Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 7/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Bahari Zimo Hatarini
  • Wapaji wa Viungo
  • Mwaka Mbaya kwa Wapiga-Ramli
  • Ngono Hatari
  • Unene wa Kupita Kiasi na Maradhi ya Moyo
  • Misitu Inayotoweka
  • Upungufu wa Chakula Ulimwenguni Pote Wakadiriwa
  • Mamba wa Orinoco Wenye Kutoweka
  • Nguvu Nyingi Ajabu za Nyota
  • Kuendesha Gari na Kupiga Simu—Mchanganyiko Hatari
  • Watoto Wanene Kupita Kiasi—Suluhisho ni Nini?
    Amkeni!—2009
  • Je, Kunenepa Kupita Kiasi ni Tatizo?
    Amkeni!—2004
  • Je, Kunenepa Kupita Kiasi Ni Tatizo la Ulimwenguni Pote?
    Amkeni!—2003
  • Kunenepa Kupita Kiasi Husababishwa na Nini?
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 7/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Bahari Zimo Hatarini

Wanasayansi wa bahari na wanabiolojia wa hifadhi wazidio 1,600 kutoka mataifa 65 wameidhinisha “mwito wa kuchukua hatua” ya kuzilinda bahari ili zisiendelee kuharibiwa, laripoti The Journal of Commerce. “Bahari imo hatarini kabisa, hatari kubwa kuliko tulivyowazia hapo awali,” asema mtaalamu wa mazingira ya bahari Elliot Norse. Mfano mmoja uliotajwa ni eneo la bahari la kilometa 18,000 za mraba katika Ghuba ya Mexico ambalo huitwa eneo la kifo. Kama jina lake lionyeshavyo, hilo eneo la kifo halina samaki, uduvi, na viumbe vingine vya bahari. Wanasayansi wanataja kwamba tatizo ni wingi wa mimea ya mwani ambayo hupata rutuba nyingi kutokana na Mto Mississippi. Mwani ufapo, huanguka kwenye sakafu ya bahari. Bakteria zianzapo kuvunjavunja mwani uliokufa, sakafu ya bahari hukosa kupata oksijeni. Mwanasayansi wa bahari Dakt. Nancy Rabalais asema: “Chochote ambacho hakiwezi kutoka kwenye sakafu ya bahari hatimaye hufa.”

Wapaji wa Viungo

Je, unataka wengine wadai viungo vyako unapokufa? Hilo ndilo swali ambalo Wabrazili wengi wanakabili tangu sheria mpya ianze kutekelezwa mnamo Januari 1, 1998. Sheria hiyo inasema kwamba Wabrazili wote wenye umri wa zaidi ya miaka 18 watakuwa wapaji wa viungo ila tu wakitia sahihi hati zinazosema hawataki kufanya hivyo. Lakini “kuna ishara za kutosha zinazoonyesha kwamba Wabrazili wengi wangependa wabaki wakiwa na viungo vyao vyote baada ya kufa,” laripoti The Miami Herald. “Katika miezi sita iliyopita, kila watu watatu kati ya wanne waliokuwa wakipata leseni ya udereva walikataa mpango huo wa upaji wa viungo.” Kwa nini? Watu wengine wanaogopa kwamba huenda madaktari wakapata msongo wa kutangaza haraka kwamba mgonjwa amekufa ili wavune viungo vyao vya mwili hata kabla hawajafa kabisa.

Mwaka Mbaya kwa Wapiga-Ramli

Wapiga-ramli wote nchini Ujerumani “walipatwa na upofu” mwaka wa 1997, laripoti Nassauische Neue Presse la Frankfurt. Kati ya utabiri 70 uliochunguzwa na Shirika la Utafiti wa Kisayansi wa Mambo Yasiyojulikana (GWUP), hakuna hata utabiri mmoja uliotimia. Matukio ambayo hasa yalishtua katika mwaka wa 1997 hayakufunuliwa kwa wapiga-ramli hao. Kwa mfano, hakuna hata mpiga-ramli mmoja aliyetabiri kifo cha ghafula cha Princess Diana. Wapiga-ramli wengi wametahadhari hivi kwamba wao hujaribu tu kutabiri matukio kutokana na mielekeo, kama vile matatizo ya kiuchumi na kisiasa. Hayo ni “mambo ambayo hata kila msomaji wa gazeti angeweza kuyatabiri,” asema Edgar Wunder wa GWUP.

