Sura 109
Yesu Ashutumu Wapinzani Wake
YESU ametatanisha kabisa fikira za wapinzani wake wa kidini hivi kwamba wanahofu kumuuliza tena jambo lolote. Kwa hiyo yeye achukua hatua ya kwanza kufichua ukosefu wao wa maarifa. “Nyinyi mwafikiri nini kuhusu Kristo?” yeye auliza. “Ni mwana wa nani?”
“Wa Daudi,” Mafarisayo wajibu.
Ingawa Yesu hakani kwamba Daudi ndiye babu wa kale wa kimwili wa Kristo, au Mesiya, yeye auliza hivi: “Basi, ikoje kwamba Daudi kwa uvuvio [kwenye Zaburi 110] amwita ‘Bwana,’ akisema ‘Yehova alisema kwa Bwana wangu: “Keti kwenye mkono wangu wa kulia mpaka niweke adui zako chini ya nyayo zako”’? Ikiwa, basi, Daudi amwita ‘Bwana,’ yeye ni mwana wake jinsi gani?”
Mafarisayo wakaa kimya, kwa maana hawajui utambulisho wa kweli wa Kristo, au mpakwa-mafuta. Mesiya si mzao wa kibinadamu tu wa Daudi, kama ionekanavyo kuwa ndivyo Mafarisayo waamini, bali yeye alikuwa mbinguni na alikuwa mkuu wa Daudi, au Bwana.
Sasa akigeukia umati wa watu na wanafunzi wake, Yesu aonya kuhusu waandishi na Mafarisayo. Kwa kuwa hawa wafundisha Sheria ya Mungu, wakiwa ‘wamejiketisha wenyewe katika kiti cha Musa,’ Yesu ahimiza hivi: “Mambo yote ambayo wao waambia nyinyi, yatendeni na kuyashika.” Lakini aongezea: “Msitende kulingana na matendo yao, kwa maana wao husema lakini hawafanyi.”
Wao ni wanafiki, na Yesu awashutumu kwa usemi ule ule aliotumia alipokuwa anakula mlo katika nyumba ya Farisayo mmoja miezi kadhaa mapema. “Kazi zote ambazo wao hutenda,” yeye asema, “huzitenda ili waonwe na wanadamu.” Naye aandaa vielezi, akionelea hivi:
“Wao hupanua vikasha vyenye maandiko ambayo wao huvaa kama vilinda-usalama.” Vikasha hivi ambavyo ni vidogo kiasi, vyenye kuvaliwa katika kipaji cha uso au katika pingili ya mkono, vina visehemu vinne vya Sheria: Kutoka 13:1-10, 11-16; na Kumbukumbu 6:4-9; 11:13-21. Lakini Mafarisayo huongeza ukubwa wa vikasha hivi ili kutoa wazo la kwamba wao ni wenye bidii ya kuifuata Sheria.
Yesu aendelea kusema kwamba wao “hupanua matamvua ya mavazi yao.” Kwenye Hesabu 15:38-40 Waisraeli waamriwa wafanye matamvua katika mavazi yao, lakini Mafarisayo hufanya matamvua yao yawe makubwa kuliko ya mtu mwingine yeyote. Kila kitu hufanywa kwa kujionyesha! “Wao hupenda mahali penye umashuhuri mkubwa zaidi,” Yesu ajulisha wazi.
Kwa huzuni, wanafunzi wake mwenyewe wameathiriwa na tamaa hii ya umashuhuri. Kwa hiyo ashauri hivi: “Lakini nyinyi, nyinyi msiitwe Rabi, kwa maana ni mmoja aliye mwalimu wenu, hali nyinyi nyote ni ndugu. Zaidi ya hilo, msiite mtu yeyote baba duniani, kwa maana mmoja ni Baba yenu, yule Mmoja wa kimbingu. Wala msiitwe ‘viongozi,’ kwa maana Kiongozi wenu ni mmoja, aliye Kristo.” Ni lazima wanafunzi wajiondolee kabisa ile tamaa ya kuwa namba moja! “Aliye mkubwa zaidi miongoni mwenu nyinyi ni lazima awe mhudumu wenu,” Yesu aonya kwa upole.
Ndipo yeye atamka mfululizo wa ole juu ya waandishi na Mafarisayo, akiwaita wanafiki. Wao “hufunga kabisa ufalme wa mbingu mbele ya wanadamu,” yeye asema, na “wao ndio wenye kumeza nyumba za wajane na kwa kisingizio hufanya sala ndefu-ndefu.”
“Ole wenu, viongozi vipofu,” Yesu asema. Yeye ashutumu kukosa kwa Mafarisayo viwango vyenye thamani vya kiroho, kama inavyoshuhudiwa na mapambanuzi yenye ugeugeu ambayo wao wayafanya. Kwa kielelezo, wao wasema kwamba, ‘Si kitu mtu yeyote akiapa kwa hekalu, lakini mtu yuko chini ya wajibu akiapa kwa dhahabu ya hekalu.’ Kwa kutia mkazo mwingi juu ya dhahabu ya hekalu kuliko ule watiao juu ya thamani ya kiroho ya mahali hapo pa ibada, wao wafunua upofu wao wa kiadili.
Ndipo, kama alivyofanya mapema, Yesu awalaani vikali Mafarisayo kwa kutoyajali “mambo ya Sheria yenye uzito zaidi, yaani, haki na rehema na uaminifu” na huku wakiweka uangalifu mkubwa juu ya kutoa zaka, au sehemu ya kumi ya mimea miteketeke isiyo na maana.
Yesu awaita Mafarisayo “viongozi vipofu, ambao huchuja inzi na kuakia ngamia!” Wao huchuja inzi atoke katika divai si kwa sababu tu ni mdudu, bali kwa sababu yeye si safi kisherehe. Na bado, kupuuza kwao mambo ya Sheria yaliyo mazito zaidi kwalingana na kumeza ngamia, ambaye pia ni mnyama asiye safi kisherehe. Mathayo 22:41–23:24; Marko 12:35-40; Luka 20:41-47; Walawi 11:4, 21-24, NW.
▪ Kwa nini Mafarisayo wakaa kimya Yesu awaulizapo kuhusu alivyoyasema Daudi katika Zaburi 110?
▪ Kwa nini Mafarisayo hupanua vikasha vyao vyenye Maandiko na kupanua matamvua ya mavazi yao?
▪ Yesu awapa wafuasi wake shauri gani?
▪ Nimapambanuzi gani yenye ugeugeu ambayo Mafarisayo hufanya, na Yesu awalaanije vikali kwa kutojali mambo mazito zaidi?