Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 11/8 kur. 26-27
  • Kufanyia Wanyama Ukatili—Je, Ni Vibaya?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kufanyia Wanyama Ukatili—Je, Ni Vibaya?
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kwa Nini Ukatili Ni Mbaya?
  • Kitulizo kwa Wanyama
  • Wanyama
    Amkeni!—2015
  • Je, Wanyama Wanaenda Mbinguni?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Je, Mungu Anawajali Wanyama?
    Amkeni!—2011
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2003
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 11/8 kur. 26-27

Maoni ya Biblia

Kufanyia Wanyama Ukatili—Je, Ni Vibaya?

KATIKA uwanja mmoja wa michezo wa Amerika ya Kati, majogoo wawili, mmoja mwekundu, yule mwingine mweupe, wamekaziwa macho yote. Umati washangilia wakati jogoo mwekundu, aliyefungiwa wembe mkali mguuni, anapompiga yule mweupe. Refa awaokota ndege hao wawili. Yule mweupe sasa amekwisha, amekufa, naye avuja damu. Vita ya jogoo imekwisha.

Kusini mwa Filipino, farasi-dume wawili wachochewa kupambana. Watazamaji watazama tamasha hiyo yenye kuchukiza wakati farasi hao wanapoumana masikio, shingo, pua, na sehemu nyingine za mwili. Ijapokuwa wote huenda wakaondoka wakiwa hai, angalau mmoja wao huenda akawa kilema au kipofu au awe na majeraha ambayo mwishowe yatasababisha kifo.

Mbwa wawili nchini Urusi wanashambuliana. Baada ya muda mfupi, macho yameng’olewa na masikio yameraruliwa-raruliwa, wanapigana huku miguu ikiwa na majeraha mabaya sana, damu ikivuja kutoka kwenye mwili wao ulioraruliwa-raruliwa.

Kwa karne nyingi mwanadamu amechochea mapigano baina ya wanyama eti ni mchezo, kichocheo mara nyingi kikiwa kucheza kamari. Orodha ya michezo hiyo yatia ndani kupigana na fahali, kuwinda mbweha na kupigana kwa buibui. Kwa kuongezea, wanyama wengi huteseka kwa sababu ya sayansi. Zaidi ya hilo, wanyama wengi hata zaidi huteseka kutokana na kupuuzwa na wenyewe, iwe ni kimakusudi au la.

Katika nchi fulani, kuna sheria zinazohusu jinsi wanyama wanavyopaswa kutendewa nazo hukataza matendo ya ukatili. Huko nyuma mwaka wa 1641, Koloni ya Massachusetts Bay iliunda “The Body of Liberties,” iliyosema: “Hakuna mtu yeyote atakayefanyia Udhalimu au Ukatili Kiumbe ambacho kwa kawaida hufugwa kwa matumizi ya mwanadamu.” Tangu wakati huo, sheria imepitishwa na mashirika yameanzishwa ili kupinga ukatili dhidi ya wanyama.

Hata hivyo, wengi ambao huchochea michezo ya kupigana iliyotajwa hapo juu hawajioni wenyewe kuwa waendelezaji wa ukatili dhidi ya wanyama. Baadhi yao hudai kupenda wanyama ambao husababishia mateseko na kifo cha ukatili. Wanaopenda mapigano ya jogoo hudai kwamba ndege wao huishi kwa muda mrefu kuliko kuku wa kawaida anayekusudiwa kupikwa—faraja ndogo kwelikweli!

Kwa Nini Ukatili Ni Mbaya?

Mungu huturuhusu tunufaike kutokana na wanyama. Kanuni za Biblia huturuhusu kuua wanyama ili kujiandalia chakula na mavazi au kujilinda wenyewe na madhara. (Mwanzo 3:21; 9:3; Kutoka 21:28) Hata hivyo, uhai ni mtakatifu kwa Mungu. Kutawala kwetu wanyama lazima kufanywe kwa usawaziko unaoonyesha staha kwa uhai. Biblia husema kwa kulaumu mwanamume aliyeitwa Nimrodi, ambaye kwa wazi aliua wanyama na labda wanadamu ili tu afurahie.—Mwanzo 10:9.