Ngono Hatari

Tokea 1994 hadi 1996, watafiti kwenye Hospitali ya Rhode Island na Hospitali ya Boston City, Marekani, waliwahoji wagonjwa 203 walioambukizwa virusi vya HIV kuhusu tabia zao za ngono. Uchunguzi huo ulionyesha nini? “Watu wanne kati ya kila watu kumi walioambukizwa virusi vya H.I.V. hawakuwaambia watu waliofanya nao ngono kwamba walikuwa na UKIMWI, na karibu thuluthi mbili kati ya hao hawakutumia kondomu kila wakati,” laripoti The New York Times. Kutotaja habari kama hiyo kuhusu kuambukizwa virusi vya HIV ni jambo la kawaida, watafiti hao wasema. “Hili si tatizo la kutojua,” asema Dakt. Michael Stein wa Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Brown, katika Providence, Rhode Island. “Watu wanajua hatari za kuambukizwa H.I.V. Si kwamba hawajui mambo haya. Hilo ni jambo la kila mtu kuwajibika.”

Unene wa Kupita Kiasi na Maradhi ya Moyo

“Mbinu bora zaidi ya kuzuia maradhi ya mishipa ya moyo [CAD] katika watu wazima huenda ikawa ni kupunguza unene wa kupita kiasi wakati wa utotoni,” laripoti The Journal of the American Medical Association. Maofisa wa afya wamejua kwa muda fulani kwamba unene wa kupita kiasi wakati wa utotoni huongeza hatari ya kushikwa na msongo wa juu wa damu, kisukari, mafuta mengi sana katika damu, maradhi ya mishipa ya moyo, na magonjwa mengine ya kudumu. Lakini japo mapendekezo ya madaktari ya kupunguza mafuta na kufanya mazoezi kwa ukawaida, inasemekana kwamba thuluthi moja ya watu wa Amerika Kaskazini wana uzito kupita kiasi au ni wanene kupindukia. “Kwani tunahitaji habari nyingi kadiri gani ili tuchochewe kuchukua hatua za kuzuia unene wa kupita kiasi kwa kufundisha watoto wetu mlo ufaao na mazoezi mazuri?” auliza Linda Van Horn wa Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Northwestern kule Chicago. “Manufaa ziwezazo kupatikana hazilinganiki. Unene wa kupita kiasi usipotibiwa, matokeo ya matatizo ya moyo yanajulikana, yanadhoofisha, na ni ghali kutibu.” Hata hivyo, matokeo ya uchunguzi wa karibuni zaidi yaliyotokea katika The New England Journal of Medicine yasema kwamba unene wa kupita kiasi ni hatari kwa afya kwa kadiri fulani tu. Uchunguzi huo ulipata kwamba unene wa kupita kiasi “huongeza uwezekano wa kufa mapema lakini si kwa kadiri ambayo wataalamu wengi walivyoshuku,” laripoti The New York Times.

Misitu Inayotoweka

Thuluthi mbili hivi za misitu ambayo ilifunika dunia kabla ya watu kuanza kuharibu misitu sasa imetoweka, lasema shirika la Hazina ya Ulimwengu ya Mambo ya Asili (WWF). Japo jitihada nyingi za binadamu za kutahadharisha watu juu ya tatizo hilo, ukataji wa misitu katika mwongo huu umeongezeka kufikia hatua ambapo karibuni nchi kadhaa zinaweza kukosa misitu ya asili. Kukatwa kwa misitu kwa ajili ya mbao na mashamba huangamiza aina nyingi za mimea na wanyama. Isitoshe, kuchoma miti huingiza kaboni dioksidi kwenye angahewa la dunia, jambo ambalo wengi huhofu kwamba litasababisha kuongezeka kwa joto duniani. Shirika la WWF linahimiza ulinzi uongezwe kwa angalau asilimia 10 ya aina zote za misitu ulimwenguni kufikia mwaka wa 2000, laripoti gazeti la habari la Guardian la London.

