Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • gt sura 66
  • Kwenye Sikukuu ya Mahema

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kwenye Sikukuu ya Mahema
  • Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
  • Habari Zinazolingana
  • Kwenye Sikukuu ya Mahema
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
  • Akiwa Yerusalemu kwa Ajili ya Sherehe ya Vibanda
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
  • “Saa Yake Ilikuwa Haijaja Bado”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
  • ‘Hakuna Mtu Mwingine Ambaye Amewahi Kuzungumza Hivyo’
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
Pata Habari Zaidi
Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
gt sura 66

Sura 66

Kwenye Sikukuu ya Mahema

YESU amekuwa mwenye kujulikana sana wakati wa ile miaka karibu mitatu tangu ubatizo wake. Maelfu wengi wameona miujiza yake, na ripoti juu ya utendaji wake mbalimbali zimeenea katika sehemu zote za nchi. Sasa, wakati watu wanapokusanyika kwa ajili ya ile Sikukuu ya Mahema (Vibanda) katika Yerusalemu, wao wanamtafuta huko. “Yuko wapi yule mwanamume?” wao wanataka kujua.

Yesu amekuwa kibishanio. “Yeye ni mwanamume mwema,” watu fulani wanasema. “Yeye si mwema, bali yeye anaongoza vibaya umati wa watu,” wengine wanakazania. Maongezi mengi ya namna hiyo yafanywa kwa sauti za chini-chini wakati wa zile siku za mwanzoni za sikukuu hiyo. Na bado hakuna mtu mwenye ushujaa wa kunena peupe kwa kumtetea Yesu. Hiyo ni kwa sababu watu wanaogopa kisasi cha viongozi Wayahudi.

Wakati nusu ya sikukuu inapokuwa imemalizika, Yesu anawasili. Yeye anapanda kwenda hekaluni, ambako watu wanastaajabia uwezo wake wa kufundisha ulio mzuri sana. Kwa kuwa Yesu hakuhudhuria kamwe zile shule za kirabi, Wayahudi wanaanza kuuliza kwa mshangao: “Mwanamume huyu alipataje maarifa ya herufi, hali yeye hajajifunza kwenye zile shule?”

“Ninayofundisha si yangu mimi,” Yesu anaeleza, “bali ni ya yule aliyenituma. Ikiwa mtu yeyote anatamani kufanya mapenzi Yake, yeye atajua kuhusu mafundisho hayo kama yatoka kwa Mungu au mimi nanena yaliyo ya asili yangu mwenyewe.” Mafundisho ya Yesu yanashikamana sana na sheria ya Mungu. Hivyo, inapasa kuwa wazi kwamba yeye anatafuta utukufu wa Mungu, si wake mwenyewe. “Musa aliwapa nyinyi ile Sheria, sivyo?” Yesu anauliza. Kwa njia ya kukemea, yeye anaendelea kusema: “Hakuna hata mmoja wenu nyinyi anayeitii Sheria.”

Kisha Yesu auliza: “Kwa nini nyinyi mnatafuta kuniua?”

Watu walio miongoni mwa ule umati, ambao labda ni watu waliozuru kwenye sikukuu hiyo, hawana habari kwamba kuna jitihada kama hizo. Wao wanaona ni jambo lisilowazika kwamba mtu yeyote angetaka kuua mwalimu mwenye kufundisha vizuri hivyo. Kwa hiyo wao wanaamini kwamba lazima Yesu awe ana kasoro fulani kwa kufikiri hivyo. “Wewe una roho mwovu,” wanasema. “Ni nani anatafuta kukuua?”

Viongozi Wayahudi wanataka Yesu auawe, hata ingawa huenda ule umati wa watu ukawa haung’amui jambo hilo. Wakati Yesu alipoponya mwanamume mmoja siku ya Sabato mwaka mmoja na nusu kabla ya hapo, viongozi hao walijaribu kumuua. Kwa hiyo sasa Yesu anaonyesha ukosefu wao wa kufikiri vizuri kwa kuwauliza: “Ikiwa mwanamume hupokea tohara siku ya sabato ili sheria ya Musa isivunjwe, je! nyinyi mnanikasirikia kijeuri kwa sababu mimi nilifanya mwanamume awe mzima kabisa katika afya siku ya sabato? Acheni kuhukumu kutokana na sura ya nje, bali hukumuni kwa hukumu yenye uadilifu.”

Wakaaji wa Yerusalemu, ambao wanajua hali ile, sasa wanasema hivi: “Huyu ndiye yule mwanamume ambaye wanamtafuta wamwue, sivyo? Na bado, ona! yeye ananena peupe, nao hawamwambii kitu. Watawala hawajapata kujua hakika kwamba huyu ndiye Kristo, sivyo?” Wakaaji hawa wa Yerusalemu wanaeleza ni kwa nini hawaamini kwamba Yesu ndiye Kristo: “Sisi tunajua mwanamume huyu atoka wapi; lakini wakati Kristo ajapo, hakuna mtu atajua atoka wapi.”

Yesu anajibu: “Nyinyi mnanijua na hata mnajua nitokako. Vilevile, mimi sikuja kwa kujichukulia hatua mwenyewe, bali yeye aliyenituma ni halisi, na nyinyi hammjui. Mimi namjua, kwa sababu mimi ni mwakilishi wa kutoka kwake, na Yeye ndiye aliyenituma.” Kusikia hivyo, wao wanajaribu kumkamata, labda ili wamtie gerezani au wakafanye auawe. Hata hivyo hawafanikiwi kwa sababu sio wakati wa Yesu kufa.

Na bado, wengi wanaweka imani katika Yesu, kama vile inavyowapasa kufanya kweli kweli. Kwani, yeye ametembea juu ya maji, amezituliza pepo, amenyamazisha bahari zenye dhoruba, kwa muujiza akalisha maelfu mikate na samaki wachache, akaponya wagonjwa, akafanya viwete watembee, akafungua macho ya vipofu, akaponya wenye ukoma, na hata akawainua wafu. Kwa hiyo wao wanauliza: “Wakati Kristo awasilipo, yeye hatafanya ishara nyingi zaidi ya zile ambazo mwanamume huyu amefanya, sivyo?”

Wakati Mafarisayo wanaposikia ule umati wa watu ukinung’unika juu ya mambo hayo, wao na wakuu wa makuhani wanatuma maofisa wakakamate Yesu. Yohana 7:11-32, NW.

▪ Yesu anawasili lini kwenye ile sikukuu, na watu wanasema nini juu yake?

▪ Huenda ni kwa nini watu fulani wakawa wanasema kwamba Yesu ana roho mwovu?

▪ Wakaaji wa Yerusalemu wana maoni gani juu ya Yesu?

▪ Kwa nini watu wengi wanaweka imani katika Yesu?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki