“Binti Yenu Ana Ugonjwa wa Kisukari!”
UZITO wa maneno hayo ya daktari hautasahaulika upesi. Binti yangu Sonya, alikuwa na umri wa miaka kumi wakati huo. Alionekana kuwa mwenye afya nzuri na mwenye nguvu—hata nyakati nyingine kupita kiasi. Mara ya mwisho alipotibiwa ugonjwa alikuwa na umri wa miaka mitano.
Hata hivyo, siku kadhaa kabla tu ya kumwendea daktari safari hii, mambo hayakuwa rahisi. Sonya alionekana kuwa mgonjwa. Alitaka kunywa sana, na alipokunywa, hakukawia kwenda msalani—nyakati nyingine baada ya kila dakika 15. Usiku alikuwa akienda msalani mara tatu hivi. Mwanzoni, nilijaribu kupuuza tatizo lake—nikifikiria ni ambukizo la kibofu cha mkojo tu, na atapona. Lakini baada ya siku chache, nilikata kauli kwamba labda alihitaji dawa za kutibu ambukizo hilo.
Ndipo nilipompeleka kwa daktari. Nilieleza kile ambacho nilifikiri kuwa ugonjwa wake. Aliomba mkojo upimwe, nami nikagundua kwamba mkojo huo uliokuwa katika kikombe ulikuwa umejaa vipande vidogo-vidogo vinavyofanana sana na vipande vidogo vya theluji. Muuguzi aliona hilo pia. Ugonjwa walioshuku ukathibitishwa alipopimwa damu. Alikuwa na ugonjwa wa kisukari Aina ya Kwanza.
Sonya alielewa jambo hilo. Ijapokuwa alikuwa na umri wa miaka kumi tu, alikuwa amejifunza juu ya ugonjwa wa kisukari shuleni. Alionyesha hofu na msononeko kama mimi. Daktari alisema kwamba ili kuepuka hatari zaidi, alihitaji kwenda hospitalini mara moja. Alifanya mipango alazwe kwenye chumba cha wagonjwa mahututi kwenye hospitali moja ya huko Portland, Oregon, Marekani. Sonya alikasirika sana kuwa alikuwa akipatwa na tatizo hilo. Hakutaka awe akijidunga sindano ili aendelee kuwa hai. Alikuwa akilia na kuuliza kwa nini iwe hivyo. Nilikuwa na ugumu wa kudhibiti huzuni yangu mwenyewe. Kisha nikashindwa kuidhibiti. Kwa hiyo, sisi tukiwa tumeketi katika chumba cha kungojea, tuliegemeana, tukilia na kumwomba-omba Yehova atusaidie na kututegemeza katika taabu hii.
Magumu Hospitalini
Daktari aliniruhusu nimpeleke Sonya nyumbani kuchukua vitu kadhaa, nimpigie simu mume wangu Phil, na kupanga mtu amchukue mwana wetu Austin kutoka shuleni. Baada ya muda wa saa moja mimi na mume wangu tulikuwa tukimpeleka Sonya hospitalini. Mara hiyo wakaanza kumweka umajimaji kupitia mishipani ili kuondoa sukari ya ziada na ketones kwenye damu yake.a Hilo likawa jambo gumu sana. Sonya alikuwa amepoteza kilogramu tatu za uzani wa mwili kwa sababu ya kuishiwa na maji mwilini. Mishipa yake iliyojificha haikuwa inapatikana kwa urahisi. Hatimaye muuguzi alifanikiwa, mambo yakatulia—kwa muda. Tulipewa kitabu na makaratasi mengi ambayo tulitazamiwa kusoma na kuelewa kabla ya kuruhusiwa kumpeleka Sonya nyumbani.
Tulikutana na madaktari wengi, wauguzi, na wanalishe. Tulionyeshwa jinsi ya kutumia sindano na kumdunga Sonya sindano mbili za insulini ambazo angehitaji kuanzia siku hiyo na kuendelea. Tulifundishwa jinsi ya kupima damu ambako Sonya angepaswa kufanya mara nne kwa siku ili kuangalia viwango vyake vya sukari. Tulipokea habari nyingi sana! Pia ilipasa tuagizwe jinsi ya kumlisha. Angepaswa kuepuka vyakula vilivyokuwa na sukari nyingi, na zaidi ya kupewa lishe yenye usawaziko kwa ajili ya mwili wake wenye kukua, kila chakula kilipaswa kuwa na kiwango sahihi cha kabohidrati.
Alitoka hospitalini baada ya siku tatu. Aliniruhusu nimdunge sindano, lakini alikuwa akijipima damu mwenyewe. Baada ya mwezi mmoja alitaka kujidunga sindano zenye insulini, naye amekuwa akifanya hivyo tangu hapo. Lilikuwa jambo la ajabu kumwona akizoea maradhi hayo na kujifunza kuishi nayo. Alibadili mawazo aliyokuwa nayo ya kutaka kufa na aamke katika Paradiso akawa chonjo kutambua dalili za mwili wake, hisia, mapungukio na kuweza kuongea alipokuwa na uhitaji.
Kipindi cha Marekebisho
Mambo hayakuwa rahisi miezi michache ya kwanza. Kila mshiriki wa familia alilazimika kushughulika na hisi nyingi tofauti-tofauti. Nilikuwa nikijaribu kufanya mengi zaidi mpaka nikafikia hatua ya kutaka kutoroka. Ratiba hiyo ilikuwa ngumu kudumisha, hasa ilipohitilafiana na mikutano ya Kikristo na kuhubiri kwetu—licha ya kutaja shughuli za shule na likizo. Lakini kwa kutoa sala nyingi, mimi na mume wangu tulijifunza kuachia kila siku mambo yake na kuanza kukubali madaraka yetu mapya.
Tumepata daktari mzuri ambaye ni mtaalamu wa matezi ya ndani na ambaye sikuzote hutusaidia katika mahangaiko yetu, hata kuwasiliana nasi kupitia E-mail. Sisi hutembelea ofisi yake kwa ukawaida kwa kuwa hiyo ni sehemu ya ratiba yetu. Kumwona baada ya kila miezi mitatu hutufanya tuchunguze maendeleo ya hali ya Sonya na vilevile hutuhakikishia kwamba twamfanyia yote tuwezayo.
Kama kawaida, mwana wetu alikuwa na ugumu wa kukabiliana na hali ya uangalifu mwingi unaoelekezewa dada yake. Wengine kutanikoni na pia mwalimu wake shuleni alitambua hilo na kumsaidia awe mwenye shughuli nyingi na kutambua kwamba ilikuwa lazima kuwe na mabadiliko. Sasa amekuwa mwenye msaada sana akimchunga Sonya. Tukiwa wazazi wake, nyakati nyingine tuna mwelekeo wa kumlinda kupita kiasi na kuwa na hofu zenye kupita kiasi kwa hali yake njema. Tumeona kwamba njia iliyo bora zaidi ya kuzuia hofu hizo ni kufanya utafiti wa maradhi hayo na kujifunza kile yanachoweza kuufanyia mwili hasa.
Twaendeleaje Sasa?
Mara nyingi sisi huongea juu ya ahadi za Yehova na juu ya wakati ambapo hivi karibuni ugonjwa hautakumbukwa tena. (Isaya 33:24) Hadi wakati huo, ni mradi wetu tukiwa familia kuendelea tukiwa watendaji katika kumtumikia Yehova, tukishiriki kikamili iwezekanavyo kusema na wengine juu ya baraka za Ufalme wa Mungu. Pia twajaribu tuwezavyo kuhudhuria mikutano kwa ukawaida.
Miaka michache iliyopita, mume wangu alipewa mgawo fulani wa muda wa kazi huko Israel. Kwa sababu ya hali ya kitiba ya Sonya, tulifikiria kwa uangalifu kuhama na tukasali juu ya jambo hilo. Tuliamua kwamba tukijitayarisha vizuri, na pia kupata lishe nzuri kwa ajili ya Sonya, kuhama huko kungeweza hata kuleta baraka za kiroho. Tulikuwa na pendeleo la kuwa sehemu ya Kutaniko la Kiingereza la Tel Aviv kwa mwaka mmoja na nusu. Tulifurahia aina tofauti kabisa ya mahubiri, na lilikuwa jambo zuri sana kwa familia yetu.
