Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w79 10/15 kur. 8-12
  • Mtu wa Kwanza Kutiwa Mafuta Kwa Roho Takatifu na Nguvu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mtu wa Kwanza Kutiwa Mafuta Kwa Roho Takatifu na Nguvu
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
  • Habari Zinazolingana
  • Yesu Kristo Ni Nani?
    Biblia Inafundisha Nini Hasa?
  • Masihi Atokea
    Imani ya Kweli—Siri ya Kuwa na Maisha Yenye Furaha
  • Masihi Afika
    Biblia—Ina Ujumbe Gani?
  • Yesu Kristo Ni Nani?
    Biblia Inatufundisha Nini?
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
w79 10/15 kur. 8-12

Mtu wa Kwanza Kutiwa Mafuta Kwa Roho Takatifu na Nguvu

(Funzo la Kitabu)

1, 2. (a) Masihi aliyeahidiwa angetiwa mafuta na nani na kwa kitu gani? (b) Angetaja unabii gani wa Isaya na kuutumia juu yake mwenyewe?

WAFALME na makuhani wakuu wa Israeli wa kale waliwekwa katika cheo kwa kumwagiwa kichwani mafuta rasmi. Je! Masihi aliyeahidiwa angetiwa mafuta hivyo? Sivyo! Masihi halisi alipaswa kutiwa mafuta na Mungu ‘kwa roho takatifu na nguvu.’ (Matendo 10:38) Yeye ndiye aliyekuwa na ruhusa ya kutumia maneno ya unabii wa Isaya 61:1-3 juu yake mwenyewe:

2 “Roho ya Bwana Yehova Mwenye Enzi Kuu ya Ulimwengu Wote i juu yangu, kwa sababu Yehova amenitia mafuta nisimulie habari njema kwa wapole. Yeye amenituma mimi kuganga waliovunjika moyo, kutangaza uhuru kwa wale waliochukuliwa mateka na kufunguliwa wazi kwa macho hata kwa wafungwa; kutangaza mwaka wa nia njema upande wa Yehova na siku ya kisasi upande wa Mungu wetu; kufariji wote waombolezao; na kuwapa migawo wale wanaoombolezea Sayuni, na kuwapa vazi la kichwa badala ya majivu, mafuta ya shangwe badala ya kuomboleza, vazi la sifa badala ya roho ya kushuka moyo; nao waitwa miti mikubwa ya haki, iliyopandwa na Yehova, ili yeye apate uzuri.” (NW)

3. Ni kwa sababu gani watu wa nyakati zilizotangulia ambao roho ya Mungu ilifanya kazi juu yao hawakuwa Masihi aliyeahidiwa?

3 Watu wa zamani walifunikwa na roho ya Mungu au ikatenda kazi juu yao au wakajawa nayo. Lakini hawakutiwa mafuta kwayo. Kwa hiyo wao hawakuwa Masihi aliyetazamiwa kwa muda mrefu. Ndivyo ilivyokuwa kwa habari ya Yohana Mbatizaji, ambaye malaika Gabrieli alikuwa amemwambia baba yake, kuhani Zekaria hivi: “Naye atajazwa [roho takatifu] hata tangu tumboni mwa mamaye.”​—⁠Luka 1:15:

4. Yohana Mbatizaji, ajapojazwa roho takatifu tangu alipokuwa katika tumbo la uzazi la mamaye, alikiri nini kwa habari ya Kristo?

4 Makuhani na Walawi walitumwa kutoka Yerusalemu wakamwagize Yohana mwenyewe awaeleze yeye alikuwa nani rasmi kwa sababu ya kazi aliyokuwa akifanya. Yohana alionaje? “Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo. Wakamwuliza, Ni nini basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La. Basi wakamwambia, U nani? tuwape majibu wale waliotupeleka. Wanenaje juu ya nafsi yako? Akasema, mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana! kama vile alivyosema nabii Isaya.”​—⁠Yohana 1:19-23; Isa. 40:3; Mal. 4:5, 6; Kum. 18:15-19.

5, 6. (a) Mungu alimtuma Yohana afanye nini kwa habari ya Kristo? (b) Yohana alijitofautishaje na Masihi wa kweli au Kristo?

