Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • te sura 8 kur. 35-38
  • Jirani Mwema

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Jirani Mwema
  • Kumsikiliza Mwalimu Mkuu
  • Habari Zinazolingana
  • Jinsi ya Kuwa Mwenye Fadhili
    Jifunze Kutoka kwa Mwalimu Mkuu
  • Msamaria Athibitika Kuwa Jirani wa Kweli
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
  • Namna Yesu Anavyofundisha
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
  • Kuwa “Msamaria Mwema” Kunamaanisha Nini?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
Pata Habari Zaidi
Kumsikiliza Mwalimu Mkuu
te sura 8 kur. 35-38

Sura ya 8

Jirani Mwema

JE! WAMJUA ye yote mwenye rangi ya ngozi tofauti na yako?⁠— Mahali pengine rangi ya ngozi ya karibu watu wote ni nyeusi au rangi ya kunde. Mahali pengine karibu kila mtu ana ngozi nyeupe. Wanazaliwa hivyo.

Je! inakufanya bora kuliko watu wengine ikiwa unayo rangi ya ngozi tofauti na yao? Je! mtu mwenye ngozi nyeusi afikiri yeye ni bora kuliko mwingine mwenye ngozi nyeupe? Au mtu fulani mwenye ngozi nyeupe afikiri yeye ni bora kuliko mtu mwenye ngozi nyeusi? Wewe waonaje?⁠—

Tukimsikiliza Mwalimu Mkuu, Yesu Kristo, tutakuwa wema kwa kila mtu. Haifanyi tofauti yo yote mtu ni mtoka taifa gani au ana rangi ya ngozi gani. Yatupasa tuwapende watu wa namna zote. Hivi ndivyo Yesu alifundisha.

Siku moja, Myahudi akaja kumwuliza Yesu ulizo gumu. Mtu huyu alifikiri Yesu asingejua kujibu. Akasema: ‘Yanipasa nifanye nini niishi milele?’

Hili lilikuwa ulizo jepesi kwa Mwalimu Mkuu. Lakini pahali pa kujibu mwenyewe, Yesu alimwuliza yule mtu: ‘Sheria ya Mungu inasema yatupasa tufanye nini?’

Yule mtu akajibu: ‘Sheria ya Mungu inasema, “Yakupasa umpende Yehova Mungu wako kwa moyo wako wote, na yakupasa umpende jirani yako kama wewe mwenyewe.”

Yesu akasema: ‘Umejibu vizuri. Endelea kufanya hivi nawe utapata uzima wa milele.’

Lakini yule mtu hakutaka ampende kila mtu. Basi akajaribu kutoa sababu. Akamwuliza Yesu: “Na jirani yangu ni nani?” Wewe ungalijibuje hilo? Zaidi aliye jirani yako ni nani?—

Mtu huyu labda alitaka Yesu aseme: ‘Jirani zako ni rafiki zako.’ Lakini namna gani watu wengine? Je! wao vile vile ni jirani zetu?⁠—

Ili kujibu ulizo, Yesu alisimulia hadithi. Ilikuwa juu ya Myahudi na Msamaria. Ilikuwa kama hivi:

Mtu alikuwa akienda njiani kutoka mji wa Yerusalemu kwenda Yeriko. Mtu huyu alikuwa Myahudi. Alipokuwa akitembea, wanyang’anyi walimkamata. Wakamwangusha chini, wakachukua fedha na nguo zake. Wanyang’anyi wakampiga sana wakamwacha kando ya njia karibu kufa.

Muda kidogo kuhani akapita njia hiyo. Akamwona yule mtu aliyeumizwa vibaya. Alifanya nini? Wewe ungalifanya nini?⁠—

Kuhani akapita njia nyingine. Hakusimama hata. Hakufanya lo lote ili amsaidie yule mtu.

Akaja mwingine mtu wa dini sana njia ile ile. Alikuwa Mlawi, aliyetumikia katika hekalu katika Yerusalemu. Yeye angesimama asaidie? Akafanya lile lile kama kuhani. Hakutoa msaada. Je! hivyo ilikuwa vizuri kufanya?⁠—

Wa mwisho Msamaria akaja njia ile. Akamwona Myahudi amelala hapo ameumizwa vibaya. Sasa, karibu Wasamaria na Wayahudi wote hawakupendana. Basi je! Msamaria huyu angemwacha yule mtu bila kumsaidia? Je! angejiambia mwenyewe: ‘Sababu gani nimsaidie Myahudi huyu? Yeye asingenisaidia ikiwa ningeumia’?

Basi, Msamaria huyu akamtazama yule mtu aliyelala kando ya njia, akamhurumia sana. Asingeweza kumwacha afe.

Basi Msamaria akashuka kutoka mnyama wake. Akamwendea yule mtu, akaanza kumganga vidonda vyake. Akamwagia mafuta na divai juu ya vidonda. Hii ingesaidia vidonda kupona. Halafu akafunga vidonda kwa kitambaa.

Polepole Msamaria akamwinua mtu aliyeumizwa akamweka juu ya mnyama wake. Kisha wakaenda polepole njiani mpaka wakafika kwenye nyumba ya wageni, au hoteli ndogo. Hapa Msamaria akampatia mtu mahali pa kukaa, naye akamwangalia vizuri.

Sasa Yesu alimwuliza yule mtu ambaye alikuwa akisema naye: ‘Unafikiri nani kati ya watu hawa watatu alikuwa jirani mwema?’ Wewe ungejibu namna gani? Je! alikuwa kuhani, Mlawi au Msamaria?⁠—

Yule mtu akajibu: ‘Msamaria alikuwa jirani mwema. Yeye alisimama akamtunza mtu aliyeumizwa.’

Yesu akasema: ‘Wasema kweli. Basi nenda zako kafanye vivyo hivyo mwenyewe.’—Luka 10:25-37.

Je! hiyo haikuwa hadithi nzuri? Inaonyesha wazi nani walio jirani zetu. Jirani zetu si rafiki zetu wa karibu tu. Jirani zetu si watu wa nchi ya kwetu tu, au watu wenye rangi ya ngozi ile ile kama sisi. Jirani zetu ni watu wa namna zote.

Basi ukimwona mtu anaumia, utafanya nini?— Namna gani ikiwa mtu huyo ni wa nchi nyingine au rangi ya ngozi yake ni tofauti na yako?— Hata hivyo yeye ni jirani yako. Hivyo imekupasa umsaidie. Ukiona wewe ni mdogo mno kusaidia, basi unaweza kuniambia nisaidie. Au unaweza kuita polisi, au mwalimu wa masomo. Huko ndiko kuwa kama Msamaria.

Mwalimu Mkuu anataka tuwe wema. Anataka tusaidie wengine, si kitu ni nani. Ndiyo sababu alisimulia hadithi juu ya mtu aliyekuwa jirani mwema.

(Juu ya shauri hili la namna imetupasa kuwaona watu wa makabila na mataifa mengine, soma tena Matendo 10:34, 35; 17:26; Mathayo 5:44-48.)

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki