Parachichi—Tunda Linalotumiwa kwa Njia Nyingi Sana!
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Kolombia
WASHINDI wa Kihispania wa mapema karne ya 16 hawakuwahi kuona tunda kama hilo. Lilikuwa na ukubwa na umbo kama la pea kubwa, lakini lilibaki kijani kibichi hata baada ya kuiva. Nyama yake ilikuwa laini na nyororo kama siagi, lenye ladha ya njugu. Hatimaye, likaja kuitwa avocado [parachichi], kutokana na neno ahuacatl la Kiazteki.
Parachichi lilipelekwa kwa mara ya kwanza Ulaya na Martín Fernández de Enciso mnamo mwaka wa 1519. Enciso alikuwa ameliona tunda hilo karibu na sehemu inayoitwa sasa Santa Marta, Kolombia, alipokuwa akielekea Amerika Kusini katika mojawapo ya safari zake za kwanza za uvumbuzi wa Hispania. Katika miaka hiyo ya uvumbuzi, Wazungu walionja kwa mara ya kwanza vyakula vipya mbali na parachichi, kutia ndani chokoleti, mahindi, na viazi.
Bila shaka, vyakula hivyo vyote havikuwa vipya kikweli. Wenyeji wa maeneo yenye joto la wastani katika Amerika Kaskazini na Kusini walivijua na kuvipenda vyakula hivyo vyote kwa karne nyingi. Parachichi lilipendwa sana na baadhi ya makabila ya asili hivi kwamba lilitolewa likiwa zawadi arusini vilevile zawadi ya kuwakaribisha wageni.
Kukuza Parachichi
Leo parachichi hukuzwa katika sehemu nyingi zenye tabia ya nchi ya joto au ya wastani, kutia ndani Amerika Kaskazini na Kusini, Australia, Filipino, Israel, Kenya, na New Zealand. Ni mojawapo ya matunda 20 hivi ya tropiki yaliyo muhimu kibiashara kotekote ulimwenguni.
Hata hivyo, kuna aina nyingi za parachichi katika nchi za tropiki za Amerika, aina moja ni ndogo kama yai la kuku na nyingine ni kubwa kama tikiti maji la wastani, lenye uzito wa kilogramu mbili. Rangi yake yaweza kutofautiana kuanzia kijani kibichi hadi zambarau iliyokoza, na ganda la parachichi fulani lina miparuzo na ni gumu, ilhali ganda la nyingine ni nyembamba na laini. Hata hivyo, inawezekana kukuza maparachichi ya aina moja katika shamba moja.
Miparachichi inapochanua hufunikwa na maelfu ya maua ya rangi ya manjano hafifu. Hata hivyo, ni ua 1 tu kati ya maua 5,000 linalopata kuwa parachichi. Jambo la pekee kuhusu maua hayo ni kwamba kila ua huwa na stameni, au sehemu inayotoa chavua, na wakati huohuo, pistili, au sehemu inayotoa mbegu. Ua haliwezi kujichavusha kwa sababu ya utaratibu wa ajabu wa mparachichi unaotendesha sehemu hizo wakati tofauti-tofauti.
Kama tokeo, maua ya miparachichi fulani hufunguka wakati wa asubuhi ili yapokee chavua na hufungika wakati wa mchana. Maua yaleyale hufunguka tena wakati wa jioni ili kutoa chavua. Miparachichi mingine ya karibu hufuata utaratibu ulio kinyume na huo. Uchavushaji hutukia wakati mti unaotoa chavua unapokuwa karibu na mti unaopokea chavua wakati uleule. Pia, nyuki au wadudu wengine ni muhimu katika kuhamisha chavua. Hivyo, upatano wenye kutatanisha ajabu wa nuru ya jua, wadudu, upepo, na mahali hufanikisha uzalishaji wa tunda hili.
Lenye Lishe na Manufaa
Parachichi lina lishe bora ajabu, kwa kuwa lina protini nyingi, riboflavini, niacin, potasiamu, na vitamini C. Inasemekana kuwa lina zaidi ya vitamini 11 na madini 14. Katika sehemu fulani za Amerika ya Kati, parachichi na tortilla huonwa kuwa mlo kamili. Parachichi huwa pia na mafuta mengi, mafuta yake hufanana na mafuta ya zeituni kwa sababu ni mafuta sikifu. Mafuta hayo hutumiwa pia katika utengenezaji wa sabuni na vipodozi.
Karibu kila sehemu ya mparachichi ina manufaa. Mbao zake hutumiwa zikiwa fueli. Kokwa yake, au mbegu, hutumiwa huko Amerika Kusini kutia alama kwenye mavazi, kwa kuwa huacha alama idumuyo. Katika sehemu fulani za Filipino, matawi yake hutumiwa kutayarishia chai. Inasemekana kwamba gamba la mparachichi laweza kutumiwa kutayarisha ngozi.
Kununua na Kula Tunda Hilo
Uendapo sokoni kununua maparachichi, usikadirie kuiva kwake kwa rangi ya maganda yake, kwa kuwa kila aina huwa tofauti. Jaribu kuyabonyeza kwa uangalifu. Iwapo ni mororo kiasi, yameiva. Maparachichi yahitaji kuhifadhiwa katika sehemu zenye joto, hewa ya kutosha, na waweza kuharakisha uivaji kwa kuyafunga kwenye gazeti. Waweza pia kuyatia katika friji, hata baada ya kuyakata. Waweza kuizuia nyama yake kuwa kahawia kwa kunyunyiza maji ya ndimu upande wa parachichi uliokatwa.
Watu wengi hufurahia kula maparachichi pamoja na balungi au nyanya. Ladha yake yaweza kuboreshwa kwa kutia masala kali. Kwa kuongezea, parachichi hulika vizuri na uduvi, kaa, au kambamti, na pia maparachichi yaweza kuchanganywa na saladi nyingi mbalimbali. Watu fulani huyachanganya na matunda mengine na kutengeneza maji ya matunda yenye kuburudisha.
Maparachichi yanapopondwa pamoja na vikolezo na viungo vingine, hutokeza mchanganyo mtamu unaoweza kupakwa kwenye mkate mgumu. Bila shaka hatuwezi kusahau guacamole, mchanganyo mashuhuri wa maparachichi, nyanya, vitunguu, pilipili hoho, na vikolezo. Tunda hilo laweza pia kuandaliwa na vyakula vilivyopikwa, likiwa sehemu ya mlo. Katika hali hiyo, lapasa kuandaliwa mwisho, na liwekwe mbali na moto.
Huenda tayari parachichi ni sehemu muhimu ya mlo wako. Hata hivyo, katika sehemu nyingine za ulimwengu, laweza kuonwa kuwa tunda adimu na la kigeni. Endapo hujawahi kuonja parachichi, mbona usilionje mara upatapo fursa. Huenda ukagundua kwamba tunda hili lenye kutumiwa kwa njia nyingi sana ni tamu pia!