Yesu alisema Mungu huwajali wanyama kwa maneno haya: “Shore watano huuzwa kwa sarafu mbili za thamani ndogo, sivyo? Na bado hakuna hata mmoja wao hupata kusahaulika mbele ya Mungu.” (Luka 12:6) Pia, Mungu mwenyewe alipobadili kauli yake kuhusu kuliangamiza jiji lililojaa wazoeaji wa uovu ambao walitubu, alisema hivi: “Mimi, je! haikunipasa kuuhurumia Ninawi, mji ule mkubwa; ambao ndani yake wamo watu zaidi ya mia na ishirini elfu . . . , tena wamo wanyama wa kufugwa wengi sana?” (Yona 4:11) Kwa wazi, yeye haoni wanyama kuwa vitu viwezavyo kuangamizwa tu, kutupwa kama mtu atakavyo.

Mungu alipokuwa akiwapa Waisraeli sheria, aliwafundisha kutunza wanyama vizuri. Aliwataka warudishe mnyama aliyepotea kwa mwenyewe na kusaidia wanyama waliokuwa wanataabika. (Kutoka 23:4, 5) Wanyama walipaswa kunufaika na pumziko la Sabato, kama vile wanadamu. (Kutoka 23:12) Kulikuwa na sheria zilizohusu kutendea vizuri wanyama wa kufugwa. (Kumbukumbu la Torati 22:10; 25:4) Kwa wazi, wanyama walipaswa kutunzwa na kulindwa bali si kutendwa vibaya.

Mithali 12:10 husema wazi maoni ya Mungu: “Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake; bali huruma za mtu mwovu ni ukatili.” Ufafanuzi mmoja wa Biblia hufasili mstari huu hivi: “Fadhili ya mtu mwadilifu hufikia hata wanyama wasio na uwezo wa kusema, bali mtu mwovu ni mkatili, hata afikiripo kuwa anakuwa mpole zaidi.”—Believer’s Bible Commentary, ya William MacDonald.

Mtu mwadilifu hutendea wanyama kwa fadhili naye hutafuta kujua mahitaji yao. Mtu mwovu huenda akaeleza kwa maneno upendo wake kwa wanyama, lakini “huruma” zake, hata zikiwa bora zaidi kwa kweli huwa ni ukatili. Matendo yake hufichua nia yenye ubinafsi aliyo nayo akilini. Hilo ni kweli kama nini kuhusu wale ambao huchochea mapigano baina ya wanyama wakitumaini kushinda fedha!

Kitulizo kwa Wanyama

Kwa kweli, kusudi la Mungu la awali lilikuwa kwamba mwanadamu ‘atawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.’ (Mwanzo 1:28) Kusudi hilo haliruhusu kuwatenda wanyama kwa ukatili. Kuwatenda wanyama kikatili hakutaendelea milele. Tuna sababu ya kuamini kwamba Mungu atakomesha kuteseka kote kusiko kwa lazima. Lakini jinsi gani?

Yeye aahidi kuwamaliza waovu na wakatili. (Mithali 2:22) Kuhusu wanyama, Hosea 2:18 husema hivi: “Nami siku hiyo nitafanya agano na wanyama wa mashamba kwa ajili yao, tena na ndege wa angani, tena na wadudu wa nchi; . . . nami nitawalalisha salama salimini.” Itakuwa vizuri kama nini kuishi wakati huo, wakati ambapo hali za amani zitanufaisha si wanadamu wanyofu peke yao bali pia na wanyama!

[Picha katika ukurasa wa 26]

“Kupigana na fahali Kijijini,” ya Francisco Goyay

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki