Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 2/22 kur. 26-27
  • Mchikichi Mti Wenye Matumizi Mengi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mchikichi Mti Wenye Matumizi Mengi
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Historia Yenye Mambo Mengi
  • Kutengeneza Uowevu Wenye Thamani Sana
  • Kutoka Aiskrimu Hadi Krimu ya Uso
  • Mafuta
    Ufahamu wa Kina wa Maandiko
  • Mafuta Hutoka Wapi?
    Amkeni!—2003
  • Mafuta Yenye Thamani ya Mediterania
    Amkeni!—2008
  • Mafuta Je, Yana Faida na Hasara?
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 2/22 kur. 26-27

Mchikichi Mti Wenye Matumizi Mengi

Na mleta-habari wa Amkeni! katika Visiwa vya Solomon

KISIWA Guadalcanal—kwa watu wengi jina la kisiwa hicho linahusiana na mapigano fulani yenye ukatili ya Vita ya Ulimwengu ya Pili. Hata hivyo, leo, mtu yeyote anayerudi kwenye sehemu hii iliyokuwa uwanja wa mapigano katika Visiwa vya Solomon atapata mandhari tofauti kabisa—vikosi visivyoisha, si vya askari-jeshi, bali vya michikichi yenye ukubwa wa kuvutia.

Ardhi iliyo chini ya michikichi hii yenye kusitawi sana na mikubwa mno wakati mmoja ilifunika mabomu yaliyobaki na zana nyingine za vita zilizo hatari. Lakini zana hizi za vita zimeondolewa ili michikichi iweze kupandwa. Ulimaji wa miti hii ulianza namna gani? Na kwa nini twaweza kusema kwamba mti huu maridadi na mrefu ni wenye matumizi mengi?

Historia Yenye Mambo Mengi

Ufafanuzi wa kwanza wa kisasa wa mti unaofanana na mchikichi ulirekodiwa katikati ya karne ya 15 na Alvise Ca’da Mosto wa Venetia, aliyetalii pwani ya magharibi mwa Afrika. Kisha, yapata miaka 500 iliyopita, watumwa wa Afrika walichukua tunda hilo hadi nchi zilizo ng’ambo ya Atlantiki. Hivyo, mawese yameibuka kuwa mojawapo ya mafuta ya mboga yanayotumiwa zaidi ulimwenguni leo. Michikichi hutokeza mafuta mengi zaidi kwa ekari moja kuliko mmea wowote wenye kutokeza mafuta. Kwa kuongezea, mchikichi ni mmea wa kudumu ambao huzaa matunda na mafuta kwa miaka kati ya 25 na 30.

Jambo muhimu katika utokezwaji wa mawese, hasa katika nchi fulani huko Mashariki ya Mbali, lilikuwa ugunduzi uliofanywa mnamo mwisho-mwisho wa miaka ya 1970. Hapo awali ilifikiriwa kwamba michikichi ilichavushwa hasa na upepo. Kwa hiyo, ilidhaniwa kuwa mazao mabaya yalisababishwa na hali zisizofaa za tabia ya nchi. Hata hivyo, utafiti wa karibuni umefunua kwamba uchavushaji hufanywa hasa na wadudu! Hivyo, kuhamishwa kwa wadudu wanaoweza kuchavusha miti kutoka Afrika Magharibi hadi Mashariki ya Mbali kulithibitika kuwa kwenye manufaa.

Tunda la mchikichi lenye rangi nyekundu na ya kimachungwa hutokeza aina mbili za mafuta. Aina zote mbili hutumika katika bidhaa za namna nyingi, yaelekea unatumia nyingine zao. Kabla ya kuzifikiria, acheni tuzuru kiwanda cha mawese na kuona jinsi ambavyo mafuta huziduliwa.

Kutengeneza Uowevu Wenye Thamani Sana

Tunapokaribia kinu hicho, kiongozi wetu atusalimu na kutuingiza ndani. Mashine kubwa-kubwa zinazotuzunguka zinafanya kazi. Hatua ya kwanza katika kutengeneza tunda la mchikichi, aeleza, ni kuliweka katika joko kubwa la mvuke lenye umbo la pia. Kila kole lina matunda madogo karibu 200 yanayotoshana na tende, ambayo yametungwa pamoja. Joko la mvuke hufisha vijidudu vilivyo katika matunda na husaidia kulegeza matunda madogo yatoke kwenye kole.

Hatua inayofuata ni kutenganisha matunda madogo kutoka kwenye kole kwa kutumia mashine ya kuambulia. Kisha matunda madogo yaliyobanduliwa hupelekwa kwenye mashine kubwa ya kusagia matunda, ambapo sehemu nyororo ya nje hutenganishwa na kokwa. Kisha sehemu hii ya nje yenye nyuzinyuzi hukamuliwa ndani ya kifaa kikubwa cha kuzidulia, au shinikizo, ili kupata mawese yasiyosafishwa. Baada ya kusafishwa na kutakaswa, mawese yako tayari kusafirishwa.

Hata hivyo, kuna aina ya pili ya mafuta. Haya hutoka kwenye kokwa. Kwanza lazima kokwa la mchikichi lipasuliwe ili kufikia kiini cha mbegu. Baadaye, viini vya mbegu hushinikizwa ili kutokeza umajimaji wao wenye thamani. Mafuta haya yanaitwa mafuta ya kokwa la mchikichi.

Machicha kutoka kwenye kokwa yanatumiwa kutengeneza chakula cha mifugo chenye lishe. Vivyo hivyo, baada ya matunda madogo kutolewa, mabaki ya makole ya matunda hurudishwa mashambani kutumika kama matandazo. Pia nyuzinyuzi za matunda na makaka hutumiwa tena, kama fueli ya bwela za kinu. Ni utendaji wenye matokeo makubwa!

Kutoka Aiskrimu Hadi Krimu ya Uso

Mawese ndiyo mafuta namba mbili yanayotumika kwa wingi zaidi ulimwenguni, kufuatia mafuta ya maharagwe aina ya soya. Kichapo The World Book Encyclopedia chasema: “Katika miaka ya 1700, Waingereza walitumia mawese kama dawa na kama krimu ya mikono.” Hata hivyo, leo yanaweza kupatikana katika aiskrimu, majarini, mafuta ya kukaanga, na mafuta ya kupikia, vilevile katika bidhaa zisizoliwa kama sabuni na vipodozi.

Pia mafuta ya kokwa za mchikichi hutumiwa katika utengenezaji wa majarini na vilevile chokoleti na bidhaa nyingine tamutamu. Lakini huo sio mwisho wa matumizi ya mafuta hayo. Baada ya hatua za ziada za utengenezaji, visehemu vya mawese na vya mafuta ya kokwa za mchikichi hutumiwa kutengenezea sabuni, dawa za kusafishia, mishumaa, na hata baruti!

Kwa kweli, mawese yanapendwa sana katika Visiwa vya Solomon. Sehemu kubwa ambayo imechangiwa na mawese kwa uchumi inakaziwa na uhakika wa kwamba asilimia 13 ya bidhaa za nchi hiyo zinazouzwa nje hutokana na mti huo.

Tunapotazama juu ya mchikichi, ni jambo lenye kuchekesha kuwazia kwamba bidhaa inayotokana na tunda hili la rangi nyangavu ya machungwa yaweza kuwa ikidondoka mdomoni mwa mtoto anayecheka kwa namna ya aiskrimu na yaweza kuwa usoni mwa mama yake, katika vipodozi vyake. Naam, mchikichi ni mti wenye matumizi mengi, na twaweza kuwa wenye shukrani kwa sababu ya matunda yake mengi.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 27]

Tani Mbili Zakusanywa kwa Mkono kwa Siku

Kuanguka pu! Kuna kelele ya matunda yanayoanguka wafanyakazi wanapovuna katika mashamba ya michikichi. Wao hufikiaje matunda yakiwa juu sana kwenye miti?

Wakitumia ubapa ­mkali uliopindika ambao umeshikanishwa na ufito unaoweza kurefushwa, wa­vunaji hukata matunda kutoka kwenye miti ambayo nyakati fulani inakuwa na urefu unaotoshana na jengo lenye orofa nne. Katika siku ya wastani, kila mfanyakazi atavuna kati ya makicha ya matunda 80 hadi 100 na kuyapeleka kando ya barabara ili yachukuliwe. Kila kicha cha matunda kikiwa na uzito unaokaribia kilogramu 25, huwa ni mzigo mzito kuinua! Ili kupata tani moja ya mawese utahitaji tani nne na nusu za matunda.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki