Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 3/14 kur. 14-15
  • Unapohisi Umechoshwa na Ndoa Yako

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Unapohisi Umechoshwa na Ndoa Yako
  • Amkeni!—2014
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • KIKWAZO
  • Urafiki Unapokuwa wa Karibu Kupita Kiasi
    Amkeni!—2013
  • Jinsi ya Kusamehe
    Amkeni!—2013
  • “Ndoa na Iheshimiwe”
    “Jitunzeni Katika Upendo wa Mungu”
  • Ndoa Yako-Yaweza Kuokolewa
    Amkeni!—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2014
g 3/14 kur. 14-15
Mwanamke anayehisi kwamba amechoshwa na ndoa

MSAADA KWA AJILI YA FAMILIA | NDOA

Unapohisi Umechoshwa na Ndoa Yako

KIKWAZO

Mume na mke wakiwa wamefungwa mnyororo miguuni

Kabla hamjaoana, wewe na mwenzi wako mlifurahia kufanya mambo mengi pamoja. Lakini sasa, kuna kizuizi kati yenu, hivyo mnahisi mko katika kifungo cha jela badala ya kufurahia ndoa.

Mnaweza kuboresha uhusiano wenu. Lakini kwanza, chunguza mambo yanayoweza kufanya uchoshwe na ndoa yako.

KWA NINI JAMBO HILO HUTUKIA

Unaanza kuona ukweli wa mambo. Shughuli za kila siku kama vile kazi, kulea watoto, na kushughulika na watu wa ukoo zinaweza kuvuruga furaha ya ndoa hatua kwa hatua. Isitoshe, mambo yasiyotazamiwa​—kama vile matatizo ya kifedha au kutunza mmoja wa familia mwenye ugonjwa wa kudumu—yanaweza kuleta mkazo kwenye ndoa.

Mnashindwa kupatana. Watu wanapochumbiana hawatilii maanani tofauti zao. Lakini baada ya kuoana, wanatambua kwamba wanatofautiana sana katika mambo kama vile kuwasiliana, kupangia matumizi ya pesa, na kusuluhisha matatizo. Sasa wanashindwa kabisa kuvumilia tofauti ambazo mwanzoni hazikuwaudhi sana.

Hujali hisia za mwenzako. Baada ya muda, maneno au matendo ya kuumiza na mizozano ambayo haijasuluhishwa inaweza kusababisha mume au mke aache kueleza hisia zake au hata aanzishe urafiki wa karibu na mtu mwingine.

Matarajio yenu hayakuwa halisi. Watu fulani huingia kwenye ndoa wakiamini kwamba wamempata mwenzi anayewafaa kabisa. Ingawa huenda hilo likaonekana kuwa jambo linalochochea upendo, linaweza kukuvunja moyo baadaye. Matatizo yanapotokea, wazo la kwamba mlifaana kikamili linatoweka, na kuwaacha mkihisi kwamba mlikosea kuoana.

MAMBO UNAYOWEZA KUFANYA

Zingatia sifa nzuri za mwenzi wako. Jaribu kufanya hivi: Orodhesha sifa tatu nzuri za mwenzi wako. Iweke orodha hiyo karibu nawe, labda nyuma ya picha ya harusi au kwenye simu ya mkononi. Iangalie orodha hiyo mara kwa mara ili ukumbuke sababu iliyokufanya uvutiwe naye. Kuzingatia sifa nzuri za mwenzi wako kutasitawisha amani na kukusaidia uvumilie tofauti zenu. —Kanuni ya Biblia: Waroma 14:19.

Pangeni muda wa kuwa pamoja. Kabla hamjaoana, bila shaka mlipangia muda wa kufanya mambo pamoja. Mlifurahia kusitawisha urafiki, lakini ilihitaji jitihada. Kwa nini msifanye hivyo sasa? Panga muda wa kipekee ambao wewe na mwenzi wako mnaweza kuwa pamoja, kama ilivyokuwa wakati wa uchumba. Kufanya hivyo kutaimarisha uhusiano wenu na kuwawezesha kukabiliana na matatizo yasiyotarajiwa.—Kanuni ya Biblia: Methali 5:18.

Zungumzia hisia zako. Ikiwa umeumizwa na maneno au matendo ya mwenzi wako, je, unaweza kumsamehe? Ikiwa huwezi, usiamue kumnyamazia tu. Ongea na mwenzi wako kwa utulivu bila kukawia, ikiwezekana siku hiyohiyo.—Kanuni ya Biblia: Waefeso 4:26.

Ikiwa umeumizwa na maneno au matendo ya mwenzi wako, je, unaweza kumsamehe?

Tambua tofauti kati ya hisia zako na nia ya mwenzi wako. Inawezekana kwamba hakuna yeyote kati yenu mwenye nia ya kumuumiza mwenziye. Mhakikishie mwenzi wako hilo kwa kumwomba msamaha kwa unyoofu ikiwa umemwumiza hisia. Halafu, zungumzieni mambo mnayoweza kufanya ili kuepuka kuumizana bila kukusudia. Fuateni ushauri huu wa Biblia: “Iweni wenye fadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma nyororo, mkisameheana kwa hiari.”—Waefeso 4:32.

Uwe na matarajio halisi. Biblia inasema kwamba wale wanaoingia kwenye ndoa “watakuwa na dhiki katika mwili wao.” (1 Wakorintho 7:28) Mkipatwa na dhiki, msiamue haraka-haraka kwamba mlikosea kuoana. Badala yake, shirikiana na mwenzi wako kutatua matatizo na mwendelee “kuvumiliana na kusameheana kwa hiari.”—Wakolosai 3:13.

MAANDIKO MUHIMU

  • “Tufuatilie mambo yanayofanya kuwe na amani.”​—Romans 14:19.

  • “Ushangilie pamoja na mke wa ujana wako.”​—Proverbs 5:18.

  • “Jua lisitue mkiwa katika hali ya kuchokozeka.”​—Ephesians 4:26.

ISHI KULINGANA NA NADHIRI YAKO YA NDOA

Je, unakumbuka maneno ya nadhiri yako ya ndoa? Kwa nini usiyatafakari tena na ujiulize: ‘Je, ninatimiza ahadi yangu?’ Usifikirie sana jinsi mwenzi wako anavyotimiza nadhiri yake. Nadhiri yako ilikuwa na maneno ambayo wewe ulisema ungefanya. Ikiwa kila mmoja wenu atazingatia kutimiza nadhiri yake, inaelekea kwamba nyote mtafurahia matokeo.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki