Calcutta—Jiji Lenye Pilikapilika na Utofautiano
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA INDIA
KWA maoni ya mwandikaji wa kitabu aliye Mwingereza Rudyard Kipling, Calcutta lilikuwa “jiji lenye usiku wa maogofyo,” “mji hatari uliojaa watu.” Lakini kwa maoni ya mshairi maarufu wa Kiurdu Mīrzā Ghālib, Calcutta lilikuwa “jiji lenye kuburudisha” na “jiji la kimbingu.” Mwandikaji wa vitabu Dominique Lapierre aliona kila ziara yake kwenye jiji hilo kuwa “uvutio mpya wa ajabu,” ilhali Peter T. White, akiandika katika National Geographic, alinukuu wengine ambao walitaja kwamba jiji hilo lilikuwa “lenye kuogofya, lenye kuchukiza, na lenye kuhofisha. Mtaa mkubwa zaidi wa mabanda ulimwenguni.” Bila shaka, Calcutta (Kibengali, Kalikata) ni jiji lenye utofautiano.
Mwanzo wa Calcutta
Calcutta, ambalo liko kwenye pwani ya kaskazini-mashariki ya India katika jimbo la West Bengal, halipo katika historia ya kale ya India. Likilinganishwa na majiji kama Delhi na Thanjavur, Calcutta ni jiji changa. Kama ilivyo na majiji mengi, mwanzo wa Calcutta ulitegemea ule mto mkubwa wa Ganges. Unapokaribia Ghuba ya Bengal, mto Ganges hujigawanya na kuwa mito miwili na mingine zaidi na kufanyiza delta kubwa zaidi ulimwenguni. Kingo ya magharibi ya delta hiyo ina mto ambao zamani uliitwa Bhagirathi-Ganga, baadaye ukaitwa Hooghly, ambao huelekea kusini hadi baharini.
Katika karne ya 15 na 16, wafanyabiashara Wareno, Waholanzi, na Waingereza waliabiri hadi Hooghly na kwa idhini ya watawala wa huko, walianzisha vituo vya biashara. Job Charnock, ofisa mmoja wa Kampuni ya British East India, alichagua kijiji cha Sutanuti kuwa kituo cha biashara. Baada ya kushindwa mara kadhaa, aliabiri hadi Sutanuti na baada ya kushawishi vijiji vya Govindpur na Kalikata, akaanzisha makazi ya Uingereza badala ya kituo tu cha biashara. Ilikuwa Agosti 24, 1690. Calcutta likaanzishwa!
Waingereza walipata haki ya kukaa huko mnamo 1698, na kufikia mwaka wa 1757 Waingereza waliwalipa kodi watawala wa Mogul. Waingereza wakajenga ngome iliyoitwa Fort William ili kulinda kijeshi jiji hilo lililokuwa likikua. Wafanyabiashara wakaanza kujenga majumba makubwa kwa sababu ya usalama wa Fort William. Wakati huo idadi ya watu katika mji huo na vijiji vilivyokuwa karibu ilikuwa imefikia 400,000, na biashara ilikuwa ikileta meli zipatazo 50 kwa mwaka kwenye Mto Hooghly.
Gereza la Adhabu la Calcutta
Mnamo 1756, mtawala mmoja mchanga aliye kimbelembele, Sirāj-ud-Dawlah wa Bengal, alishambulia Calcutta. Wakazi wengi walitoroka, lakini Wazungu fulani ambao walikimbilia himaya katika Fort William walisalimu amri na kufungwa katika gereza dogo wakati wa joto kali la Juni. Siku iliyofuata, wengi walipatikana wakiwa wamekufa kwa kukosa hewa. Hapo pakaitwa Gereza la Adhabu la Calcutta.
Tukio hilo likaghadhabisha Kampuni ya East India, na mnamo 1757, Robert Clive aliongoza kikosi cha wanajeshi wa Uingereza wautwae tena mji huo. Inasemekana kwamba Vita vya Plassey vilivyofuata ndivyo vilivyoanzisha utawala wa Uingereza katika India. Na matokeo yakawaje kwa Calcutta? Mnamo 1773 likawa jiji kuu la British India, likidumu hivyo mpaka 1911.
Calcutta Larekebishwa
Mali nyingi sana zilipomiminika katika jiji hilo, majengo yenye fahari yalijengwa, yakifanya Calcutta liitwe Jiji la Kasri. Barabara pana zilijengwa, na majumba ya makumbusho na maktaba yakajengwa. Mengi ya majengo hayo yenye kuvutia ambayo yangali yapo leo yathibitisha jambo hilo.
Baada ya kutawalwa na Uingereza kwa miaka 190, India ilipata uhuru mwaka wa 1947, ikiongozwa na Mohandas Gandhi na Jawaharlal Nehru, na mgawanyiko ukatokea. Mataifa mapya ya Kiislamu ya Pakistan Mashariki na Pakistan Magharibi nayo yakafanyizwa, yakiongozwa na Mohammed Ali Jinnah. Kisha, katika mwaka wa 1971, Pakistan Mashariki ikawa Bangladesh. Matukio hayo yalifanya wakimbizi wamiminike Calcutta; na leo eneo la jiji hilo linakadiriwa kuwa na zaidi ya watu 12,000,000.
Mmiminiko wa ghafula wa watu wengi ambao hawana ruzuku ulitokeza matatizo makubwa sana. Kwa sababu ya ukosefu wa makao, mamilioni ya watu waliishi katika mitaa ya mabanda ya hali ya chini zaidi ambayo ilijengwa kwa makaratasi mazito na kitani na ambayo haikuwa na njia za kuondolea maji machafu, wala umeme, wala maji. Maelfu wengine waliishi barabarani. Mwaka wa 1967, wataalamu tisa wa mpango wa mji waliripoti kwamba hali ya Calcutta ilikuwa “inazorota haraka kufikia hatua ambapo haingeweza kusimamiwa kwa mambo ya uchumi, makao, njia za kuondolea maji machafu, usafiri na mambo mengine muhimu kwa maisha.” Wakati ujao ukaonekana kuwa mbaya sana.
Katika jitihada za kuongeza makao, hasa kwa ajili ya watu wenye mapato kidogo, eneo kubwa lenye matope ya chumvi lilitumiwa. Pia kwa kuondoa matope mtoni ili kulijaza bwawa hilo, hali ya usafiri wa majini iliboreshwa.
Katika miaka ya mapema ya 1990, watu wa mataifa mengine waliweka mali nyingi nchini India, na Calcutta halikutaka kusahauliwa. Basi kazi kubwa ya usafi ilianza kufanywa. Wakazi wa mitaa ya mabanda walihamishwa wakakae nje ya jiji, takataka zilitumiwa kufanyiza umeme na mbolea, na magari na meko yenye kutoa moshi mwingi yakapigwa marufuku. Barabara zilipanuliwa, na maduka makubwa yakajengwa. Vikundi vya wakazi vilisafisha jiji na kulipaka rangi. Calcutta liliokolewa lisipatwe na msiba na kuhuishwa tena hivi kwamba jiji hilo lililokuwa ‘likifa,’ na ‘lenye msiba’ likawa lenye pilikapilika tena. Katika ripoti moja ya 1997 juu ya mafaa na kupatikana kwa vitu, Calcutta ilishinda kwa mbali majiji mengine makubwa ya India.
Kituo cha Biashara
Kwa sababu ya kuwapo kwa wakimbizi kutoka nchi za ujirani, wahamaji kutoka majimbo mengine ya India, Wabengal wenyeji, Wachina, na Waarmenia ambao ni wakazi wa muda mrefu, jiji hilo limekuwa mchanganyiko mkubwa wa lugha, tamaduni, dini, na vyakula. Ni nini kilichowavutia mamilioni ya watu hao wote kwenda Calcutta? Biashara! Meli kutoka ulimwenguni kote zilitia nanga kwenye bandari hii ambapo Mashariki ilikutana na Magharibi. Vifaa vilivyosafirishwa nje vilitia ndani shura, kitani, chai, sukari, nili, pamba, na hariri. Bidhaa nyingi sana zilikuwa zikiingia na kutoka Calcutta kupitia barabara, reli, na bahari. Baada ya kupata uhuru, viwanda vikubwa vya kukalibu vyuma na feleji vilijengwa, na madini yenye thamani yalichimbwa kwa minajili ya kutumiwa nchini na pia kusafirishwa nje.
Jambo kuu lililohitajiwa kwa sababu ya ongezeko la biashara lilikuwa bandari. Hapo awali meli za Uingereza zilikuwa zinatia nanga katika sehemu yenye kina zaidi ya Mto Hooghly kisha mizigo ilisafirishwa katika mashua ndogo-ndogo. Mnamo 1758 kituo kilianzishwa Calcutta ambacho baadaye kingekuwa bandari kuu ya India. Kazi inayoendelea ya kuboresha bandari hiyo na ongezeko la maji kutoka kwenye bwawa katika Mto Ganges zimetokeza ongezeko la meli za kimataifa na za huko zinazotumia Calcutta.
Usafiri—Wa Kale na wa Kisasa
Katika jiji lenye watu zaidi ya milioni 12, usafiri ni tatizo kubwa. Calcutta lina njia zote za usafiri ambazo hupatikana katika jiji la kisasa—na lina nyinginezo zaidi! Kwa wageni, mikokoteni iitwayo riksho huwashangaza watazamapo wanaume wepesi wakichangamana-changamana na magari mengi—mara nyingi wakiwafikisha abiria zao haraka kuliko basi au teksi. Riksho zilianzishwa mwaka wa 1900 ili kusafirisha mizigo, lakini upesi zikaanza kubeba watu; inaaminiwa kwamba kuna riksho zipatazo 25,000 kwenye barabara za jiji hilo! Ingawa zinasababisha msongamano wa magari, riksho huruzuku labda watu 50,000 na kusafirisha watu wengi hata zaidi.
Kila siku, mashua ndogo hubeba maelfu ya wasafiri kati ya stesheni kuu ya gari-moshi ya Calcutta na eneo kuu la biashara la jiji hilo. Usafiri kupitia mto unaanza kuongezwa ili kupunguza matatizo ya msongamano wa magari, kwa kuwa zaidi ya magari 50,000 na maelfu ya malori hung’ang’ana kila siku kupitia Daraja la Howrah, linalotumiwa zaidi ulimwenguni.
Labda yanayopendwa zaidi jijini ni magari-moshi madogo ya umeme. Hayo magari-moshi ni njia bora ya usafiri ambayo haichafui hewa, ni yenye uwezo mkubwa sana wa kubeba watu, na yenye kutumia nishati kidogo sana. Hayo husafirisha mamia ya maelfu ya watu jijini kila siku ingawa hayastareheshi. Kuning’inia kwenye milango ya magari hayo huhitaji stadi za kipekee! Maendeleo makubwa yalifanywa kwa kuanzishwa kwa Reli ya Chini ya Ardhi iliyokamilishwa karibuni, ambayo husafirisha zaidi ya abiria 60,000 kwa muda wa saa moja kupitia katikati ya jiji wakiwa wamestarehe.
Tamaduni za Calcutta Zenye Utofautiano
Fursa za elimu katika Calcutta zimewafanya wengi wasomee mambo ya sayansi na sheria, na sanaa inasitawi katika jiji hilo ambalo limekuwa kituo cha kitamaduni cha India. Zaidi ya wanafunzi robo milioni huhudhuria Chuo Kikuu cha Calcutta ambacho kimekuwapo kwa miaka 140, na ambacho ni mojawapo ya vyuo vikuu vikubwa zaidi ulimwenguni.
Ikiwa Mumbai ni kituo cha sinema cha India, kwa hakika Calcutta ndicho kituo cha sinema bora zinazoonyesha uhalisi wa maisha. Majina kama Satyajit Ray na Mrinal Sen yamejulikana ulimwenguni pote kwa mchango wao wa sanaa. Calcutta lina washairi wengi kuliko Roma na Paris zikijumlishwa pamoja, lina magazeti mengi ya fasihi kuliko New York na London na, kwenye Barabara ya College, kuna mojawapo ya masoko makubwa zaidi ulimwenguni ya vitabu vilivyotumiwa tayari.
