Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 2/22 kur. 24-25
  • Zumaridi za Thamani Sana Kati ya Vito

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Zumaridi za Thamani Sana Kati ya Vito
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Zimechimbwa Tangu Nyakati za Kale
  • Usalama wa Hali ya Juu Uliokosa Kufaulu
  • Mnunuzi Jihadhari!
  • Kutafuta Hazina ya Aina Tofauti
    Amkeni!—1993
  • Mashahidi wa Yehova Ulimwenguni Pote—Kolombia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • “Je, Umeona Jiwe la Bolivianita?”
    Amkeni!—2005
  • Mabomu ya Ardhini—Kuchunguza Athari Zake
    Amkeni!—2000
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 2/22 kur. 24-25

Zumaridi za Thamani Sana Kati ya Vito

ZIKITUNUKIWA kwa rangi yake ya kijani kibichi yenye kung’aa, zumaridi zimepamba taji zenye vito na kupamba viti vya ufalme vya baadhi ya nasaba za kifalme za kale zaidi katika historia. Leo, kama ilivyokuwa wakati wa kale, hizo ni ishara ya utajiri na mamlaka.

Ulimwenguni pote, kwa kawaida zumaridi huonwa kuwa zenye thamani zaidi kuliko almasi. Kwa kawaida, ni yakuti pekee ambazo huonwa kuwa zenye thamani zaidi kuliko zumaridi. Na bado, fundi-sanifu wa jiolojia Terri Ottaway, adai kwamba, “kwa kulinganisha vito mbalimbali kwa kutegemea kipimo cha uzito, zumaridi zenye ubora wa juu zaidi ndizo vito ghali zaidi ulimwenguni.” Ikitegemea ubora wake, zumaridi ambayo ingetoshea kwenye kitanga cha mkono wako na yenye uzito wa gramu tatu ingeweza kuwa na thamani ya dola milioni moja!

Kinachochangia kwa sehemu thamani ya zumaridi ni kutopatikana kwa urahisi. Hizo ni aina ya fuwele za beroli. Zumaridi hufanyizwa kutokana na muunganiko wa elementi za kawaida alumini na silikoni pamoja na elementi iliyo nadra sana berili. Kiasi kidogo cha elementi katiti, ama kromi ama vanadimu, huzipa zumaridi rangi ya kivulivuli ya kijani kibichi ya kustaajabisha.

Zimechimbwa Tangu Nyakati za Kale

Kwa maelfu mengi ya miaka, karibu zumaridi zote ulimwenguni zilitoka Misri. Machimbo ya Kleopatra yanayosimuliwa katika hekaya, ambayo hupatikana kilometa 700 hivi kusini-mashariki ya Cairo, yalichimbwa kwa bidii kwanza na Wamisri na baadaye na Waroma na Waturuki. Lazima iwe ilikuwa shughuli ngumu kama nini! Lazima jua la jangwani lililo kali sana na vumbi lenye kuchukiza na uchafu ulioko chini ya machimbo viwe vilisababisha magumu makubwa sana kwa wafanyakazi. Kwa kuongezea, ugavi wote ulihitaji kuletwa na msafara kutoka Mto Naili, safari ya juma moja, chini ya hali zinazofaa zaidi. Kujapokuwa magumu haya makubwa mno, machimbo yaliendelea kuchimbwa karibu kwa mfululizo kuanzia mwaka wa 330 K.W.K. hivi hadi 1237 W.K.

Katika nyakati za kale watu walitamani zumaridi, kwa sababu ya uzuri wake, na kwa uwezo wake uliodhaniwa kuwa wenye kuponya kimzungu. Zumaridi zilitangazwa kuwa ponyo la aina nyingi ya maradhi. Pia zilidhaniwa kuwa zingeweza kuchochea uzazi na ashiki katika wanawake. Kwa kueleweka, biashara iliyofanywa kwa bidii na yenye faida ilisitawi kati ya Misri na mataifa mengineyo ikisambaa mbali sana kufikia India.

Haki hii ya pekee ilidumu hadi washindi Wahispania walipowasili Amerika Kusini mwanzoni mwa karne ya 16. Muda mfupi baadaye, Jiménez de Quesada alishinda nchi ambayo sasa inaitwa Kolombia. Miaka kadhaa baadaye, katika mwaka wa 1558, Wahispania walipata machimbo hayo katika Muzo. Zumaridi zilizopatikana huko zilikuwa za kustaajabisha katika ubora na ukubwa.

