Kuutazama Ulimwengu
Athari za Kelele
Nchi ya India ina idadi ya watu inayokaribia bilioni moja. Kulingana na Dakt. S.B.S. Mann, profesa katika Taasisi ya Uzamili ya Chandigarh, India, mtu 1 kati ya 10, au takriban watu milioni mia moja, huwa na tatizo fulani la kutosikia. Akihutubu katika ufunguzi wa mkutano wa kila mwaka wa Shirika la Matabibu wa Sikio wa India, Dakt. Mann alilaumu kelele zinazosababishwa na honi, injini, mashine, na ndege kuwa visababishi vya tatizo hili baya la kiafya. Kisababishi kikuu, yeye alisema, chaweza pia kuwa fataki zinazopendwa sana wakati wa msherehekeo. Kwa mfano, wakati wa msherehekeo wa Dasehra, katika nchi nzima sanamu kubwa za watu walio katika hekaya za Kihindu zinazowakilisha kani za uovu katika jamii hujazwa mamia ya fataki kisha huwashwa, zikitokeza mishindo mikuu ya kelele. Msherehekeo huo hufuatwa na msherehekeo wa siku tano wa Diwali wakati ambapo mamilioni ya fataki hulipuliwa.
Kugawanywa kwa Msitu wa Mvua
“Uwindaji, kuharibu misitu, na mioto si mambo pekee yanayotisha kuwapo kwa mimea na wanyama,” laripoti gazeti Jornal do Commercio la Brazili. Kugawanywa kwa misitu pia hutokeza hatari za kutowesha kabisa aina mbalimbali za wanyama na miti. Kugawanywa hutukia wakati sehemu ndogo za msitu zinapoachwa zikiwa na miti. Kulingana na mwagronomia Mbrazili Marcelo Tabarelli, nyingi za sehemu hizi huwa na ukubwa unaopungua ekari 25 kila moja. “Maeneo yenye ukubwa huu hayategemezi wanyama wakubwa,” asema Tabarelli. Sababu moja ni kwamba, kugawanya msitu “huvuruga mitindo ya utawanyiko na uhamaji.” Hili hutokeza “upungufu katika idadi ya [mimea na wanyama].” Fikiria, kwa mfano, ndege wa mwituni kama vile toucan. Tabarelli asema: “Bado wanaweza kupatikana, lakini uwezekano wa kwamba bado watakuwapo ni mdogo sana.”
Baba Wanaopendezwa Wanakuwa na Wana Wenye Furaha
Akina baba wanaopendezwa kibinafsi na mahangaiko, kazi ya shule, na maisha ya kijamii ya wana wao hupata “vijana wenye juhudi na mwelekeo chanya, wenye uhakika na tumaini,” laripoti gazeti la The Times la London. Katika uchunguzi wa vijana 1,500 wenye umri wa miaka 13 hadi 19 uliofanywa na mradi wa Tomorrow’s Men, zaidi ya asilimia 90 ya vijana waliohisi kwamba baba zao walitumia wakati nao na kupendezwa kabisa na maendeleo yao walidhihirisha “kujistahi kwa hali ya juu, furaha na uhakika.” Kwa upande mwingine, asilimia 72 ya vijana waliohisi kwamba baba zao hawakupendezwa sana au hawakupendezwa kamwe nao “walijistahi kwa kiasi kidogo sana na walikosa uhakika, nao walielekea kushuka moyo, kuchukizwa na shule na kujikuta katika matata na polisi.” Adrienne Katz, wa mradi wa Tomorrow’s Men, alisema kwamba muda hususa ambao baba na mwana wanatumia pamoja hauhitaji kuwa mwingi. Yeye asema: “Jambo muhimu ni kumfanya mtoto ahisi anahitajiwa, anapendwa na anasikilizwa.”