Vitu Visivyo vya Kawaida vya Kuona
Vitu vyenye kutokeza vyatia ndani Ukumbusho wa Victoria, lililojengwa kwa marumaru kwa mtindo wa kale wa Kiitalia. Lilifunguliwa mwaka wa 1921, na ni jumba kubwa la kumbukumbu la utawala wa Uingereza katika India. Majumba ya ukumbusho ya Calcutta yanatia ndani lile Jumba la Ukumbusho la India lililo kubwa na mengineyo zaidi ya 30. Bustani ya Mimea ya India ambayo ina mbaniani wenye umri wa miaka 240, ambao una mzingo wa zaidi ya meta 400, inafaa kutembelewa, na vilevile Bustani za Wanyama. Maidan—ambalo ni eneo kubwa la ekari 1,280—linaitwa mapafu ya Calcutta na ndilo baraza kubwa zaidi la kijiji katika India. Pia Calcutta lina Birla Planetarium, ambayo ni mojawapo ya majengo ya kuigiza nyendo za nyota yaliyo makubwa zaidi ulimwenguni. Kwa mashabiki wa michezo ya kriketi, uwanja wa kriketi wa Eden Gardens hufurika zaidi ya watazamaji 100,000 wenye makelele na vifijo wanapohudhuria mechi za kimataifa.
Jengo moja lenye kuvutia kwelikweli ni Science City, ambacho ni kituo cha sayansi chenye kuhusisha wageni kilicho kikubwa zaidi katika Asia na ambacho huwafanya wageni wasikie matetemeko ya ardhi, waone kisiwa kikizama, waone tufani ikifanyizwa, na kujifunza mambo yenye kuvutia kuhusu mazingira na tabia za wanyama wengi. Lakini kwa Wahindu, kitu chenye kuvutia zaidi katika Calcutta ni sherehe ya Durga Puja, wakati ambapo jiji huwa na shamrashamra za kidini kwa siku tano na kusimamishwa kwa shughuli nyingine zozote za kawaida.
Unaweza kupata nini ukienda kununua vitu Calcutta? Karibu kila kitu! Lakini uwe tayari kusukumana na umati wenye kelele, na kuwa tayari kuwaona wanawake wakivalia sari zenye rangi nyingi za kuvutia. Unaweza kununua bidhaa zilizotengenezwa kwa ngozi kwa bei nafuu, kutia ndani viatu vizuri vya ngozi katika maduka ya Wachina. Vitu visivyoweza kushikwa na kutu, nguo, vyombo vya udongo, na vito maridadi ni bidhaa chache tu ambazo mnunuzi mwenye subira aweza kupata katika hayo masoko makubwa yaliyo “paradiso ya wanunuzi.”
Vyakula
Calcutta limeitwa paradiso ya vyakula, kwa hiyo hatuwezi kuondoka bila kuonja baadhi ya vyakula vyake vitamu. Imesemwa kwamba Wabengal hupenda sana vyakula nao hukadiria watu kupitia ubora wa upishi wao! Samaki hawakosi katika vyakula vya Calcutta, na masoko makubwa huandaa aina mbalimbali za samaki, nyama, na mboga. Vikolezo vilivyotoka tu shambani, vikiwa vimechanganywa kwa uangalifu, huongezea utamu wa hata mboga za kawaida tu. Vyakula vya Kichina ni vingi. Na zenye kuongoza katika vyakula vitamu vya Calcutta ni peremende zake maarufu. Peremende hizo ziitwazo rasagollas zina umbo la mviringo, ni migando ya maziwa, na zimekolezwa na kuchovywa katika umajimaji mzito wa sukari, ni ishara ya Bengal. Na usikose kunywa mishti doi, ambao ni mtindi upendwao sana na ambao hunywewa baada ya mlo. Je, unadondoka mate? Je, unaweza kuhisi harufu nzuri itokayo kwenye mikahawa hiyo? Naam, kwa kweli Calcutta ni jiji lenye kuvutia lenye pilikapilika na utofautiano!
[Ramani katika ukurasa wa 15]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa.)
SRI LANKA
INDIA
Calcutta
BANGLADESH
[Ramani]
CALCUTTA
Bustani za Mimea za India
Maidan
Bustani Kubwa za Wanyama
Birla Planetarium
Jumba la Makumbusho la Victoria
Jumba la Ukumbusho la India
Hooghly Mto
Ziwa la Maji Yenye Chumvi
Uwanja wa Ndege wa Dum Dum
[Hisani]
Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Science City
[Picha katika ukurasa wa 16]
Jumba la Makumbusho la Victoria
[Picha katika ukurasa wa 17]
Soko lenye pilikapilika
[Picha katika ukurasa wa 17]
Kibanda cha kinyozi kando ya barabara