Sura ya 7
Utii Unakulinda Wewe
UNGEPENDA ikiwa ungeweza kufanya lo lote ulilotaka? Je! ziko nyakati ambapo usingetaka mtu akuambie la kufanya? Basi, niambie kweli.—
Lakini bora ni nini kwako? Je! kweli ni hekima kufanya lo lote utakalo? Au mambo yanakuwa bora wakati unapomtii baba na mama yako? Mungu anasema imekupasa uwatii wazazi wako, basi lazima iweko sababu nzuri kwa kutii. Na tuone ikiwa twaweza kujua.
Una umri gani?— Unajua baba yako ana umri gani?— Mama yako ana umri gani?— Wao wameishi zaidi sana kuliko wewe. Na kadiri mtu aishivyo zaidi ndivyo anakuwa na wakati zaidi kujifunza mambo. Anasikia mambo zaidi, na anaona mambo zaidi na kufanya mambo zaidi kila mwaka. Hivyo vijana wanaweza kujifunza kwa watu wazima.
Nani ameishi zaidi kuliko wewe au mimi au mtu mwingine ye yote? Ni Yehova Mungu. Yeye anajua zaidi kuliko wewe naye anajua zaidi kuliko mimi. Anapotuambia yaliyo mema kwetu, twaweza kuwa hakika kwamba ni kweli. Tukifanya ambayo anasema, yatatulinda. Imetupasa sikuzote tumtii yeye.
Basi waona, mimi vile vile lazima nitii. Lazima nimtii Mungu. Ni kwa faida yangu mwenyewe. Na inakufaidi wewe vile vile unapomtii Mungu.
Na tuchukue Biblia yetu tuone ambayo Mungu anawaambia watoto wafanye. Unaweza kuona kitabu cha Waefeso?— Tutasoma kuanzia Waefeso sura ya sita, mistari moja, mbili na tatu. Panasema: “Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo kaki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia.”
Hilo limo katika Biblia. Basi ni Yehova Mungu anayekuambia uwatii wazazi wako.
Ina maana gani ‘kuwaheshimu’ baba yako na mama yako?— Ina maana uwaonyeshe adabu. Imekupasa uwasikilize na kufanya wanalosema pasipo kunung’unika. Na Mungu anaahidi kwamba ukitii, itakuwa “heri” kwako.
Mimi najua hadithi juu ya watu fulani ambao maisha zao ziliokolewa kwa sababu walitii. Ungependa uisikie?—
Watu hawa waliishi katika mji mkubwa wa Yerusalemu hapo kale. Karibu watu wote katika mji huo walikuwa wabaya. Hawakumsikiliza Mungu. Yehova alimtuma Mwana wake awafundishe. Lakini hata hivyo hawakusikiliza. Mungu angewafanyia nini?—
Mwalimu Mkuu aliwaonya kwamba Mungu alikusudia kuharibu mji wao. Akasema majeshi ya askari yangepiga kambi kuzunguka mji na kuuangamiza. Aliwaambia watu tena namna wangeweza kuokoka ikiwa wangependa yaliyo mema. Hivi ndiyo alivyosema:
‘Wakati mnaona majeshi kuuzunguka Yerusalemu wote, basi ndio wakati wa kutoka katika Yerusalemu kukimbilia milimani.’—Luka 21: 20-22.
Ikatukia sawasawa kama Yesu alivyosema. Majeshi ya Rumi yakaja kuushambulia Yerusalemu. Yakapiga kambi kuzunguka pande zote. Ndipo kwa sababu fulani yakaondoka. Karibu watu wote wakadhani hatari ilikwisha. Wakakaa mjini. Lakini Yesu alikuwa amesema wafanye nini?
Wewe ungalifanya nini ikiwa ungalikuwa ukiishi katika Yerusalemu?— Wale waliomwamini Yesu kweli kweli waliacha nyumba zao wakakimbia kutoka Yerusalemu kwenda milimani. Si watu wazima peke yao; watoto vile vile walikwenda nao.
Lakini kweli walilindwa kwa sababu walitii?— Mwaka mzima Yerusalemu haukupatwa na kitu. Miaka mitatu hakukutukia kitu. Lakini basi katika mwaka wa nne majeshi ya Rumi yaka-rudi. Kwa wale waliokaa katika Yerusalemu ikawa sasa kuchelewa mno kuokoka. Wakati huu majeshi yakauharibu mji. Karibu watu wote ndani waliuawa.
Lakini ilikuwaje kwa wale waliokuwa wamemtii Yesu?— Wao walikuwa mbali sana na Yerusalemu. Hivyo hawakuumia. Utii uliwalinda.
Ikiwa unatii, je! itakulinda na wewe? Ndiyo. Ebu nikuonyeshe namna ilivyo. Pengine nitakuambia usicheze barabarani hata mara moja. Kwa sababu gani nafanya hivyo?— Ni kwa sababu huenda ukagongwa na gari ukauawa. Lakini pengine siku fulani utafikiri: “Sasa hakuna magari. Sitaumia. Watoto wengine wanacheza barabarani, nami sijawaona wakiumia.”
Hivyo ndivyo karibu watu wote katika Yerusalemu walivyofikiri. Majeshi ya Rumi yalipokwisha kuondoka, ikaonekana salama. Wengine walikuwa wakikaa mjini. Basi nao wakakaa. Walikuwa wameonywa, lakini hawakusikiliza. Kama matokeo, wakapoteza maisha zao. Na watoto wachezao barabarani wanaweza vile vile kupoteza maisha zao. Lo! namna ilivyo bora sana kutii!
Kutii wakati fulani tu hakufai. Lakini ukitii sikuzote, kweli itakulinda.
Nani anakuambia, “Watiini wazazi wenu”?— Ni Mungu. Na, kumbuka, anasema hivyo kwa sababu kweli akupenda wewe.
(Haya ni maandiko zaidi mazuri kuonyesha faida ya utii: Mhubiri 12:13; Wakolosai 3:20; Mithali 23:22.)