Upesi Wahispania walianza kudhibiti machimbo hayo na kuwatumikisha wenyeji wa hapo, wakiwatumia kufanya kazi yenye kuchosha na ngumu ya kuchimba vito hivyo. Katika kipindi cha miaka michache, kiasi kikubwa sana cha zumaridi halisi ambazo karibu hazikuwa na kasoro zilifika Ulaya, nyingi zao zikawafikia Waturuki, Maofisa wa Uajemi, na hata jamaa za mfalme wa India. Mawe haya yalichongwa na kutiwa nakshi, na kuwa msingi wa mkusanyo mwingi wa vito vyenye thamani kubwa.

Usalama wa Hali ya Juu Uliokosa Kufaulu

Leo watu walio maskini zaidi ulimwenguni huchimba vito hivi kutoka kwenye ardhi ngumu, isiyo nyororo, kukifanya mwandishi wa habari Fred Ward aseme: “Ni mojawapo ya jambo lililo kinyume sana la biashara ya zumaridi kwamba watu wengi wanaochimba mawe haya hawawezi hata kuwazia kulundika pesa za kutosha kuvalia hata moja.” Kwa kuwa kuna kishawishi kikubwa sana kwa wafanyakazi kuficha jiwe hili na kulifanyia magendo, machimbo mengi yana askari wao wenyewe wa usalama. Walinzi wenye kubeba bombomu huwalinda wafanyakazi kwa bidii wachimbapo na kukwangua kwa jasho.

Hata hivyo, kujapokuwa hatua hizi, wataalamu wanadai kwamba biashara nyingi inayofanywa ulimwenguni pote ya zumaridi ni haramu. “Zumaridi nyingi zinauzwa bila hati, bila kulipiwa kodi, bila kuonekana, zikisitiriwa katika soko la magendo. Karibu kila zumaridi yenye thamani ya juu hufanyiwa magendo wakati fulani wa historia yake,” lasema gazeti National Geographic.

Mnunuzi Jihadhari!

Kwa sababu ya namna ambavyo hukua, fuwele za zumaridi zina kasoro nyingi za kiasili, za kindani zinazoitwa inclusion. Kasoro hizi zinapofikia sehemu ya juu ya jiwe, hutokea kama nyufa, zikiharibu umaridadi wa jiwe na kupunguza sana thamani yake. Kwa karne nyingi wauza-bidhaa wameficha dosari hizi zilizo katika sehemu ya juu kwa kulowesha vito safi na vilivyong’arishwa katika mafuta moto, kama vile mafuta ya mwerezi au mawese. Hatua ya kuzipasha moto hutoa hewa nje ya nyufa zilizo katika mawe na kuruhusu mafuta yapenye ndani, hivyo yakisitiri kwa njia yenye matokeo dosari hizo. Kisha vito vilivyochovywa ndani ya mafuta huuzwa kama vya thamani ya juu. Hata hivyo, baada ya mwaka mmoja au miaka miwili, mafuta huyeyuka na kufunua dosari hizo, jambo ambalo huacha wateja wakiwa wameshangaa na kuvunjika moyo.

Mteja anayetazamia kuzinunua apaswa pia kujihadhari na miigizo. Kufikia Enzi za Kati, matumizi ya kioo cha kijani kibichi kilichong’arishwa na kukatwa ili kuigiza zumaridi yalikuwa zoea lililoimarika. Kwa miaka mingi watu wengi wasiokuwa na habari wamedanganywa waamini kwamba walikuwa wamepata kitu halisi na kuja kugundua tu kwamba kwa kweli walipata mwigizo. Gazeti National Geographic lasema: “Wataalamu hudanganywa kwa kushirikiana na umma.” Hata hivyo, kuna majaribio yanayomwezesha mtaalamu wa vito aliye mashuhuri kuhakikisha uasilia wa zumaridi.

Ijapokuwa pupa ya mwanadamu imeharibu sifa yake, hata hivyo zumaridi zingali maridadi, nadra, na zenye thamani. Zabaki kuwa kitu cha kustaajabisha chenye thamani kilichoumbwa na Mungu.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Zumaridi zote: S. R. Perren Gem and Gold Room, Royal Ontario Museum; Ancient Egypt Gallery, Royal Ontario Museum

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki