Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g03 6/8 kur. 21-23
  • Kuelewa Mshuko wa Moyo Baada ya Kujifungua

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuelewa Mshuko wa Moyo Baada ya Kujifungua
  • Amkeni!—2003
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Magonjwa
  • Visababishi
  • Unazidi Kueleweka
  • Tiba
  • Jinsi Wengine Wanavyoweza Kusaidia
  • Nilipambana na Ugonjwa wa Kushuka Moyo Baada ya Kujifungua
    Amkeni!—2002
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—2003
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—2003
  • Jinsi ya Kutibu Ugonjwa wa Kushuka Moyo
    Amkeni!—2009
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2003
g03 6/8 kur. 21-23

Kuelewa Mshuko wa Moyo Baada ya Kujifungua

Sijui kinachonisumbua. Nilijifungua mtoto mrembo, mwenye afya. Ninapaswa kufurahi na kujivunia mtoto wangu, lakini nahisi vibaya, nina wasiwasi, na hata nimekasirika. Je, mimi ni mama asiyejali? Kwa nini nimeshuka moyo sana?

IWAPO umejifungua karibuni, huenda umehisi kama ilivyoelezwa hapa juu. Ikiwa unahisi hivyo, hauko peke yako. Inakadiriwa kwamba asilimia 70 hadi 80 ya akina mama waliojifungua karibuni huwa na hisia kama hizo wakati mwingine. Lakini mshuko wa moyo baada ya kujifungua ni nini, nao husababishwa na nini? Mtu anawezaje kukabiliana na ugonjwa huo? Watu wa familia na wengineo wanawezaje kusaidia?

Magonjwa

Ugonjwa wa kushuka moyo baada ya kujifungua ni vile vipindi vya kushuka moyo ambavyo humpata mama baada ya kujifungua. Mshuko huo unaweza kumpata mama yeyote aliyejifungua karibuni, lakini si lazima awe amejifungua kwa mara ya kwanza. Ugonjwa huo unaweza hata kumpata mama ambaye mimba yake imetolewa au kuharibika. Kulingana na Idara ya Afya ya Wanawake katika Wizara ya Afya na Huduma za Jamii ya Marekani, wanawake wenye ugonjwa huo huonyesha dalili tofauti-tofauti.

Wanawake wengi wenye ugonjwa huo huhuzunika kwa kadiri fulani, hupatwa na wasiwasi, hasira, hisia zinazobadilika-badilika, na uchovu. Hayo ni mambo ya kawaida kwa akina mama waliojifungua karibuni, na yanaweza kuisha baada ya siku kumi hivi bila matibabu yoyote.

Hata hivyo, Chuo cha Wataalamu wa Ukunga na Magonjwa ya Akina Mama cha Marekani kinakadiria kwamba asilimia 10 ya akina mama waliojifungua karibuni, hupata hisia hizo kwa muda mrefu zaidi. Huenda hata zikaendelea kwa miezi kadhaa baada ya kujifungua. Wakati huo ugonjwa wa kushuka moyo baada ya kujifungua huwa umefikia kiwango cha juu, na hisia za huzuni, wasiwasi, au kukata tamaa huwa nyingi mno hivi kwamba ni vigumu kwa akina mama kufanya kazi za kila siku.

Isitoshe, karibu mama 1 hadi 3 kati ya kila akina mama 1,000 waliojifungua karibuni, hushuka moyo vibaya zaidi na kuona maono ambayo mara nyingi humfanya atake kujiumiza au aumize mtoto wake. Aina hii ya kushuka moyo inahitaji kutibiwa haraka.a

Visababishi

Hakuna kisababishi cha wazi cha kushuka moyo baada ya kujifungua. Inaonekana matatizo ya kimwili na ya kihisia yanahusika. Saa 24 hadi 48 baada ya kujifungua, viwango vya homoni za estrojeni na projesteroni vya mama hushuka hadi chini ya viwango alivyokuwa navyo kabla ya kupata mimba, na hilo hutokeza badiliko la ghafula katika utendaji wa mwili. Mabadiliko hayo yanaweza kumfanya mama ashuke moyo kama ilivyokuwa kabla ya vipindi vya hedhi. Pia viwango vya homoni vinavyotokezwa na tezi za dundumio vyaweza kushuka baada ya kujifungua. Hali hiyo yaweza kutokeza dalili zinazofanana na zile za mtu aliyeshuka moyo. Hiyo imewafanya watafiti wauite ugonjwa huo “ugonjwa wa badiliko la kemikali na homoni mwilini.”

Gazeti moja la kitiba lilisema kwamba mshuko wa moyo baada ya kujifungua huenda unasababishwa na ukosefu wa lishe fulani, labda aina fulani ya vitamini B.

Uchovu na kukosa usingizi kunaweza kuchangia tatizo hilo pia. Dakt. Steven I. Altchuler, mtaalamu wa akili katika Kliniki ya Mayo huko Minnesota, Marekani, anasema hivi: “Mwanamke akidhoofika na ashindwe kulala vya kutosha punde tu anapojifungua, tatizo dogo linaweza kuonekana kuwa kubwa sana. Wanawake fulani huenda wakafadhaika ikiwa hawawezi kufanya mambo kama walivyofanya kabla ya kujifungua, wakati ambapo hawakuwa wameshuka moyo, wakati waliweza kulala usingizi mtamu.” Hisia zinazoletwa na kupata mimba isiyotarajiwa, kujifungua kabla ya wakati, kukosa uhuru, kuhangaikia sura, na kutoungwa mkono zinaweza pia kuchangia mshuko wa moyo.

Isitoshe, maoni ya kawaida kuhusu uzazi yanaweza kumfanya mama ashuke moyo au ahisi ameshindwa. Maoni hayo ni kama yale yanayosema kwamba mama anapaswa kujua kulea watoto bila kupata uzoefu wowote, kwamba anapaswa kuwa na uhusiano mzuri na mtoto wake mara anapojifungua, kwamba mtoto ni malaika hivyo hana kasoro na hawezi kulialia, na kwamba mama aliyejifungua karibuni anapaswa kuwa mkamilifu. Hayo si maoni ya kweli. Mama anahitaji kujifunza ulezi, uhusiano wake na mtoto huimarika kadiri muda unavyopita, watoto fulani ni wagumu kulea kuliko wengine, na hakuna mama ambaye amekamilika, asiye na kasoro yoyote.

Unazidi Kueleweka

Zamani kushuka moyo baada ya kujifungua hakukuonwa kuwa ugonjwa. Dakt. Laurence Kruckman, anasema hivi: “Magonjwa ya akili ya wanawake yalipuuzwa na kusemwa kuwa ni wasiwasi tu. Hati ya mwongozo ya Shirika la Marekani la Magonjwa ya Akili haijautambua kamwe ugonjwa wa kushuka moyo baada ya kujifungua, na hivyo madaktari hawajapewa mafunzo yoyote kuuhusu wala haujafanyiwa utafiti wowote wenye kutegemeka. . . . Na tofauti na ilivyokuwa miaka 30 iliyopita, akina mama huruhusiwa kurudi nyumbani siku hiyohiyo baada ya kujifungua. Akina mama huugua magonjwa mengi ya akili siku tatu hadi 14 baada ya kujifungua. Kwa hiyo wao huwa nyumbani mbali na wataalamu ambao wanajua dalili za magonjwa hayo.

Hata hivyo, kulingana na Dakt. Carol E. Watkins wa Shirika la Wataalamu wa Magonjwa ya Akili la Northern County huko Baltimore, Maryland, ugonjwa huo usipotambuliwa au kutibiwa unaweza kumfanya mama ashuke moyo kwa muda mrefu na kuathiri uhusiano wake na mtoto. Akina mama walioshuka moyo wanaweza kupuuza mahitaji ya watoto wao au washindwe kujizuia na kuwaadhibu vikali watoto wao wachanga. Jambo hilo laweza kuathiri ukuzi wa mtoto wa kiakili na kihisia.

Kwa mfano, makala moja katika gazeti American Family Physician yadokeza kwamba watoto wa akina mama walioshuka moyo hawafaulu katika mitihani ya kiakili wakilinganishwa na watoto wengine. Isitoshe, mshuko wa moyo unaweza kuathiri watoto wengine na mume.

Tiba

Suluhisho ni nini? Je, unapaswa kujikaza na kuvumilia tu? Inafariji kujua kwamba mshuko wa moyo baada ya kujifungua ni wa kitambo na unaweza kutibiwa.b Ingawa kushuka moyo kidogo kunaweza kwisha mama akipumzika na kupata utegemezo kutoka kwa familia, Idara ya Afya ya Wanawake inasema kwamba unapaswa kumwona daktari iwapo mshuko wa moyo unakufanya ushindwe kutekeleza shughuli zako za kila siku.

Matibabu ambayo hutumiwa kwa ukawaida yanatia ndani kutumia dawa,c kutafuta ushauri wa mtaalamu wa magonjwa ya akili, matibabu ya homoni, au ikiwa hali ni mbaya sana, matibabu hayo yote yanaweza kutumiwa pamoja. Ugonjwa huo unaweza kupunguzwa kwa kumweka mtoto katikati ya matiti ya mama yake na kumnyonyesha.d Pia kuna aina nyingine za tiba kama vile kutumia mitishamba, tiba ya kuchoma sindano ili kuamsha mishipa ya fahamu, na tiba nyinginezo.

Hata hivyo, kuna mambo unayoweza kufanya ili uweze kukabiliana na mshuko wa moyo. Mambo hayo yanatia ndani kula chakula chenye lishe (kama vile matunda, mboga, na nafaka nzima); kuepuka kafeini, pombe, na sukari; kufanya mazoezi ya kadiri; na kulala kidogo mtoto anapolala. Zoraya, mama Mkristo ambaye alilia daima alipojifungua mtoto msichana mwenye afya, anasema kilichomsaidia kurudia hali yake ya kawaida haraka iwezekanavyo ni kufanya shughuli zake za utumishi akiwa Shahidi wa Yehova.—Ona sanduku kwa madokezo zaidi.

Jinsi Wengine Wanavyoweza Kusaidia

Kwa kuwa kisababishi kimoja cha mshuko wa moyo baada ya kujifungua ni kukosa usingizi wa kutosha, wengine wanaweza kusaidia kufanya kazi za nyumbani na kumtunza mtoto. Utafiti unaonyesha kwamba ugonjwa huo hautokei sana mahali ambapo watu wa ukoo huishi pamoja na kuwasaidia akina mama na kuwazoeza. Wakati mwingi mtu anaweza kusaidia kwa kumsikiliza mama kwa fadhili, kumfariji, kuepuka kumkosoa au kumchambua. Kumbuka kwamba mshuko wa moyo baada ya kujifungua ni ugonjwa na si tatizo la kujiletea. Kama Shirika la Kuelimisha Wanawake Waliojifungua linavyosema, “wanawake hulemewa na ugonjwa huo kama vile wanavyoweza kulemewa na mafua, kisukari, au ugonjwa wa moyo.”

Kutokana na mambo tuliyozungumzia, ni wazi kwamba ingawa kipindi cha baada ya kujifungua chaweza kuwa wakati wenye furaha kwa akina mama, kinaweza pia kuwa kipindi chenye magumu. Kuelewa jambo hilo kunaweza kutusaidia tuwape akina mama waliojifungua karibuni utegemezo wanaohitaji.

[Maelezo ya Chini]

a Kushuka moyo baada ya kujifungua ni tofauti na mfadhaiko ambao huwapata akina mama waliopata matatizo wakati wa kujifungua. Mama anaweza kuugua magonjwa yote mawili wakati mmoja.

b Ona makala “Nilipambana na Ugonjwa wa Kushuka Moyo Baada ya Kujifungua,” katika toleo la Amkeni! la Julai 22, 2002.

c Dawa nyingine zinaweza kuharibu maziwa ya mama, kwa hiyo iwapo unaendelea kumnyonyesha mtoto, muulize daktari kuhusu tiba inayofaa.

d Ona makala “Njia ya Kipekee ya Kuokoa Uhai wa Watoto Wachanga” katika toleo la Amkeni! la Juni 8, 2002.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]

Kukabiliana na Mshuko wa Moyo Baada ya Kujifungua

1. Mweleze mtu fulani jinsi unavyohisi, hasa akina mama wengine.

2. Waombe wengine wakusaidie kumtunza mtoto, kufanya kazi za nyumbani, na kununua vitu. Mwombe mume wako akusaidie kumlisha mtoto usiku na kufanya kazi nyingine za nyumbani.

3. Tafuta jambo unaloweza kujifanyia ili kujitia moyo, hata kama ni kwa muda wa dakika 15 tu kila siku. Jitahidi kusoma, kutembea, na kuoga ili ustarehe.

4. Hata ukiweza kufanya jambo moja tu kwa siku, hayo ni maendeleo. Kuna siku ambazo huwezi kufanya jambo lolote. Usiudhike jambo hilo likitukia.

5. Kujitenga hukufanya ushuke moyo zaidi. Valia vizuri, kisha utoke nje ya nyumba angalau kwa muda mfupi kila siku. Kupata hewa safi na kubadilisha mandhari kutakufaidi sana wewe na mtoto wako.

[Hisani]

Yametolewa na Chuo cha Matabibu cha Marekani, Chuo cha Wataalamu wa Ukunga na Magonjwa ya Akina Mama cha Marekani, na Idara ya Afya ya Wanawake.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki