Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 5/22 kur. 16-17
  • Kuzuru Ghuba ya Vietnam ya Dragoni Ateremkaye

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuzuru Ghuba ya Vietnam ya Dragoni Ateremkaye
  • Amkeni!—1999
  • Habari Zinazolingana
  • Shark Bay—Eneo la Ajabu la Baharini
    Amkeni!—2007
  • Uvumbuzi Kwenye Ghuba ya Red
    Amkeni!—2005
  • Wakazi wa Mapangoni wa Siku ya Kisasa
    Amkeni!—2000
  • Umaridadi Uliofichwa Mapangoni
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 5/22 kur. 16-17

Kuzuru Ghuba ya Vietnam ya Dragoni Ateremkaye

ASUBUHI moja yenye joto kali katika Hanoi, tulipanda basi na kuelekea kilometa 165 upande wa mashariki hadi mojawapo ya maeneo yenye kupendeza zaidi katika Vietnam, Ghuba ya Ha Long—au Ghuba ya Dragoni Ateremkaye, iliyo mashuhuri sana ulimwenguni. Mara nyingi tulikuwa tumesikia juu ya uzuri wenye kuvutia wa ghuba hiyo, na sasa, mwishowe, tulikuwa tunaenda kujionea.

Wakati wa adhuhuri basi letu lilisimama kwenye ukingo wa ghuba hiyo. Lakini hatukuwa tumefika mwisho wa safari yetu. Kile kinachofanya Ghuba ya Ha Long ipendwe na wengi si maji yake ya rangi ya zumaridi bali pia uzuri wa asili wa visiwa 3,000, vinavyotawanyika katika eneo la kilometa za mraba 1,500. Kwa sababu kila kisiwa ni cha kipekee, tulitaka kuzuru vichache kati ya visiwa hivyo. Hivyo tulipanda mashua, na baada ya muda mfupi tukawa na tukio lisiloweza kusahaulika.

Tulikuwa tumesafiri kwa mashua kwa muda upatao saa moja tulipoona ghuba yenye kuvutia ambayo imezungukwa na visiwa vidogo. Wenye mashua walitia nanga. Ulikuwa wakati wa kujiburudisha kwa kuogelea katika maji yenye baridi ya rangi ya kijani! Upesi kuogelea kwetu kukavutia kikundi cha watoto wadadisi waliopiga makasia kuja kukutana nasi katika mitumbwi yao. Watoto hao na familia zao huishi kwenye ghuba katika mashua zilizofanywa kuwa nyumba, au katika majahazi.

Huenda ikawa ulikisia kwamba wakazi wa Ghuba ya Ha Long ni wavuvi. Lakini huenda hukukisia kwamba wao pia ni wasanii wa sanaa inayotoweka—kushona matanga. Kitabu cha Michael Buckley Moon Travel Handbook on Vietnam chasema hivi: “Halong ni mojawapo ya mahali pachache ambapo matanga ya jahazi yangali yakishonwa kwa mkono na familia zinazoshona matanga. Pamba zenye chengachenga hushonelewa pamoja kwa uzi wa hariri, kila upindo ukishonwa kwa mkono. Ili kuzuia kuoza na kuota kwa kuvu, tanga iliyomalizika huchovywa ndani ya umajimaji unaotokana na mmea unaofanana na kiazi-sukari wa jamii ya kiazi kikuu. Tanga huchovywa na kukaushwa mara tatu au nne, hatua ambayo hufanya tanga liwe na rangi nyekundu iliyo nyeusi-nyeusi.”

Je, unastaajabishwa na jinsi Ghuba ya Ha Long ilivyopata jina yake—Ghuba ya Dragoni Ateremkaye? Hatukuona dragoni yeyote katika safari yetu! Hata hivyo, kulingana na hekaya tulijifunza kwamba visiwa vya Ghuba ya Ha Long vilifanyizwa na dragoni mkubwa sana aliyeishi milimani. Kichapo The Lonely Planet Guidebook on Vietnam chaeleza hivi: “[Dragoni] huyo alipokuwa akikimbia kuelekea pwani, mkia wake uliokuwa ukipigapiga ulichimba mabonde na nyufa; alipokuwa akitumbukia ndani ya bahari, maeneo yaliyochimbwa na mkia huo yalijaa maji, yakibakisha tu milima michache inayoonekana.”

