Pantanal Hifadhi Yenye Kuvutia Sana
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA BRAZILI
MTALII alikasirika Jerônimo alipomhimiza asitupe mkebe wa bia kwenye mto. “Kwani mto huu ni wako?” akauliza. “La,” Jerônimo akajibu, “ni wetu. Lakini ukiendelea kutupa takataka ndani yake, karibuni hakuna mtu atakayeweza kuvua samaki humu.”
Jambo hilo laonyesha mojawapo tu ya njia ambazo Pantanal—eneo kubwa ambalo limeenea kwenye sehemu za Brazili, Bolivia, na Paraguai—linatishwa sana leo. Neno la Kireno pântano lamaanisha “bwawa au kinamasi.” Lakini Pantanal si tambarare, kwa hiyo maji yake hayabaki mahali pamoja. Badala yake, maji hayo husonga polepole kwa utaratibu, yakifanya uwanda huo wenye rutuba ujae aina nyingi za nyasi. Je, ungependa kujifunza mengi kuhusu eneo hili kubwa? Basi jiunge nami ninaposafiri pamoja na kikundi cha watalii kuelekea mojawapo ya hifadhi zenye kuvutia sana ulimwenguni za wanyama na mazingira.
Aligeta na Anakonda!
Kutoka São Paulo twapanda basi kuelekea upande wa magharibi tukienda Corumbá, umbali wa kilometa 1,200 hivi. Tuingiapo kwenye eneo la Pantanal, ndege wakubwa wapaa juu kana kwamba wanatukaribisha. Kuna jabiru (ambaye huitwa pia tuiuiú), ndege ambaye mabawa yake yakipanuka yanafikia futi nane na nusu kutoka mwisho mmoja hadi mwisho mwingine. Ni kama yeye huhitaji barabara ndefu kama ya ndege ili aweze kuruka! “Mapigo ya haraka-haraka ya mabawa yake hutokeza sauti kutokana na mapigo ya mabawa hewani,” aandika Haroldo Palo, Jr., ambaye alikaa Pantanal kwa miaka miwili. “Wakati wa kujamiiana,” yeye aendelea kusema, “[jabiru] wawili au watatu wa kiume hupaa pamoja . . . , wakipiga mbizi za ajabu zinazoweza kuonekana kwa mbali sana.”
Majira ya kiangazi yamefika na maji yamepungua. Basi, ndege wanaweza kuwala samaki kwa urahisi. Tazama! Kuna jabiru na kulasitara wanaovua samaki miongoni mwa aligeta! Aligeta wanakula samaki wakali wanaoitwa piranha. Kama ambavyo huenda umejua, piranha wana meno makali kama wembe nao huvutiwa na mnyama ambaye anatoka damu. Ingawa hatuwezi kukaribia hata kidogo mmoja wa samaki hao, hao aligeta hata hawana habari kwamba samaki hawa ni hatari wala hawawezi kudhuriwa na samaki hawa.
Baada ya kuvuka mto kwa feri, twapanda gari kuelekea shamba moja la wanyama. Kwa ghafula, dereva wetu asimamisha gari na kutuonyesha joka linalovuka barabara ya mchanga. “Ni [chatu aina ya] anakonda,” yeye asema. “Afadhali ulipige picha haraka. Si rahisi kuyaona majoka hayo kwa ukaribu hivi!” Kuliona tu joka hilo kwanitetemesha, kwa kuwa anakonda huyo—akifikia urefu wa futi 30—ni mmojawapo wa nyoka wakubwa zaidi. Nikatambua kwamba anakonda naye yuaenda haraka anapopotea vichakani. Hata ni afadhali alienda haraka. Kwa kweli, hata kama hangalitoroka, bila shaka mikono yangu iliyokuwa ikitetemeka ingeharibu picha hiyo!
