Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 3/8 kur. 10-12
  • Ndege Ni Salama Kadiri Gani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ndege Ni Salama Kadiri Gani?
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Usalama Kwenye Chumba cha Rubani
  • Unaweza Kufanya Nini?
  • Je, Unaogopa Kusafiri kwa Ndege?
  • Kuhangaikia Usalama
    Amkeni!—2002
  • Mawaidha Kutoka kwa Rubani Stadi
    Amkeni!—2003
  • Kufanya Usafiri wa Ndege Uwe Salama Zaidi
    Amkeni!—2000
  • Kuongoza Ndege Kunukulindaje?
    Amkeni!—2008
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 3/8 kur. 10-12

Ndege Ni Salama Kadiri Gani?

KATIKA mwaka mmoja takriban watu nusu milioni hufa barabarani ulimwenguni pote. Kwa kutofautisha, vifo 1,945 vilitokana na aksidenti za ndege mwaka wa 1996. Mwaka wa 1997 jumla ilipungua na kufikia 1,226. Kulingana na takwimu za watengenezaji wa Boeing, “ndege za biashara hazianguki zaidi ya mara 2 kwa kila safari milioni 1.”

Na bado, kila anguko la ndege hutangazwa sana, huku vifo vingi vinavyotokea barabarani vikionwa kuwa jambo la kawaida. Huko Marekani kusafiri kwa basi tu ndiko huonwa kuwa salama kidogo kuliko kusafiri kwa ndege.

Kwa nini ndege huwa salama zaidi kuliko gari? Sababu moja iliyo wazi ni kwamba tofauti na magari barabarani, kwa kawaida ndege hazisafiri zikiwa zimekaribiana. Sababu nyingine ni kwamba wafanyakazi wengi wa ndege wamepewa mazoezi ya hali ya juu na ni wataalamu kwa namna ambavyo wanashughulikia madaraka yao. Kwa kawaida rubani mkuu wa ndege aina ya Boe­ing 747 ana umri wa miaka 50 na kitu na uzoefu wa miaka 30 hivi wa kuendesha ndege. Jambo la msingi kwa wafanyakazi wote wa ndege ni usalama. Kwani, uhai wao huwa hatarini pia.

Usalama Kwenye Chumba cha Rubani

Ukiingia kwenye chumba cha rubani cha ndege ya abiria, utaona kwamba vifaa vyote vya msingi na vya kuelekeza ndege ni viwili-viwili—seti moja ya rubani upande wa kushoto na seti nyingine ya rubani msaidizi upande wa kulia.a Hivyo, kulingana na kichapo The Air Traveler’s Handbook, “wakati wa tukio lisilotazamiwa la rubani mmoja kuzirai, yule mwingine ana vifaa vyote vya kuelekeza ndege vinavyohitajiwa ili kusafiri salama. Wakati wa safari, kila rubani anaweza kuchunguza vifaa vya mwenzake, na kuhakikisha kwamba vinaonyesha ishara zilezile kwenye sehemu zote mbili za kuendeshea ndege.”

Jambo jingine linalochangia usalama kwenye chumba cha rubani ni kwamba tahadhari huchukuliwa ili rubani na rubani msaidizi wale chakula tofauti. Kwa nini? Ili kwamba iwapo kwa tukio lisilotazamiwa chakula kingedhuru, ni mmoja wao tu ambaye angeathiriwa.

Ili kuhakikisha kwamba sehemu zinazosonga kama vile pindo, vifaa vya kutua na breki zinadhibitiwa, “kwa kawaida ndege huwa na mifumo miwili au zaidi ya haidroli endapo mfumo mmoja utakosa kufanya kazi.” Ndege nyingi za kisasa zina mifumo miwili-miwili au mitatu-mitatu kama kiwango cha usalama.

Unaweza Kufanya Nini?

Zifuatazo ni tahadhari sahili ambazo abiria wote wanaweza kuzingatia: Soma kadi ya maagizo kuhusu hali za dharura, na uwasikilize wahudumu wa ndege wanapoelezea hatua za usalama mwanzoni mwa kila safari. Unapopata kiti chako, angalia uone mahali mlango wa kutokea ulio karibu nawe ulipo. Katika hali ya dharura, fuata maagizo ya wahudumu wa ndege. Wote wamepewa mazoezi ya hali ya juu ya kushughulikia hali ngumu, endapo zitatokea. Maagizo yanapotolewa, ni muhimu abiria wafanye haraka bila kujali mizigo yao. Uhai ni wa maana zaidi kuliko vitu.

Kwa kawaida ndege za kisasa hupaa juu au kuzunguka sehemu iliyo na halihewa mbaya, hivyo nyingi za safari ndefu za angani huwa tulivu sana. Tokeo ni kwamba watu wachache sana hupatwa na kichefuchefu. Ikiwa mchafuko wowote wa halihewa unatazamiwa, kwa kawaida rubani huwashauri abiria wahakikishe kwamba wamefunga mikanda yao ya usalama kama hatua ya tahadhari.

Je, kusafiri kwa ndege kwaweza kuwa salama zaidi? Ndiyo. Lakini abiria wengi hawangekubali badiliko linalotakikana. Badiliko hilo lingekuwa gani? Abiria watazame nyuma badala ya mbele! Kungekuwa na manufaa gani kwa kufanya hivyo? Abiria wangetegemezwa na viti wakati ndege inapoanza kuelekea chini kwa ghafula badala ya kuwa tu na mkanda wa kiti uliofungwa kuzunguka fumbatio, ambao si salama kabisa unapolinganishwa na mikanda mingi ya usalama ya magari ambayo kwa kuongezea hufungwa kuzunguka kifua pia. Hata hivyo, watu hupenda kuona mahali wanapoelekea badala ya kutazama nyuma!

Je, Unaogopa Kusafiri kwa Ndege?

Inakadiriwa kwamba Mmarekani 1 kati ya 6 huogopa kusafiri kwa ndege. Wengine wao wana hofu kubwa isiyofaa inayoweza kuongoza kwenye wasiwasi mwingi sana. Ni nini kinachoweza kusaidia?

Jambo linaloweza kupunguza wasiwasi ni kujifunza habari nyingi ukiwa abiria. Kila mwaka ulimwenguni pote takriban ndege 15,000 zinazohudumia viwanja vya ndege vipatavyo 10,000 husafirisha watu zaidi ya bilioni 1.2 kukiwa na aksidenti au mikasa michache sana. “Kulingana na [kampuni ya bima] ya Lloyd ya London, ni salama kusafiri kwa ndege mara 25 kuliko kusafiri kwa gari.”

Ikiwa una wasiwasi kuhusu kusafiri kwa ndege, soma vitabu vinavyohusu usafiri wa angani, ndege, na mazoezi anayopokea rubani. Soma kuhusu viwango vya juu vya mazoezi vinavyotakiwa kwa marubani na sheria wanazopaswa kufuata kuhusu saa za kulala, kiasi cha vileo wanachoruhusiwa kutumia kabla ya kuendesha ndege, na kupimwa bila kutazamia ikiwa wametumia dawa za kulevya. Pia kuna ukaguzi unaofanywa mara mbili kwa mwaka ambao lazima marubani wafanikiwe kuupita ndani ya chombo kinachoonyesha hali halisi za usafiri ili kupima jinsi watakavyotenda hali za dharura zitokeapo. Vyombo hivi huigiza hali halisi hivi kwamba marubani fulani hutoka huko “wakitetemeka na kulowa jasho.” Rubani akikosa kufaulu mtihani wa vyombo, anaweza kupo­teza leseni yake ya kuendesha ndege za biashara.

Viwango hivi vyapita kwa mbali sana vyovyote vinavyowekewa madereva. Kwa hiyo, kadiri ujifunzavyo mengi kuhusu ndege na marubani, ndivyo uhakika wako utakavyoweza kukua.

Huenda ikasaidia pia kuzuru uwanja wa ndege. Angalia utaratibu unaofuatwa na abiria, na uone jinsi watu wanavyotenda. Utaona kwamba watu wengi hushuka kutoka kwenye ndege kana kwamba wanatoka tu kwenye basi. Kusafiri kwa ndege ni jambo la kawaida kwao. Zitazame ndege zikipaa na kutua. Jaribu kuelewa na kuvutiwa na kanuni za mwendo wa hewani ambazo hufanya iwezekane kusafiri angani salama.

Hatimaye utakaposafiri angani mara yako ya kwanza, mweleze mhudumu wa ndege kwamba hii ni mara yako ya kwanza kupanda ndege na kwamba huenda utakuwa na wasiwasi kidogo. Wataalamu hawa wanajua jinsi ya kukusaidia utulie na kukufanya uwe na uhakika kwamba safari itakuwa salama. Jaribu kutulia. Rubani anaposema kwamba ni sawa kutembea ndani ya ndege, amka na utembee-tembee katika chumba unamoketi. Huenda ikawa kwamba utakuwa ukifanya maendeleo ya kushinda kabisa hofu yako ya kusafiri kwa ndege!

[Maelezo ya Chini]

a Kwenye ndege nyingi rubani atakuruhusu kutazama ndani ya chumba cha rubani ndege inapokuwa imeegeshwa. Pia atajibu maswali yako.

[Blabu katika ukurasa wa 11]

“Kulingana na [kampuni ya bima] ya Lloyd ya London, ni salama kusafiri kwa ndege mara 25 kuliko kusafiri kwa gari”

[Picha katika ukurasa wa 12]

Kujifunza kutulia kwaweza kufanya kusafiri kwa ndege kupendeze

[Picha katika ukraasa wa 10 zimeandaliwa na]

Photograph courtesy of Boeing Aircraft Company

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki