Urithi wa Upapa
Maana: Fundisho la kwamba wale mitume 12 wana warithi ambao wamepokea mamlaka iliyopitishwa kutoka kwa Mungu. Katika Kanisa Katoliki, inasemekana kwamba maaskofu wakiwa kikundi ni warithi wa mitume, na papa anadaiwa kuwa mrithi wa Petro. Inaaminiwa kwamba mapapa Wakatoliki wanamfuata Petro, ambaye inasemwa kwamba Kristo alimpa ukuu wa mamlaka juu ya Kanisa zima, wakichukua cheo cha Petro na kutimiza kazi zake. Hilo si fundisho la Biblia.
Je, Petro ndiye “mwamba” ambao kanisa lilijengwa juu yake?
Mt. 16:18, UV: “Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.” (Katika muktadha [mstari wa 13 na wa 20], ona kwamba mazungumzo hayo yanakazia utambulisho wa Yesu.)
Mitume Petro na Paulo walielewa nani kuwa “mwamba,” lile “jiwe la pembeni”?
Mdo. 4:8-11, UV: “Ndipo Petro, akijaa Roho Mtakatifu, akawaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee . . . kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni.”
1 Pet. 2:4-8, UV: “Mmwendee yeye [Bwana Yesu Kristo], . . . ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo. Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, na kila amwaminiye hatatahayarika. Basi, heshima hii ni kwenu ninyi mnaoamini. Bali kwao wasioamini, jiwe walilolikataa waashi, limekuwa jiwe kuu la pembeni. Tena, jiwe la kujikwaza mguu, na mwamba wa kuangusha.”
Efe. 2:20, UV: “Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni.”
Agustino (ambaye Kanisa Katoliki lilimwona kuwa mtakatifu) aliamini nini?
“Katika kipindi hicho cha upadre wangu, mimi pia niliandika kitabu dhidi ya barua ya Donato . . . Kwenye fungu fulani katika kitabu hicho, nilisema hivi kumhusu Mtume Petro: ‘Kanisa lilijengwa juu yake kana kwamba juu ya mwamba.’ . . . Lakini najua kwamba baadaye, nilieleza mara nyingi yale ambayo Bwana alisema: ‘Wewe ni Petro, na juu ya mwamba huu nitajenga Kanisa langu,’ kwamba ieleweke kuwa lilijengwa juu ya Yule ambaye Petro alimkiri akisema: ‘Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai,’ na kwa hiyo Petro, aliyeitwa jina la mwamba huo, aliwakilisha mtu wa Kanisa lililojengwa juu ya mwamba huo, na amepokea ‘funguo za ufalme wa mbinguni.’ Kwa maana aliambiwa, ‘Wewe ni Petro’ wala hakuambiwa, ‘Wewe ndiwe mwamba.’ Lakini, kwa kumkiri yule ambaye Kanisa lote pia linamkiri, ‘mwamba ulikuwa Kristo,’ Simoni aliitwa Petro.”—The Fathers of the Church—Saint Augustine, the Retractations (Washington, D.C.; 1968), kilichotafsiriwa na Mary I. Bogan, Buku 1, uku. 90.
Je, mitume wengine walimwona Petro kuwa mkuu kati yao?
Luka 22:24-26, UV: “Yakatokea mashindano kati yao, kwamba ni nani anayehesabiwa kuwa mkubwa. Akawaambia, Wafalme wa Mataifa hutawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili; lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye.” (Ikiwa Petro ndiye aliyekuwa “mwamba,” je, yeyote angeuliza ni yupi kati yao anayepaswa ‘kuhesabiwa kuwa mkubwa’?)
Kwa kuwa Yesu Kristo, aliye kichwa cha kutaniko, yu hai, je, anahitaji kuwa na warithi?
Ebr. 7:23-25, UV: “Tena wale walifanywa makuhani wengi [katika Israeli], kwa sababu wazuiliwa na mauti wasikae; bali yeye [Yesu Kristo], kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka. Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye.”
Rom. 6:9, UV: “Tukijua ya kuwa Kristo akiisha kufufuka katika wafu hafi tena, wala mauti haimtawali tena.”
Efe. 5:23, UV: “Kristo naye ni kichwa cha Kanisa.”
“Funguo” alizokabidhiwa Petro zilikuwa nini?
Mt. 16:19, UV: “Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.”
Katika Ufunuo, Yesu alitaja ufunguo wa mfano ambao yeye mwenyewe anautumia kuwafungulia wanadamu mapendeleo na nafasi
Ufu. 3:7, 8, UV: “Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye. . . . Nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako.”
Petro alizitumia “funguo” alizokabidhiwa ili kuwafungulia (Wayahudi, Wasamaria, Mataifa) nafasi ya kupokea roho ya Mungu wakiwa na tumaini la kuingia katika Ufalme wa mbinguni
Mdo. 2:14-39, UV: “Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu . . . Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo. Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.”
Mdo. 8:14-17, UV: “Mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana; ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; Kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu.” (Mstari wa 20 unaonyesha kwamba Petro ndiye aliyekuwa akiongoza katika pindi hiyo.)
Mdo. 10:24-48, UV: “Wakaingia Kaisaria. Na Kornelio [Mtu wa mataifa ambaye hakuwa ametahiriwa] alikuwa akiwangojea. . . . Petro akafumbua kinywa chake, akasema, . . . Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno.”
Je, mbingu ilimngojea Petro afanye maamuzi ndipo ifuate uongozi wake?
Mdo. 2:4, 14, UV: “Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. . . . Lakini [baada ya Kristo, kichwa cha kutaniko, kuwachochea kupitia roho takatifu] Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia.” (Ona mstari wa 33.)
Mdo. 10:19, 20, UV: “Roho akamwambia, Wako watu watatu wanakutafuta. Basi ondoka ushuke ufuatane nao [hadi kwenye nyumba ya Kornelio, mtu wa mataifa], usione tashwishi, kwa maana ni mimi niliyewatuma.”
Linganisha na Mathayo 18:18, 19.
Je, Petro ndiye huamua ni nani anayestahili kuingia katika Ufalme?
2 Tim. 4:1, UV: “Kristo Yesu . . . atakayewahukumu walio hai na waliokufa.”
2 Tim. 4:8, UV: “Baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana [Yesu Kristo], mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.”
Je, Petro alikuwa Roma?
Roma pametajwa katika mistari tisa ya Maandiko Matakatifu; na hakuna hata mmoja kati ya mistari hiyo unaosema kwamba Petro alikuwa huko. Barua ya Kwanza ya Petro 5:13, huonyesha kwamba alikuwa katika Babiloni. Je, hilo ni jina la Roma la kifumbo? Kuwa kwake katika Babiloni kulipatana na mgawo wake wa kuwahubiria Wayahudi (kama inavyoonyeshwa katika Wagalatia 2:9), kwa kuwa kulikuwa na Wayahudi wengi katika jiji la kale la Babiloni na kandokando yake. Encyclopaedia Judaica (Yerusalemu, 1971, Buku la 15, safu ya 755), kinapozungumzia kufanyizwa kwa Talmud ya Babiloni, hurejelea “shule kubwa za Babiloni” za dini ya Kiyahudi katika Wakati wa Kawaida.
Je, kumekuwa na mfuatano usiokatizwa wa warithi kuanzia Petro mpaka mapapa wa siku hizi?
Mjesuti John McKenzie, alipokuwa profesa wa theolojia katika Notre Dame, aliandika hivi: “Hakuna uthibitisho wa kihistoria wa kuwapo kwa mfuatano usiokatizwa wa mamlaka ya kanisa.”—The Roman Catholic Church (New York, 1969), uku. 4.
New Catholic Encyclopedia hukiri hivi: “ . . . uchache wa hati huacha mengi ambayo hayako wazi juu ya usitawi wa kwanza wa uaskofu . . . ”—(1967), Buku la 1, uku. 696.
Madai ya kwamba wamechaguliwa na Mungu ni ya bure ikiwa wale wanaodai hivyo hawamtii Mungu na Kristo
Mt. 7:21-23, UV: “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”
Ona pia Yeremia 7:9-15.
Je, wanaodaiwa kuwa warithi wa mitume wameshikamana na mafundisho na matendo ya Yesu Kristo na mitume wake?
A Catholic Dictionary inasema hivi: “Kanisa Katoliki ni la Mitume, kwa sababu fundisho lake ndilo imani iliyofunuliwa kwa Mitume wakati mmoja, imani ambayo linalinda na kueleza, bila kuiongezea neno wala kuiondolea neno.” (London, 1957, W. E. Addis na T. Arnold, uku. 176) Je, mambo ya uhakika yanathibitisha hilo?
Mungu alivyo
“Utatu ndilo neno linalotumiwa kuonyesha fundisho kuu la dini ya Kikristo.”—The Catholic Encyclopedia (1912), Buku la 15, uku. 47.
“Neno Utatu, wala fundisho la wazi kama hilo, halionekani katika Agano Jipya . . . Fundisho hilo lilisitawishwa hatua kwa hatua kwa muda wa karne kadhaa na kwa mabishano mengi.”—The New Encyclopædia Britannica (1976), Macropædia, Buku la 10, uku. 126.
“Wafafanuzi na wanatheolojia wa Biblia, kutia ndani idadi inayoongezeka ya Wakatoliki, wanatambua kwamba haimpasi mtu kusema juu ya Utatu katika Agano Jipya bila ufafanuzi mzito. Pia, wanahistoria wa mafundisho ya kidini na wanatheolojia wanatambua kwamba mtu anaposema juu ya Utatu usiohitaji kufafanuliwa, huwa ameondoka katika kipindi cha mwanzo wa Ukristo akaingia, tuseme, kwenye ile robo ya mwisho ya karne ya 4.”—New Catholic Encyclopedia (1967), Buku la 14, uku. 295.
Useja wa makasisi
Papa Paulo wa Sita, katika waraka wake Sacerdotalis Caelibatus (Useja wa Makasisi, 1967), aliidhinisha useja kuwa takwa kwa makasisi, lakini alikiri kwamba “Agano Jipya linalohifadhi mafundisho ya Kristo na ya Mitume . . . halidai waziwazi useja wa wahudumu watakatifu . . . Yesu Mwenyewe hakuufanya uwe takwa Alipokuwa akiwachagua wale Kumi na Wawili, wala Mitume hawakudai wale waliosimamia jumuiya za kwanza za Kikristo wawe waseja.”—The Papal Encyclicals 1958-1981 (Falls Church, Va.; 1981), uku. 204.
1 Kor. 9:5, UV: “Hatuna uwezo kuchukua pamoja nasi mke aliye ndugu, kama wao mitume wengine, na ndugu wa Bwana, na Kefa?” (“Kefa” ni jina la Kiaramu alilopewa Petro; ona Yohana 1:42. Ona pia Marko 1:29-31, ambapo mama-mkewe wa Simoni, au Petro, anatajwa.)
1 Tim. 3:2, UV: “Basi imempasa askofu awe . . . mume wa mke mmoja [“ameoa mara moja tu,” NAB].”
Kabla ya enzi ya Ukristo, dini ya Ubudha iliwataka makasisi na watawa wake wa kiume wawe waseja. (History of Sacerdotal Celibacy in the Christian Church, London, 1932, chapa ya nne, iliyosahihishwa, Henry C. Lea, uku. 6) Hata mapema zaidi, makasisi wakuu wa Kibabiloni walitakiwa wawe waseja, kulingana na The Two Babylons cha A. Hislop.—(New York, 1943), uku. 219.
1 Tim. 4:1-3, UV: “Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; . . . wakiwazuia watu wasioe.”
Kujitenga na ulimwengu
Papa Paulo wa Sita, alipokuwa akihutubia Umoja wa Mataifa katika mwaka wa 1965, alisema hivi: “Watu wa dunia wanageukia Umoja wa Mataifa kuwa tumaini la mwisho la upatano na amani; Tunatoa sifa yao ya heshima na ya tumaini, pamoja na Yetu wenyewe.”—The Pope’s Visit (New York, 1965), Time-Life Special Report, uku. 26.
Yoh. 15:19, UV: “[Yesu Kristo akasema:] Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia.”
Yak. 4:4, UV: “Hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu?”
Kutumia silaha za vita
Mwanahistoria Mkatoliki E. I. Watkin aliandika hivi: “Ingawa ni vigumu kukubali, hatuwezi kukataa wala kupuuza uhakika wa kihistoria kwamba nyakati zote Maaskofu wameunga mkono vita vyote vinavyopiganwa na serikali ya nchi yao ili kuendeleza mafundisho ya uwongo au ushikamanifu usio wa kweli. Kwa hakika, sijui kisa chochote ambapo makasisi wa taifa walishutumu vikali vita vyovyote kuwa si vya haki . . . Hata nadharia rasmi iwe gani, kwa matendo, wakati wa vita Maaskofu wa Wakatoliki wamefuata kanuni ya kwamba ‘nchi yangu ni sawa sikuzote.’”—Morals and Missiles (London, 1959), kilichohaririwa na Charles S. Thompson, uku. 57, 58.
Mt. 26:52, UV: “Ndipo Yesu akamwambia, Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga.”
1 Yoh. 3:10-12, BHN: “Asiyempenda ndugu yake, huyo si mtoto wa Mungu. Hiyo ndiyo tofauti iliyoko kati ya watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi. . . . Tunapaswa kupendana! Tusiwe kama Kaini ambaye, kwa kuongozwa na yule Mwovu, alimwua ndugu yake.”
Kutokana na yaliyotangulia, je, kwa kweli wale wanaodai kuwa warithi wa mitume wamefundisha na kutenda yale ambayo Kristo na mitume wake walitenda?