Kusomea Ndani ya Blanketi
Kusomea katika nuru hafifu ndani ya blanketi huenda kukadhuru macho ya mtoto, charipoti kijarida cha afya cha Ujerumani Apotheken Umschau. Uchunguzi uliofanyiwa kuku katika Chuo Kikuu cha Tübingen, ulionyesha kwamba ukuzi wa jicho unaweza kuathiriwa hata wakati ambapo mtu haoni vizuri sana na nuru inapokuwa hafifu. Mtoto anaposomea ndani ya blanketi kitandani, hali zote mbili zinakuwapo: kutoona vizuri, kwa kuwa jicho haliwezi kuona vizuri kitabu kinapowekwa karibu sana na jicho, na nuru inapokuwa hafifu sana. “Matineja wengi, wamesoma kwa hima hadithi wazipendazo ndani ya blanketi wakitumia tochi, na kwa kufanya hivyo wamepatwa na tatizo la kutoweza kuona mbali licha ya kufuata zoea hilo katika elimu yao,” chataarifu kijarida hicho.
Je, Treni Zinazoendeshwa kwa Mvuke Zinarudi Tena?
Wapenzi wa treni hukumbuka kwa utashi treni za kale zenye kuvutia zilizoendeshwa kwa mvuke. Ijapokuwa utendaji wake wa chini na uchafuzi mkubwa wa hewa ulifanya treni hizo za kale karibu ziache kutumiwa kabisa, Roger Waller, mhandisi katika kiwanda cha treni huko Uswisi, aamini kwamba kutumia nguvu za mvuke kutafaa sana wakati ujao. Tayari injini nane za kampuni yake zinazotumia magurudumu yenye meno zinatumiwa katika Alps, laripoti gazeti Berliner Zeitung, na hivi majuzi Waller alitengeneza upya injini ya kale ya mvuke ili iweze kutumiwa katika reli za kawaida. Treni hiyo iliyotengenezwa upya hutumia mafuta mepesi kuwa fueli badala ya makaa ya mawe, na hivyo kupunguza uchafuzi wa hewa. Inatumia pia beringi zenye rola ili kupunguza msuguano na kihami kizuri ili kupunguza nishati inayopotea na muda unaohitajiwa ili kufikia joto la kawaida. Waller asema hivi: “Yaweza kusafiri kwa gharama ndogo zaidi na haichafui mazingira kama treni zinazotumia dizeli.”
Kujifunza Kutabasamu
Katika Japani, ambako watu hupendezwa sana na huduma bora, makampuni mengi “yanapeleka waajiriwa kwenye shule ili wajifunze jinsi ya kuwa wenye urafiki zaidi,” laripoti gazeti la Asahi Evening News. “Makampuni huona tabasamu, kicheko na ucheshi kuwa njia rahisi na yenye matokeo ya kuvutia wanunuzi wengi licha ya kushuka sana kwa uchumi.” Katika shule moja, wanafunzi huketi mbele ya vioo na kujizoeza kutabasamu—“wakijaribu kutokeza tabasamu yenye kupendeza zaidi.” Wao huambiwa wafikirie mtu wanayempenda zaidi. Wafunzi hujitahidi sana kuwasaidia wanafunzi wastarehe na hivyo waweze kutabasamu kwa njia ya asili. Mbali na shule, makampuni fulani huwapa waajiriwa wao kazi ya kuhudumia wateja kwenye mikahawa inayotayarisha vyakula vyepesi ambamo wanazoezwa kutabasamu kwa kuendelea. Je, kutabasamu kunafanikisha biashara? Kulingana na gazeti hilo, kampuni moja ya vipodozi iliyozoeza waajiriwa wake zaidi ya 3,000 katika mtaala wa kutabasamu ilipata ongezeko la ghafula la asilimia 20 la mauzo ya mwaka huo. Mwajiriwa mmoja alisema kwamba mtaala huo uliboresha hali ofisini mwake pia. “Ni jambo zuri kuzungukwa na wasimamizi wanaopendeza ambao wanatabasamu sana,” yeye akasema.
Kugundua Mapema Huokoa Uhai
“Siri ya kushughulika na kutibu kwa matokeo maradhi ya kansa ni kugundua mapema,” yataarifu ripoti moja katika gazeti la Times of Zambia. Kwa kusikitisha, katika sehemu fulani za Afrika, idadi ya watu isiyojulikana hufa kutokana na maradhi ya kansa ambayo yangeweza kugunduliwa mapema ikiwa watu hao wangefanyiwa uchunguzi wa kitiba. Aina ya maradhi haya inayowakumba sana wanawake ni kansa ya mlango wa kizazi na kansa ya matiti. Wanaume wengi huugua kansa ya tezi kibofu na kansa ya matumbo. Kwa hiyo Baraza Kuu la Afya la Zambia linapendekeza kwamba watu waende hospitalini kupimwa kansa. Gazeti la Times lataarifu kwamba kugundua mapema “humaanisha maumivu machache na kiwewe kwa mgonjwa na familia yake. Kwa kuongezea, huwawezesha madaktari wachukue hatua mapema.”
Mashine ya Kukamua Maziwa
“Ng’ombe hulazimika kufuata zoea lisilo la kiasili la kukamuliwa maziwa mara mbili kwa siku,” asema Sue Spencer, mshiriki wa kikundi kilichobuni mashine ya kukamua maziwa. Kulingana na Spencer, viwele vilivyojaa maziwa vyaweza kusababisha ulemavu na magonjwa mengine. Kwa hiyo, ng’ombe wa maziwa anaweza kufanya nini anapotaka kukamuliwa japo wakati wa kukamuliwa na mkulima haujafika? Huenda jibu likawa mashine ya kukamua maziwa! Tayari mashine hiyo inatumiwa katika shamba moja huko Sweden, lasema gazeti la New Scientist. Wakati wowote wanapohisi uhitaji, ng’ombe hawa wa Sweden wanaweza tu kwenda katika banda lililo wazi ambalo lina mashine hiyo. Kila ng’ombe katika kundi hilo lenye ng’ombe 30 huwa na ukanda wa kielektroni shingoni unaowezesha mtambo huo kumtambua. Ikiwa ni wakati wa ng’ombe huyo kukamuliwa, lango linaloelekea kwenye kibanda cha kukamulia hufunguka. Kisha, mkono wa mashine hiyo unaoongozwa na miale ya leza hutafuta polepole matiti ya ng’ombe na kushikiza vikombe vya kukamulia.
Kupungua kwa Kima cha Uzazi cha Ulaya
“Mwaka uliopita, kima cha uzazi katika Muungano wa Ulaya (EU), kilishuka hadi kiwango cha chini sana tangu mwisho wa Vita ya Ulimwengu ya Pili,” laripoti gazeti la Süddeutsche Zeitung. Shirika la Eurostat, ambalo ni shirika la takwimu la EU, lilitangaza kwamba mnamo mwaka wa 1998 takriban watoto milioni nne walizaliwa katika EU, wakilinganishwa na watoto milioni sita waliozaliwa kila mwaka katika miaka ya kati ya 1960. Kwa wastani, idadi ya watoto wanaozaliwa kila mwaka katika mataifa ya EU ni 10.7 kwa kila watu 1,000. Ni taifa jipi lililo na kiwango cha chini zaidi cha watoto wanaozaliwa? Ni Italia, licha ya msimamo wa Kanisa Katoliki ya Kiroma wa kupinga kudhibiti uzazi. Idadi ya watoto wanaozaliwa ni 9.2 tu kwa kila raia 1,000. Nchi ya Ireland ina idadi kubwa sana ya watoto wanaozaliwa, watoto 14.1 kwa kila watu 1,000.
Kula Pamoja
Katika nchi nyingi, wazazi hulalamika kwamba ni nadra sana kwa watoto wao kula pamoja nao, mara nyingi wao wakipendelea milo myepesi. Lakini nchi ya Ufaransa huenda ni tofauti. Kulingana na gazeti la Kifaransa La Croix, uchunguzi wa hivi karibuni ulionyesha kwamba asilimia 84 ya familia katika Ufaransa zilikula mlo wa jioni pamoja. Kwa kweli, uchunguzi huo uligundua kwamba asilimia 95 ya vijana wenye umri wa kati ya miaka 12 hadi 19 walihisi kwamba hali ya kula pamoja kama familia ilikuwa yenye kujenga. Wataalamu hukazia umuhimu wa kula milo pamoja kwa ukawaida mkiwa familia. Dakt. François Baudier, wa Kituo cha Elimu ya Afya cha Ufaransa asema: “Wakati wa mlo si wakati tu wa kula bali ni wakati hasa wa kuzungumza.”