Yale maneno machache “Binti yenu ana ugonjwa wa kisukari!” yalibadili maisha yetu kabisa. Lakini badala ya kukata tamaa, tulifanya hali ya kimwili ya binti yetu kuwa mradi wa familia, na jambo hilo limefanya tuwe na uhusiano wa karibu zaidi. Yehova, yule “Mungu wa faraja yote,” ametusaidia tukabili hali hiyo. (2 Wakorintho 1:3)—Kama ilivyosimuliwa na Cindy Herd.
[Maelezo ya Chini]
a “Ugonjwa wa kisukari ambao hautibiwi husababisha ketosis, kukusanyika kwa ketones, ambazo ni mafuta yaliyovunjwa-vunjwa katika damu; hilo hufuatwa na acidosis (kukusanyika kwa asidi katika damu) na kichefuchefu na kutapika. Sumu za kabohidrati iliyo na kasoro na uvunjaji wa mafuta zinapoendelea kuongezeka, mgonjwa hupoteza fahamu kwa sababu ya ugonjwa wa kisukari.”— Encyclopædia Britannica.
[Sanduku katika ukurasa wa 21]
Ugonjwa wa Kisukari Ni Nini?
Miili yetu hugeuza chakula tunachokula kuwa nishati tunayoweza kutumia. Utendaji huu ni muhimu kama vile kupumua kulivyo muhimu. Ndani ya tumbo na matumbo, chakula huvunjwa-vunjwa kiwe sehemu za msingi, kutia ndani aina ya sukari inayoitwa glukosi. Kongosho hutenda dhidi ya sukari kwa kutokeza insulini, ambayo husaidia sukari ipitie chembe za mwili. Kisha sukari yaweza kugeuzwa iwe nishati.
Mtu anapokuwa na ugonjwa wa kisukari, kongosho yake haitokezi insulini ya kutosha au mwili wake hautumii insulini vizuri. Tokeo huwa kwamba sukari iliyo ndani ya damu haiwezi kupitia chembe za mwili ili itumiwe. Kitabu Understanding Insulin Dependent Diabetes chaeleza: “Kisha sukari iliyo katika damu hupanda juu sana na kufurika kupitia figo hadi kwenye mkojo.” Wagonjwa wa kisukari wasiotibiwa huenda wakawa na dalili za kukojoa mara nyingi na dalili nyinginezo.
[Sanduku katika ukurasa wa 21]
Ugonjwa wa Kisukari Aina ya Kwanza
Aina hii ya ugonjwa wa kisukari zamani ulikuwa ukiitwa ugonjwa wa watoto wa kisukari, kwa kuwa ulikuwa aina iliyopatikana sana kwa watoto na vijana. Lakini waweza kuwapata watu wa umri wowote. Ingawa kinachosababisha ugonjwa wa kisukari hakijulikani, kuna mambo mbalimbali ambayo watu fulani wanaamini yanahusiana na ugonjwa wa kisukari Aina ya Kwanza:
1. Urithi
2. Autoimmunity (Hali ya mwili kuathirika kwa mojawapo ya tishu zake au chembe zake za aina fulani—katika kongosho)
3. Kimazingira (virusi au kemikali)
Inawezekana kwamba maambukizo ya virusi na mambo mengine hudhuru vijisiwa (vikundi vya chembe vilivyo kwenye kongosho ambako insulini hufanyizwa). Kadiri chembe nyingi zinavyoharibiwa, mtu huelekea zaidi kuwa na ugonjwa wa kisukari.
Wagonjwa wa kisukari huonyesha dalili kadhaa:
1. Kukojoa mara nyingi
2. Kiu kali sana
3. Njaa mara kwa mara, mwili una njaa ya nishati usiyoipata
4. Kupunguza uzani. Mwili ukosapo kupeleka sukari kwenye chembe zake, hugeuza mafuta yake wenyewe na protini ili upate nishati, hiyo ikisababisha kupunguza uzani
5. Kukasirika-kasirika. Mgonjwa wa kisukari akiamka mara nyingi usiku kwenda haja ndogo, hawezi kulala vizuri. Mabadiliko ya tabia huenda yakatokea
Katika ugonjwa wa kisukari Aina ya Kwanza, kongosho hutokeza insulini kidogo au haitokezi kabisa. Katika hali hizo, insulini lazima iingizwe mwilini kila siku, mara nyingi kwa sindano (insulini huharibiwa tumboni ikinywewa kupitia mdomo).
[Sanduku katika ukurasa wa 21]
Ugonjwa wa Kisukari Aina ya Pili
Huu ni tofauti na ugonjwa wa kisukari Aina ya Kwanza nao ni hali ambayo mwili hautokezi insulini ya kutosha au hauitumii vizuri. Ndiyo aina inayopata watu wazima wengi zaidi wenye umri wa zaidi ya miaka 40 nayo huelekea kuja polepole. Ugonjwa huu unahusiana na urithi, na mara nyingi huzidishwa kwa sababu ya ulaji usiofaa au uzito wa kupita kiasi. Mara nyingi tembe zaweza kutumiwa, angalau mwanzoni, ili kuchochea kongosho kutoa insulini zaidi. Tembe hizo si insulini.
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
Hatari za Ugonjwa wa Kisukari
Mwili wahitaji nishati ili uendelee kufanya kazi. Ukishindwa kutumia glukosi, hugeukia mafuta ya mwili na protini. Hata hivyo, mwili ugeuzapo mafuta, vitu visivyofaa viitwavyo ketones hufanyizwa. Hizo ketones hukusanyika katika damu na kutapakaa kwenye mkojo. Kwa sababu ketones ni zenye asidi zaidi kuliko tishu za mwili, viwango vya juu vya ketones katika damu vinaweza kusababisha hali mbaya sana iitwayo ketoacidosis.
Pia ni jambo la hatari wakati sukari iliyo katika damu ya mwenye ugonjwa wa kisukari inapopungua zaidi ya kiwango cha kawaida (hypoglycemia). Mgonjwa wa kisukari hutahadharishwa na hali yake kwa dalili zisizopendeza. Huenda akahisi kutetemeka, kutoa jasho, kuchoka, njaa, kukasirika-kasirika, au kutatanishwa au huenda moyo wake ukapiga upesi-upesi, kutoona vizuri, kuumwa na kichwa, kuwa na ganzi, au kuwashwa midomo. Huenda hata akapatwa na mishtuko ya moyo au kuzimia. Mara nyingi lishe bora na nyakati zilizodhibitiwa za kula zaweza kuzuia matatizo hayo.
Dalili zilizotajwa juu zitokeapo, kula glukosi, labda maji ya matunda au tembe za glukosi, kwaweza kurudisha kiwango kinachofaa cha sukari iliyo katika damu hadi wakati wa kula chakula kingine. Katika hali mbaya zaidi, lazima mtu adungwe sindano ya glucagon. Hii ni homoni ambayo huchochea ini liachilie sukari iliyohifadhiwa, na kufanya sukari katika damu iongezeke. Ni vizuri mzazi aliye na mtoto mwenye ugonjwa wa kisukari ajulishe dereva wa basi la shule au mwenye kumtunza kuhusu hali ya mtoto huyo.
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
Matatizo ya Muda Mrefu
Huenda mtu mwenye ugonjwa wa kisukari akapatwa na matatizo ya muda mrefu, kutia ndani maradhi ya moyo, mshtuko wa akili, matatizo ya macho, maradhi ya figo, matatizo ya nyayo au miguu, na maambukizo ya kila mara. Matatizo hayo husababishwa na madhara yanayopata mishipa ya damu, neva, na kutoweza kushindana na maambukizo. Hata hivyo, si wagonjwa wote wa kisukari wanaopata matatizo haya ya muda mrefu.
Kudumisha viwango vya sukari katika damu vikiwa karibu na hali ya kawaida kwaweza kukawiza au kupunguza matokeo yenye kudhuru ya matatizo haya. Kwa kuongezea, kudumisha uzani na msongo wa damu katika kiwango cha kawaida na kutovuta sigareti kwaweza kuwa njia zenye matokeo sana za kupunguza hatari. Lazima mgonjwa wa kisukari afanye mazoezi mengi, adumishe lishe bora, na aendelee kutumia dawa alizoagizwa atumie.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Familia ya Herd