Bila shaka, zile zinazodhaniwa kuwa dragoni ni upepo na maji, ambazo zimeunda visiwa hivi katika maumbo na saizi mbalimbali. Kwa kielelezo, ukiwazia mwenyewe, utaona kwamba Hon Ga Choi, Fighting Cock Islet, kinafanana na majimbi wawili wanaopigana.

Tulirudi mahali pa kuegesha mashua wakati wa utusitusi, tukiwa tayari kutazamia kwa hamu uvumbuzi wa siku itakayofuata. Baada ya kifungua-kinywa asubuhi iliyofuata, tulifunga safari kwa kutumia mashua ya matanga ili kutazama kwa makini baadhi ya mapango katika eneo hilo. Ghuba ilikuwa imefunikwa na ukungu, na kufanya kila kitu kionekane kuwa na uzuri usioelezeka. Tulizuru mapango kadhaa. Mojawapo inaitwa Hang Dau Go—Pango la Vigingi vya Mbao. Pango hilo lina vyumba vitatu vinavyounganishwa na vidato 90 vya ngazi. Pango hilo lilipataje jina lake? Kitabu The Lonely Planet Guidebook on Vietnam chaeleza hivi: “Pango hilo linapata jina lake la Kivietnam kutokana na chumba cha tatu, kinachosemekana kuwa kilitumiwa katika karne ya 13 kuhifadhi vigingi vya mwanzi vyenye ncha kali ambavyo [shujaa wa kijeshi wa Vietnam] Tran Hung Dao alisimamisha chini ya Mto Bach Dang” ili kuzuia mashambulizi ya Kublai Khan.

Tulipanda juu kwenye pango hilo na kugeuka ili kutazama mandhari iliyokuwa chini. Tulichoona kilistaajabisha kweli kweli. Leteni kamera, haraka! Huku mawe yenye kuning’inia yakiwa mbele yetu na mashua yetu ikiyumbayumba polepole katika ghuba ya rangi ya kijani kule nyuma, tulipata fursa nzuri ya kupiga picha bora kabisa! Kwa kweli Ghuba ya Ha Long ni kama paradiso kwa mpiga-picha na uvutio kwa msanii.

Baadaye wakati wa mchana, tulipanda motaboti ndogo ili kuona vizuri kisiwa fulani kikubwa. Kwa ghafula, tulikuwa ndani ya giza tititi. Ilikuwa kana kwamba mlima ulikuwa umetumeza kabisa! Tulikuwa tukipita kwenye pango. Ingawa hivyo, upesi baada ya hapo, tulifika upande wa pili. Kwa kushangaza, tukawa katika ziwa kubwa. Kulikuwa na kuta ndefu za mawe ya chokaa kwenye kila upande. Tuliona mimea ikiwa imejishikilia kwenye kuta. Wenye boti walizima injini. Kimya kilivurugwa tu na sauti za ndege. Tutaendelea kukumbuka kwa muda mrefu pindi hiyo yenye utulivu.

Upesi, wakati ulikuwa umewadia wa kufunga safari ya kurudi Hanoi. Safari haikuchukua muda mrefu vya kutosha. Hata hivyo, tulikuwa na mambo mengi ya kukumbuka—vilele vya milima vyenye mawemawe, majahazi yenye matanga na, hasa, Ghuba ya Ha Long, ambayo ni mfano mmoja tu wa uzuri wa Vietnam.

Tunatazamia kwa hamu kuona sehemu nyinginezo zenye kupendeza katika nchi hii maridadi. Tunamshukuru Muumba, Yehova Mungu, kwa kuandaa unamna-namna huo na uzuri katika uumbaji na kwa kuahidi kwamba siku moja dunia yote itakuwa nzuri kama Ghuba ya Ha Long.—Imechangwa.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki