Sura 57
Huruma kwa Wanaosumbuka
BAADA ya kushutumu vikali Mafarisayo kwa ajili ya mapokeo yao ya kujitumikia wenyewe, Yesu anaondoka akiwa na wanafunzi wake. Huenda ukakumbuka kwamba, muda mfupi kabla ya hapo, jaribio lake la kuondoka akiwa pamoja nao ili wakapumzike kidogo lilivurugwa wakati umati ulipowapata. Sasa, akiwa na wanafunzi wake, yeye anaondoka na kuelekea majimbo ya Tiro na Sidoni, kilometa nyingi upande wa kaskazini. Yaonekana hii ndiyo safari pekee anayofunga Yesu akiwa pamoja na wanafunzi wake kuvuka mipaka ya Israeli.
Baada ya kupata nyumba ambamo wangekaa, Yesu anawajulisha kwamba hataki yeyote ajue walipo. Na bado, hata katika eneo hili lisilo la Waisraeli, yeye hawezi kuepuka kutambuliwa. Mwanamke mmoja Mgiriki ambaye alizaliwa hapa Foinike katika Siria, anampata na kuanza kumsihi: “Uwe na rehema kwangu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa vibaya sana na roho waovu.” Hata hivyo, Yesu hasemi lolote kwa kumjibu.
Hatimaye, wanafunzi wake wanamwambia Yesu: “Mwambie aende zake; kwa sababu yeye huendelea kupiga kelele nyuma yetu.” Akieleza sababu ya kumpuuza, Yesu anasema: “Mimi sikutumwa kwa yeyote ila kwa wale kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.”
Hata hivyo, mwanamke huyo hakati tamaa. Yeye anakaribia Yesu na kusujudu mbele yake. Anasihi, “Bwana, nisaidie!”
Lazima moyo wa Yesu uwe unasukumwa kama nini na sihi hiyo ya moyo wa bidii! Na bado, Yeye anaelekeza tena kwenye daraka lake la kwanza, kuwahudumia watu wa Mungu wa Israeli. Wakati uo huo, kwa wazi ili kutahini imani ya mwanamke huyo, yeye anatumia maoni ya Wayahudi ya kuwabagua watu wa mataifa mengine, akitoa hoja hivi: “Haifai kutwaa mkate wa watoto na kuwatupia mbwa wadogo.”
Kwa namna ya sauti yake yenye huruma na wonyesho wa sura ya uso wake, kwa kweli Yesu anafunua hisia nyororo zake mwenyewe kuelekea wasio Wayahudi. Yeye hata analainisha ulinganisho wake wa Mataifa kwa mbwa kwa kuwataja kuwa “mbwa wadogo,” au vitoto vya mbwa. Badala ya kuchukizwa, mwanamke huyo anaendeleza rejezo la Yesu kwa ubaguzi wa Kiyahudi naye anasema maoni haya kwa unyenyekevu: “Ndiyo, Bwana; lakini kwa kweli mbwa wadogo hula sehemu ya makombo yanayoanguka kutoka meza ya bwana-wakubwa wao.”
“O mwanamke [huyu], imani yako ni kubwa,” ajibu Yesu. “Acha itukie kwako kama utakavyo.” Na inakuwa hivyo! Anaporudi nyumbani kwake, anakuta binti yake kitandani, akiwa ameponywa kabisa.
Kutoka jimbo la pwani ya Sidoni, Yesu na wanafunzi wake wanavuka kwenda upande ule mwingine wa nchi kuelekea penye chemchemi ya Mto Yordani. Yaonekana wanavuka Yordani kwa miguu mahali fulani upande wa juu wa Bahari ya Galilaya na kuingia jimbo la Dekapoli, mashariki mwa bahari. Huko wanapanda mlima, lakini umati unawapata na kumletea Yesu vilema, viwete, vipofu, na mabubu, na wengine wengi ambao ni wagonjwa au wamelemaa. Wanawatupa kabisa miguuni pa Yesu, naye anawaponya. Watu wanastaajabu wanapowaona mabubu wakiongea, vilema wakitembea, na vipofu wakiona, nao wanamsifu Mungu wa Israeli.
Yesu anamwelekezea fikira kwa njia ya pekee mwanamume mmoja ambaye ni kiziwi na hawezi hata kuongea. Mara nyingi viziwi wanafadhaika kwa urahisi, hasa wakiwa katika umati. Huenda Yesu aliona wasiwasi wa mwanamume huyu hasa. Kwa hivyo Yesu kwa huruma anamchukua kutoka kwa umati na kumweka faraghani. Wakiwa peke yao, Yesu aonyesha jambo ambalo atamfanyia. Anaviweka vidole vyake masikioni mwa mwanamume huyo na, baada ya kutema mate, anaugusa ulimi wake. Kisha, akitazama kuelekea mbingu, Yesu augua sana na kusema “Funguka.” Mara hiyo, uwezo wa kusikia wa mwanamume huyo unarudishwa, naye anaweza kuongea kwa njia ya kawaida.
Yesu akiisha kutenda maponyo hayo yote, umati unaitikia kwa kuthamini. Wao wanasema: “Ametenda mambo yote vema. Hata awafanya viziwi wasikie na wasiosema wanene.” Mathayo 15:21-31; Marko 7:24-37, NW.
▪ Kwa nini Yesu hamponyi mara hiyo mtoto wa mwanamke Mgiriki?
▪ Baadaye, Yesu anawapeleka wapi wanafunzi wake?
▪ Yesu anamtendeaje kwa huruma mwanamume kiziwi ambaye hawezi kusema hata kidogo?