Upungufu wa Chakula Ulimwenguni Pote Wakadiriwa

Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, “ukuzi wa idadi ya watu usipopungua na mazao ya mashamba kuongezeka haraka, kufikia mwaka wa 2025 hakutakuwa na chakula cha kutosha watu wakadiriwao kuwa watakuwa bilioni 8,” yaripoti taarifa ya shirika la habari la Associated Press. Watafiti watabiri kwamba “hali ya kuzaa isipopungua kufikia watoto wawili hivi kwa kila mwanamke,” itabidi uzalishaji wa chakula uongezeke maradufu kufikia mwaka wa 2025 ili kuandaa “chakula cha kutosha chenye kufaa na chenye lishe” ili watu wawe na afya. Kuongezea tatizo hilo ni uhaba wa maji, uchafuzi wa ardhi, kupotezwa daima kwa udongo wa juu kwa sababu ya mmomonyoko, na mabadiliko ya tabia ya nchi. Hata leo, kila mwaka watu wapatao milioni 18 hufa kutokana na njaa, hata ingawa kuna chakula cha kutosha watu bilioni 6 hivi wanaoishi duniani leo.

Mamba wa Orinoco Wenye Kutoweka

Mamba wa Mto Orinoco wa Venezuela wamo hatarini, kulingana na gazeti Estampas la Caracas. Wanyama hao wamewindwa kwa ajili ya ngozi zao tangu 1930. Gazeti hilo lasema kwamba wakati huo “mamba hao huko Venezuela walikuwa wengi kuliko watu.” Lakini kati ya 1931 na 1934, karibu kilogramu milioni 1.5 hivi za ngozi za mamba hao, kutoka kwa angalau mamba milioni 4.5 zilisafirishwa nje. Kufikia 1950, “baada ya miaka mingi ya kuwindwa daima,” mamba hao walipungua sana hivi kwamba ni kilogramu 30,000 “tu” za ngozi ambazo zingeweza kusafirishwa. Leo, mamba wa Orinoco wanapungua 3,000, na wataalamu wasema kwamba pamoja na aina nyinginezo 312 za wanyama wa Venezuela, wao wamo hatarini mwa kutoweshwa na wanadamu.

Nguvu Nyingi Ajabu za Nyota

Picha moja ya karibuni ya Hubble yaandaa uthibitisho zaidi kwamba nyota moja katika kundi letu la nyota ni aina nadra ya nyota iitwayo “buluu nyangavu yenye kubadilika-badilika.” Kulingana na wataalamu wa anga, nyota hiyo nyangavu na mavumbi yanayoizunguka ina umbo la bunduki, na hivyo imeitwa Bastola. Inakadiriwa kwamba Bastola ni kubwa kuliko Jua letu kwa angalau mara 60 na ina nguvu kuliko jua letu karibu mara milioni 10. Huenda ikawa hiyo ndiyo “nyota yenye nguvu zaidi katika anga,” lasema gazeti Science News. Lakini kwa sababu ya mavumbi yanayoizuia, nyota hiyo inaweza kutambuliwa kupitia miali ya inforedi ambayo haiwezi kuonekana kwa macho. Hiyo inaonyesha ni kwa nini Bastola, ambayo iko umbali wa miaka-nuru 25,000 kutoka kwenye Dunia, haikugunduliwa mpaka mapema katika miaka ya 1990. Ni nyota nyingine sita tu za aina hiyo zimegunduliwa katika kundi letu la nyota.

Kuendesha Gari na Kupiga Simu—Mchanganyiko Hatari

Madereva ambao hupiga simu wanapoendesha magari waweza kufanya makosa makubwa bila hata wao kujua. Huo ulikuwa mkataa mmoja uliofikiwa katika uchunguzi mmoja uliofanywa kwa niaba ya Chama cha Wenye Magari cha Ujerumani. Madereva waliombwa wapige kona mahali pa majaribio mara tatu. Mara ya kwanza, hawakutumia simu. Mara ya pili, walitumia simu wasiyohitaji kushika; na mara ya tatu walitumia simu ya kushikwa mkononi. Madereva hao walifanyaje? Kwa wastani, madereva ambao hawakupiga simu walifanya makosa 0.5 ya kushika breki na kubaki kwenye upande wao wa barabara, wale waliotumia simu wasizohitaji kushika walifanya makosa 5.9, na madereva waliotumia simu za kushikwa mkononi walifanya makosa 14.6. Basi, Süddeutsche Zeitung laripoti kwamba uchunguzi huo ulikata kauli ya kwamba kutumia simu za mkononi unapoendesha gari “ni hatari sana kwa usalama.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki