Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 12/8 kur. 22-23
  • “Naomba Tortilla”

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • “Naomba Tortilla”
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kutoka Mahindi Hadi Kuwa Tortilla
  • Desturi
  • Mhindi—Mmea wa Ajabu
    Amkeni!—2008
  • Je, Ungependa Kuonja Maua ya Mung’unye?
    Amkeni!—2004
  • Vyakula Bora Unavyoweza Kupata
    Amkeni!—2002
  • Si Balaa, Bali Ni Chakula Kitamu
    Amkeni!—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 12/8 kur. 22-23

“Naomba Tortilla”

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA MEXICO

FIKIRIA kitu kilichobuniwa ambacho ni “kifuniko, kijiko, sahani, na chakula, kwa wakati uleule, na kinachoweza kuliwa pamoja na chakula kingine chochote.” Hivyo ndivyo Héctor Bourges mtaalamu wa lishe alivyoeleza uvumbuzi ambao umeweza kupitishwa kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine kwa maelfu ya miaka. Watu wengi bado hula mlo huo kila siku. Ni tortilla, chapati nyembamba ya unga wa mahindi iliyo sehemu muhimu ya mlo wa Wamexico.a

Maandishi ya kale yanaonyesha jinsi ambavyo mahindi yalikuwa muhimu sana kwa watu wa Mesoamerica. Nafaka hii, iliyopandwa na wanadamu maelfu ya miaka iliyopita katika nchi inayoitwa sasa Mexico, ilisaidia sana kusitawisha tamaduni zenye sifa kama za Olmec, Maya, Teotihuacán, na Mexica.

Kutoka Mahindi Hadi Kuwa Tortilla

Njia ya kawaida ya kutayarisha tortilla ni kuchanganya sehemu moja ya mahindi yaliyokomaa na sehemu mbili za maji yaliyotiwa asilimia moja ya ndimu. Mchanganyo huo huchemshwa mpaka maganda membamba ya mahindi yanapoweza kumenywa kwa urahisi. Maji baridi huongezwa ili kukomesha uchemshaji, na mchanganyo huo huachwa usiku kucha ili utulie.

Siku ifuatayo mahindi hayo mororo, ambayo sasa huitwa nixtamal, hupakuliwa kutoka katika chombo hicho na kutiwa katika chombo kingine, ambamo maji yanayosalia huondolewa. Mahindi ya nixtamal husagwa, kisha huchanganywa na chumvi na maji hadi mchanganyo huo uwapo kinyunya chororo kinachoitwa masa. Kwa kawaida, masa hugawanywa katika vibonge vidogo ambavyo hufinyangwa kwa mikono na kuwa chapati nyembamba, kisha huwekwa kwenye kiokeo moto cha udongo kilicho bapa. Chapati hizo hupinduliwa mara moja kisha mara ya pili. Tabaka ya juu nyembamba ya tortilla hufura, na huwa imeiva!

Hatua ya kwanza ya kuongeza ndimu wakati wa kutayarisha, imethibitika kuwa muhimu sana katika kuzuia matatizo fulani ya kiafya. Jinsi gani? Ukosefu wa vitamini iitwayo niacin husababisha maradhi yanayoitwa pelagra, maradhi ya uvimbe wa ngozi, kuharisha, kichaa, na labda kifo. Maradhi hayo huwashika hasa watu wanaokula sana mahindi na wanaokula vyakula visivyokuwa na protini nyingi au visivyokuwa na protini yoyote.

Tatizo ni kwamba niacin iliyo kwenye mahindi haiwezi kumeng’enywa na mwili. Kwa upande mwingine, ndimu huifanya niacin iweze kumeng’enywa na mwili. Kwa hiyo, chapati ya tortilla yaweza kuwa ndiyo inayofanya maradhi ya pelagra yawe adimu katika maeneo maskini ya Mexico, isipokuwa maeneo ambako kwa kawaida wanafanya kinyunya cha masa kiwe cheupe kwa kusafisha mahindi ya nixtamal, usafishaji ambao huondoa niacin.