Maisha ya Pantaneiro
Pantanal ina ng’ombe wengi sana. Ng’ombe hao huchungwa na pantaneiro. Hao pantaneiro ni wachungaji na wakulima, na ni wazao wa Wahindi wa Marekani, Waafrika, na Wahispania. Hao hufuga farasi na ng’ombe kotekote katika eneo hilo. Twaona makundi kadhaa ya ng’ombe, kila kundi likiwa na ng’ombe elfu moja hivi. Kila kundi linachungwa na watu sita. Mpishi yuaongoza, akifuatwa na mchungaji mwenye tarumbeta iliyotengenezwa kwa pembe ya fahali. Wachungaji wengine wafuata nyuma. Mmoja wao ni mwenye ng’ombe hao, na wengine huwarudisha ng’ombe wanaobaki nyuma au wanaoacha kundi hilo.
Jerônimo, aliyetajwa mwanzoni, ni pantaneiro. Yeye apiga makasia kwenye Mto Abobral badala ya kutumia motaboti kwa sababu sauti ya injini inaweza kuogofya ndege. Sauti yake yenye kicho yaonyesha jinsi anavyopenda makao yao, Pantanal, na kuyafurahia. “Tazameni! Palee penye ukingo wa mto—pana aligeta anayeota jua,” Jerônimo asema. Mbele tena, atuonyesha tundu la fisi-maji wawili. “Hayo ni makao yao,” asema. “Sikuzote mimi huwaona hapo.” Pindi kwa pindi, Jerônimo ajaza kikombe chake kwa maji ya mto ili akate kiu yake. “Je, hayo maji si machafu?” twauliza. “Bado hayajachafuliwa,” yeye ajibu. “Mnaweza kunywa pia mkitaka.” Hatusadiki kabisa kama ni safi.
Hao pantaneiro wana mtazamo mzuri wa maisha. Hawatamani mambo mengi, nao wanafurahia kazi yao. Hao huondoka nyumbani alfajiri na kurudi usiku, wakichuma pesa kidogo (karibu dola 100 za Marekani kwa mwezi) huku wakiwa wamepewa chumba na kuandaliwa mlo—nao wanaweza kula nyama kadiri watakavyo. “Katika shamba langu,” asema mkulima mmoja, “pantaneiro hula chochote anachotaka na kadiri atakavyo. Yeye si mtumwa. Kama haridhiki, anaweza kusema: ‘Tajiri, nipe pesa zangu. Ninaondoka.’”
Makao ya Wanyama Bila Vizuizi
Hoteli tulimokaa katika shamba hilo pia ina ndege wengi na wanyama wengi, kama vile kasuku mkia-mrefu, kasuku, kasuku-mdogo, jabiru, jaguar, capybara, na paa-mwekundu. Mtu mmoja wa kabila la Guaná la Wahindi wa Amerika ambaye familia yao imeishi katika Pantanal kwa miaka 100 alituambia: “Sisi huwalisha ndege hawa hapa. Wengi wao walitwaliwa na polisi wa kulinda misitu kutoka kwa watu walioshukiwa kuwa majangili.” Mke wake alisema kwamba mwanzoni walikuwa na kasuku-mdogo 18 pekee, lakini sasa wana kasuku-mdogo wapatao 100. “Lengo letu ni kuwarudisha katika mazingira yao,” yeye asema.
Katika makao hayo ya wanyama yasiyo na vizuizi, tulipiga picha za kasuku mkia-mrefu wakila kwa amani pamoja na nguruwe na kuku. Watalii kutoka kotekote ulimwenguni hufurahia wingi wa ndege na wanyama na mandhari ya Pantanal. Na machweo yake yanastaajabisha ajabu! Siku moja mtalii mmoja kutoka Japani alishangazwa sana na makundi ya ndege waliokuwa wakirudi kwenye viota vyao wakati wa machweo. Kisha onyo la mtumishi mmoja—“Jihadhari! Kuna jaguar huku!”—likafanya atifue vumbi hadi chumbani mwake. Lakini, kufikia kesho yake, aliweza kudhibiti woga wake akaanza kuwalisha kasuku mkia-mrefu biskuti. Hata tulimpiga picha akilisha kasuku mkia-mrefu kwa mdomo wake. Hofu yake ikatokomea kabisa!
Alfajiri moja tulienda nje kutazama nyota. Ilionekana kana kwamba tungeweza kuzishika. Ulikuwa mwono wa ajabu sana! Hapa Pantanal, ukimya umetanda sana. Mambo tuliyoyaona na kuyasikia yalitufanya tumshukuru Muumba wa mahali hapa palipo kama paradiso. Karatasi moja ya matangazo ilisema: “Siku moja mtu akikuuliza iwapo kuna paradiso, unaweza kusema: ‘Bila shaka, Pantanal ni sehemu yake.’”
Hifadhi ya Mazingira Yachafuliwa
Katika miaka 20 ambayo imepita, vyombo vya habari vimekuwa vikijadili sana matatizo yanayokabili Pantanal. Katika kitabu chake Pantanal, Haroldo Palo, Jr., aandika kuhusu njia tofauti-tofauti ambazo mazingira ya Pantanal yanachafuliwa. Kifupi, zinatia ndani mambo yafuatayo.
◼ Mito inajaa matope. “Katika miaka ya karibuni, Mto Taquari umejaa matope hivi kwamba haiwezekani kuabiri karibu na mlango wake, na hivyo kuwatenga . . . wale wanaoishi kwenye ukingo wake. Na ndivyo ilivyo na mito mingine ambayo inaingia kwenye bonde la Pantanal.”
◼ Ukame wa mara kwa mara. “Nahofu kwamba . . . ukame wa kila baada ya miaka 15 au 20 ukitokea, kama ambavyo imekuwa ikitukia, mimea na wanyama wa eneo hili wanaweza kupatwa na madhara makubwa sana.”
◼ Dawa za kuua magugu na zebaki. “Kutumia mashine kwa ukulima nje ya Pantanal huhusisha matumizi ya dawa za kuua magugu ambazo huingia kwenye maji ya chini ya ardhi na kuchafua mito iliyo karibu. Au dawa hizo hubebwa na maji pamoja na udongo na kufanya mito ijae matope. Katika Pantanal ya Poconé, tisho jingine kubwa ni uchimbaji wa dhahabu, ambao huchafua maji kwa zebaki.”
◼ Uwindaji. “Ijapokuwa uwindaji ni haramu kisheria, bado watu wanawinda sana katika sehemu nyingi za Pantanal. Mbali na wakulima wachache wenye akili ambao wanalinda utajiri huo wa asili na wengine wanaolinda sehemu hizo kwa sababu ya faida inayotokana na utalii, wanyama na mazingira yanatishwa sana na watu wenye pupa.”
Twarudi Mjini
Twaona tofauti kubwa kama nini turudipo São Paulo! Badala ya kuona miti aina ya ipês ya manjano, ipês ya urujuani, na red sage, twaona majengo marefu. Badala ya mito safi myangavu yenye samaki tele, twaona mito iliyogeuzwa kuwa mitaro ya kupelekea maji machafu. Badala ya nyimbo tamu za ndege, twasikia kelele nyingi za malori na magari yakipiga honi. Badala ya anga jangavu la buluu, twaona ishara zinazotangaza “Hewa ni Chafu.” Badala ya amani kati ya mwanadamu na mnyama, kuna hofu ya wanadamu hatari.
Tulikaa Pantanal kwa majuma mawili, muda mfupi sana wa kuweza kujua maeneo yake tofuati-tofauti na majina yao ya kipekee, kama vile Poconé, Nhecolândia, Abobral, Nabileque, na Paiaguás—kila eneo likiwa na hali zake za kipekee. Lakini hatuwezi kusahau mambo tuliyoyaona. Mimea na wanyama walikuwa kama kitulizo kwa macho, wimbo mtamu kwa masikio na faraja kwa moyo.
[Ramani katika ukurasa wa 15]
Bolivia
Paraguai
Brazili
PANTANAL
[Hisani]
Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 16]
Yellow swallowtail
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Jaguar
[Picha katika ukurasa wa 17]
Yangeyange mkubwa
[Hisani]
Georges El Sayegh
[Picha katika ukurasa wa 17]
Anakonda na aligeta
[Hisani]
Georges El Sayegh
[Picha katika ukurasa wa 18]
Kasuku mkia-mrefu
[Hisani]
[Picha katika ukurasa wa 18]
Piranha hawa wenye ukubwa wa inchi sita wana meno makali kama wembe
[Hisani]
© Kjell B. Sandved/Visuals Unlimited
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
Georges El Sayegh