Kitabu Cha Biblia Namba 9—1 Samueli
Waandikaji: Samweli, Gadi, Nathani
Mahali Kilipoandikiwa: Israeli
Uandikaji Ulikamilishwa: c. (karibu) 1078 K.W.K.
Wakati Uliohusishwa: c. (karibu) 1180—1078 K.W.K.
1. Ni badiliko gani kubwa katika tengenezo la taifa la Israeli lilitokea katika 1117 K.W.K., na ni masharti gani yalifuata baada ya hapo?
KATIKA mwaka 1117 K.W.K., kulitokea badiliko kubwa katika tengenezo la kitaifa la Israeli. Mfalme wa kibinadamu aliwekwa! Hilo lilitukia wakati Samweli alipokuwa akitumikia akiwa nabii wa Yehova katika Israeli. Ingawa Yehova alikuwa ametangulia kujua hilo na kulitabiri, bado badiliko la kuwa na mfalme, kama walivyodai watu wa Israeli, lilikuwa pigo lililomduwaza Samweli. Akiwa mwenye kujitoa sana kwa utumishi wa Yehova tangu kuzaliwa, na akiwa amejawa na utambuzi wenye staha wa ufalme wa Yehova, Samweli alitangulia kuona matokeo yenye msiba kwa washiriki wenzake wa taifa takatifu la Mungu. Ni chini ya mwelekezo wa Yehova tu kwamba Samweli alikubali madai yao. “Kisha Samweli aliwaambia watu madaraka ya ufalme, akayaandika katika kitabu, akakiweka mbele za BWANA [Yehova, NW].” (1 Sam. 10:25) Hivyo ukafikia mwisho wa muhula wa waamuzi, na ukaanza muhula wa wafalme wa kibinadamu ambao wangeona Israeli ikiinuka kufikia kwenye mamlaka na umashuhuri usiotangulia kuonwa, kisha mwishowe waangukie aibu na kuondolewa kwenye kibali cha Yehova.
2. Ni nani waliandika Samweli wa Kwanza, na walikuwa na sifa zipi?
2 Ni nani angestahili kufanya maandishi ya kimungu ya kipindi hicho cha maana sana? Kwa kufaa, Yehova alichagua Samweli mwaminifu aanzishe uandikaji. Samweli humaanisha “Jina la Mungu,” na yeye kwa hakika alitokeza kuwa mtegemezaji wa jina la Yehova katika siku hizo. Yaonekana kwamba Samweli aliandika sura 24 za kwanza za kitabu hiki. Kisha, alipokufa, Gadi na Nathani waliendeleza uandikaji, wakikamilisha miaka michache ya mwisho ya maandishi hayo kufikia kifo cha Sauli. Hilo laonyeshwa na 1 Mambo ya Nyakati 29:29, panaposomwa hivi: “Basi habari za mfalme Daudi, mwanzo na mwisho, angalia, zimeandikwa katika tarehe ya Samweli, mwonaji, na katika tarehe ya Nathani, nabii, na katika tarehe ya Gadi, mwonaji.” Tofauti na Wafalme na Mambo ya Nyakati, vitabu vya Samweli kwa ujumla havirejezei kamwe maandishi ya mapema zaidi, na kwa hiyo Samweli, Gadi, na Nathani walioishi wakati mmoja na Daudi wanathibitishwa kuwa waandikaji. Wote watatu kati ya wanaume hao walikuwa na vyeo vya amana wakiwa manabii wa Yehova na walipinga ibada ya sanamu iliyokuwa imedhoofisha taifa hilo.
3. (a) Samweli wa Kwanza kilikujaje kuwa kitabu kilicho peke yake? (b) Kilikamilishwa lini, nacho kinahusisha kipindi gani?
3 Vitabu viwili vya Samweli hapo awali vilikuwa kunjo moja, au buku moja. Samweli kiligawanywa kuwa vitabu viwili wakati sehemu hii ya Septuagint ya Kigiriki ilipochapishwa. Katika Septuagint, Samweli wa Kwanza kiliitwa Wafalme wa Kwanza. Mgawanyo huo na jina Wafalme wa Kwanza ulifuatwa na Vulgate ya Kilatini na huendelea katika Biblia za Kikatoliki hadi wa leo. Kwamba Samweli wa Kwanza na wa Pili vilifanyiza kitabu kimoja hapo awali huonyeshwa na taarifa ya Kimasora kuhusu 1 Samweli 28:24, ambayo hueleza kwamba mstari huo umo katikati ya kitabu cha Samweli. Yaelekea kitabu hicho kilikamilishwa karibu 1078 K.W.K. Kwa hiyo Samweli wa Kwanza yaelekea chahusu kipindi cha miaka inayozidi kidogo mia moja, kuanzia 1180 hivi hadi 1078 K.W.K.
4. Usahihi wa maandishi katika Samweli wa Kwanza umeungwaje mkono?
4 Kuna ushuhuda mwingi juu ya usahihi wa maandishi hayo. Sehemu za kijiografia zafaana na matukio yanayosimuliwa. Kwa kupendeza, shambulio lililofanikiwa la Yonathani juu ya kambi ya kijeshi ya Kifilisti kule Mikmashi, ambalo liliongoza kwenye kukimbizwa kabisa kwa Wafilisti, lilirudiwa katika Vita ya Ulimwengu ya Kwanza na ofisa wa Jeshi la Uingereza, ambaye yaripotiwa alikimbiza Waturuki kwa kufuata alama za bara zinazosimuliwa katika maandishi ya Samweli yaliyopuliziwa na Mungu.—14:4-14a
5. Waandikaji wa Biblia washuhudiaje uhalisi wa Samweli wa Kwanza?
5 Hata hivyo, kuna vithibitisho vyenye nguvu zaidi vya upulizio wa Mungu na uasilia wa kitabu hiki. Kina utimizo wenye kutokeza wa unabii wa Yehova kwamba Israeli wangeomba mfalme. (Kum. 17:14; 1 Sam. 8:5) Miaka mingi baadaye, Hosea alithibitisha maandishi yacho, akinukuu Yehova kuwa akisema, “Nimekupa mfalme katika hasira yangu, nikamwondoa katika ghadhabu yangu.” (Hos. 13:11) Petro alitoa wazo kwamba Samweli alipuliziwa na Mungu alipotambulisha Samweli kuwa nabii ‘aliyekuwa amehubiri habari za siku’ za Yesu. (Mdo. 3:24) Paulo alinukuu 1 Samweli 13:14 katika kukazia kifupi historia ya Israeli. (Mdo. 13:20-22) Yesu mwenyewe alitia muhuri kwenye simulizi hilo kuwa asilia kwa kuwauliza Mafarisayo katika siku yake: “Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe?” Kisha akasimulia tukio la Daudi akiomba mkate wa wonyesho. (Mt. 12:1-4; 1 Sam. 21:1-6) Ezra pia alikubali simulizi hilo kuwa halisi, kama ilivyokwisha kutajwa.—1 Nya. 29:29.
6. Ni ushuhuda gani mwingine wa kindani wa Biblia unaoonyesha Samweli wa Kwanza kuwa asilia?
6 Hilo likiwa ndilo simulizi la awali la utendaji mbalimbali wa Daudi, kila mtajo wa Daudi katika Maandiko yote huthibitisha kitabu cha Samweli kuwa sehemu ya Neno la Mungu lililopuliziwa na Mungu. Baadhi ya matukio yacho yanarejezewa hata katika maandishi ya utangulizi ya zaburi za Daudi, kama vile kwenye Zaburi 59 (1 Sam. 19:11), Zaburi 34 (1 Sam. 21:13, 14), na Zaburi 142 (1 Sam. 22:1 au 1 Sam. 24:1, 3). Kwa hiyo, ushuhuda wa kindani wa Neno la Mungu mwenyewe hushuhudia bila shaka uasilia wa Samweli wa Kwanza.
YALIYOMO KATIKA SAMWELI WA KWANZA
7. Historia iliyomo katika kitabu hicho yahusu maisha ya viongozi gani katika Israeli?
7 Kitabu hiki chahusisha kwa sehemu au kwa ujumla muda wa maisha wa viongozi wanne wa Israeli: Eli kuhani mkuu, Samweli nabii, Sauli mfalme wa kwanza, na Daudi aliyepakwa mafuta kuwa mfalme atakayefuata.
8. Ni hali gani za kuzaliwa kwa Samweli na za kuwa kwake ‘mtumishi wa Yehova’?
8 Uhakimu wa Eli na Samweli mchanga (1:1–4:22). Simulizi linapofungua, tunajulishwa kwa Hana, mke aliyependelewa zaidi na Elkana, Mlawi. Yeye hana mtoto na adhihakiwa kwa sababu hiyo na mke yule mwingine wa Elkana, Penina. Familia hiyo ikiwa inafanya mojawapo wa ziara za kila mwaka kule Shilo, ambako sanduku la agano la Yehova lakaa, Hana asali kwa bidii kwa Yehova ampe mwana. Yeye aahidi kwamba sala yake ikijibiwa, atatoa mtoto huyo kwenye utumishi wa Yehova. Mungu ajibu sala yake, naye azaa mwana, Samweli. Mara tu aachapo kunyonya, Hana amleta kwenye nyumba ya Yehova na kumwachia uangalizi wa kuhani mkuu, Eli, kuwa ‘aliyepewa Yehova.’ (1:28) Kisha Hana aeleza hisia zake katika wimbo wa shangwe wa kushukuru na furaha. Mvulana huyo ‘atumikia Yehova mbele yake Eli, kuhani.’—2:11.
9. Samweli anakujaje kuwa nabii katika Israeli?
9 Yote si sawa kwa Eli. Yeye ni mzee, na wana wake wawili wamekuwa mabaradhuli (watu ovyo) ‘wasiomjali Yehova.’ (2:12) Watumia vyeo vyao vya kikuhani kutosheleza tamaa zao zisizo za adili. Eli akosa kuwasahihisha. Kwa hiyo Yehova achukua hatua ya kupeleka ujumbe mbalimbali wa kimungu juu ya nyumba ya Eli, akionya kwamba “nyumbani mwako hatakuwako mzee” na kwamba wana wote wawili wa Eli watakufa katika siku moja. (1 Sam. 2:30-34; 1 Fal. 2:27) Hatimaye, Yeye amtuma mvulana Samweli kwa Eli akiwa na ujumbe wa hukumu wenye kuwasha masikio. Kwa njia hiyo Samweli mchanga ahesabiwa kuwa nabii katika Israeli.—1 Sam. 3:1, 11.
10. Yehova anatekelezaje hukumu juu ya nyumba ya Eli?
10 Punde si punde Yehova atekeleza hukumu yake kwa kuwaleta Wafilisti. Nguvu za pigano zigeukiapo Israeli, Waisraeli, wakipiga kelele kubwa, waleta sanduku la agano kutoka Shilo hadi kwenye kambi yao ya kijeshi. Kwa kusikia kelele na kujua kwamba Sanduku limeletwa ndani ya kambi ya Israeli, Wafilisti wajiimarisha na kupata ushindi wenye kushtua, wakiwakimbiza kabisa Waisraeli. Sanduku latekwa, na wana wawili wa Eli wafa. Moyo wake ukiwa watetemeka, Eli asikia ripoti hiyo. Sanduku litajwapo, aanguka kinyume-nyume kutoka kwenye kiti chake na kufa kwa kuvunjika shingo. Ndivyo uhakimu wake wa miaka 40 unavyokwisha. Kweli kweli, “utukufu umeondoka katika Israeli,” kwa maana Sanduku lawakilisha kuwapo kwa Yehova pamoja na watu wake.—4:22.
11. Ni jinsi gani Sanduku lathibitika kuwa si hirizi ya bahati njema?
11 Samweli ahukumu Israeli (5:1–7:17). Sasa Wafilisti nao wapaswa kujifunza kwa majonzi makubwa kwamba sanduku la Yehova halipasi kutumiwa kuwa hirizi ya bahati njema. Wachukuapo Sanduku ndani ya hekalu la Dagoni kule Ashdodi, mungu wao aanguka kifudifudi. Siku ya pili Dagoni aanguka chini kwenye mwingilio, safari hii kichwa chake na viganja vyote viwili vya mkono vyakatika. Hilo laanzisha zoea la kiushirikina la Kifilisti la ‘kutokanyaga kizingiti cha nyumba ya Dagoni.’ (5:5) Wafilisti waharakisha kupeleka Sanduku huko Gathi kisha hadi Ekroni lakini wapi! Mateso yaja kwa namna ya hofu kuu, majipu, na tauni ya panya. Mabwana-mhimili wa Kifilisti, katika jaribio la mwisho huku hesabu ya vifo ikipanda, warudisha Sanduku kule Israeli likiwa juu ya mkokoteni mpya wenye kuvutwa na ng’ombe wawili waliokuwa wakinyonyesha. Kule Beth-shemeshi msiba wapata baadhi ya Waisraeli kwa sababu ya kulitazama Sanduku. (1 Sam. 6:19; Hes. 4:6, 20) Hatimaye, Sanduku laja kupumzika katika nyumba ya Abinadabu katika jiji la Kilawi la Kiariath-yearimu.
12. Ni baraka gani zinazoletwa na uteteaji wa Samweli wa ibada inayofaa?
12 Kwa miaka 20 Sanduku labaki katika nyumba ya Abinadabu. Samweli, akiwa amekua kufikia mwanamume mzima, asihi Israeli waondoshe Mabaali na mifano ya Ashtorethi na kutumikia Yehova kwa moyo wao wote. Wafanya hivyo. Wakusanyikapo Mispa ili kuabudu, mabwana-mhimili wa Wafilisti wanyakua nafasi hiyo kupigana na kuwafikia ghafula Israeli. Israeli wamwitia Yehova kupitia Samweli. Sauti kubwa ya ngurumo kutoka kwa Yehova yavuruga Wafilisti, nao Waisraeli, wakiwa wametiwa nguvu kwa dhabihu na sala, wapata ushindi mkubwa. Kuanzia wakati huo na kuendelea ‘mkono wa Yehova waendelea kuwa juu ya Wafilisti siku zote za Samweli.’ (7:13) Hata hivyo, Samweli hastaafu. Maisha yake yote aendelea kuhukumu Israeli, akifanya mzunguko wa kila mwaka kuanzia Rama, kaskazini tu mwa Yerusalemu, hadi Betheli, Gilgali, na Mispa. Katika Rama ajengea Yehova madhabahu.
13. Israeli wanakujaje kukataa Yehova kuwa Mfalme, na Samweli aonya juu ya matokeo gani?
13 Mfalme wa kwanza wa Israeli, Sauli (8:1–12:25). Samweli amezeeka katika utumishi wa Yehova, lakini wana wake hawatembei katika njia za baba yao, kwa maana wakubali hongo na kupotosha hukumu. Katika wakati huu wanaume wazee wa Israeli wamfikia Samweli wakiwa na dai hili: “Tufanyie mfalme atuamue, mfano wa mataifa yote.” (8:5) Kwa kuhangaika sana, Samweli amtafuta Yehova katika sala. Yehova ajibu: “Hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi. . . . Basi, sasa, isikilize sauti yao.” (8:7-9) Hata hivyo, kwanza lazima Samweli awaonye juu ya matokeo mabaya ya ombi lao la uasi: kuandikishwa jeshini, kutozwa ushuru, kupoteza uhuru, na hatimaye majonzi machungu na kulilia Yehova. Kwa tamaa isiyozuilika, watu wadai wapewe mfalme.