Tokeo jingine muhimu la kuongeza ndimu ni kwamba huongeza kiwango cha kalisi mbali na mambo mengine, kirutubishi muhimu kwa mifupa na neva. Isitoshe, chapati za tortilla ni chanzo bora sana cha nyuzinyuzi kwa sababu hupikwa kwa unga ambao haujakobolewa.

Baada ya kupitia mambo hayo yote muhimu, je, wewe pia usingeziita chapati za tortilla uvumbuzi bora? Hivi sasa, sawa na uvumbuzi mwingineo wote ni lazima tuone jinsi ambavyo wataalamu huandaa tortilla ili waweze kuzifurahia zaidi.

Desturi

Katika karne ya 16, Friar Bernardino de Sahagún alisimulia namna ambavyo tortilla ziliandaliwa: ‘Chapati za tortilla zilikuwa nyeupe, moto, na zilikunjwa. Zilipangwa kikapuni na kufunikwa kwa kitambaa cheupe.’

Zoea hilo bado halijabadilika baada ya karne nyingi. Bado tortilla huandaliwa zikiwa moto, na kwa kawaida huwekwa kikapuni, na kufunikwa kwa kitambaa safi. Pia, sawa na nyakati za kale, kuna aina nyingi za tortilla: nyeupe, za manjano, buluu, na nyekundu-nyekundu. Hizo huwa na ukubwa mbalimbali vilevile. Na bila shaka, Wamexico wengi hula tortilla kila siku pamoja na chakula cha mchana na labda hata wakati wa kifungua-kinywa na wa chakula cha jioni pia.

Kikapu kilichojaa tortilla huwekwa mezani kwa ajili ya familia nzima. Kila mtu aliye mezani anajitahidi kuweka tortilla zikiwa moto hadi mwisho wa mlo. Kwa hiyo, kila mtu anayefunua kikapu chenye tortilla huchukua moja tu na kisha hufunika vema tortilla zilizobaki kwa kitambaa tena. Watu waendeleapo kula na kuhitaji tortilla zaidi, bila kujali kichwa cha maongezi, usemi “naomba tortilla” husikika mara kwa mara.

Huenda sasa ukawa unafikiria, ‘Je, wake wa nyumbani wa Mexico hutayarisha tortilla kwa mikono kila siku?’ Wengi wao hawafanyi hivyo. Mashine za kutayarisha tortilla zimebuniwa tangu mwaka wa 1884. Mashine za mkono za kutayarisha tortilla zingali zatumiwa na wake wengi nyumbani, hasa katika maeneo ya mashambani. Lakini Wamexico wengi hununua tortilla kutoka katika duka la tortilla, ambamo mashine huweza kutayarisha kati ya tortilla 3,000 na 10,000 kwa saa.

Kwa kawaida watoto huwa na daraka la kununua tortilla kabla tu ya mlo. Kwa hiyo, mnukio, sauti, na joto la mashine ya kutayarisha tortilla hubaki katika kumbukumbu za wakati wa utoto za Wamexico wengi. Na hilo ni kweli hata katika familia maskini, kwa kuwa tortilla zina bei nafuu sana. Kwa kweli, ni kama anavyosema Dakt. Bourges, aliyenukuliwa mapema, “ni mlo wa bei nafuu kikweli, tuliorithi kutoka kwa wazazi wetu wa kale waliokufa.”

Kwa hiyo unapoonja tortilla, unakumbuka historia ya kikundi fulani cha watu. Kumbuka: Waweza kujihisi huru kusema, “Naomba tortilla,” mara nyingi upendavyo.

[Maelezo ya Chini]

a Ijapokuwa tortilla zilizopikwa kwa unga wa ngano huliwa pia katika baadhi ya maeneo huko Mexico, hazipendwi sana na Wamexico.

[Picha katika ukurasa wa 22]

“Tortilla” zilizotayarishwa kwa mikono

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki