kwamba watu walikuwa wametukaribisha kwa furaha nyumbani mwao. Je, angewanyima haki ya kujifunza Biblia? Akawa mwenye uhasama akatisha kututia gerezani kwa ajili ya kuingia bila ruhusa.

Nilirudi Chickasaw mara kwa mara na kila wakati nilikamatwa. Lakini kila wakati, niliachiliwa kwa dhamana. Hatimaye, dhamana hiyo iliongezwa kuwa kiasi kikubwa sana cha pesa, na ningetumia wakati mwingi zaidi na zaidi katika gereza hadi tulipoweza kupata hizo pesa. Hali za gerezani zilikuwa chafu—hakukuwa na choo, magodoro yalikuwa machafu bila shuka za kulalia, na blanketi moja chafu ya kujifunikia. Likiwa tokeo, matatizo yangu ya afya yaliibuka tena.

Katika Januari 27, 1944, kesi za Mashahidi sita ambao walikamatwa Desemba 24, 1943, zilisikizwa pamoja, na ushuhuda wangu ulionwa kuwa mwakilishi wa washtakiwa wale wengine. Hata ingawa kesi hiyo ilionyesha ubaguzi wa wazi dhidi ya Mashahidi wa Yehova, nilipatikana na hatia. Tulikata rufani kwa ajili ya uamuzi huo.

Katika Januari 15, 1945, mahakama ya kukata rufani ilitangaza uamuzi: Nilipatikana na hatia ya kuingia bila ruhusa. Zaidi ya hilo, Mahakama Kuu Kuliko Zote ya Alabama ilikataa kusikiliza kesi yangu. Katika Mei 3, 1945, Hayden Covington, mmoja wa Mashahidi wa Yehova aliye wakili jasiri na mwenye nguvu, alitoa ombi la bidii kwa Mahakama Kuu Kuliko Zote ya Marekani kwa ajili ya kukata rufani.

Huku Aileen nami tukingojea kusikia kutoka kwa Mahakama Kuu Kuliko Zote, tuligeuza mashtaka kuelekea washtaki wetu na tukafungua mashtaka dhidi ya E. B. Peebles na waliomuunga mkono katika idara ya liwali, tukiomba kulipwa hasara. Washtaki wetu walijaribu kubadili shtaka lao dhidi yetu liwe kwamba tulizuia upitaji wa watu badala ya kuwa tuliingia bila ruhusa, lakini nilipokuwa gerezani, nilikuwa nimechukua kisiri karatasi iliyokuwa na sahihi ya Naibu wa Chatham, ikitushtaki kuwa tuliingia bila ruhusa. Wakati ushuhuda huu ulipotolewa kortini, Liwali Holcombe aliruka akasimama na karibu ameze biri yake! Kesi ya Februari 1945, iliishia na baraza la mahakama lisiloweza kuamua.

Mahakama Kuu Kuliko Zote Yaamua

Mahakama Kuu Kuliko Zote ya Marekani ilipendezwa na kesi yangu kwa sababu kuingia bila ruhusa katika mali ya kibinafsi kulitokeza mwelekeo wa lile swali la uhuru wa kidini. Covington alithibitisha kuwa kanuni ya Chickasaw ilihalifu si uhuru wa washtakiwa tu bali pia wa umma kwa ujumla.

Katika Januari 7, 1946, Mahakama Kuu Kuliko Zote ya Marekani ilibadili uamuzi uliokuwa umetolewa na mahakama ya chini, ikatoa uamuzi wa kihistoria uliotupendelea. Hakimu Black alitoa uamuzi, ambao ulitia ndani maneno haya: “Kwa kiasi ambacho Serikali [ya Alabama] imejaribu kutwika adhabu ya uhalifu juu ya mkata-rufani [Grace Marsh] kwa kuchukua daraka la kugawanya fasihi za kidini katika mji wa kampuni, hatua yake haiwezi kuvumilika.”

Pigano Linaloendelea

Mwishowe Herbert nami tulifanya makao huko Fairhope, Alabama, tukaendelea kufanyia kazi masilahi ya Ufalme kwa muda wote. Herbert alikufa katika mwaka wa 1981, lakini nina kumbukumbu nyingi zenye furaha za wakati tulipokuwa pamoja. Mwana wangu, Harold, aliacha kumtumikia Yehova baadaye maishani na kufa upesi baada ya hapo, katika mwaka wa 1984. Hilo lilikuwa mojawapo ya maumivu makali zaidi ya moyoni niliyopata maishani.

Hata hivyo, ninafurahi kwamba Harold na mke wake, Elsie, walinipatia wajukuu watatu wazuri wa kike na kwamba sasa nina vitukuu ambao ni Mashahidi waliobatizwa. Watatu kati ya dada zangu, Margaret, Ellen Jo, na Crystal, wangali hai na wanaendelea wakiwa watumishi wa Yehova waaminifu. Crystal aliolewa na Lyman Swingle, ambaye ni mshiriki wa Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova. Wanaishi katika makao makuu ya ulimwengu ya Mashahidi wa Yehova, katika Brooklyn, New York. Licha ya matatizo makubwa ya afya katika miaka michache iliyopita, Crystal amebaki akiwa kielelezo bora na kitia-moyo kwangu.

Katika miaka yangu zaidi ya 90, nimejifunza kutohofu kamwe kile mwanadamu aweza kufanya, kwani Yehova ni mwenye nguvu zaidi kuliko liwali yeyote, hakimu yeyote, mtu yeyote. Ninapofikiria matukio haya ya wakati uliopita, ninathamini sana pendeleo la kuwa na sehemu katika “kutetea na kuthibitisha kisheria habari njema”!—Wafilipi 1:7.

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

Kutiwa Nguvu kwa Kulindwa na Katiba

Katika 1995, Merlin Owen Newton aliandika kitabu Armed With the Constitution, kitabu ambacho hutokeza fungu la Mashahidi wa Yehova katika kuelewesha matumizi ya Mabadiliko ya Kwanza ya Katiba ya Marekani. Wakati huo, Bi. Newton alikuwa profesa mshiriki wa historia na sayansi ya siasa katika Chuo cha Huntingdon katika Montgomery, Alabama. Kitabu chake kilichofanyiwa utafiti kikamili na chenye uthibitisho wa kutosha hupitia kesi mbili katika Alabama ambazo zilipelekwa hadi kwenye Mahakama Kuu Kuliko Zote ya Marekani.

Mojawapo ya kesi hizi ilihusisha Grace Marsh, ambaye hadithi yake inayomtaja iko katika makala inayoandamana. Kesi ile nyingine, Jones v. City of Opelika, ilihusisha haki ya kueneza itikadi za kidini kwa njia ya ugawanyaji wa fasihi. Rosco na Thelma Jones, wenzi weusi waliooana, walikuwa wahudumu wa wakati wote wa Mashahidi wa Yehova.

Alipokuwa akitayarisha kitabu chake, Profesa Newton alitumia magazeti ya wakati uleule na majarida ya kisheria, habari za maisha na barua za Mashahidi, mahojiano na habari iliyochapishwa na Mashahidi wenyewe, na uchunguzi wa kisomi wa utendaji wa Mashahidi. Mambo yenye kina ya kuvutia sana na mrudisho wa kibinafsi uliotolewa na washtakiwa, mawakili, na mahakimu, katika kitabu Armed With the Constitution yametokeza sehemu ya historia ya kisheria ya Mashahidi wa Yehova.

[Picha katika ukurasa wa 20]

Nikiwa na babu yangu Sim Waldrop

[Picha katika ukurasa wa 23]

Grace Marsh leo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki