Sura 122
Kutoka kwa Pilato Mpaka kwa Herode na Kurudi Tena
INGAWA Yesu hafanyi jaribio lolote la kumficha Pilato kwamba yeye ni mfalme, aeleza kwamba Ufalme wake si tisho kwa Roma. “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu,” Yesu asema. “Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.” Hivyo Yesu akiri mara tatu kwamba yeye ana Ufalme, ingawa si wa chanzo cha kidunia.
Hata hivyo, Pilato amkaza zaidi: “Wewe u mfalme basi?” Yaani, wewe ni mfalme hata ingawa Ufalme wako si sehemu ya ulimwengu huu?
Yesu amjulisha Pilato kwamba amekata shauri vizuri, akijibu: “Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.”
Ndiyo, kusudi hasa la Yesu kuwako duniani ni kuitolea “kweli” ushahidi, hasa ile kweli juu ya Ufalme wake. Yesu yuko tayari kuwa mwaminifu kwa kweli hiyo hata ikiwa itamgharimu uhai wake. Ingawa Pilato auliza: “Kweli ni nini?” hangojei maelezo zaidi. Amesikia ya kutosha ili atoe hukumu.
Pilato arudia umati unaongoja nje ya jumba lile. Kwa wazi Yesu akiwa kando yake, awaambia makuhani wakuu na wale walio pamoja nao: “Sioni neno lililo ovu katika mtu huyu.”
Kwa kukasirishwa na uamuzi huo, umati unaanza kusisitiza hivi: “[Yeye] huwataharakisha watu, akifundisha katika Uyahudi wote, tokea Galilaya mpaka huku.”
Ni lazima ushupavu huo usiotumia akili kufikiri wa Wayahudi uwe unashangaza Pilato. Hivyo basi, makuhani wakuu na wanaume wazee wanapoendelea kupaaza sauti, Pilato ageukia Yesu na kuuliza: “Husikii ni mambo mangapi wanayokushuhudia?” Bado, Yesu hafanyi jaribio la kujibu. Utulivu wake katika kukabiliana na yale mashtaka yasiyo na msingi wowote wafanya Pilato kustaajabu.
Anapojua kwamba Yesu ni Mgalilaya, Pilato aona njia ya kujiondoa asiwe na daraka juu yake. Mtawala wa Galilaya, Herode Antipa (mwana wa Herode Mkuu), yumo Yerusalemu kwa ajili ya Sikukuu ya Kupitwa, hivyo basi Pilato ampeleka Yesu kwake. Mapema kidogo, Herode Antipa alikuwa ameagiza Yohana Mbatizaji akatwe kichwa, halafu Herode akaogopa aliposikia juu ya kazi za kimuujiza ambazo Yesu alikuwa akifanya, akihofu kwamba huenda ikawa kwa kweli Yesu ni Yohana ambaye ameinuliwa kutoka kwa wafu.
Sasa, Herode ana shangwe mno kwa tazamio la kumwona Yesu. Hii si kwa sababu ahangaikia hali njema ya Yesu au kwamba ataka kufanya jaribio lolote halisi juu ya kama mashtaka anayofanyiwa ni ya kweli au sivyo. Bali, yeye ni mdadisi tu na atumainia kuona Yesu akifanya muujiza fulani.
Hata hivyo, Yesu akataa kutosheleza udadisi wa Herode. Kwa uhakika, Herode anapokuwa akimuuliza maswali, yeye hasemi neno. Kwa kukata tamaa, Herode na askari-walinzi wake wamdhihaki Yesu. Wamvika vazi jangavu na kumfanyia mzaha. Halafu wampeleka tena kwa Pilato. Tokeo ni kwamba, Herode na Pilato, ambao hapo kwanza walikuwa wamekuwa maadui, wanakuwa marafiki wakubwa.
Yesu anaporudi, Pilato aita makuhani wakuu, watawala wa Wayahudi, na watu wakusanyike pamoja na kusema hivi: “Mtu huyu mmemleta kwangu kana kwamba anapotosha watu; nami, tazama, nimeamua mambo yake mbele yenu, ila sikuona kwake kosa lo lote katika mambo hayo mliyomshitaki; wala hata Herode, kwa maana amemrudisha kwetu; basi tazama, hakuna neno lo lote alilotenda lipasalo kufa. Kwa hiyo nitamrudi, kisha nitamfungua.”
Hivyo, Pilato amejulisha rasmi mara mbili kwamba Yesu hana hatia. Ana hamu ya kumwacha huru, kwa maana afahamu kwamba ni kwa sababu ya wivu tu kwamba makuhani wamemtia mikononi mwake. Lakini Pilato anapoendelea kujaribu kumwachilia Yesu, apata kichocheo kingine imara afanye hivyo. Anapokuwa katika kiti chake cha hukumu, mke wake apeleka ujumbe, akimhimiza hivi: “Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto [kwa wazi yenye asili ya kimungu] kwa ajili yake.”
Hata hivyo, Pilato aweza kufunguaje mwanamume huyu asiye na hatia, kama vile anavyojua inampasa? Yohana 18:36-38; Luka 23:4-16; Mathayo 27:12-14, 18, 19; 14:1, 2; Marko 15:2-5.
▪ Yesu ajibuje swali kuhusu ufalme wake?
▪ Ni nini “kweli” ambayo Yesu alitumia maisha yake ya kidunia akiitolea ushahidi?
▪ Hukumu ya Pilato ni nini, watu waitikiaje, na Pilato afanyia Yesu nini?
▪ Herode Antipa ni nani, kwa nini ana shangwe nyingi mno kumwona Yesu, naye amfanyia nini?
▪ Kwa nini Pilato ana hamu ya kumweka Yesu huru?