14. Sauli anakujaje kuimarishwa katika ufalme?
14 Sasa twakutana na Sauli, mwana wa Kishi wa kabila la Benyamini na ndiye mwanamume mwenye sura nzuri zaidi na mrefu zaidi katika Israeli. Yeye aelekezwa kwa Samweli, ambaye amheshimu kwenye karamu, kumpaka mafuta, na kisha kumjulisha kwa Israeli wote kwenye kusanyiko kule Mispa. Ingawa hapo kwanza Sauli ajificha miongoni mwa mizigo, mwishowe atokezwa kuwa uchaguzi wa Yehova. Kwa mara nyingine Samweli akumbusha Israeli deni lililo haki ya ufalme, akiandika hilo katika kitabu. Hata hivyo, cheo cha Sauli akiwa mfalme chaimarishwa baada tu ya ushindi wake juu ya Waamoni, unaoondoa mazingiwa kule Yabeshi katika Gileadi, kwa hiyo watu wathibitisha ufalme wake kule Gilgali. Kwa mara nyingine Samweli awasihi wahofu, watumikie, na kutii Yehova, naye aita Yehova apeleke ishara kwa namna ya ngurumo na mvua isiyo ya majira wakati wa mavuno. Kwa wonyesho wenye kuogofya, Yehova aonyesha kasirani yake kwa kumkataa yeye kuwa Mfalme.
15. Ni dhambi gani ya kujitanguliza inayoongoza kwenye kushindwa kwa Sauli?
15 Kukosa kutii kwa Sauli (13:1–15:35). Wafilisti wanapoendelea kusumbua-sumbua Israeli, Yonathani, mwana wa Sauli mwenye moyo mkuu apiga dharuba kambi ya Kifilisti. Ili kulipa kisasi hicho, adui wapeleka jeshi kubwa ‘kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari’ katika hesabu, nao wapiga kambi kule Mikmashi. Mfadhaiko wakumba Waisraeli, ‘Laiti Samweli angekuja kutupa mwelekezo wa Yehova!’ Akikosa subira ya kungojea Samweli, Sauli afanya dhambi kwa kujitanguliza kutoa dhabihu ya kuteketezwa yeye mwenyewe. Ghafula Samweli atokea. Akikataa udhuru wa Sauli usio na msingi, atangaza hukumu ya Yehova: “Lakini sasa ufalme wako hautadumu; BWANA [Yehova, NW] amejitafutia aupendezaye moyo wake, naye BWANA [Yehova, NW] amemwamuru yeye kuwa mkuu juu ya watu wake, kwa sababu wewe hukulishika neno lile BWANA [Yehova, NW] alilokuamuru.”—13:14.
16. Haraka-haraka ya Sauli yatokeza magumu gani?
16 Yonathani, mwenye bidii kwa ajili ya jina la Yehova, kwa mara nyingine ashambulia ngome ya Kifilisti, safari hii akiwa na mchukua deraya yake tu, na upesi wapiga dharuba wanaume karibu 20. Tetemeko la ardhi lazidisha mvurugiko wa adui. Wakimbizwa, Israeli wakiwafuatia mbiombio. Hata hivyo, nguvu kamili za ushindi huo zadhoofishwa na kiapo cha haraka-haraka cha Sauli cha kukataza mashujaa wasile kabla ya pigano kwisha. Wanaume wachoka haraka na kisha wamtenda Yehova dhambi kwa kula nyama ambayo imetoka tu kuuawa bila kuchukua wakati kuondoa damu kabisa. Kwa upande wake Yonathani, amejiburudisha kwa sega la asali kabla ya kusikia kiapo hicho, ambacho kwa ujasiri anakilaani vikali kuwa kipingamizi. Yeye aokolewa na kifo na watu kwa sababu ya wokovu mkubwa aliofanya katika Israeli.
17. Ni kukataliwa gani kwingine kwa Sauli kunakofuata dhambi yake nzito ya pili?
17 Sasa wawadia wakati wa kutimiza hukumu ya Yehova juu ya Waamaleki wa kudharaulika. (Kum. 25:17-19) Lazima wafagiliwe mbali kabisa. Kitu chochote kisiachwe, binadamu wala mnyama. Hakuna nyara za kutekwa. Lazima kila kitu kitolewe kwa uharibifu. Hata hivyo, Sauli kwa kukosa kutii amhifadhi Agagi, mfalme Mwamaleki, na makundi bora zaidi ya mifugo, kwa kisingizio cha kuzitoa dhabihu kwa Yehova. Hilo lamkasirisha sana Mungu wa Israeli kwamba ampulizia Samweli aeleze kukataliwa kwa Sauli mara ya pili. Akipuuza visababu vya Sauli vya kutetea heshima yake, Samweli ajulisha rasmi hivi: “Je! BWANA [Yehova, NW] huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu sawasawa na kutii sauti ya BWANA [Yehova, NW]? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu . . . Kwa kuwa umelikataa neno la BWANA [Yehova, NW], Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.” (1 Sam. 15:22, 23) Kisha Sauli anashika koti la Samweli ili kumsihi, lakini linararuka. Samweli amhakikishia kwamba Yehova atararua vivyo hivyo ufalme kutoka kwa Sauli na kumpa mwanamume bora. Samweli atwaa upanga, na kumwua Agagi, ampa Sauli kisogo, asimwone tena kamwe.
18. Yehova achagua Daudi kwa msingi gani?
18 Kupakwa mafuta kwa Daudi, uhodari wake (16:1–17:58). Kisha Yehova amwelekeza Samweli kwenye nyumba ya Yese katika Bethlehemu ya Yuda akachague na kupaka mafuta mfalme wa wakati ujao. Mmoja baada ya mwingine wa wana wa Yese wapita waangaliwe lakini wakataliwa. Yehova amkumbusha Samweli hivi: “BWANA [Yehova, NW] haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA [Yehova, NW] huutazama moyo.” (16:7) Hatimaye, Yehova aonyesha kibali chake juu ya Daudi, aliye mchanga zaidi, anayeelezwa kuwa “mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza,” na Samweli ampaka mafuta. (16:12) Sasa roho ya Yehova yaja juu ya Daudi, lakini Sauli asitawisha roho mbaya.
19. Ni ushindi gani wa mapema anaopata Daudi katika jina la Yehova?
19 Kwa mara nyingine Wafilisti washambulia Israeli, wakitokeza bingwa wao, Goliathi, jitu lenye kimo cha mikono sita na shibiri moja (meta 2.9) Yeye ni jitu hata kwamba dirii yake ina uzito wa karibu kilo 57 na kichwa cha mkuki wake karibu kilo 6.8. (17:4, 5, 7) Siku baada ya siku Goliathi huyo kwa kukufuru na kwa dharau aambia Israeli wathubutu kuchagua mwanamume ajitokeze kupigana, lakini hakuna anayejibu. Sauli atetemeka katika hema lake. Hata hivyo, Daudi apata kusikia juu ya dhihaka za Mfilisti huyo. Kwa ghadhabu ya uadilifu na kwa kutiwa nguvu na moyo mkuu, Daudi atangaza hivi: “Mfilisti huyu asiyetahiriwa ni nani hata awatukane majeshi ya Mungu aliye hai?” (17:26) Akikataa deraya ya Sauli kwa maana hakuwa amepata kuijaribu hapo mbele, Daudi aenda kwenye pigano, vifaa vyake pekee vikiwa ni fimbo ya mchungaji, kombeo, na mawe laini matano. Akiona pambano pamoja na huyu mvulana mchungaji mchanga kuwa ni kumvunjia heshima, Goliathi aita uovu juu ya Daudi. Jibu hili la uhakika latolewa: “Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA [Yehova, NW] wa majeshi.” (17:45) Jiwe moja lililolengwa shabaha vizuri latupwa kutoka kwenye kombeo la Daudi, na bingwa wa Wafilisti aanguka chini! Akimkimbilia, mbele ya majeshi yote mawili, Daudi afuta upanga wa jitu hilo na kuutumia kukata kichwa cha mwenye upanga huo. Ni ukombozi mkubwa kama nini kutoka kwa Yehova! Shangwe iliyoje katika kambi ya Israeli! Sasa kwa kuwa bingwa wao amekufa, Wafilisti wakimbia, wakifuatiwa mbiombio na Waisraeli wenye shangwe ya ushindi.
20. Mtazamo wa Yonathani kuelekea Daudi watofautianaje na ule wa Sauli?
20 Sauli amwinda Daudi (18:1–27:12). Tendo la Daudi la kutokuwa na hofu kwa ajili ya jina la Yehova lamfungulia urafiki mzuri sana. Huo ni pamoja na Yonathani, ambaye ni mwana wa Sauli na ndiye kiasili anayefuata kupokea ufalme. Yonathani “akampenda kama roho [nafsi, NW] yake mwenyewe,” hata kwamba wote wawili wafanya agano la urafiki. (18:1-3) Umashuhuri wa Daudi unapokuja kusifiwa katika Israeli, kwa kasirani Sauli atafuta kumwua, hata ajapompa bintiye Mikali katika ndoa. Uadui wa Sauli wawa wenye kichaa zaidi na zaidi, hata kwamba mwishowe Daudi alazimika kutoroka kwa msaada wenye upendo wa Yonathani. Wote wawili watoa machozi wakati wa kuagana, na Yonathani athibitisha tena uaminifu wake wa ushikamanifu kwa Daudi, akisema: “BWANA [Yehova, NW] atakuwa kati ya mimi na wewe, na kati ya uzao wangu na uzao wako milele.”—20:42.
21. Ni matukio gani yanayotia alama kutoroka kwa Daudi kutoka kwa Sauli?
21 Akiwa anamtoroka Sauli mwenye uchungu, Daudi na kikundi chake kidogo chenye njaa kali wafika Nobu. Hapa kuhani Ahimeleki, akiisha kuhakikishiwa kwamba Daudi na wanaume wake hawajajinajisi na wanawake, awaruhusu wale mkate mtakatifu wa wonyesho. Sasa akiwa na upanga wa Goliathi, Daudi atorokea Gathi katika eneo la Kifilisti, ambako asingizia kichaa. Kisha asonga mbele kwenye pango la Adulamu, kisha Moabu, na baadaye, kwa kushauriwa na Gadi aliye nabii, arudi kwenye bara la Yuda. Akihofu maasi ya kupendelea Daudi, Sauli mwenye wivu wenye kichaa amwamuru Doegi Mwedomi achinje idadi ya kikuhani ya Nobu, Abiathari pekee akiponyoka akajiunge na Daudi. Awa kuhani kwa kikundi hicho.
22. Daudi aonyeshaje uaminifu-mshikamanifu kwa Yehova na staha kwa ajili ya tengenezo Lake?
22 Akiwa mtumishi wa Yehova mwenye uaminifu-mshikamanifu, kwa kufanikiwa sasa Daudi apigana na Wafilisti kwa kuvizia. Hata hivyo, Sauli aendelea na kampeni yake ya kufa-na-kupona ya kumnasa Daudi, akikusanya wanaume wake wa vita na kumwinda “katika nyika ya Engedi.” (24:1) Daudi, mpendwa wa Yehova, sikuzote afaulu kuwa hatua moja mbele ya wenye kumwinda. Katika pindi moja apata nafasi ya kupiga Sauli dharuba, lakini ajiepusha, akikata tu rinda la joho la Sauli kuwa ushuhuda wa kwamba ameponya uhai wake. Hata kitendo hiki kisicho na dhara chachoma Daudi moyoni. Ni staha nzuri kama nini aliyo nayo kwa ajili ya tengenezo la Yehova!
23. Abigaili afanyaje amani pamoja na Daudi na mwishowe kuwa mke wake?
23 Ingawa sasa kifo cha Samweli chaandikwa (25:1), mwandikaji-mwandamizi wake aendeleza simulizi hilo. Daudi auliza kwamba Nabali, wa Maoni katika Yuda, aandae chakula kwa ajili yake na wanaume wake kama malipo ya kufanya urafiki na wachungaji wa Nabali. Nabali ‘awatukana’ tu wanaume wa Daudi, na Daudi aondoka akamwadhibu. (25:14) Akitambua hatari hiyo, mke wa Nabali, Abigaili, apeleka kisiri-siri vyakula kwa Daudi na kumtuliza. Daudi ambariki kwa ajili ya kitendo hicho cha busara na kumrejeza kwa amani. Abigaili ajulishapo Nabali yaliyotukia, moyo wake wapigwa, na siku kumi baadaye afa. Daudi mwenyewe sasa amwoa Abigaili mwenye neema na aliye mzuri wa sura.
24. Daudi anaponyaje tena uhai wa Sauli?
24 Kwa mara ya tatu, Sauli amwinda kwa kichaa Daudi, na kwa mara nyingine apokea rehema ya Daudi. “Usingizi mzito kutoka kwa BWANA [Yehova]” waangukia Sauli na wanaume wake. Hilo lawezesha Daudi aingie ndani ya kambi na kuchukua mkuki wa Sauli, lakini ajiepusha kunyoosha mkono wake ‘juu ya masihi wa Yehova.’ (26:11, 12) Daudi alazimishwa mara ya pili kukimbia kwa Wafilisti apate maficho, nao wampa Sikilagi kuwa mahali pa makao. Kutoka hapo aendelea na mavizio yake juu ya maadui wengine wa Israeli.
25. Ni dhambi gani nzito ya tatu anayofanya Sauli?
25 Mwisho wa Sauli kwa kujiua (28:1–31:13). Mabwana-mhimili wa Wafilisti wapeleka jeshi lililounganishwa kule Shunemu. Sauli, kwa upande wake, atwaa kikao chake kwenye Mlima Gilboa. Kwa mfadhaiko atafuta uongozi lakini hapati jibu lolote kutoka kwa Yehova. Kama tu ingewezekana kuwasiliana na Samweli! Akificha utambuzi wake, Sauli afanya dhambi nyingine nzito aendapo kutafuta mwasiliani-roho kule Endori, nyuma ya jeshi la Kifilisti. Ampatapo, amwomba-omba awasiliane na Samweli kwa ajili yake. Akifanya haraka sana kukata maneno, Sauli awazia kwamba mzuka huo ni Samweli mfu. Hata hivyo, “Samweli” hana ujumbe wa kufariji mfalme. Kesho atakufa, na kwa kutimiza maneno ya Yehova, ufalme utatwaliwa kutoka kwake. Katika kambi ile nyingine, mabwana-mhimili wa Wafilisti wanasonga kwenye pigano. Kwa kuona Daudi na wanaume wake miongoni mwao, wakiwatilia shaka wawarudisha nyumbani. Wanaume wa Daudi warejea Sikilagi kwa wakati unaofaa! Kikosi chenye kushambulia cha Waamaleki kimeondoka na familia na mali za Daudi na wanaume wake, lakini Daudi na wanaume wake wawakimbiza, na vyote vyapatikana tena bila dhara lolote.
26. Utawala wenye maafa wa mfalme wa kwanza wa Israeli wamalizikaje?
26 Pigano limechacha sasa kwenye Mlima Gilboa. Israeli washindwa kwa njia yenye maafa, na Wafilisti wamiliki maeneo muhimu kijeshi ya bara hilo. Yonathani na wana wengine wa Sauli wauawa, na Sauli aliyejeruhiwa mahututi ajiua mwenyewe kwa upanga wake. Wafilisti walioshinda waning’iniza maiti ya Sauli na za wana wake watatu juu ya kuta za jiji la Beth-shani, lakini zaondolewa na wanaume wa Yabesh-gileadi kutoka kwa hali hiyo ya kuvunjia heshima. Utawala wenye msiba wa mfalme wa kwanza wa Israeli umefikia mwisho wenye maafa.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
27. (a) Eli na Sauli walikosea wapi? (b) Ni katika mambo gani Samweli na Daudi ni vielelezo vizuri kwa waangalizi na kwa ajili ya wahudumu wachanga?
27 Ni historia kweli kweli iliyomo katika Samweli wa Kwanza! Kikiwa na unyofu ulio wazi katika kila jambo, chafunua mara moja udhaifu na nguvu za Israeli. Hao walikuwa viongozi wanne katika Israeli, wawili waliotii sheria ya Mungu na wawili ambao hawakutii. Angalia jinsi Eli na Sauli walivyoshindwa: Yule wa kwanza alipuuza kuchukua hatua, na huyu wa pili alitenda kwa kujitanguliza. Kwa upande ule mwingine, Samweli na Daudi walionyesha upendo kwa ajili ya njia ya Yehova tangu ujanani na kuendelea, nao walifanikiwa kwa sababu hiyo. Ni masomo yenye thamani kama nini tunayopata hapa kwa waangalizi wote! Jinsi ilivyo lazima kwa hawa kuwa imara, wenye kulinda usafi na utaratibu katika tengenezo la Yehova, wakiheshimu mipango yake, wakiwa bila hofu, wenye kuzuia kasirani, wenye moyo mkuu, wenye kufikiria kwa upendo wengine! (2:23-25; 24:5, 7; 18:5, 14-16) Angalia pia kwamba wale wawili waliofanikiwa walikuwa na faida ya mazoezi mazuri ya kitheokrasi tangu ujana wao kuendelea na kwamba walikuwa na moyo mkuu tangu umri wa mapema katika kunena ujumbe wa Yehova na kutunza faida walizokabidhiwa. (3:19; 17:33-37) Waabudu wote wachanga wa Yehova leo na wawe “Samweli” na “Daudi” wachanga!
28. Utii wakaziwaje, na ni shauri gani la Samweli wa Kwanza linalorudiwa baadaye na waandikaji wengine wa Biblia?
28 Ya kukumbukwa waziwazi kati ya maneno yote yenye mafaa ya kitabu hiki ni yale ambayo Yehova alipulizia Samweli atamke katika hukumu yake juu ya Sauli kwa ajili ya kushindwa ‘kufuta ukumbuko wa Amaleki chini ya mbingu.’ (Kum. 25:19) Somo la kwamba ‘kutii ni bora kuliko dhabihu’ larudiwa katika vikao mbalimbali kwenye Hosea 6:6, Mika 6:6-8, na Marko 12:33. (1 Sam. 15:22) Ni muhimu kwamba sisi leo tunufaike na maandishi hayo yaliyopuliziwa na Mungu na kutii kabisa na kikamili sauti ya Yehova Mungu wetu! Utii katika kutambua utakatifu wa damu wavutwa kwenye uangalifu wetu kwenye 1 Samweli 14:32, 33. Kula nyama bila kuondoa damu vizuri kulionwa kuwa ‘kukosa juu ya Yehova.’ Hilo pia latumika kwa kundi la Kikristo, kama inavyoonyeshwa wazi kwenye Matendo 15:28, 29.
29. Samweli wa Kwanza hutoa kiolezo cha matokeo gani ya kosa la kitaifa kwa upande wa Israeli, kukiwa na onyo gani kwa watu washupavu?
29 Kitabu cha Samweli wa Kwanza chatoa kielezi cha kosa lenye kusikitisha la taifa ambalo lilikuja kuona utawala wa Mungu kutoka mbinguni kuwa usio na mafaa yenye kutumika. (1 Sam. 8:5, 19, 20; 10:18, 19) Mitego na ubatili wa utawala wa kibinadamu vyaonyeshwa kihalisi na kiunabii. (8:11-18; 12:1-17) Sauli aonyeshwa mwanzoni kuwa mwanamume mwenye kiasi aliyekuwa na roho ya Mungu (9:21; 11:6), lakini uhakimu wake uliingia giza na moyo wake ukawa mchungu wakati upendo wa uadilifu na imani katika Mungu vilipofifia. (14:24, 29, 44) Maandishi yake ya mapema ya bidii yalibatilishwa na vitendo vyake vya baadaye vya kujitanguliza, kukosa utii, na kukosa uaminifu kwa Mungu. (1 Sam. 13:9; 15:9; 28:7; Eze. 18:24) Ukosefu wake wa imani ulizaa kukosa usalama, uliozorota ukawa husuda, chuki, na uuaji. (1 Sam. 18:9, 11; 20:33; 22:18, 19) Alikufa kama alivyoongoza maisha yake, alimkosea Mungu wake na watu wake, na kuwa onyo kwa wowote ambao huenda wakawa “wenye ushupavu” kama yeye.—2 Pet. 2:10-12.
30. Ni sifa gani za Samweli zinazoweza kusitawishwa kwa faida na wahudumu wa kisasa?
30 Hata hivyo, kuna wema unaotofautisha. Kwa kielelezo, angalia mwendo wa uaminifu wa Samweli, aliyetumikia Israeli maisha yake yote bila udanganyifu, kuegemea upande mmoja, au upendeleo. (1 Sam. 12:3-5) Yeye alikuwa na tamaa ya kutii tangu uvulana wake na kuendelea (3:5), mpole na mwenye staha (3:6-8), mwenye kutegemeka katika kutimiza wajibu wake (3:15), asiye na kigeu-geu katika wakfu na ujitoaji wake (7:3-6; 12:2), mwenye nia ya kusikiliza (8:21), tayari kutegemeza maamuzi ya Yehova (10:24), imara katika uhakimu wake bila kujali mtu ni nani (13:13), mwenye nguvu kwa ajili ya utii (15:22), na mdumifu katika kutimiza utume (16:6, 11). Pia yeye alikuwa mtu mwenye kuripotiwa vizuri na wengine. (2:26; 9:6) Si kwamba tu huduma yake ya uchanga yapasa kutia moyo wachanga wachukue huduma leo (2:11, 18) bali pia uendelevu wake bila kustaafu hadi mwisho wa siku zake wapasa kutegemeza wale waliodhoofishwa na uzee.—7:15.
31. Yonathani alikuwa kielelezo chema katika jambo gani?
31 Kisha kuna kielelezo kizuri sana cha Yonathani. Yeye hakuwa na mfundo (chuki) kwa sababu ya uhakika wa kwamba Daudi alipakwa mafuta apate ufalme ambao yeye angalirithi. Badala yake, yeye alitambua sifa njema za Daudi na kufanya agano la urafiki pamoja naye. Uenzi kama huo usio na ubinafsi waweza kuwa wenye kujenga sana na wenye kutia moyo miongoni mwa wale wanaotumikia Yehova leo kwa uaminifu.—23:16-18.
32. Ni tabia gani nzuri za kuangaliwa katika wanawake Hana na Abigaili?
32 Kwa ajili ya wanawake kuna kielelezo cha Hana, aliyeandamana na mume wake kwa ukawaida kwenye mahali pa ibada ya Yehova. Yeye alikuwa mwanamke wa sala, mnyenyekevu, aliacha uenzi wa mwana wake ili atimize ahadi yake na kuonyesha uthamini kwa ajili ya fadhili za Yehova. Hakika thawabu yake ilikuwa nzuri sana kwa kuona mwana wake akianza utumishi wa Yehova wenye mazao wa maisha yote. (1:11, 21-23, 27, 28) Zaidi ya hayo, kuna kielelezo cha Abigaili, aliyeonyesha utiisho wa kimwanamke na akili hata kupata sifa ya Daudi, hivi kwamba baadaye akawa mke wake.—25:32-35.
33. Upendo wa Daudi usio na hofu na uaminifu-mshikamanifu vyapasa kutusukuma sisi kwenye mwendo gani?
33 Upendo wa Daudi kwa ajili ya Yehova unaelezwa kwa njia yenye kuchochea katika zaburi ambazo Daudi alitunga alipokuwa akiwindwa nyikani na Sauli, ‘masihi wa Yehova’ aliyepotoka. (1 Sam. 24:6; Zab. 34:7, 8; 52:8; 57:1, 7, 9) Na lo! jinsi Daudi alivyotakasa jina la Yehova kwa uthamini wa moyoni alipokaidi mdhihaki Goliathi! “Mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA [Yehova, NW] wa majeshi . . . Siku hii ya leo BWANA [Yehova, NW] atakutia mkononi mwangu, . . . Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba BWANA [Yehova, NW] haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya BWANA [Yehova, NW], naye atawatia ninyi mikononi mwetu.” (1 Sam. 17:45-47) Daudi, “masihi” wa Yehova mwenye moyo mkuu na mwenye uaminifu-mshikamanifu, aliadhimisha Yehova kuwa Mungu wa dunia yote na Chanzo pekee cha kweli cha wokovu. (2 Sam. 22:51) Daima sisi na tufuate kielelezo cha kutokuwa na hofu!
34. Makusudi ya Ufalme ya Yehova yanakunjukaje zaidi kuhusiana na Daudi?
34 Samweli wa Kwanza kina nini la kusema juu ya ukuzi wa makusudi ya Ufalme wa Mungu? Hilo latuleta kwenye jambo kuu halisi la kitabu hiki cha Biblia! Maana hapa ndipo twakutana na Daudi, ambaye yawezekana jina lake humaanisha “Mpendwa.” Daudi alipendwa na Yehova na alichaguliwa kuwa “mtu aupendezaye moyo wake,” aliyefaa kuwa mfalme katika Israeli. (1 Sam. 13:14) Kwa hiyo ufalme ulipitishwa kwenye kabila la Yuda, kwa kupatana na baraka ya Yakobo kwenye Mwanzo 49:9, 10, na ufalme ungebaki katika kabila la Yuda mpaka aje Mtawala ambaye utii wa watu ni wake.
35. Jina la Daudi lilikujaje kushirikishwa na lile la Mbegu ya Ufalme, na ni sifa gani za Daudi ambazo bado Mbegu huyo ataonyesha?
35 Zaidi ya hayo, jina la Daudi lashirikishwa na lile la Mbegu ya Ufalme, ambaye pia alizaliwa katika Bethlehemu na alikuwa wa nasaba ya Daudi. (Mt. 1:1, 6; 2:1; 21:9, 15) Huyo ni Yesu Kristo aliyetukuzwa, “Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi,” na “Shina na Mzao wa Daudi; ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi.” (Ufu. 5:5; 22:16) Akitawala katika mamlaka ya Ufalme, huyu “mwana wa Daudi” ataonyesha uthabiti na moyo mkuu wote wa babu yake mwenye kutokeza katika kupigana na maadui wa Mungu awashinde na kutakasa jina la Yehova katika dunia yote. Jinsi uhakika wetu unavyopasa kuwa wenye nguvu katika hii Mbegu ya Ufalme!
[Maelezo ya Chini]
a The Romance of the Last Crusade, 1923, Major Vivian Gilbert, kurasa 183-6.