5 Hivyo Yohana alikana kwamba yeye hakuwa Aliyeahidiwa na kutiwa mafuta kwa roho ya Mungu, ingawa alikuwa amejawa na roho takatifu. Hakujaribu kuwa Kristo wa uongo, bali alikiri kwamba alikuwa mtangulizi tu wa Kristo wa kweli au Masihi. Mungu alimtuma akambatize Kristo wa kweli au Masihi katika maji.​—⁠Yohana 1:29-34.

6 Jambo lililoandikwa katika Luka 3:15-17 linazidi kuhakikisha kwamba Yohana alikuwa mwaminifu: “Basi, watu walipokuwa wakingoja yatakayotokea, wote wakiwaza-waza mioyoni mwao habari za Yohana, kama labda yeye ndiye Kristo, Yohana alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye atawabatiza kwa [roho takatifu] na kwa moto; ambaye pepeo lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake, na kuikusanya ngano ghalani mwake, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.”

7. Kwa sababu gani kubatizwa kwa roho kungetamanika zaidi kuliko kubatizwa kwa moto?

7 Maneno ya Yohana yalionyesha wazi kwamba Masihi asingebatizwa au kutiwa mafuta kwa roho ya Mungu tu bali pia angeweza kubatiza wengine kwa roho takatifu. Ingekuwa afadhali zaidi mtu abatizwe kwa roho takatifu kuliko kubatizwa kwa moto ambao ungemharibu kama makapi yasiyofaa kitu yanayoharibiwa motoni usiozimwa mapaka makapi yote yameteketezwa.​—⁠Mt. 3:7-12.

8. Ni kwa sababu gani wakati huo watu walikuwa wakimtazamia Masihi atokee, na ni kwa sababu gani jambo hilo lilikuwa la haraka kwao?

8 Si ajabu kwamba ‘watu walikuwa wakingoja.’ Inaelekea kwamba walikuwa wameangalia Maandiko wakaona wakati wa kutokea Masihi umefika. Kwa hiyo walianza kuwaza kama Yohana Mbatizaji ndiye Masihi aliyeahidiwa. (Dan. 9:24-27) Shauri la Masihi au Kristo lilikuwa la haraka. Mungu, Mwenye kumtuma Masihi, asingeukokota wakati milele. Alikuwa ameamua kumtuma Masihi, na alikuwa na wakati barabara wa kufanya hivyo. Yeye si mtu wa kuahirisha mambo, bali hushikamana na orodha yake ya wakati iliyoonyeshwa katika Neno lake.

9. Wagalatia 4:4, 5 yaonyeshaje kwamba Mungu haahirishi mambo?

9 Wagalatia 4:4, 5 yasema: “Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.”

10. Mungu alimtuma Mwanawe kwa wakati wake kutoka wapi, na azaliwe na mwanamke wa taifa gani?

10 Mwandikaji wa maneno hayo, mtume Paulo, alikuwa na mengi ya kusema juu ya nyakati na majira katika mipango ya Mungu. Asema kwamba Mwana wa Mungu angekuwa mkombozi wa Wayahudi kwa kuwanunua. Kwa hiyo angekuwa Masihi wao, Kristo. Mungu alimtuma kutoka wapi? Kutoka mbinguni, ambako “Mwanawe pekee” huyu alikuwa amekuwa tangu Mungu alipomwumba kale ya kale. Kupata kwake kuwa “chini ya sheria” kulimaanisha kwamba alizaliwa kama Myahudi, Mwisraeli, mshiriki wa taifa lililokuwa katika agano la Torati na Yehova ambalo Musa ndiye aliyekuwa amekuwa mpatanishi wake. Kwa hiyo mwanamke ambaye alizaa Mwana wa Mungu alipaswa kuwa Myahudi, yeye mwenyewe akiwa chini ya sheria ya Musa.​—⁠Gal. 3:19-25.

11. Kwa sababu ya tofauti ya makao ya Mwana wa Mungu na ya mwanamke, ni jambo gani lililokuwa la lazima ili Mwana huyo awe Masihi?

11 “Ilikuwa lazima mwujiza utokee, na Mungu Mwenye Nguvu Zote peke yake ndiye angeweza kuufanya. Mwanawe “mzaliwa wa kwanza,” Neno au Logos, alikuwa juu mbinguni akiwa mtu wa kiroho mwenye nguvu nyingi, na hali mwanamke aliyepaswa kumzaa kama akitaka kuwa Masihi, alikuwa hapa chini duniani. Mwana asingeweza kuingia katika tumbo la uzazi la mwanamke huyo Myahudi akiwa katika cheo hicho. Halafu? Basi, Mwana alipaswa kujiondolea vyeo vyote alivyokuwa navyo alipokuwa “yuna namna ya Mungu.” Alipaswa kuhamishwa uhai wake kutoka mbingu zisizoonekana utiwe katika tumbo la uzazi la mwanamke huyo. Hivyo angekuja azaliwe “ana umbo kama mwanadamu.” Hiyo ilimtaka Mwana wa Mungu ajinyenyekeze sana. (Flp. 2:5-8) Lakini Mwana huyo alikuwa na nia ya kufanya hivyo kwa sababu alimpenda Baba yake na kusudi la kutimiza malengo ya Baba yake wa mbinguni.

12. “Mwanamke” aliyechaguliwa na Mungu alikuwa nani, na ni kwa sababu gani ilikuwa lazima Masihi awe mwanawe “mzaliwa wa kwanza”?

12 Baba wa mbinguni alifanyaje mwujiza huu? Alitumia nini? Alitumia “mwanamke.” Wanawake wengi Waisraeli, hasa wale wa kabila la Yuda, pengine walitaka wao ndio wamzae Masihi aliyeahidiwa. Lakini haikuwa haki yao kujichagulia kuwa mama ya Masihi. Baba wa mbinguni wa Masihi peke yake Ndiye angeweza kuchagua. Alichagua. Mwanamke aliyemchagua alikuwa “bikira” asiyeolewa. (Isa. 7:14) Kama angalikuwa amekwisha olewa akapata watoto, hiyo ingetia mashaka juu ya ubaba na urithi na haki. Kwa hiyo “bikira” ambaye Mungu alichagua alikuwa “bikira.” (Mt. 1:22, 23) Kuzaliwa kwa “mzaliwa wa kwanza” wa Mungu kama mwanadamu mkamilifu mwenye damu na nyama kulipaswa kulingane na kuzaliwa kwa “mzaliwa wa kwanza” wa mwanamke huyo pia.​—⁠Linganisha Wakolosai 1:15; Yohana 3:16, 17.

13. Mungu alimtuma Gabrieli kwa nani katika safari ya pili, naye Gabrieli aliwezaje kuonekana kwake?

13 Mwanamke aliyechaguliwa alipaswa kuwa mzao wa Mfalme Daudi mwana wa Yese pia. Akiwa na uhusiano huo na Mfalme Daudi, mwanamke huyo angeweza kumpa mwana mzaliwa wake wa kwanza haki ya asili ya kuwa mfalme wa ufalme wa Daudi juu ya makabila kumi na mawili ya “nyumba ya Yakobo” (Israeli). Kwa kufaa, mwanamke aliyechaguliwa alikuwa amezaliwa katika “mji wa Daudi,” mji wa Bethlehemu, katika jimbo la Yuda. (Luka 2:11) Lakini wakati Mungu alipomjulisha mwanamke huyo kwamba angempa pendeleo kuu, mwanamke huyo alikuwa akiishi katika Nazareti, mji wa Galilaya. Karibu miezi sita kabla ya hili, Mungu alikuwa amemtuma malaika Gabrieli amtangazie kuhani Zekaria kuzaliwa kunakokuja kwa mwana atakayeitwa Yohana, na kwa kufaa Mungu sasa alimtuma Gabrieli kwa yule mama ambaye angemzaa Masihi ambaye Yohana angemjulisha kwa watu. Mwanamke huyo alikuwa bikira Myahudi aliyeitwa Mariamu, binti ya Eli wa ukoo wa kifalme wa Daudi. Gabrieli alijivika mwili wa kibinadamu amtokee Mariamu. Salamu zake zilimstaajabisha Mariamu. Kwa sababu gani mgeni huyo wa ghafula alisema kwamba Yehova alikuwa na Mariamu? Sababu gani awe naye?

14. Gabrieli alisema nini alipokuwa akimweleza Mariamu sababu gani Mungu alikuwa pamoja naye?

14 Ni kwa sababu Yehova alikuwa amemchagua awe mama ya mfalme mtukufu wa Kimasihi. Kwa hiyo Gabrieli alisema hivi: “Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukuwa mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na [Yehova] Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.”​—⁠Luka 1:26-33.

