Sura 103
Kuzuru Tena Hekalu
YESU na wanafunzi wake wamemaliza sasa hivi tu kukaa usiku wao wa tatu katika Bethania tangu walipowasili kutoka Yeriko. Sasa nuru ya mapambazuko ya asubuhi ya Jumatatu, Nisani 10, yawakuta tayari wakiwa barabarani kwenda Yerusalemu. Yesu ana njaa. Kwa hiyo aonapo mtini wenye majani, auendea aone kama ungeweza kuwa na tini fulani.
Majani ya mti ule yametokea mapema kuliko majira yao, kwa kuwa majira ya tini hayaji mpaka Juni, na sasa ni mwishoni mwa Machi tu. Hata hivyo, kwa uwazi Yesu ahisi kwamba kwa kuwa majani hayo yametokea mapema, tini zingeweza pia kuwa zimetokea mapema. Lakini yeye atamaushwa. Majani yale yameupa mti sura ya udanganyifu. Ndipo Yesu alaani mti ule akisema: “Tangu leo hata milele mtu asilie matunda kwako.” Matokeo ya tendo la Yesu na umaana walo yajulikana asubuhi ifuatayo.
Wakiendelea mbele, upesi Yesu na wanafunzi wake wafika Yerusalemu. Aenda kwenye hekalu, ambalo alikuwa amekagua alasiri iliyotangulia. Hata hivyo, leo, achukua hatua, kama alivyofanya miaka mitatu mapema kidogo alipokuja kwenye Sikukuu ya Kupitwa katika 30 W.K. Yesu atupa nje wale wanaouza na kununua katika hekalu na apindua meza za wabadili fedha na mbao za kukaliwa na wale wanaouza njiwa. Hata haruhusu mtu yeyote aende akiwa na chombo kimoja kupita hekaluni.
Akilaani vikali wale wanaobadili fedha na kuuza wanyama katika hekalu, yeye asema hivi: “Je! haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.” Wao ni wanyang’anyi kwa sababu wadai bei kubwa mno kutoka kwa wale ambao hawana jambo jingine la kufanya isipokuwa kununua kutoka kwao wanyama wenye kuhitajiwa kwa ajili ya dhabihu. Kwa hiyo Yesu aziona shughuli hizi za biashara kuwa namna ya unyakuzi au unyang’anyi.
Wakati wakuu wa makuhani, waandishi, na wakuu wa watu wasikiapo jambo ambalo Yesu amefanya, watafuta njia wanayoweza kufanya auawe. Kwa njia hiyo wathibitisha kwamba hawawezi kubadilishwa wawe wema. Hata hivyo, wao hawajui jinsi ya kumharibu Yesu, kwa kuwa watu wote waendelea kumfuata-fuata ili wamsikie.
Zaidi ya Wayahudi wa asili, Wasio Wayahudi wamekuja pia kwenye Sikukuu ya Kupitwa. Hawa ni waongofu, ikimaanisha kwamba wameongoka wakafuata dini ya Wayahudi. Wagiriki fulani, ambao kwa wazi ni waongofu, sasa wamfikia Filipo na kumwomba wamwone Yesu. Filipo amwendea Andrea, labda kuuliza kama mkutano kama huo ungefaa. Yaonekana kwamba Yesu angali hekaluni, ambako Wagiriki waweza kumwona.
Yesu ajua ana siku chache tu zilizobakia za maisha yake, kwa hiyo yeye atoa kielezi kizuri kuhusu hali yake: “Sasa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu. Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.”
Punje moja ya ngano ina thamani kidogo. Hata hivyo, namna gani ikiwa ndani ya udongo na ‘ife,’ ikimaliza uhai wayo wa kuwa mbegu? Hapo ndipo huchipuka na baada ya muda hukua ikawa bua lenye kuzaa punje nyingi sana za nafaka. Vivyo hivyo, Yesu ni mwanadamu mmoja tu mkamilifu. Lakini akifa akiwa mwaminifu kwa Mungu, hapo yeye awa ndiyo njia ya kuwatolea uhai wa milele waaminifu walio na roho ile ile ya kujidhabihu aliyo nayo. Hivyo, Yesu asema hivi: “Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.”
Ni wazi Yesu hajifikirii yeye mwenyewe tu, kwa maana ndipo yeye aeleza hivi: “Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.” Ni thawabu nzuri kama nini kwa kumfuata Yesu na kumhudumia! Ndiyo thawabu ya kuheshimiwa na Baba ili kushirikiana na Kristo katika ule Ufalme.
Akifikiria mteseko na kifo chenye maumivu makali ambacho chamngojea, Yesu aendelea kusema: “Sasa roho yangu imefadhaika; nami nisemeje? Baba, uniokoe katika saa hii?” Laiti yale yamngojeayo yangeweza kuepukika! Lakini, sivyo, kama asemavyo: “Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii.” Yesu akubaliana na mpango mzima wa Mungu, kutia na kifo chake mwenyewe cha dhabihu. Mathayo 21:12, 13, 18, 19; Marko 11:12-18; Luka 19:45-48; Yohana 12:20-27.
▪ Kwa nini Yesu atarajia kupata tini hata ingawa siyo majira yazo?
▪ Kwa nini Yesu awaita “wanyang’anyi” wale wanaouza katika hekalu?
▪ Ni kwa njia gani Yesu alivyo kama punje ya ngano ambayo hufa?
▪ Yesu ahisije kuhusu mteseko na kifo ambacho chamngojea?