Ewe Mpenda-jua— Linda Ngozi Yako!
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA BRAZILI
JE, WEWE hupenda kulikiza ufuoni? Vipi kupanda milima? Basi wewe ni mmoja wa mamilioni ambao hufurahia shughuli za nje ya nyumba. Hata hivyo, tahadhari: Hilo mara nyingi humaanisha kujiweka zaidi juani. Je, kuna hatari yoyote? Ikiwa iko, unaweza kujilindaje?
“Ngozi yako ni kiungo kikubwa mno kati ya viungo vyenye kuonekana katika mwili wako,” aandika Dakt. W. Mitchell Sams, Jr. Ngozi yako husaidia kulinda mwili wako dhidi ya kuishiwa na maji na kukufanya uendelee kuwa na joto. Hukufanya uweze kuhisi baridi, joto, maumivu, na mtikisiko, na vilevile mahali penye kukwaruza na mahali pororo. Ngozi yako pia huwa na fungu muhimu katika kutokeza vitamini D, ambayo ni ya maana katika kuunda mifupa. Kutokezwa huku kwa vitamini D huwezekana kwa msaada wa nuru ya jua.
Hata hivyo, kuna hatari nyingi kwa ngozi unapokuwa kwenye nuru ya jua. Mnururisho wa jua unaofikia dunia umefanyizwa kwa miale isiyoonekana na nuru inayoonekana, na pia urujuanimno katika mfiko wa A na B (UVA na UVB). Kwa uzuri, angahewa hufyonza mialianga, miali gama na miali X inayotokezwa na jua. Tabaka ya ozoni la angahewa huzuia kwa matokeo mnururisho wa urujuanimno aina ya C (UVC) na kuchuja mnururisho mwingi aina ya UVA na UVB. Kwa kusikitisha, tabaka ya ozoni hili linaharibika mahali-mahali. Wanasayansi wengi wanalaumu vizizimshi (vipoza joto) fulani na visukumia erosoli kwa tatizo hilo. Kwa vyovyote, unapokuwa kwenye jua unakabili hatari zaidi ya afya.
Mbali na kubabuliwa na jua, miali urujuanimno yaweza kukusababishia madoa-doa ya rangi ya hudhurungi na kuongezeka kwa unene wa ngozi na kunyauka kwa ngozi. Urujuanimno pia waweza kudhoofisha nyuzinyuzi zenye kunyumbulika za ngozi yako, hiyo ikisababisha kuzeeka mapema, kutia ndani makunyanzi yenye kuhofiwa mno. Hata vibaya zaidi, urujuanimno unaopita kiasi waweza kuharibu mfumo wa kinga wa mwili wako na huenda hilo likaongoza kwenye vidonda na kansa ya ngozi. Na kuongezea, ngozi iliyoharibika au iliyo na maradhi huathiri sura ya mtu na katika visa vingine, huenda ikachangia kuhisi wasiwasi na kushuka moyo.
Unaweza Kufanya Nini?
Ngozi yako yahitaji ulinzi siku baada ya siku kutokana na jua kama ilivyo pia katika vipindi vifupi-vifupi vya kuwa chini ya jua kali. Waweza kufanya nini? Mbali na kuvaa nguo za kujilinda na kutumia wakati mchache chini ya jua, unaweza kufuata shauri la wataalamu ambao wanapendekeza kutumia losheni ya kujikinga na jua. Unaweza kuchaguaje losheni nzuri ya kujikinga na jua? Chunguza habari inayohusu kinga (SPF) inayoonyeshwa na watengenezaji. Namba inapokuwa kubwa zaidi ndivyo itakavyokuwa na kinga pia. Watu wenye ngozi nyeupe wanahitaji losheni ya kujikinga na jua iliyo na namba kubwa ya SPF kuliko wale ambao ni weusi zaidi. Tahadhari: SPF hurejezea tu kinga ya losheni dhidi ya mnururisho wa UVB. Kwa hiyo, chagua losheni zinazoweza kukukinga na minururisho ya namna mbalimbali, ambazo pia zitakulinda kwa kiasi fulani na mnururisho wa UVA.
Watoto, hasa wale walio na ngozi nyeupe-nyeupe, huathirika sana kutokana na jua. Zaidi ya hilo, kichapo Fotoproteção, chasema, mara nyingi watoto hupatwa na nuru nyingi ya jua kuliko watu wazima. Kuchukua hatua za kulinda ngozi ya mtoto wako kutokana na jua katika miaka 18 ya kwanza ya maisha yake, kwaweza kupunguza sana uwezekano wa kupata kansa ya ngozi, ndivyo kinavyosema kichapo Fotoproteção.
Nuru ya jua ni ya lazima kwa uhai duniani. Na ni nani asiyefurahia halihewa ya jua yenye kupendeza? Lakini usidanganywe na picha mashuhuri zinazoonyesha ngozi ya rangi ya shaba (nyeusi-nyeusi) kuwa kifano cha urembo na ujana! Linda afya yako—linda ngozi yako kutokana na jua.
[Sanduku katika ukurasa wa 23]
Linda Ngozi Yako!
1. Jilinde na jua hasa kati ya saa 4:00 asubuhi na saa 10:00 jioni, wakati miali ya jua inapokuwa kali sana.
2. Hata katika siku zenye mawingu mengi, tumia losheni ya kujikinga na jua inayokukinga dhidi ya miali ya aina ya UVA na UVB na iliyo na kinga dhidi ya jua yenye namba 15 au zaidi.
3. Jipake losheni tena baada ya kila muda wa saa mbili unapokuwa nje, hasa kama unaogelea au unatokwa na jasho.
4. Vaa kitu cha kukukinga, nguo zilizofumwa na nyuzi nyingi. Rangi nyeusi hukinga zaidi.
5. Vaa kofia iliyo na ukingo wenye inchi 4 hivi na miwani ya jua ya lenzi zenye kukinga urujuanimno.
6. Kaa kivulini wakati wowote inapowezekana.
7. Epuka sehemu zinazoakisi nuru ya jua, kama vile maji, changarawe, na theluji, ambazo huakisi miali mingi yenye kudhuru ya jua.
[Hisani]
(Yategemea Skin Savvy, kilichochapishwa na American Academy of Dermatology)
[Picha katika ukurasa wa 23]
Linda afya na sura yako—linda ngozi yako
Utunzi zaidi wahitajiwa katika sehemu ambazo zinaakisi miali ya jua