15. Malaika huyo alisema ni jambo gani lingetukia kwa Mariamu, kukiwa na matokeo gani?

15 Hilo lingewezekanaje kutukia kwa mwanamwali, “bikira” asiyeolewa? Hilo ndilo lilikuwa ulizo la Mariamu, nasi pia tungaliuliza hivyo kama tungalikuwako. Kwa hiyo sasa acheni tuone kile ambacho kingetenda kazi juu ya Mariamu. “Akajibu akamwambia, [roho takatifu itakujilia] juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.”​—⁠Luka 1:34, 35.

16. (a) Ni kwa sababu gani kilichozaliwa na Mariamu kingekuwa “kitakatifu”? (b) Mariamu angeweza kumwambiaje Gabrieli, walakini alimjibuje?

16 ‘Roho takatifu’ ilikuwa ikianza kutenda kazi, na ingefanya kitu ‘kitakatifu’ kizaliwe. Kingezaliwa kibikira. Huo haukuwa mwujiza asioweza kufanya Mungu kwa maana malaika Gabrieli alimalizia kwa kumwambia Mariamu hivi: “Hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.” (Luka 1:37) Mariamu alijibuje alipoambiwa hayo yote? Angaliweza kusema: ‘Lakini, angalia! mimi nimekwisha poswa niolewe na seremala Yusufu mwana wa Yakobo, wa nyumba ya kifalme ya Daudi. Lazima niwe mama ya watoto wake. Siwezi kuvunja uchumba wangu na Yusufu. Tafadhali niache!’ Hivyo kulielekea kuwa na matatizo, lakini Mungu pia aliyajua. Kwa hiyo, Mariamu aliamini akamjibu Gabrieli hivi: “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.”​—⁠Luka 1:38.

17. Sasa ni jambo gani lililotukia kwa Mwana wa Mungu “mzaliwa wa kwanza” mbinguni, naye Yusufu aliyemchumbia Mariamu aliambiwa afanye nini?

17 Sasa ilifaa Mariamu azae kwa mwujiza wa Mungu Mwenye Nguvu Zote. Kwa ghafula, bila ya Mariamu kujua duniani, Mwana “mzaliwa wa kwanza” wa Mungu alitoweka mbinguni. Nguvu ya uhai wake ikahamishwa ikashushwa kutiwa ndani ya mwili wa bikira Mariamu. Kwa hiyo, “Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa [roho takatifu]. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa [Yehova] alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa [roho takatifu]. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.”​—⁠Mt. 1:18-21.

18. Kwa Kweli Yesu alikuwa mwana wa nani, nalo jina lake lilikuwa la unabii namna gani?

18 Jina Yesu lilikuwa la unabii. Ndiyo namna fupi ya jina Yehoshua, mana yake “Yehova Ni Wokovu.” Kwa kufaa, mwenye jina hilo ‘angeokoa watu wake na dhambi zao.’ Angekuwa “Mwana wa Mungu” kama Gabrieli alivyosema, si wa Yusufu.

19. Ni kwa sababu gani mwana wa Mariamu Yesu hakuwa Mwana mpya wa Mungu, na kwa sababu gani yeye hakuwa “Mungu mwenye mwili” au “Mungu-mwanadamu”?

19 Mwana mzaliwa wa kwanza Wa Mariamu aliyemzaa kwa mwujiza hakupaswa kuwa Mwana mpya wa Mungu, bali alikuwa Mwana wa Mungu yule yule aliyekuwako muda mrefu ambaye uhai wake ulihamishwa kutoka mbinguni ukaletwa duniani Mariamu akiwa ndiye mama yake wa kibinadamu. Kwa kufaa, asingeweza kuitwa anavyoitwa na wanadini wa Jumuiya ya Wakristo, “Mungu mwenye mwili,” usemi usiopatikana katika Biblia iliyoongozwa na Mungu. Katika mbingu Mwana “mzaliwa wa kwanza” wa Mungu alikuwa na cheo Neno (au Logos). Kwa hiyo, katika Yohana 1:14, twasoma hivi: “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba.” Viongozi wa dini za Jumuiya ya Wakristo wanakosea kumwita “Mungu-mwanadamu,” kwa maana, katika 1 Timotheo 2:5, 6, anaitwa “Mwanadamu Kristo Yesu.” Yeye hakudai na asingeweza kudai kuwa Mungu Aliye Juu Zaidi.​—⁠Yohana 20:31; Luka 1:32.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki