Chuki Imeenea Ulimwenguni Pote
KUNA hali ya kutisha inayoenea. Hali hiyo ni chuki. Nayo inaongezeka ulimwenguni pote.
Katika jimbo moja katika nchi za Balkani, watu bado wanateseka baada ya mauaji ya jamii nzimanzima yaliyotukia hivi karibuni. Uadui ambao umekuwepo kwa karne nyingi umesababisha mauaji mengi, ubakaji, kuhamishwa kutoka nyumbani, uchomaji na uporaji wa nyumba na vijiji, uharibifu wa mazao na mifugo, na njaa. Mabomu ya ardhini bado yapo.
Katika Timor Mashariki, Kusini-mashariki mwa Asia, watu 700,000 wenye hofu walilazimika kutoroka mauaji, kupigwa, kupigwa risasi ovyoovyo, na kuhamishwa kinguvu kutoka makwao. Maeneo waliyoacha yaliharibiwa na majeshi ya mgambo. Mwathiriwa mmoja aliomboleza hivi: “Ninahisi kama mnyama anayewindwa.”
Huko Moscow, nyumba moja ya orofa ililipuliwa kwa bomu la magaidi. Miili ya watu 94 wasio na hatia—wakiwemo watoto—ilirushwa kila mahali kwa mlipuko huo. Zaidi ya watu 150 walijeruhiwa. Tendo kama hilo lenye kuogofya litukiapo, watu hujiuliza hivi, ‘Ni nani wengine watakaopatwa na maovu hayo?’
Huko Los Angeles, California, mbaguzi mmoja wa rangi aliwapiga risasi watoto Wayahudi wa shule ya watoto wadogo na baadaye akamfyatua tarishi mmoja Mfilipino.
Yafaa kusema kwamba chuki imeenea ulimwenguni pote. Karibu kila siku, ripoti za habari huonyesha matendo ya kijeuri yanayosababishwa na uadui wa kijamii, wa kikabila, na wa kidini. Sisi huona mataifa, jamii, na familia zikivunjika. Sisi huona nchi mbalimbali zikishiriki katika mauaji ya kikatili ya watu wengi. Sisi huona matendo ya kinyama yakifanywa eti kwa sababu watu fulani wako “tofauti.”
Ili chuki imalizwe, twapaswa kuelewa vyanzo vya ujeuri wa aina hiyo. Je, chuki imeingizwa ndani ya chembe za urithi za wanadamu? Je, ni tabia ambayo watu hujifunza? Je, chuki yaweza kukomeshwa?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Kemal Jufri/Sipa Press