Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • gt sura 14
  • Wanafunzi wa Kwanza wa Yesu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wanafunzi wa Kwanza wa Yesu
  • Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
  • Habari Zinazolingana
  • Wanafunzi wa Kwanza wa Yesu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1985
  • Yesu Aanza Kufanya Wanafunzi
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
  • Wale Walioitwa Wawe Wanafunzi wa Yesu
    Jifunze Kutoka kwa Mwalimu Mkuu
  • Yohana Anambatiza Yesu
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
Pata Habari Zaidi
Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
gt sura 14

Sura 14

Wanafunzi wa Kwanza wa Yesu

BAADA ya kukaa siku 40 jangwani, Yesu amrudia Yohana aliyembatiza. Anapokaribia, kwa wazi Yohana akielekeza kwa Yesu apaaza sauti hivi: “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu.” Ijapokuwa Yohana ana umri mkubwa kidogo kuliko binamu yake Yesu, Yohana ajua kwamba Yesu alikuwako kabla ya yeye akiwa mtu wa kiroho mbinguni.

Hata hivyo, majuma machache mapema kidogo, wakati Yesu alipokuja abatizwe, kwa wazi Yohana hakujua hakika kwamba Yesu angekuwa ndiye Mesiya. “Wala mimi sikumjua,” akiri Yohana, “lakini kusudi adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nilikuja nikibatiza kwa maji.”

Yohana aendelea kuwaeleza wasikilizaji wake jambo lililotukia wakati alipobatiza Yesu: ‘Nimeiona roho ikishuka kama hua kutoka mbinguni; nayo ikakaa juu yake. Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye ambaye utaona roho ikishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa roho takatifu. Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu.’

Kesho yake Yohana amesimama pamoja na wawili wa wanafunzi wake. Tena, Yesu anapokaribia, yeye asema: “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu!” Kusikia hivyo, wanafunzi hao wawili wa Yohana Mbatizaji wamfuata Yesu. Mmoja wao ni Andrea, na kwa wazi yule mwingine ni mtu yule yule aliyeandika mambo haya, ambaye pia aitwa Yohana. Yohana huyu, kulingana na vionyeshi, ni binamu ya Yesu pia, yaonekana kuwa ni mwana wa Salome, dada ya Mariamu.

Akigeuka na kuona Andrea na Yohana wakimfuata, Yesu auliza: “Mnatafuta nini?”

“Rabi,” wauliza, “unakaa wapi?”

“Njoni, nanyi mtaona,” ajibu Yesu.

Ni karibu saa kumi za alasiri, nao Andrea na Yohana wakaa na Yesu muda uliobaki wa siku hiyo. Baadaye Andrea asisimka sana hivi kwamba afanya haraka kumtafuta ndugu yake, ambaye aitwa Petro. “Tumemwona Masihi,” amwambia. Halafu ampeleka Petro kwa Yesu. Labda Yohana naye amtafuta Yakobo ndugu yake wakati ule ule na kumleta kwa Yesu; hata hivyo, kulingana na tabia yake, Yohana hatii habari hizo za kibinafsi katika Evanjeli yake.

Kesho yake, Yesu amwona Filipo, ambaye atoka Bethsaida, jiji ambako Andrea na Petro walitoka hapo kwanza. Amwalika: “Nifuate.”

Kisha Filipo akamwona Nathanaeli, ambaye aitwa pia Bartholomayo, na kusema: “Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti.” Nathanaeli anatia shaka. “Laweza neno jema kutoka Nazareti?” auliza.

“Njoo uone,” Filipo amhimiza. Wanapokuwa wakimjia Yesu, Yesu asema kuhusu Nathanaeli: “Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake.”

“Umepataje kunitambua?” Nathanaeli auliza.

“Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona,” Yesu ajibu.

Nathanaeli astaajabu. “Rabi [maana yake, Mwalimu], wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli,” akasema.

“Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini?” Yesu auliza. “Utaona mambo makubwa kuliko haya.” Kisha aahidi: “Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”

Upesi baada ya hapo, Yesu, pamoja na wanafunzi wake ambao amejipatia sasa hivi, waondoka Bonde la Yordani na kusafiri kwenda Galilaya. Yohana 1:29-51.

▪ Ni nani walio wanafunzi wa kwanza wa Yesu?

▪ Petro, na labda pamoja na Yakobo wajulishwaje kwa Yesu?

▪ Ni nini chasadikisha Nathanaeli kwamba Yesu ndiye Mwana wa Mungu?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki